top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Helen L, M.D

2 Aprili 2026, 16:17:51

Usifanye ‘dieting’ kupunguza uzito, uepuke ongezeko la uzito mara mbili zaidi ya uliopoteza

Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa, asilimia 80 hadi 90 ya watu wanaofanya ‘dieting’, baada ya kupungua na kufikia malengo ya uzito wanaoutaka na kuacha, miili yao hupata ongezeka la uzito mara mbili ya ule ulioupotea kwa kufanya ‘dieting’. Kula vema kila siku kama mbadala wa kufanya ‘dieting’


Dieting ni nini?


‘Dieting’ ni kitendo cha kuzingatia utumiaji wa chakula na vinywaji kwa lengo la kupunguza, kuongeza au kubaki na uzito ulionao kama njia ya kujikinga au kutibu magonjwa kama shinikizo la juu la damu, kisukari na obeziti.


Watu wengi duniani wamekuwa wakitumia njia ya ‘dieting’ ili kupunguza uzito. Njia hii ya ‘dieting’ ni njia nzuri ya kupunguza uzito kwa muda mfupi lakini kwa bahati mbaya si njia inayoshauriwa kiafya. Matumizi ya njia hii hufanya mwili ujipe adhabu ya kuongezeka uzito mara dufu zaidi ya ule wa awali mara baada ya kuacha kufanya ‘dieting’. Unashauriwa kutumia njia za kiafya kupunguza uzito badala ya kufanya ‘dieting’.


Sababu za uzito kujirudia mara dufu baada ya kuacha kufanya ‘dieting’


Wanasayansi wamefanya uchunguzi wa mwili wa binadamu kwa miaka kadhaa na kugundua kuwa, homoni zinazotolewa kwenye utumbo, kongosho na kutoka kwenye mafuta huchangia kwa kiasi kikubwa kurekebisha uzito, hisia za njaa pamoja na matumizi ya nishati mwilini. Wakati unajizuia kula vyakula aina fulani ili kupunguza uzito, mabadiliko ya homoni mwilini mwako hutokea, yanayofanya ubongo utume taarifa ya kukabiliana na mabadiliko hayo. Kwa mfano, endapo kiwango cha mafuta kimepungua mwilini, kiwango cha homoni leptin kinachouambia ubongo kwamba umeshiba hupungua, na kiwango cha homoni za kuongeza njaa kama ghrelin huongezeka na kusabisha upate njaa na ule sana. Kujinyima kwa muda mfupi kula vyakula aina fulani kwa lengo la kupunguza uzito, husababisha mabadiliko ya muda mfupi ambayo huamsha mwili wako kurejesha uzito wa awali kwa kuongeza homoni zinazoleta njaa na kusababisha upende kula zaidi, na hivyo kuongezeka uzito mara dufu.


Njia nzuri za kuwa na uzito wa kiafya


  • Kula matunda na mboga za majani kwa wingi

  • Acha kula vyakula na vinywaji vyenye sukari kama soda, keki na pipi

  • Tumia mafuta ya kiafya kutoka yanayotokana na mimea kama, mzeituni, karanga, ufuta, alizeti n.k yatakayokufanya ujihisi umeshiba na kupunguza unene

  • Fanya mazoezi ya kutoa jasho na kufanya misuli ifanye kazi mfano, tembea mwendao wa dakika 30 kwa siku, lima, palilia bustani, endesha baiskeli n.k

  • Fanya mazoezi ya misuli ili kufanya misuli yako ifanye kazi na kutumia sukari iliyo kwenye damu

  • Kula chakula ulichokipika mwenyewe badala ya kula mgahawani au hotelini ili kujiepusha na viungo vinavyoongeza uzito pia ufurahie ladha ya chakula chako mwenyewe.

  • Pata kifungua kinywa chenye protini kwa wingi mfano mayai, maziwa mgando, nyama ya samaki, juisi yenye maziwa mtindi n.k badala ya wanga

  • Usitumie vinywaji wa kuongeza nguvu, kama vinywaji vya wanamichezo, ‘energy drink’ n.k, badala yake tumia maji

  • Kunywa maji ya kutosha kila siku, kunywa maji ya uvuguvugu dakila 30 kabla ya kula mlo mzito

  • Epuka kula kila kinachokuja mbele yako, kula kwa ratiba uliyojipangia

  • Usitumie mazao ya vyakula vilivyokobolewa kama mahindi, n.k

  • Usitumie vyakula vya kupunguza uzito

  • Kuwa na timu ya marafiki wenye malengo ya kufanya mazoezi na kula vema

  • Unapokuwa na mawazo au msongo, jipe muda wa kufanya vitu/mambo unavyopenda kufanya ili kuepuka mawazo mengi yanayoweza kupelekea kula sana na kuongezeka uzito

  • Penda kutumia vyakula asilia kama mbadala wa vyakula vya kusindikwa

  • Penda kujifunza kuhusu mambo ya kiafya na njia salama za kuwa na uzito unaotakiwa kiafya

Imeandikwa:

2 Aprili 2026, 16:17:51

ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.

Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.

bottom of page