top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Je, naweza zuia mimba kwa kutumia p2 siku moja kabla?

P2 (levonorgestrel) ni kidonge cha dharura kinachofanya kazi kwa kuchelewesha au kuzuia yai kutoka. Ukimeza kabla ya tendo, huweza kutoa kinga fulani kama yai halijatoka bado, lakini haitoi kinga ya uhakika kwa siku zinazofuata, haikukingi tendo la siku 2–3 baadaye kwa uhakika, na matumizi ya mara kwa mara huvuruga hedhi. Ndiyo maana P2 si njia ya kawaida ya uzazi wa mpango. Ikiwa umekunywa P2 jana na leo umefanya tendo bila kinga, kinga yako si ya uhakika – njia bora ni kitanzi cha shaba ndani ya siku 5, au kuanza njia ya kudumu. Kwa anayehitaji kinga ya mara kwa mara, vidonge vya kila siku, sindano au kipandikizi ni salama na bora zaidi.

Namna ya kufahamu urefu wa mzunguko wa hedhi

Urefu wa mzunguko ni idadi ya siku kuanzia siku ya KWANZA ya hedhi moja hadi siku moja kabla ya hedhi inayofuata kuanza. Kwa mfano: hedhi 13/12, 11/1, 13/2 na 12/3 – mizunguko ni siku 29, 33 na 28; wastani karibu siku 30. Mzunguko wa kawaida kwa mtu mzima ni siku 24 hadi 38, na kutofautiana hadi siku 7 hadi 9 kati ya miezi ni kawaida. Kwa wastani wa siku 30, uovuleshaji ni karibu siku ya 16 na siku za hatari karibu siku ya 11 hadi 16.

Namna ya kusafisha uke kwa usalama?

Uke wa ndani hujisafisha wenyewe kwa ute wake na bakteria wazuri (lactobacilli) wanaoweka mazingira ya tindikali yanayozuia vijidudu. Kinachohitaji kuoshwa ni sehemu ya nje tu (vulva) – kwa maji safi, au sabuni laini isiyo na manukato nje kabisa. Kusafisha ndani kwa kidole, maji, sabuni, dawa, mitishamba au mvuke huvuruga mazingira hayo na kuongeza fangasi, bakteria vaginosis, PID, na hata hatari ya kuambukizwa VVU.

Kutokwa na ute mweupe mzito ukeni ni dalili ya mimba?

Ute mweupe usio na harufu mbaya ni wa kawaida kwa mwanamke katika mzunguko wake wote wa hedhi, na huongezeka wakati wa ujauzito kwa sababu ya homoni ya estrojeni na damu nyingi kwenye uke. Ute mzito na mweupe huonekana pia baada ya yai kutoka hadi kabla ya hedhi kwa sababu ya homoni ya projesteroni – kwa hiyo peke yake hauthibitishi mimba. Wakati wa yai kutoka (uovuleshaji), ute huwa mwepesi, unaoteleza na kuvutika kama ute wa yai bichi.

Kutapika nyongo yenye chembe za damu kwa mjamzito

Michirizi au vitone vidogo vya damu kwenye matapishi ya mjamzito mara nyingi hutokana na kutapika kwa nguvu na kwa muda mrefu, kunakochubua koo au umio (mchaniko wa Mallory-Weiss), tindikali kurudi juu (kiungulia), fizi kutoa damu, au damu ya pua iliyomezwa. Haya yote hutokea zaidi wakati wa ujauzito. Mara chache chanzo ni kidonda cha tumbo. Nyongo ya njano au kijani ni kawaida tumbo likiwa tupu. Damu nyingi, matapishi kama unga wa kahawa, choo cheusi, kizunguzungu, au kushindwa kubakiza maji kwa zaidi ya masaa 24, ni dharura zinazohitaji hospitali mara moja.

Shahawa kuwa nzito na mabonge mabonge ni kawaida?

Ndiyo, kwa kawaida. Shahawa hutoka zikiwa nzito kama jeli au zenye mabonge kwa sababu ya protini kutoka kwenye vifuko vya shahawa (seminal vesicles) zinazozigandisha kwa muda – kusaidia mbegu kubaki ukeni. Kisha vimeng'enya vya tezi dume huziyeyusha kuwa maji ndani ya dakika 15–60 (WHO 2021). Huwa nzito zaidi baada ya kukaa siku nyingi bila kumwaga, na huweza kuonekana nzito zaidi ukiwa na upungufu wa maji. Ishara za tatizo: shahawa zisizoyeyuka baada ya saa 1 (hupimwa maabara – huweza kuathiri uzazi), damu, rangi ya njano/kijani, harufu mbaya, maumivu wakati wa kumwaga, homa, au tatizo la kupata mtoto – hizi zinahitaji uchunguzi (maambukizi ya tezi dume, magonjwa ya zinaa, kipimo cha shahawa).

bottom of page