Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya
Kutokwa na jasho mkono moja husababishwa na nini?
Jasho zaidi kwenye mkono mmoja mara nyingi ni haipahaidrosisi ya kawaida inayoonekana zaidi upande mmoja, au mkono unaotumika zaidi. Lakini jasho la upande mmoja pia huweza kutokea kwa sababu upande mwingine umeacha kutoa jasho (jasho la kufidia) – kutokana na tatizo la mishipa ya fahamu ya simpathetiki: kiharusi, uti wa mgongo, kisukari, au uvimbe wa sehemu ya juu ya pafu au shingo. Dalili kama kope kulegea, mboni ndogo upande mmoja, ganzi au udhaifu zinahitaji uchunguzi.
Umri wa mimba ni wiki ngapi?
Mimba huchukua wastani wa wiki 40, sawa na siku 280 au karibu miezi 9 na siku 7, tangu siku ya kwanza ya hedhi ya mwisho. Hesabu hii haianzii siku ya kushika mimba, ambayo kwa mzunguko wa siku 28 huwa karibu wiki 2 baadaye. Wanawake wengi hujifungua kati ya wiki 37 na 42, na wachache tu hujifungua siku hasa ya tarehe iliyokadiriwa. Ultrasound ya mapema, kabla ya wiki 14, hukadiria umri wa mimba kwa usahihi zaidi.

Homa baada ya kujifungua husabbaishwa na nini?
Homa baada ya kujifungua ni joto la 38°C au zaidi baada ya kujifungua; homa ndani ya siku 10 (hasa ikipimwa mara mbili tofauti) inahitaji kutafuta chanzo. Visababishi vikuu: maambukizi ya mfuko wa uzazi (endometritis – hasa baada ya upasuaji, uchungu mrefu, mabaki ya kondo), kidonda cha upasuaji au msamba, maambukizi ya mkojo, matiti kujaa au mastitis, nimonia, damu kuganda kwenye mishipa, na Tanzania – malaria. Maambukizi yanaweza kusambaa kwenye damu (sepsis), ambayo ni chanzo kikuu cha vifo vya akina mama. Dalili za hatari ni homa na kutetemeka, lokia yenye harufu mbaya, maumivu ya tumbo, moyo kwenda mbio, kupumua haraka na kuchanganyikiwa. Matibabu ni hospitalini: vipimo (damu, malaria, mkojo, ultrasound), antibiotiki kwa mshipa, maji, na kuondoa mabaki.
Kinyesi chenye kamasi: Je ni kawaida au kinaashiria tatizo?
Utumbo mpana hutengeneza ute (kamasi) kulainisha kinyesi, kwa hiyo kiasi kidogo cha ute mweupe au wa njano mara moja moja ni kawaida. Kamasi nyingi au za mara kwa mara husababishwa na maambukizi ya tumbo (bakteria kama shigella na salmonella, amiba, giardia, virusi), sindromu ya utumbo sumbufu (IBS) yenye kamasi bila damu na maumivu yanayopungua baada ya choo, choo kigumu, mzio au kutovumilia chakula kama laktosi, bawasiri na mpasuko wa njia ya haja kubwa, na magonjwa ya uchochezi ya utumbo kama kolaitisi ya vidonda na Crohn, ambayo mara nyingi huambatana na damu, kuharisha kwa wiki na kupungua uzito. Mara chache, hasa baada ya miaka 45, chanzo ni saratani ya utumbo mpana. Kamasi yenye damu, homa, kupungua uzito au kuharisha kwa muda mrefu vinahitaji uchunguzi.
Nawezaje kuongeza nguvu za kiume?
Nguvu za kiume hutegemea mishipa ya damu, mishipa ya fahamu, homoni na akili. Kinachothibitishwa kusaidia ni: kufanya mazoezi mara kwa mara, kupunguza uzito uliozidi, kuacha sigara, kupunguza pombe, kulala vizuri, kudhibiti kisukari na presha, na mlo wenye mboga, matunda, nafaka zisizokobolewa, maharagwe, samaki na karanga. Hakuna tunda moja (zabibu, tikiti maji, machungwa) lililothibitishwa kuongeza nguvu za kiume peke yake. Upungufu unaoendelea unahitaji uchunguzi – mara nyingi ni dalili ya mapema ya ugonjwa wa moyo au kisukari.
Kuota vipele katika ngozi husababishwa na nini?
Vipele vya ngozi (vinundu vidogo vilivyoinuka) husababishwa na: chunusi na vinyweleo kuziba, maambukizi ya vinyweleo (folikulaitisi), kuumwa na wadudu, mzio, vipele vya jasho, virusi (molluscum, sunzua, tetekuwanga), upele (scabies), na vinundu vya ngozi kama keratosis pilaris (mikononi na mapajani). Vipele vikubwa vinavyouma vyenye usaha ni majipu. Mahali, kama vinawasha, vinauma au vina usaha husaidia kutambua chanzo.
