Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Je, ukubwa wa uume una mchango kwa mwanamke kuridhika kwa kingono?
Tafiti zinaonyesha ukubwa wa uume unaweza kuchangia kuhisi raha kwa baadhi ya wanawake, hasa unene, lakini hauamui peke yake kiwango cha kuridhika kingono. Kwa ujumla, mawasiliano, msisimko unaofaa, ukaribu wa kihisia na kuelewana na mwenza vinaweza kuwa muhimu zaidi kuliko kuwa na uume mkubwa.

Kutembea Pekupeku
Kumehusishwa katika tafiti na mabadiliko chanya mwilini ikiwa pamoja na kupungua kwa maumivu na uchovu, kuongezeka kwa nguvu, kuboreka kwa mtiririko wa damu, kupungua kwa huzuni na sukari kwenye damu. Kwa ujumla, tafiti zinaonyesha kuwa kutembea peku ni njia rahisi ya kuuweka mwili katika mawasiliano ya moja kwa moja na ardhi na inaweza kuleta manufaa mbalimbali kwa afya na ustawi wa mwili.

Athari ya Nosibo
Inaonyesha kuwa akili inaweza kuuchochea mwili kuitikia fikra na hofu kana kwamba tishio ni la kweli, hivyo mtu anaweza kupata au kuhisi dalili halisi hata bila ugonjwa unaohofiwa kuwepo. Kuelewa uhusiano wa akili na mwili husaidia kupunguza hofu na dalili za magonjwa yasiyo halisi, huku tukitambua kuwa magonjwa halisi bado yanahitaji uchunguzi na matibabu sahihi.

Kupima Virusi vya UKIMWI (VVU)
Hufanyika kwa kuchukua damu au majimaji ya mdomoni, kulingana na aina ya kipimo, na majibu chanya yanahitaji kuthibitishwa kituo cha afya. Wakati sahihi wa kupima ni baada ya tukio la hatari kwa kipimo cha awali, kisha kurudia kipimo baada ya dirisha la matazamio la kipimo husika kukamilika ili kupata jibu linaloaminika.

Ngono ya kinywa na magonjwa ya zinaa
Ngozo ya kinywa kwa uke au uume inaweza kueneza magonjwa ya zinaa kama kisonono, kaswende, herpes na HPV, hivyo si salama kabisa hata kama hakuna dalili. Kuepuka ngono ya kinywa huondoa hatari yake, huku kondomu hutumika kupunguza hatari kwa wale wanaochagua kufanya tendo hilo.

Chumvi na ukinzani wa homoni ya insulini
Tafiti zinaonyesha kupunguza chumvi kwa kiwango kikubwa sana kunaweza kuongeza ukinzani kwenye utendaji kazi wa insulini, hali ambayo kwa muda mrefu inaweza kuchangia ongezeko la hatari ya kisukari aina ya pili. Hata hivyo, ushahidi huu hautoshi kusema kwamba chumvi kidogo husababisha kisukari aina ya pili, wala kwamba kula chumvi nyingi huzuia kisukari; kinachohitajika ni ulaji wa chumvi wenye uwiano pamoja na mtindo bora wa maisha.
