top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Je, unahitaji fanya vipimo kabla ya kuanza kutumia majira?

Kwa wanawake wengi, vidonge vya majira vyenye vichocheo viwili vinaweza kuanzishwa bila uchunguzi wa ndani wa nyonga, vipimo vya damu au maabara, kipimo cha saratani ya shingo ya kizazi wala uchunguzi wa matiti. Kinachohitajika ni kuhakikisha huna mimba (kwa maswali, dalili au kipimo cha mkojo) na kupima presha – WHO inashauri presha ipimwe kabla ya kuanza vidonge mchanganyiko.

Wasiwasi wa kupitiliza muda wa kujifungua

Mimba hukaa wastani wa wiki 40; kujifungua kati ya wiki 37 na 41 na siku 6 ni kawaida. Wiki 42 au zaidi ni kupitiliza. Sababu ya kawaida zaidi ni tarehe kukosewa (hasa bila ultrasound ya mapema), mimba ya kwanza, historia ya kupitiliza, unene na urithi. Kupitiliza huongeza hatari ya kondo kuchoka, maji ya chupa kupungua, mtoto kumeza kinyesi na kifo tumboni. Kwa hiyo WHO hushauri kuanzisha uchungu hospitalini mimba ikifika wiki 41, baada ya kuthibitisha tarehe na hali ya mtoto.

Dalili za gonorrhea kwa mwanaume: Hatari ya kujitibu bila vipimo sahihi

Kisonono, au gono, ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria. Kwa mwanaume huleta usaha wa njano au kijani kutoka kwenye uume, kuungua wakati wa kukojoa, na hisia za kutekenya ndani ya uume. Hutibiwa kwa antibiotiki maalumu, mara nyingi sindano ya ceftriaxone pamoja na dawa ya kumeza ya klamidia kulingana na mwongozo wa tiba wa taifa, si kwa metronidazole.

Hedhi ni nini? Maelezo kamili kwa Mwanamke

Hedhi ni kutoka kwa ukuta wa ndani wa mfuko wa uzazi (endometrium) pamoja na damu kupitia uke, pale mimba haikutungwa katika mzunguko huo. Kila mwezi, homoni ya estrogen hujenga ukuta huo; baada ya yai kutoka, progesterone huuandaa kupokea mimba; mimba isipotokea, progesterone hushuka na ukuta hutoka – hiyo ndiyo hedhi. Damu ya hedhi ina damu, vipande vya ukuta wa mfuko, ute wa mlango wa kizazi na seli za uke – haina yai hai; yai lisilorutubishwa huyeyuka siku 1 baada ya kutoka, kabla ya hedhi. Mzunguko wa kawaida ni siku 24–38, damu hadi siku 8.

Kwanini mtoto hucheza sana tumboni wakati wa usiku?

Ni kawaida mtoto kucheza zaidi usiku. Mchana, mwendo wa mama anapotembea na kufanya kazi humtikisa mtoto na kumtuliza, na mama mwenye shughuli hatambui mateke mengi. Jioni na usiku mama akitulia, huhisi kila mwendo, na sukari ya mlo wa jioni pia huweza kumchangamsha mtoto. Mtoto ana vipindi vyake vya kulala na kuamka. Kinachojalisha ni mpangilio wake – ukibadilika au mwendo kupungua, nenda kituo cha afya siku hiyo hiyo.

Kuchubuka kwenye tendo, maumivu na uchafu mweupe ukeni, je dalili za nini?

Maumivu wakati wa ngono, kuchubuka na uchafu mweupe kama maziwa mara nyingi ni fangasi (candida) – fangasi huifanya ngozi ya uke na mashavu ya uke kuwa nyekundu, kuvimba na kupasuka kwa urahisi wakati wa msuguano. Kama tatizo linarudi baada ya tiba – mara 3 au zaidi kwa mwaka (fangasi wa kujirudia) – uchunguzi zaidi unahitajika: culture ya ute (baadhi ya aina za fangasi hazijibu dawa za kawaida), sukari ya damu (kisukari), kipimo cha VVU, na kuangalia matumizi ya antibiotiki, steroids au uzazi wa mpango wenye estrojeni nyingi. Visababishi vingine: ukavu wa uke (maandalizi kidogo, kunyonyesha, komahedhi, Depo), mzio wa kondomu ya mpira, vilainishi au sabuni, BV, trichomonas, herpes (vidonda vidogo vinavyouma), na misuli ya uke kukaza kwa hofu (vaginismus). Tiba ya fangasi wa kujirudia ni ya muda mrefu kwa maelekezo ya mtaalamu. Mwenza wa kiume hatibiwi kwa fangasi kwa kawaida, isipokuwa ana dalili (wekundu, kuwasha uumeni).

bottom of page