top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Sospeter B, MD

Imeboreshwa:

3 Machi 2026, 08:38:36

Kitovu cha mtoto mchanga: Mwongozo kamili

Kitovu cha mtoto ni sehemu ya mabaki ya kiungamwana kinachobaki baada ya kukatwa mara tu baada ya kuzaliwa. Kiasili, kitovu hutumika wakati wa ujauzito kama njia ya kupitisha virutubisho, oksijeni na kuondoa taka mwilini kati ya mama na mtoto. Baada ya kuzaliwa, kazi hii hukoma na sehemu iliyobaki hugeuka kuwa kitovu, ambacho hupitia hatua za kukauka, kunyauka na hatimaye kudondoka.


Makala hii inazungumzia kuhusu kitovu cha mtoto, kuanzia pale mtoto anapozaliwa hadi kitovu kinapodondoka kabisa. Inafafanua hatua za mabadiliko ya kitovu, jinsi kinavyotunzwa, dalili za hatari zinazoweza kuashiria maambukizi, na wakati sahihi wa kutafuta huduma ya afya. Pia inaeleza mbinu salama za kuhakikisha kitovu kinapona kwa haraka bila madhara.


Katika makala hii, neno kitovu limetumika kumaanisha kipande cha kiungamwana kinachobaki kwenye tumbo la mtoto baada ya kukatwa wakati wa kuzaliwa. Neno kiunga mwana pia limetajwa ndani ya makala, likirejea chanzo cha kitovu kabla ya kukatwa, lakini neno kuu linalotumika katika maelezo haya ya kitaalamu ni kitovu.


1. Mabadiliko ya Kitovu kuanzia Kuzaliwa hadi kudondoka

Baada ya mtoto kuzaliwa, sehemu ya kiungamwana inayobaki tumboni mwa mtoto huitwa kitovu. Kitovu hiki hupitia mabadiliko kadhaa ya kimaumbile kabla ya kudondoka au kuanguka, na neno kudondoka katika muktadha huu humaanisha pia kukatika kwa kitovu kutoka kwenye kitako cha ngozi ya tumbo la mtoto. Mabadiliko haya ni ya hatua kwa hatua na ni sehemu ya mchakato wa kawaida wa kupona kwa jeraha la kuzaliwa. Utunzaji sahihi huwezesha kitovu kukauka, kunyauka na kujitenga wenyewe bila maumivu.


Mara baada ya kuzaliwa

  • Kitovu huwa cheupe au bluu nyepesi, kikiwa kimetengenezwa kwa tishu laini zenye unyevunyevu.

  • Hufungwa “kubanwa” au kufungwa kwa kamba maalumu ili kuzuia kutokwa damu.

  • Katika saa chache za kwanza, watoto wengi huwa na mabaki kidogo ya damu kwenye kitako cha kitovu , hali hii huwa ya kawaida isipokuwa ikizidi.


Siku 1–3 baada ya kuzaliwa

  • Kitovu huanza kukauka, rangi hubadilika kuwa ya kijivu, kahawia au nyeusi.

  • Tishu hupungua unyevunyevu na kuwa ngumu zaidi.


Siku 4–14

  • Kitovu huanza kunyauka kabisa, huanza kulegea kwenye sehemu ya kitako chake inapogusana na tumbo.

  • Wakati wowote baina ya wiki 1–2, kitovu cha kichanga hudondoka chenyewe bila maumivu.


2. Wakati kitovu kudondoka

Kwa kawaida kitovu hudondoka au kukatika;

  • Wiki 1 hadi 2 baada ya kuzaliwa.

  • Watoto wengine vitovu vyao hudondoka mapema zaidi, na wengine huchukua muda mrefu kidogo, mradi hakuna dalili za maambukizi.


3. Mambo ya Msingi ya kutunza Kitovu cha kichanga


Kuhakikisha Kitovu kinakuwa kikavu na kisafi

Huu ndio msingi wa matunzo salama:

  • Hakikisha kitovu kinabaki kikavu.

  • Epuka kumwagia maji moja kwa moja wakati wa kumuosha mtoto; tumia kitambaa kilicholowekwa maji safi kwa usafi wa mwili.

  • Endapo maji yamegusa kitovu, kausha kwa kitambaa kisafi kilichokamuliwa vizuri.


Nguo na Pampasi

  • Funga pampasi chini ya kitovu, kuepuka msuguano na unyevu wa mkojo/kinyesi.

  • Kama pampasi inagusa kitovu, kata sehemu ya mbele ili kuacha kitovu wazi na kikavu na huru.


Epuka matumizi ya dawa au mafuta

  • Usipake dawa yoyote (ikiwa pamoja na mafuta, majivu, dawa za kienyeji, au spiriti kali) isipokuwa kwa maelekezo ya mtaalamu wa afya.

  • Dawa zisizo sahihi huchelewesha kupona na kuongeza hatari ya maambukizi.


4. Mabadiliko ya kawaida kabla ya kudondoka kwa kitovu

Ni kawaida kuona:

  • Rangi kubadilika kutoka nyeupe → kijivu → kahawia → nyeusi

  • Kitovu kuwa kikavu na kigumu

  • Msingi kuwa na wekundu mdogo mara kitovu kinapokuwa karibu kudondoka

  • Kitovu kunuka kidogo wakati wa kukauka, ikiwa hakuna usaha


Haya siyo dalili za ugonjwa ikiwa hakuna maumivu, uvimbe au majimaji yasiyo ya kawaida.


5. Baada ya kitovu Kudondoka ni nini hutokea?

  • Unaweza kuona wekundu mdogo kwenye eneo la kitovu.

  • Kuonekana kwa tone dogo la damu ni kawaida ndani ya siku chache.

  • Majimaji mepesi ya kupona kwa kitovu yanaweza kuendelea kutoka kwa siku kadhaa hadi wiki moja.

  • Maeneo haya yanapaswa kuendelea kuwa safi na kavu.


6. Nini ufanye kama kitovu hakijadondoka?

Jedwali 1 linaeleza kwa urahisi hatua muhimu za kuchukua pale kitovu cha mtoto kinapochelewa kudondoka. Linawaongoza wazazi na walezi kujua namna sahihi ya kukitunza, matatizo yanayoweza kuchelewesha kupona, na dalili za hatari zinazohitaji ushauri wa daktari mara moja. Utangulizi huu unasaidia kuhakikisha kitovu kinapona kwa usalama na ndani ya muda unaotarajiwa.


 Jedwali 1:Nini cha Kufanya Ikiwa Kitovu Hakijadondoka

Tatizo / Hali

Nini cha kufanya

Kwa nini ni muhimu

Kitovu hakijadondoka baada ya wiki 1–2

Endelea na “kukikausha kama kina majimaji” – weka kitovu kikavu na kisafi

Unyevu huchochea bakteria na kuchelewesha kukauka

Kitovu kulowana wakati wa kuoga

Futa kwa kitambaa kisafi chenye unyevunyevu kidogo, kisha kikaushe

Kuzuia maambukizi na kuharakisha kukauka

Pampasi kugusa au kufunika kitovu

Funga pampasi chini ya kitovu au kata sehemu ya juu ili isiguse kitovu

Kuepuka msuguano na unyevu unaochelewesha kudondoka

Kitovu kuonekana kimelegea lakini bado hakijadondoka

Usivute, usinyofoe, usikiondoe

Kuepuka kutokwa damu na uambukizaji wa jeraha

Majimaji au harufu isiyo kali tu

Endelea kufuatilia huku ukikiweka kikavu

Inaweza kuwa sehemu ya mchakato wa kukauka

Majimaji mengi, harufu kali, wekundu au maumivu

Wasiliana na daktari mara moja

Inaashiria maambukizi ya kitovu (omphalaitisi)

Damu nyingi kutoka kwenye eneo la kitovu

Mhimize mzazi kutafuta huduma ya afya haraka

Inaweza kuashiria jeraha au tatizo la kuganda damu

Kitovu hakijadondoka baada ya wiki 3

Muone daktari kwa uchunguzi

Inaweza kusababishwa na unyevu sugu au granuloma

Baada ya kudondoka, nyama laini nyekundu inaonekana

Usipake dawa za nyumbani – muone mtaalamu

Inaweza kuwa granuloma ya kitovu inayohitaji matibabu

Mtoto kulia ukigusa kitovu

Pata ushauri wa haraka wa afya

Maumivu ni ishara ya tatizo lisilo la kawaida


7. Wakati gani wa kumwona Daktari haraka?

Muone mtaalamu wa afya haraka endapo:


Kuna dalili za maambukizi kwenye Kitovu (Omphalaitisi)

Dalili hizo ni pamoja na;

  • Kutotoa harufu kali isiyo ya kawaida

  • Majimaji ya njano/ya kijani (usaha)

  • Ngozi kuzunguka kitovu kuwa nyekundu, yenye joto au kuvimba

  • Mtoto kulia kila kitovu kinapoguswa

  • Homa au ishara nyingine za ugonjwa


Dalili zingine za hatari

  • Kitovu hakijadondoka ndani ya wiki 3

  • Kutoka damu nyingi au isiyokoma

  • Kuota nyama laini nyekundu baada ya kudondoka (granuloma ya kitovu)

  • Fistula ya kitovu (majimaji yanayotoka bila kukoma)

  • Viungo vya ndani kuonekana kupitia kitovu (ngiri ya kitovu—hii mara nyingi si dharura isipokuwa ikizidi)



8. Jinsi ya kuharakisha kitovu kinadondoka au kukatika kwa kwa Usalama

  • Kipaumbele ni kukausha kitovu, si kukilazimisha kidondoke au kukatika.

  • Epuka kulowanisha kitovu kila mara.

  • Hakikisha hakipati msuguano wa nguo au pampasi.

  • Usikivute, kukinyofoa au kukikata hata kama kinaonekana kimelegea.


9. Maneno mbadala yanayomaanisha kitovu

Watu hutumia maneno tofauti kama:

  • Kitovu cha mtoto

  • Kipande cha kiungamwana

  • Shina la umbiliko

  • Shina la kitovu

Kwa uhalisia wa kitiba, kitovu ndiyo neno sahihi kwa kipande kinachobaki baada ya mtoto kuzaliwa.


Hitimisho

Kitovu cha mtoto ni sehemu inayohitaji uangalizi wa karibu lakini wa kawaida. Utunzaji sahihi kama kuhakikisha eneo la kitovu ni safi na kavu- hupunguza hatari ya maambukizi na huruhusu kitovu kudondoka kwa wakati. Wazazi na walezi wanaonufaika na maelezo haya wanapaswa kupewa elimu ya kujua mabadiliko ya kawaida na dalili za hatari ili kuamua lini kutafuta huduma za afya.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake ya kina

1. Je, kitovu cha mtoto huanza kubadilika lini baada ya kuzaliwa?

Kubadilika kwa kitovu huanza mara tu baada ya kuzaliwa, pale ambako kibanio kimefungwa na sehemu iliyobaki imekatwa. Ndani ya saa chache, kitovu huanza kupoteza unyevu wake wa awali, hubadilika rangi na kuwa kigumu. Mabadiliko haya ni sehemu ya mchakato wa kupona ambapo kitovu kinajiandaa kukauka, kunyauka na hatimaye kujitenga na ngozi ya mtoto bila maumivu.

2. Kwa kawaida kitovu cha mtoto hudondoka baada ya muda gani?

Kitovu cha mtoto mara nyingi hudondoka baina ya wiki 1 hadi 2 baada ya kuzaliwa. Hata hivyo, baadhi ya watoto huchukua muda mrefu zaidi bila kuwa na tatizo mradi hakuna dalili za maambukizi. Kiwango cha unyevu, usafi na jinsi kitovu kinavyolindwa dhidi ya msuguano vinaathiri kasi ya kudondoka kwake.

3. Je, nifanye nini kuhakikisha kitovu cha mtoto kinadondoka haraka na salama?

Njia salama zaidi ni kuhakikisha kitovu kinabakia kikavu, kisafi, na kisiguswe mara kwa mara. Tumia kitambaa au taulo ya mtoto iliyookamuliwa maji yote kumfuta mtoto badala ya kumwagia maji. Pampasi iachwe chini ya kitovu ili kuepuka unyevu na msuguano. Epuka kupaka mafuta, dawa za kienyeji au vitu vyovyote visivyoelekezwa na mtaalamu wa afya.

4. Je, ni kawaida kitovu kutoa harufu au kubadilika rangi?

Ndiyo, ni kawaida kitovu kutoa harufu isiyo kali na kubadilika rangi kuwa kijivu, kahawia au nyeusi huku kikikauka. Harufu kali, usaha, au maji yenye rangi isiyo ya kawaida ndiyo dalili zinazoweza kuashiria maambukizi na zinahitaji kuwasiliana na mtaalamu wa afya.

5. Je, endapo kitovu cha mtoto kimechelewa kukatika nifanyaje?

Kama kitovu hakijadondoka ndani ya wiki 3, ni vyema kumpeleka mtoto kufanyiwa tathmini ya afya. Kuchelewa huku kunaweza kusababishwa na unyevu wa mara kwa mara, msuguano, au kwa nadra sana kuashiria tatizo la kiafya linalohitaji uangalizi. Usijaribu kukivuta wala kukikata. Mtaalamu wa afya ataangalia kama kuna dalili za maambukizi au nyama laini ( granuloma ya kitovu) ambayo inaweza kuhitaji matibabu maalumu.

6. Je, ninawezaje kutambua kama kitovu cha mtoto kimepata maambukizi?

Dalili za maambukizi zinaweza kujumuisha:

  • Ngozi kuzunguka kitovu kuwa nyekundu, yenye joto au kuvimba

  • Kutoka kwa usaha, harufu kali isiyo ya kawaida

  • Mtoto kulia kila unapogusa kitovu

  • Kutoka damu isiyoisha

  • Homa au mtoto kuonekana dhaifu

Ukiona dalili hizi, muone mtaalamu wa afya mara moja.

7. Je, ni salama kumwogesha mtoto kabla kitovu hakijadondoka?

Ndiyo, ni salama kumwogesha mtoto mradi maji hayagusi kitovu mara kwa mara. Wataalamu wengi hupendekeza kutumia kitambaa kumfuta kwa siku za mwanzo ili kuzuia kitovu kulowana. Kama utahitaji kumwogesha kwa maji, hakikisha eneo la kitovu linakaushwa vizuri bila kuweka msuguano.

8. Je, baada ya kitovu kudondoka ni kawaida kuona damu au majimaji?

Ndiyo, baada ya kitovu kudondoka unaweza kuona tone dogo la damu au majimaji meupe ndani ya siku chache. Hii ni sehemu ya kupona kwa jeraha. Hata hivyo, kama damu inatoka kwa wingi, majimaji yanatoka kwa wingi au kuna harufu kali, muone mtaalamu wa afya.

9. Kwa nini kitovu cha mtoto kinaweza kuwa na nyama nyeupe au nyekundu baada ya kudondoka?

Mwonekano wa nyama ndogo laini nyekundu (granuloma ya kitovu) unaweza kutokea kwa baadhi ya watoto baada ya kitovu kudondoka. Hii si hatari mara nyingi, lakini inaweza kuhitaji matibabu ya kliniki ili kusaidia eneo hilo kupona haraka. Usijaribu kutibu nyumbani bila maelekezo ya mhudumu wa afya.

10. Je, umbile la kitovu cha mtoto linaweza kusababisha kitovu kutoka nje (ngiri ya kitovuni)?

Ndiyo, baadhi ya watoto hupata kitovu kinachojitokeza nje wanapolia au wanapokaz tumbo, hali inayojulikana kama ngiri ya kitovu. Mara nyingi hali hii si hatari na hujifunga yenyewe kadri mtoto anavyokua. Hata hivyo, kama kitovu kinakuwa kigumu, chenye rangi isiyo ya kawaida au mtoto anaonekana kuwa na maumivu, pata ushauri wa kitaalamu haraka.


Elimu inayotolewa hapa ni kwa ajili ya ushauri tu na hivyo ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma makala hii.

Kwa ushauri zaidi na tiba, wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kupitia mawasiliano yetu

Imeandikwa,

3 Machi 2026, 08:27:56

Rejea za mada hii

  1. World Health Organization. WHO recommendations on postnatal care of the mother and newborn. Geneva: World Health Organization; 2014. Available from: https://www.who.int/publications/i/item/9789241506649

  2. World Health Organization. Care of the umbilical cord: a review of the evidence. Geneva: WHO; 2010. Available from: https://apps.who.int/iris/handle/10665/69567

  3. Centers for Disease Control and Prevention (CDC). Umbilical cord care for newborns. CDC; 2022. Available from: https://www.cdc.gov

  4. United Nations Children’s Fund (UNICEF). Newborn care guidelines. UNICEF; 2021. Available from: https://www.unicef.org

  5. Mullany LC. Neonatal umbilical cord care practices in low-income countries: a review of the evidence. Trop Med Int Health. 2006;11(6):819-26.

  6. Imdad A, Bautista R, Senen KA, Uy ME, Mantaring JB, Bhutta ZA. Umbilical cord antiseptics for preventing sepsis and death among newborns. Cochrane Database Syst Rev. 2013;2013(5):CD008635.

  7. Sankar MJ, Chandrasekaran A, Ravindranath A, Agarwal R, Paul VK. Umbilical cord cleansing with chlorhexidine in neonates: a systematic review. J Perinatol. 2016;36(S1):S12-20.

  8. Pezzati M, Biagioli E, Martelli E, Gambi B, Rubaltelli FF. Umbilical cord care: the effect of eight different cord-care regimens on the time to cord separation. Pediatrics. 2002;110(2):e32.

  9. Zupan J, Garner P. Topical umbilical cord care at birth. Cochrane Database Syst Rev. 2001;(2):CD001057.

  10. Kaplan HC, Lannon C, Walsh MC. Newborn care: normal newborn care and care of the umbilical cord. In: Manual of neonatal care. 7th ed. Philadelphia: Lippincott Williams & Wilkins; 2012.

bottom of page