Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Peter A, MD
8 Novemba 2021
Lishe ya mtoto
Wazazi wengi wanaweza kuandaa lishe ya watoto, lakini changamoto iliyopo ni kwamba hawajui wanatakiwa wawe na vitu gani vya msingi na kwa kiasi gani mchanganyiko unaotakiwa uwe.
Endapo wazazi/walezi wanaweza kuandaa lishe ya mtoto vema basi mtoto atakuwa vema kiakili na kimwili
Kwanini uwe na mchanganyiko mzuri wa chakula?
Kwanza kabisa na ijulikane kwamba mtoto hukua haraka zaidi kuliko mtu mzima, hivyo anahitaji aina fulani ya vyakula ili apate kukua vema, mtoto mdogo anahitaji ale mara kwa mara ili akue haraka. Mtoto mchanga anapozaliwa anatakiwa kunyonya maziwa ya mama tu katika kipindi chote cha miezi sita. Usimpe mtoto vyakula vingine ikiwa pamoja na maji.
Ni kwanini ufanye hivyo?
Maziwa ya mama huwa yanatosha kabisa kwa mtoto,
Yana kinga za mwili kutoka kwa mama hivyo hujenga kinga ya mwili ya mtoto dhidi ya maradhikama kuharisha n.k
Maziwa ya mama pia yapo safi na tayari kutumika mda wowote ule
Maziwa ya mama yana vitamini, na viinirishi vingi vinavyomtosha mtoto na kumsaidia akue vema
Mtoto aliye chini ya miezi sita atatakiwa kunywa maziwa ya mama kwa afya bora na kuepuka magonjwa ya kuharisha na mengine ya mfumo wa tumbo
Ni makundi gani ya vyakula yanayotakiwa?
Yapo makundi mbalimbali ya vyakula vinavyohitajika katika kuandaa lishe ya mtoto, makundi hayo ni ;
Protini
Wanga
Mafuta
Pia mtoto anatakiwa kupata maji, vitamini na madini.
Nafaka/Vyakula venye wanga kwa wingi ni kama hivi vifuatavyo;
Mchele
Mtama
Uwele
Ngano
Vyakula/nafaka zenye protini kwa wingi ni kama vile;
Soya
Mchele wa brauni
Choroko
Mbaazi
Kunde
Dagaa
Vyakula/nafaka zenye mafuta kwa wingi ni kama vile;
Karanga
Blue band
Siagi
Ufuta
Alizeti
Jinsi gani ya kuchanganya lishe ya mtoto?
Jambo la msingi linalotakiwa kufanyika kwa ajili ya kuandaa lishe ya mtoto ni;
Mtoto anatakiwa apate protini kwa wingi maana huhitajika kujenga mwili yaani misuli mifupa, chembe hai za mwili, kinga ya mwili, nywele ubongo, mishipa ya fahamu n.k
Kiasi cha wanga kinahitajika lakini ni kwa kiasi kidogo, wanga huu hutoa (nishati) nguvu katika mwili (wanga hubadilishwa kwenda kuwa glucose ambayo hutumiwa na chembe hai za mwili kuzalisha nguvu), mtoto anapolia, anapokula, anapocheza na anapoongea hutumiwa nguvu hivyo ni lazima apate mchanganyiko wa wanga katika chakula anachopata
Mafuata huhitajika pia kwa kiasi, kazi ya mafuta ni kutunza joto mwilini
Umri wa miezi 0 hadi miezi 6
Kiasi cha maji ni mililita 700 kwa kila siku
Kiasi cha wanga ni gramu 60 kwa kila siku
Kiasi cha mafuta ni gramu 31 kwa siku
Kiasi cha protini ni gramu 9.1 kwa kila siku
Kumbuka mtoto wa mwezi 0 hadi miezi 6 ananyonya maziwa ya mama tu na huwa na kiasi cha kutosha kama kilivyoainishwa hapo juu
Mtoto mwenye umri wa miezi 7 hadi mwaka 1 anahitaji chakula kiasi hiki kwa siku
Maji mililita 800 kwa siku
Wanga gramu 95 kwa siku ( asilimia 70 ya chakula)
Mafuta gramu 30 kwa siku ( asilimia 22 ya chakula)
Protini gramu 11 kwa siku ( asilimia 8 ya chakula )
Yaani kwa maana nyingine ukiwa unaandaa chakula/lishe bora ya mtoto mdogo hakikisha asilimia 70 ya mchanganyiko inakuwa wanga, 22 inakuwa mafuta na asilimia 8 inakuwa chakula cha protini. Maji yatahitajika kwa kiasi kilekile unachotumia kuandaa chakula cha mtoto.
Jinsi gani ya kupata mchanganyo sahihi kutoka kwenye mahesabu hayo;
Ili kupata mchanganyiko sahihi, unapokuwa unaandaa lishe ni vema kufahamu unataka kuandaa kiasi gani cha lishe. Mfano unataka kuandaa kilo tano (5kg) za unga wa lishe kwa madhumuni ya kutumika kwa muda wa wiki mbili. Fuata mahesabu haya kwa mtoto aliye na umri wa mwaka mmoja na kuendelea;
Kiasi cha wanga kinatakiwa kuwa asilimia 70 ya jumla ya kilo zote yaani;
5kg× (70/100)= 3.5kg)
Kiasi cha mafuta kinatakiwa kuwa asilimia 22 ya jumla ya kilo zote yaani;
5kg × (22/100) = 1.1kg
Kiasi cha protini kinatakiwa kuwa asilimia 8 ya jumla ya kilo zote yaani;
5kg × (8/100) = gramu 400
Kumbuka
Watoto wanatakiwa kula mara kwa mara, mtoto mchanga anyonye mara nane au zaidi kwa siku(jumla ya usiku na mchana) na mtoto mkubwa ale milo isiyopungua 8 ya kiafya kwa siku(mchana na usiku)
Mfano mtoto wa miezi saba anaweza kunyonya mara 4 kwa siku na kunywa uji mara nne kwa siku kwa kiasi kinachomtosha
Mtoto anatakiwa kunyonya chuchu moja kwa muda usiopungua dakika 20 kabla ya kuhamishiwa chuchu nyingine
Bonyeza hapa kusoma kuhusu milo ya kiafya kwa watu wazima
Bonyeza hapa kusoma kuhusu namna ya kufanya mtoto ale zaidi
Elimu inayotolewa hapa ni kwa ajili ya ushauri tu na hivyo ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma makala hii.
Kwa ushauri zaidi na tiba, wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kupitia mawasiliano yetu
Imeboreshwa,
9 Novemba 2021 07:19:01
Rejea za mada hii:
Child nutrition. https://www.child-encyclopedia.com/child-nutrition. Imechukuliwa 09.11.2021