Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
ULY CLINIC
3 Julai 2025
Mlo bora kwa mtoto wa miezi 6: Mwanzo wa lishe ya nyongeza
Mtoto anapofikisha miezi 6, anahitaji kuanza kupata chakula cha nyongeza sambamba na kuendelea kunyonya. Makala hii inaeleza mlo unaofaa kwa mtoto wa miezi 6 kwa ajili ya ukuaji mzuri na kinga bora ya mwili, kwa kutumia vyakula rahisi vinavyopatikana Tanzania.
Umuhimu wa Lishe ya Nyongeza kwa Miezi 6
Watoto huzaliwa na akiba ya virutubisho kutoka kwa mama, lakini ifikapo miezi 6, mahitaji ya nishati, protini, madini (kama chuma) na vitamini huongezeka. Hivyo, kuanzia umri huu, mtoto anapaswa kuendelea kunyonya na pia kupewa chakula cha nyongeza.
Malengo ya lishe ya miezi 6
Kuanza kumzoesha mtoto ladha na muundo wa vyakula
Kutoa virutubisho vinavyoongezea yale ya maziwa ya mama
Kuimarisha ukuaji wa viungo na kinga ya mwili
Kuendelea na maziwa ya mama
Mtoto aendelee kunyonya angalau mara 6 kwa siku. Maziwa ya mama bado ni chanzo kikuu cha nishati, protini, maji, vitamini na kinga.
Jinsi ya kuanza lishe ya nyongeza
Anza na uaji mwepesi (uji wa nafaka moja mfano mchele au mahindi)
Kiasi kidogo: kijiko 1–2, mara moja au mbili kwa siku
Ongeza aina na kiasi polepole (introduce one new food at a time)
Uji uwe usio na sukari wala chumvi
Mlo wote upondwe au usagwe hadi laini kama uji mzito
Vyakula vinavyofaa kwa miezi 6
Kundi | Mfano wa Chakula |
Wanga | Uji wa mchele, mtama, mahindi |
Protini | Maharage yaliyopondwa vizuri, dagaa wachache waliopondwa |
Mafuta Bora | Mafuta ya alizeti, nazi, siagi ya karanga (kiasi kidogo sana) |
Matunda | Papai, embe, parachichi, ndizi mbivu zilizopondwa |
Mboga | Mchicha, matembele au kisamvu zilizochemshwa na kusagwa |
Ratiba ya mlo wa mtoto wa miezi 6 (Mfano wa wiki)
Siku | Asubuhi (7–8am) | Mchana (12–1pm) | Jioni (5–6pm) |
Jumatatu | Uji wa mchele | Papai lililopondwa | Uji wa mtama |
Jumanne | Uji wa mahindi + mafuta ya nazi | Ndizi mbivu iliyopondwa | Uji wa mchanganyiko wa nafaka |
Jumatano | Uji wa dona | Parachichi | Uji wa mtama + siagi ya karanga |
Alhamisi | Uji wa lishe | Maharage yaliyopondwa | Uji wa mchele |
Ijumaa | Uji wa ulezi | Papai au embe | Uji wa mchanganyiko wa nafaka |
Jumamosi | Uji wa mahindi | Ndizi mbivu | Uji wa mtama + nazi |
Jumapili | Uji wa lishe | Mboga ya mchicha iliyopondwa | Uji wa mchele |
Tahadhari muhimu kwa miezi 6
Epuka chumvi, sukari na viungo vya chakula
Epuka asali hadi mtoto atimize miezi 12 (inaweza kuwa na sumu ya botulism)
Usilazimishe kula – kuwa mvumilivu, mlishe mtoto taratibu
Kila chakula kiwe laini sana – kama uji mzito au puree
Angalia dalili za mzio unapompa chakula kipya
Hitimisho
Mtoto wa miezi 6 yuko katika hatua ya mpito muhimu kutoka kwenye maziwa pekee kwenda kwenye vyakula vya kawaida. Kwa kutumia vyakula rahisi, salama na vyenye virutubisho sahihi, unaweza kuimarisha ukuaji wa mtoto na kumkinga dhidi ya utapiamlo.
Elimu inayotolewa hapa ni kwa ajili ya ushauri tu na hivyo ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma makala hii.
Kwa ushauri zaidi na tiba, wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kupitia mawasiliano yetu
Imeboreshwa,
3 Julai 2025, 09:18:48
Rejea za mada hii:
WHO. Infant and young child feeding: Model Chapter for textbooks. Geneva: WHO; 2009.
TFNC. Lishe kwa watoto wadogo: Mwongozo kwa wazazi na walezi. Dar es Salaam: Tanzania Food and Nutrition Centre; 2018.
Ministry of Health. National Guidelines on Infant and Young Child Feeding. 2nd ed. Dar es Salaam: MoHCDGEC; 2019.
PAHO, WHO. Guiding Principles for Complementary Feeding. Washington, DC: 2003.
Dewey KG, Adu-Afarwuah S. Matern Child Nutr. 2008;4 Suppl 1:24–85.
UNICEF. Programming Guide: Infant and Young Child Feeding. New York: UNICEF; 2011.
USAID Advancing Nutrition. Essential Nutrition Actions Framework. Washington, DC: 2021.
