top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

9 Novemba 2021

Mtoto na chakula

Unawezaje kumfanya mtoto apende kula zaidi?

Makala hii imeandikwa kwa lengo la kumsadia mzazi au mlezi anayelea mtoto asiyependa kula, kuchagua chakula na hata wale wanaopenda kula . Baada ya kusoma makala hii utapata mbinu mbalimbali za kumfanya mtoto ale chakula kiafya. Maelezo ya ziada kuhusu chakula kizuri kwa mtoto na namna gani ya kuandaa lishe ya mtoto utayapata sehemu nyingine kwenye tovuti hii.


Mambo ya kumfanyia mtoto ili apende kula zaidi

Ili mwanao ale vema fanya au zingatia mambo yafuatayo;

Heshimu hamu yake ya kula

Kama hana njaa, usimlazimishe kula chakula au kitu chochote kile cha kutafuna. Vivyo hivyo usimlazimishe kumaliza chakula chote ulichomuwekea ili asijejilazimisha kisha kutapika. Kumlazimisha mtoto kula kutaamsha hofu ambayo hupelekea tumbo kupata hisia za kujaa na hivyo ashindwe kula kabisa.

Mwekee au mpe chakula kiasi kidogo

Kufanya hivi kutamfanya aone chakula kuwa kidogo ambacho anaweza kula na kukimaliza. Endapo hajashiba au atataka kingine muongezee ili ale.

Tengeneza na fuata utaratibu wa kula

Kula au mpe chakula muda na wakali ule ule kila siku. Unaweza kumpa maziwa ama juisi ya matunda pamoja na chakula.


Kati ya mlo mmoja na mwingine mpe maji na vitafunwa vingine ambavyo umeviandaa. Kama mtoto akinywa maji na juisi siku nzima, hii itafanya hamu ya kula pia iishe

Uwe mvumilifu wa chakula kigeni

Watoto wadogo mara nyigi hushika na kunusa chakula kigeni au kuweza kuweka kiasi kidogo mdomoni kisha kutema. Utahitaji muonyesha chakula hicho ili akizoee na kuanza kula siku zijazo.

Mpe hamasa mwanao kwa kuzungumzia rangi ya chakula, umbo na harufu na radha nzuri ya chakula. Weka chakula kipya kila unapokuwa unampa chakula anachokipenda ili akizoee na hicho pia.

Mshawishi

Weka chakula kwenye sahani au chombo anachokipenda. Unaweza kukata kwa kisu ili kupata chakula chenye maumbo mbalimbali kwa ili kumvutia. Mpe chakula anavyokula asubuhi kama kifungua kinywa wakati wa usiku na hakikisha chakula kinakuwa na rangi ya kuvutia.

Muhusishe kwenye manunuzi ya chakula

Wakati wa kununua vitu vya kula au kupika, mpe nafasi ya kuchagua matunda, mboga za majani na vyakula vingine vyenye afya. Usinunue chakula chochote tu ambacho hutaki mwanao ale. Ukiwa nyumbani, mshawishi mwanao akusaidie kuosha mboga, kutwanga karanga,kuosha vyombo au kuandaa meza kwa ajili ya kutenga chakula. Kumuhusisha huku kutamfanya ashawishike kula kile alichokiandaa

Kuwa mfano wa kuigwa

Kama ukila unakula chakula chenye afya njema, mwanao pia atafuata tabia yako kw akula vyakula vya kiafya.

Kuwa mbunifu

Weka vipande vidogo vya matunda kwenye sahani ya chakula cha nafaka, au weka karoti kwenye supu nk. Fanya ubunifu mbalimbali kiasi kwamba mtoto akipende chakula.

Punguza uharibifu wa mawazo ya mtoto

Zima TV na vifaa vingine vya umeme ili akili ya mtoto iwe kwenye chakula kwa wakati huo wa kula. Kumbuka pia matangazo ya TV kuhusu chakula huweza kumfanya mtoto apende kula vitu vyenye sukari ama kutokula vyakula vyenye afya.

Usimpe kitindamlo kama zawadi

Kuendelea kumpa kitindamlo mwanao kuna mpa ujumbe kwamba kitindamlo ni chakula kizuri, hii inaweza mfanya apende vitu vitamu tu. Unaweza kuchagua siku moja au mbili kwa wiki wakati wa usiku kutumia vitindamlo na usimpe siku zingine za wiki au mzoeshe mwanao kwamba vitindamlo ni matunda, maziwa au vyakula vingine vyenye afya ili awe anavipenda na kula kila siku au mara kwa mara.

Fahamu pia

Kuandaa chakula kingine mara baada ya mtoto kukataa kile ulichoandaa awali huweza sababisha mwanao kuwa mbaguzi wa chakula. Mshawishi mwanao akae mezani kwa muda wote wa kula hata kama hali hicho chakula. Endelea kumpatia chakula chenye afya mpaka pale atakapotambua na kufahamu chaguo la chakula akipendacho.

Kama una wasiwasi kwamba kubagua chakula kunamdhuru afya na maendeleo yake ya ukuaji, onana na daktari wake. Daktari atachora chati ya uzito na maendeleo ya ukuaji wake. Kwa nyongeza weka rekodi ya aina na kiasi cha chakula anachokula kwa siku tatu zilizopita. Daktari atapata picha ya tabia yake ya kula na kukutoa wasiwasi.

Kwa sasa kumbuka kuwa, tabia ya ulaji wa mtoto haiwezi kubadilika ghafla tu, lakini hatua ndogo ndogo zinazochukuliwa kila siku huweza kusaidia mtoto awe na ulaji wa chakula bora kwa maisha yake yote.

Elimu inayotolewa hapa ni kwa ajili ya ushauri tu na hivyo ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma makala hii.

Kwa ushauri zaidi na tiba, wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kupitia mawasiliano yetu

Imeboreshwa,

9 Novemba 2021 12:27:01

Rejea za mada hii:

Rejea contents

bottom of page