top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Peter A, MD

9 Novemba 2021

Ukuaji wa kawaida wa mtoto

Makala hii imezungumzia kuhusu ukuaji wa kawaida wa watoto kuanzia kichanga hadi kufikia umri wa miaka 10. Watoto huzaliwa na uzito tofauti tofauti, kila mtoto anaweza kuwa na uzito wake wa tofauti na mwingine unaotegemea chakula anachokula mama na idadi ya mtoto kunyonya. Hata hivyo, kama mazingira yote ya kina mama na watoto yanafanana, watoto hao hukua katika kiwango sawa.

Ukuaji wa kawaida wa mtoto ukoje?


Hapa chini kuna maelezo ya namna mtoto anavyotakiwa kuongezeka uzito na urefu kwa mwaka wa kwanza wa maisha yake;


 • Mtoto hupoteza uzito wake kwa asilimia 5 hadi 10 wiki la kwanza baada ya kuzaliwa na baadae uzito huo aliopoteza hujirudia ndani ya wiki mbili

 • Mtoto kuanzia siku ya kwanza kuzaliwa hadi anapofikisha miezi sita, atakuwa kwa takribani sentimeta 1.5 hadi 2.5 kwa mwezi, na kuongezeka uzito wa gramu 140 hadi 200 kwa wiki. Mtoto anapofikisha umri wa miezi mitano atakuwa na uzito mara mbili ya ule aliozaliwa nao.

 • Kuanzia miezi sita na kuendele hadi mwaka 1. Mtoto huongezeka urefu wa sentimita 1 kila mwezi na uzito wa gramu 85 hadi 140 kwa wiki moja. Kwa ujumla mtoto huwa na uzito mara tatu zaidi ya kilo alizozaliwa nazo anapofikisha umri wa miezi 12 (mwaka 1)

 • Kati ya umri wa mwaka mmoja na miaka miwili mtoto atakuwa kilo 2.2 tu

 • Kuanzia miaka 2 hadi miaka mi 5 mtoto atakuwa kwa kilo 2.2 kila mwaka

 • Kati ya miaka 2 hadi 10 mtoto hukua taratibu sana, lakini huanza kukua haraka sana kuanzia miaka 10 na kuendelea, wakati mwingine huanza kukua haraka kuanzia miaka 9

 • Mtoto anapoingia miaka mitatu hadi kumi ataongezeka sentimita 6 kila mwaka

Kwa kawaida mtoto hupimwa urefu na uzito kila anapohudhuria kliniki, uzito na urefu huchorwa kwenye kadi ya mtoto ili kuangalia ukuaji wake. Ni vema mama akaangalia ukuaji wa mtoto wake na kufuata ushauri wa daktari endapo moto hakui vema.


Kwanini mtoto hakui?

Mambo yanayo pelekea mtoto asikue vema yanajumuisha yafuatayo; ​

 • Magonjwa ya kuzaliwa kama magonjwa ya moyo (tundukwenye moyo), mgongo wazi, mtindio wa ubongo n.k

 • Magonjwa ya kuambukiza- mfano Kuharisha, kutapika sana, homa, malaria, n.k

 • Kutonyonya maziwa kwa kiwango cha kutosha- Kwa kawaida mtoto anatakiwa kunyonya miezi sita mfululizo bila kuacha maziwa ya mama. Endapo mtoto ataanza kula vyakula kipindi hiki basi anaweza kupata magonjwa ya kuambukizwa kama kuharisha n.k

 • Kutopata chakula bora chenye virutubishi muhimu kwenye matano ya makundi ya chakula

Kumbuka
 • Mtoto hukua kiakili na kimwili, endapo mtoto hapati mlo kamili, basi atadumaa kiakili na kushindwa kujifunza darasani, kuelewa na kuwa na maisha yasiyo na mafanikio. Mlishe mtoto chakula bora na asilia chenye virutubishi vyote vya muhimu kutoka kwenye makundi matano ya chakula, na si bora chakula.

 • Mtoto anatakiwa kupewa vyakula vya aina tofauti ili aweze kuchagua kile kinachomfaa

 • Mtoto asipopewa chakula aina tofauti ataweza kupendelea chakula aina moja tu kwenye maisha yake

 • Mzazi unatakiwa kuonyesha mfano wa kula chakula bora ili mwanao aige kutoka kwako

Elimu inayotolewa hapa ni kwa ajili ya ushauri tu na hivyo ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma makala hii.

Kwa ushauri zaidi na tiba, wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kupitia mawasiliano yetu

Imeboreshwa,

9 Novemba 2021 07:19:04

Rejea za mada hii:

bottom of page