top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

ULY CLINIC

kirusi mumps-ulyclinic

Methyldopa ni dawa ya kupunguza shinikizo la damu la juu (presha) inayotumika hasa kwa wanawake wajawazito na wagonjwa wenye presha sugu. Ni miongoni mwa dawa salama zaidi za presha wakati wa ujauzito, na imekuwa ikitumika kwa miongo kadhaa katika tiba ya shinikizo la juu la damu kutokana na ujauzito na shinikizo la damu linaloelekea kifafa cha mimba isiyo kali.


Methyldopa ni ya kundi la dawa za presha za mfumo wa fahamu, yaani hufanya kazi kupitia mfumo wa fahamu (ubongo) ili kupunguza presha ya damu.


Majina mengine ya kibiashara

  • Aldomet

  • Dopegyt

  • Methyldopa BP

  • Alpha-methyldopa


Fomu na uzito wa Methyldopa

Methyldopa hupatikana katika fomu zifuatazo:

  • Tembe:

    • 250 mg

    • 500 mg

  • Sindano (IV):

    • Hutumika hospitalini kwa hali maalum (sio ya kawaida sana)


Methyldopa hutibu nini?

Methyldopa hutumika kutibu:

  • Presha ya damu

  • Presha ya damu ya ujauzito

  • Presha kwa mama mjamzito mwenye presha inayoelekea kifafa cha mimba isiyo kali

  • Presha sugu kwa wagonjwa wasiovumilia dawa nyingine

  • Presha kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo (kwa tahadhari)


Namna Methyldopa inavyofanya kazi

Methyldopa hufanya kazi kwa:

  • Kuingia kwenye ubongo na kubadilishwa kuwa alpha-methylnorepinephrine

  • Kemikali hii hupunguza msisimko wa neva unaosababisha mishipa ya damu kujikunja

  • Mishipa ya damu hulegea (kutanua mishipa ya damu)

  • Mapigo ya moyo hupungua taratibu

  • Presha ya damu hushuka bila kuathiri sana mtiririko wa damu kwa mtoto tumboni


Ndiyo sababu Methyldopa hupendekezwa sana kwa wajawazito.


Ufyonzwaji na utoaji wa dawa

  • Ufyonzwaji: Hufyonzwa vizuri kupitia mfumo wa chakula

  • Nusu maisha: Saa 1.5–2, lakini athari hudumu muda mrefu zaidi

  • Utoaji: Kupitia figo (mkojo) na sehemu ndogo kupitia ini


Mambo ya Kufahamu Kabla ya Kutumia Methyldopa

Mwambie daktari wako endapo una:

  • Ugonjwa wa ini (hasa hepataitis)

  • Historia ya upungufu wa damu kutokana na kuvunjwa kwa chembe nyekundu za damu

  • Unatumia dawa za presha nyingine

  • Unatumia dawa za kisaikolojia

  • Historia ya mzio wa Methyldopa


Methyldopa na ujauzito au unyonyeshaji


Ujauzito
  • Methyldopa ni salama sana wakati wa ujauzito

  • Ni dawa ya chaguo la kwanza (dawa daraja la kwanza kwa matumizi) kwa presha ya wajawazito

  • Haina madhara makubwa kwa mtoto tumboni kulingana na tafiti nyingi za muda mrefu


Unyonyeshaji
  • Methyldopa hupita kwa kiwango kidogo kwenye maziwa ya mama

  • Inachukuliwa kuwa salama kwa mama anayenyonyesha

  • Mtoto hafanyiwi madhara makubwa yanayojulikana


Maelekezo ya matumizi

  • Tumia dozi uliyoelekezwa na daktari (mara nyingi 250–500 mg mara 2–3 kwa siku)

  • Kunywa dawa kwa wakati uleule kila siku

  • Unaweza kunywa pamoja na chakula

  • Usikatishe dawa ghafla bila ushauri wa daktari


Madhara ya Methyldopa


Maudhi ya kawaida
  • Kusinzia au kuchoka sana

  • Kizunguzungu

  • Kinywa kukauka

  • Maumivu ya kichwa

  • Kupungua hamu ya tendo la ndoa


Madhara makubwa (nadra)
  • Kuvimba kwa ini

  • Upungufu wa damu kutokana na kuvunjwa kwa chembe nyekundu za damu

  • Homa isiyoelezeka

  • Ngozi au macho kuwa ya njano

  • Msongo wa mawazo (Sonona)


Mwingiliano na dawa nyingine

Dawa zinazoweza kuingiliana
  • Dawa nyingine za presha ya kupanda (zinaweza kushusha presha kupita kiasi)

  • Madini chuma ya nyongeza (hupunguza ufyonzwaji wa Methyldopa)

  • Lithium

  • Dawa za usingizi au msongo wa mawazo


Inashauriwa kunywa dawa nyongeza ya madini chuma baada ya masaa 2–3 tangu kutumia Methyldopa.


Nusu maisha ya Methyldopa

  • Nusu maisha ni takribani saa 1.5–2

  • Athari zake hudumu muda mrefu zaidi kutokana na kazi yake kwenye ubongo

  • Ndiyo maana hutolewa mara 2–3 kwa siku


Je ukisahau dozi ufanyaje?

  • Tumia mara unapokumbuka

  • Kama muda wa dozi inayofuata umekaribia, ruka dozi uliyosahau

  • Usitumie dozi mbili kwa wakati mmoja


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Je, Methyldopa ni salama kwa mama mjamzito kwa muda mrefu?

Ndiyo. Methyldopa imefanyiwa tafiti nyingi kwa wajawazito na imeonekana kuwa salama hata ikitumiwa kwa miezi yote ya ujauzito. Haina madhara makubwa kwa ukuaji wa mtoto tumboni na hutumika duniani kote kama dawa ya msingi kwa presha ya ujauzito.

2. Mwanamke mjamzito anayetumia Methyldopa anaruhusiwa kunywa maziwa fresh kama chai?

Ndiyo, anaruhusiwa kabisa. Maziwa fresh hayana madhara yoyote kwa Methyldopa. Hata hivyo:

  • Epuka kunywa Methyldopa na madini chuma yaliyopo kwenye maziwa kwa wakati mmoja

  • Kama unatumia vidonge vya kuongeza damu (madini chuma), panga muda tofauti

Maziwa hayapandishi presha wala hayapunguzi ufanisi wa Methyldopa.

3. Kwa nini Methyldopa hunisababisha usingizi mwingi?

Methyldopa hufanya kazi kupitia ubongo, hivyo hupunguza msisimko wa mfumo wa neva. Hii husababisha usingizi au kuchoka, hasa wiki za mwanzo. Dalili hii hupungua kadri mwili unavyozoea dawa.

4. Je, Methyldopa inaweza kusababisha presha kushuka sana?

Ndiyo, hasa kama:

  • Unatumia dozi kubwa

  • Unatumia dawa nyingine za presha

  • Hukuli chakula vizuri

Dalili ni pamoja na kizunguzungu, kuzirai, au kuona giza. Mwone daktari haraka.

5. Methyldopa inaweza kuathiri ini?

Ndiyo, lakini ni nadra. Baadhi ya watu hupata kuvimba kwa ini. Dalili ni:

  • Macho kuwa ya njano

  • Mkojo wa rangi ya chai

  • Uchovu uliokithiri

Vipimo vya ini hupendekezwa kwa matumizi ya muda mrefu.

6. Je, Methyldopa inasababisha mtoto tumboni kuwa na shida ya akili?

Hapana. Tafiti za muda mrefu zimeonyesha watoto waliotokana na mama waliotumia Methyldopa hawana tofauti ya maendeleo ya akili ukilinganisha na watoto wengine.

7. Je, ninaweza kuacha Methyldopa nikiona presha imeshuka?

Hapana. Kuacha ghafla kunaweza kusababisha presha kurudi juu kwa ghafla. Dawa hupunguzwa taratibu kwa ushauri wa daktari.

8. Methyldopa inaruhusiwa kwa mama anayenyonyesha?

Ndiyo. Dawa hupita kwa kiwango kidogo sana kwenye maziwa ya mama na haijathibitishwa kusababisha madhara kwa mtoto.

9. Je, Methyldopa husababisha kuongezeka uzito?

Kwa kawaida hapana. Lakini usingizi na uchovu vinaweza kupunguza shughuli za mwili na kuleta ongezeko dogo la uzito kwa baadhi ya watu.

10. Methyldopa ni bora kuliko Labetalol au Nifedipine?

Sio suala la ubora, bali hali ya mgonjwa.

  • Methyldopa: salama sana, athari polepole

  • Labetalol/Nifedipine: hufanya kazi haraka zaidi

Daktari huchagua kulingana na hali ya mama na mtoto.


17 Januari 2026, 15:31:06

Dawa Methyldopa

Imeboreshwa,

17 Januari 2026, 16:01:00

Dawa yoyote ni sumu, usitumie dawa pasipo ushauri wa daktari kuepuka madhara kwenye ogani mbalimbali kama figo na ini. Matumizi ya dawa pasipo ushauri wa daktari unaweza kusababisha madhara na usugu wa vimelea vya maradhi kwenye dawa.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baad aya kusoma makala hii.

Kupata ushauri zaidi na tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya Mawasiliano yetu au Pata tiba.

Rejea za mada hii:

  1. Brunton LL, Hilal-Dandan R, Knollmann BC. Goodman & Gilman's: The Pharmacological Basis of Therapeutics. 14th ed. New York: McGraw-Hill; 2023. Antihypertensive agents.

  2. Sweetman SC, editor. Martindale: The Complete Drug Reference. 40th ed. London: Pharmaceutical Press; 2020. Methyldopa.

  3. McEvoy GK, editor. AHFS Drug Information 2024. Bethesda (MD): ASHP; 2024. Methyldopa.

  4. World Health Organization. WHO recommendations for prevention and treatment of pre-eclampsia and eclampsia. Geneva: WHO; 2023.

  5. Drugs.com. Methyldopa [Internet]. 2024 [cited 2025 Jun 5].

  6. Micromedex (IBM Watson). Methyldopa Drug Monograph. 2024.

bottom of page