Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
Imeboreshwa:
20 Aprili 2025, 17:12:21

Dawa ya harufu mbaya kinywani
Swali la msingi
Ni dawa ipi ninayoweza kutumia kutoa harufu mbaya kutoka kooni . Alafu na hisi kama uvimbe hata kumeza kitu inakuwa vigumu.
Majibu
Pole sana kwa hali unayopitia. Dalili unazoeleza harufu mbaya kooni, hisia ya uvimbe, na ugumu wa kumeza zinaweza kusababishwa na mambo mbalimbali ambayo kila kimoja kina matibabu yake ya kipekee. Ni vema kuwasiliana na daktari afahamu shida yako kabla ya kutumia dawa yoyote. Vifuatavyto ni baadhi ya visababishi vya harufu mbaya ya kinywa;
Visababishi vya harufu mbaya mdomoni
Magonjwa ya kinywa
Maambukizi kwenye tezi tonses
Mara nyingi husababishwa na bakteria au virusi. Dalili ni pamoja na koo kuwasha, kuuma, kumeza kwa shida, na harufu mbaya mdomoni.
Mawe madogo kwenye tezi tonses
Huundwa na mabaki ya chakula, seli, na bakteria. Hutoa harufu mbaya na hisia ya kitu kiko nyuma ya koo.
Michomokinga kwenye koo
Husababishwa na maambukizi na huambatana na koo kuuma, kumeza kwa shida, na wakati mwingine homa.
Maambukizi ya fizi au meno
Maambukizi ya mdomoni huweza kuchangia harufu mbaya inayohisiwa kama inatoka kooni.
Kucheua tindikali
Tindikali ya tumbo inapopanda juu kwenye koo, husababisha harufu kama ya kuchoma au tindikali. Dalili nyingine: kiungulia, koo kuwaka moto, au kikohozi hasa usiku.
Sindromu ya Sjögren: Huu ni ugonjwa wa shambulio binafsi la kinga ambao unaweza kusababisha upungufu wa mate na kudhoofika kwa tishu za koo na kinywa, na kusababisha ugumu wakati wa kumeza na harufu mbaya.
Magonjwa ya mfumo wa mkojo na mengine: Hali kama vile kisukari, matatizo ya figo, na matatizo ya ini pia yanaweza kuathiri harufu ya kinywa na kumeza.
Maambukizi ya Helicobacter pylori
Bakteria huyu huishi kwenye ukuta wa tumbo na kusababisha vidonda vya tumbo. Anaweza pia kuhusishwa na harufu mbaya mdomoni kwa sababu ya mabadiliko ya bakteria na asidi tumboni.
Kutokuwa na usagaji chakula vizuri(kuvimbiwa)
Chakula kinapokaa tumboni kwa muda mrefu huweza kutoa gesi na harufu inayopanda juu mdomoni.
Kuvurugika kwa utumbo
Kubadilika kwa uwiano wa bakteria wazuri na wabaya tumboni kunaweza kuathiri harufu ya pumzi.
Njia za kubaini chanzo
Kipimo cha pumzi kwa H. pylori
Endoscopy kama una maumivu ya tumbo ya mara kwa mara au kichefuchefu
Uchunguzi wa daktari wa meno na wa kinywa na koo kama tatizo linaanzia mdomoni au kooni
Matibabu ya awali
Kabla ya kutumia dawa, ni vyema uonwe na daktari kwa uchunguzi kamili, lakini hizi ni baadhi ya tiba za kawaida:
Matibabu ya magonjwa ya kinywa
Dawa ya kupunguza maambukizi na uvimbe
Antibiotiki na dawa za maamuvu hutumika, hizi utahitaji kuandikiwa na daktari wako kulingana na kisababishi.
Dawa ya kusafisha koo na kuondoa harufu
Maji ya uvuguvugu ya kusukutua kinywa- Mara 3 kwa siku.
Kiosha kinywa chenye Chlorhexidine (kama Hexidine au Corsodyl) – Husafisha koo na kuondoa bakteria wa harufu.
Kisafisha kinywa jamii ya Lozenges (kama Strepsils au Dequadin) – Hutuliza koo na kuua vijidudu.
Matibabu ya magonjwa ya tumbo na mengineyo
Tibu magonjwa ya msingi ya tumbo kama vidonda vya tumbo kwa dawa kama omeprazole au antibiotics za H. pylori
Epuka vyakula vya tindikali, pilipili, kahawa, na soda kama una cheua tindikali
Safisha kunywa vema, pamoja na kupiga mswaki vema nyuma ya ulimi
Wakati gani wa kumwona daktari?
Unapaswa kumwona daktari ikiwa utaona dalili zifuatazo pamoja na harufu mbaya ya kinywa na ugumu wakati wa kumeza:
Dalili zinazoendelea: Ikiwa dalili za harufu mbaya ya kinywa na ugumu wakati wa kumeza zitaendelea kwa zaidi ya siku chache au kurudiarudia.
Maumivu makali: Ikiwa una maumivu makali kwenye koo, kifua, au tumbo ambayo hayapungui kwa kutumia dawa za maumivu za kawaida.
Ugumu wa kupumua: Ikiwa unapata shida ya kupumua au hisia ya kushindwa kupumua, hii inaweza kuwa dalili ya hali hatari zaidi.
Homa: Ikiwa unapata homa pamoja na dalili ya harufu mdomoni, hisia za uvimbe na ugumu wa kumeza, inaweza kuwa ni maambukizi ambayo yanahitaji matibabu ya daktari.
Mabadiliko ya sauti: Ikiwa sauti yako inakuwa ya unywevu au unapopoteza sauti kabisa.
Kupungua kwa uzito: Kupungua uzito bila sababu ya wazi au kukosa hamu ya kula kunaweza kuwa dalili ya tatizo kubwa la kiafya kama saratani au ugonjwa wa mfumo wa mwili.
Damu katika mate au kutapika: Hii inaweza kuwa dalili ya tatizo kubwa kama maambukizi, kidonda, au tatizo la mfumo wa mmeng'enyo.
Matatizo ya kumeza kwa muda mrefu: Ikiwa unahisi chakula kinakwama mara kwa mara au inakuwa vigumu kumeza, hii inaweza kuwa dalili ya tatizo kwenye umio la chakula au mfumo wa mmeng'enyo.
