Mwandishi:
Dkt. Sospeter M, MD
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
5 Juni 2022, 10:41:36
Dawa bisacodyl
Bisacodyl Dawa
Bisacodyl ni dawa kwenye kundi la dawa za kulegeza matumbo na kuongeza utoaji haja kubwa. Hutumika katika matibabu haja kubwa kwa shinda, haja ngumu na kusafisha utumbo mpana kwa muda
Majina mengine ya bisacodyl
Bisacodyl hufahamika kwa majina ya kibiashara kama:
Dulcolax
Correctol
BisacEvac
Bisacolax
Codulax
Alophen
Feen A Mint
Fleet Stimulant Laxative
Laxit
Modane
Uzito na fomu ya bisacodyl
Bisacodyl hupatikana kama kidonge chenye uzito wa miligramu 5.
Dawa kundi moja na Bisacodyl
Dawa zingine zilizo kundi moja na bisacodyl ni zile ambazo huwa kundi la vilegeza matumbo na viongeza utoaji wa haja ngumu kama vile:
Sodium Docusate
Co-danthrusate
Glycerol
Senna
Sodium picosulphate
Oxyphenisatin
Bisacodyl hutibu nini?:
Bisacodyl hutumika kutibu kwa muda hali magonjwa yafuatayo:
Kinyesi kigumu
Kinyesi kutoka kwa shida (konstipesheni)
Kusafisha utumbo mpana kabla ya kufanyiwa uchuguzi
Namna bisacodyl inavyofanya kazi
Bisacodyl hufanya kazi kwa kuibughudhi misuli laini ya mfumo wa chakula na hivyo kuongeza peristalisis na haswa kupitia madhara yake ya kuamsha mishipa ya fahamu ya parasimpathetiki. Pia huongeza kiasi cha maji ndani ya utumbo kwa kuingilia uwezo wa matumbo kuweka uwiano wa maji na madini.
Wasiopaswa kutumia bisacodyl
Bisacodyl haipaswi kutumika kwa wagonjwa wenye hali, dalili na magonjwa yafuatayo:
Historia ya mzio wa dawa hii
Kuziba kwa matumbo
Hali kali ya kuziba kwa utumbo kutokana na kinyesi
Dalili za maambukizi kwenye kidole tumbo
Kutapika
Kutokwa damu kwenye puru
Tahadhari za kuchukuliwa kwa watumiaji wa bisacodyl
Usitumie kwa muda mrefu inaweza kusababisha mwili wako ukawa tegemezi kwenye dawa
Kama una harisha na kutapika, usitumie dawa hii
Usitafune kidonge, meza kwa maji
Usitumie saa 1 baada ya kunywa dawa za kupunguza uzalishaji wa tindikali
Haipaswi kutumika kwa watoto chini ya miaka 6
Haipaswi kutumika zaidi ya wiki 1
Baadhi ya fomu ya dawa hutiwa benzyl alcohol ambayo imeonekana kuambatana na usumu kwa vichanga. Usitumie dawa yenye kemikali hii au mazao yake kwa vichanga.
Matumizi ya bisacodyl na pombe
Unaweza kutumia bisacodyl na pombe, hata hivyo usitumie pombe nyingi pamoja na dawa hii.
Ufyonzwaji wa bisacodyl
Asilimia 16 tu ya dawa hufyonzwa na kuingia kwenye damu
Muda kuanza kazi - bisacodyl
Mara baada ya kutumia bisacodyl, huanza kufanya kazi baada ya masaa 6 hadi 10.
Nusu maisha ya bisacodyl
Bisacodyl huwa na nusu maisha ya masaa 8
Utoaji wa bisacodyl mwilini
Bisacodyl kwa kiasi kikubwa hutolewa mwilini upitia haja kubwa
Matumizi ya bisacodyl kwa mama mjamzito
Kiasi kidogo cha dawa huingia kwenye damu, matumizi ya muda mfupi yanachukuliwa kuwa salama. Epuka matumizi ya muda mrefu ya bisacodyl wakati huu.
Matumizi ya bisacodyl kwa mama anayenyonyesha
Hakuna kiwango cha dawa kilichogunduliwa kwenye maziwa ya mama anayenyonyesha. Kama itatumika wakati huu, inapaswa kutumika kwa tahadhari.
Dawa zenye mwingiliano mkali na bisacodyl
Dawa zifuatazo huwa na mwingiliano mkali hivyo hazipaswi kutumika pamoja na bisacodyl:
Sodium sulfate/magnesium sulfate/potassium chloride
Sodium sulfate/potassium sulfate/magnesium sulfate
Sodium sulfate/potassium sulfate/magnesium sulfate/polyethylene glycol
Dawa zenye mwingiliano wa wastani na bisacodyl
Dawa zifuatazo huwa na mwingiliano wa wastani na bisacodyl, kama zitatumika pamoja, mgonjwa anapaswa kuwa chini ya uchunguzi wa karibu wa mtaalamu wa afya:
Deflazacort
Dichlorphenamide
Potassium citrate
Dawa zenye mwingiliano mdogo na bisacodyl
Dawa zifuatazo huwa na mwingiliano mdogo na bisacodyl
Potassium acid phosphate
Potassium chloride
Maudhi ya bisacodyl
Baadhi ya maudhi ya bisacodyl ni:
Kunyonga kwa tumbo
Kupotea kwa uwiano wa madini na maji mwilini
Kuhara sana
Kichefuchefu
Hisia za kuungua kwenye puru
Kuona vitu vinazunguka
Kutapika
Je endapo umesahau kutumia dozi ya bisacody ufanyaje ?
Kama umesahau kutumia dozi ya bisacodyl, tumia mara utakapokumbuka isipokuwa endapo muda wa kunywa dozi nyingine umefika ambapo utapaswa kusubiria muda ufike ndipo utumie dozi hiyo na kuendelea kama ulivyoshauriwa na daktari wako. Usitumie dozi mbili kwa wakati mmoja.
Uhifadhi ya bisacodyl
Hifadhi dawa yako katika joto la mzingira (nyuzi joto za sentigrade 20 hadi 30). Usiweke kwenye friji au sehemu yenye mwanga wa jua au joto ili kuepuka kuharibu dawa.
ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
20 Septemba 2023, 18:36:19
Rejea za mada hii:-