top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

Dkt. Sospeter M, MD

Dkt. Lugonda B, MD

7 Septemba 2026, 12:21:26

Dawa Gynazole

Dawa Gynazole

Gynazole: Matumizi, namna inavyofanya kazi na tahadhari

Gynazole-1 ni dawa ya kuua fangasi inayotumika kutibu maambukizi ya fangasi kwenye uke, hasa maambukizi yanayosababishwa na aina za fangasi wanaojulikana kama Kandida. Kiambata hai katika Gynazole-1 ni butoconazole nitrate 2%, ambayo ni dawa ya kundi la dawa za fangasi jamii ya azole.


Dawa hii hutumika kwa kuwekwa ndani ya uke, na si dawa ya kunywa. Kwa baadhi ya wanawake inaweza kusaidia kupunguza dalili kama kuwashwa, kuungua, maumivu na uchafu mzito wa ukeni unaoweza kuambatana na maambukizi ya Kandida.


Hata hivyo, si kila uchafu, kuwashwa au harufu mbaya ukeni husababishwa na fangasi. Maambukizi mengine kama vajinosisi ya bakteria, trikomoniasisi na baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kusababisha dalili zinazofanana. Kwa hiyo, matumizi ya dawa ya fangasi bila kutambua chanzo yanaweza kuchelewesha matibabu sahihi.


Gynazole ina nini?

Gynazole-1 ina butoconazole nitrate 2% kama kiambata hai. Ni dawa ya kundi la imidazole yenye uwezo wa kuzuia ukuaji wa fangasi. Bidhaa ya Gynazole-1 hutengenezwa kama cream maalumu ya kuwekwa ndani ya uke.


Jina Gynazole-1 ni jina la biashara, wakati butoconazole ndilo jina la dawa inayofanya kazi. Majina ya biashara yanaweza kutofautiana kulingana na nchi na mtengenezaji. Kwa hiyo, unapoulizia dawa hii, ni muhimu kuangalia kiambata hai kilichoandikwa kwenye kifurushi.


Gynazole hutibu hali gani?


1. Maambukizi ya fangasi ukeni

Matumizi makuu ya Gynazole-1 ni kutibu fangsi wa vulva na ukeni jamii ya Kandida, yaani maambukizi ya Kandida kwenye uke na sehemu za nje za uke.


Maambukizi haya yanaweza kusababisha:

  • Kuwashwa ukeni au sehemu za nje za uke

  • Kuungua ukeni

  • Uwekundu au kuvimba kwa sehemu za nje za uke

  • Maumivu wakati wa tendo la ndoa

  • Maumivu au kuungua wakati wa kukojoa

  • Uchafu mzito mweupe unaoweza kufanana na jibini laini


Hata hivyo, dalili hizi si maalumu kwa Kandida pekee. Uchunguzi wa kitabibu unaweza kuhitajika ili kuthibitisha chanzo cha dalili.


2. Maambukizi ya Kandida yasiyo magumu

Butoconazole ni mojawapo ya dawa za azole zinazotumika kutibu maambukizi yasiyo magumu ya Kandida ukeni. Miongozo inatambua krimu ya butoconazole 2% kama mojawapo ya tiba za ndani ya uke kwa fangasi wa vula na ukeni jamii ya kandida.


Hata hivyo, wanawake wenye maambukizi yanayorudia mara kwa mara, maambukizi makali, kisukari kisichodhibitiwa, au hali zinazopunguza kinga wanaweza kuhitaji uchunguzi na mpango tofauti wa matibabu.


Gynazole inavyofanya kazi

Butoconazole ni dawa ya kundi la azole. Hufanya kazi kwa kuzuia utengenezaji wa ergosterol, sehemu muhimu ya utando wa seli ya fangasi.


Kwa kuathiri utando huo, dawa huzuia ukuaji na uhai wa fangasi wa Kandida.

Kwa hiyo, Gynazole haiui bakteria wanaosababisha bacterial vaginosis na si dawa ya kutibu magonjwa yote yanayosababisha uchafu au kuwashwa ukeni.


Jinsi ya kutumia Gynazole

Gynazole-1 hutumika ndani ya uke kwa kutumia kifaa maalumu kinachokuja pamoja na bidhaa.

Kwa bidhaa ya Gynazole-1 yenye butoconazole nitrate 2%, matumizi yaliyowekwa kwenye lebo ya dawa ni gramu 5 za krimu ndani ya uke mara moja.


Ni muhimu kufuata maelekezo ya bidhaa uliyonayo kwa sababu aina nyingine za butoconazole zinaweza kuwa na mpangilio tofauti wa matumizi. Miongozo pia hutofautisha krimu ya butoconazole 2% ya dozi moja yenye uwezo wa kubaki kwenye uke na baadhi ya bidhaa nyingine za butoconazole.


Usitumie kiasi kikubwa kuliko kilichoelekezwa kwa kudhani kitaponya fangasi haraka zaidi.


Je, Gynazole inaweza kutumika wakati wa hedhi?

Kwa kawaida, dawa za kuweka ukeni zinaweza kuwa na ufanisi mdogo au kuwa ngumu kutumia wakati wa kutokwa damu nyingi kwa sababu dawa inaweza kutoka pamoja na majimaji ya hedhi.


Ikiwa umeanza hedhi karibu na muda wa kutumia dawa, fuata maelekezo ya bidhaa au muulize mtaalamu wa afya kama ni bora kusubiri hadi hedhi ipungue.


Usiongeze dozi mwenyewe kwa sababu dawa inaweza kutoka nje ya uke na ukadhani haikufanya kazi.


Je, Gynazole inaweza kutumika wakati wa ujauzito?

Tahadhari ni muhimu wakati wa ujauzito. Lebo ya Gynazole-1 inaeleza kwamba usalama na ufanisi wa bidhaa hii kwa wanawake wajawazito haujaanzishwa.


Kwa hiyo, mwanamke mjamzito hapaswi kuanza kutumia Gynazole bila ushauri wa mtaalamu wa afya.

Kwa ujumla, maambukizi ya Kandida wakati wa ujauzito yanahitaji kuchaguliwa kwa uangalifu kwa sababu baadhi ya dawa za kutibu Kandida hazitumiki kwa namna ileile wakati wa ujauzito.


Je, Gynazole inaweza kutumika wakati wa kunyonyesha?

Mwanamke anayenyonyesha anapaswa kumjulisha daktari au mfamasia kabla ya kutumia Gynazole.

Uamuzi unaweza kutegemea aina ya dawa, kiasi kinachotumiwa, sababu ya matibabu na hali ya mama na mtoto.


Usitumie dawa ya uke mara kwa mara bila ushauri ikiwa maambukizi yanaendelea au kurudia.


Madhara ya Gynazole

Baadhi ya wanawake wanaweza kupata madhara baada ya kutumia Gynazole.

Madhara yanaweza kujumuisha:

  • Kuwashwa ukeni

  • Kuungua

  • Maumivu au usumbufu ukeni

  • Maumivu ya tumbo au nyonga kwa baadhi ya watumiaji

  • Uwekundu au muwasho kwenye eneo la uke


Dawa za kuua fangasi zinazowekwa ndani ya uke kwa kawaida husababisha madhara machache ya mwili mzima kwa sababu sehemu kubwa ya dawa hufanya kazi eneo lililowekwa. Hata hivyo, madhara ya eneo husika yanaweza kutokea.


Ikiwa dalili zinazidi kuwa kali baada ya kutumia dawa, ni muhimu kuwasiliana na mtoa huduma wa afya.


Gynazole na kondomu

Hili ni tahadhari muhimu. Krimu ya Gynazole inaweza kuwa na msingi wa mafuta ambao unaweza kudhoofisha kondomu za lateksi na kiwambo, hivyo kupunguza uwezo wao wa kuzuia mimba au maambukizi ya magonjwa ya zinaa.


Kwa hiyo, usidhani kwamba kutumia Gynazole pamoja na kondomu ya latex ni salama bila kuangalia maelekezo ya bidhaa.


Angalia maelekezo kwenye kifurushi kuhusu muda ambao unapaswa kusubiri kabla ya kutegemea kondomu ya latex au diaphragm baada ya kutumia dawa.


Je, Gynazole ni dawa ya magonjwa ya zinaa?

Gynazole hutibu maambukizi ya fangasi ya Kandida, lakini si dawa ya kutibu magonjwa mengi ya zinaa kama:

  • Kisonono

  • Klamidia

  • Trikoomoniasis.

  • Kaswende.

  • Herpes ya sehemu wa siri.


Kwa mfano, trichomoniasis inaweza kusababisha uchafu ukeni na kuwashwa, lakini inahitaji dawa tofauti.

Kwa hiyo, kuwa na uchafu ukeni hakumaanishi moja kwa moja kwamba una fangasi.


Je, mwenza wa tendo la ndoa anahitaji matibabu?

Kwa maambukizi ya kawaida ya Kandida ukeni, matibabu ya mwenza wa kiume kwa kawaida hayahitajiki ikiwa hana dalili.


Hata hivyo, mwanaume anaweza kupata uvimbe wa kichwa cha uume, kuwashwa au uwekundu unaohusiana na Kandida. Mtu mwenye dalili anapaswa kuchunguzwa na kutibiwa inapohitajika.


Je, Gynazole inaweza kutumika kila ninapopata uchafu ukeni?

Uchafu wa uke unaweza kuwa na sababu nyingi. Kandida kwa kawaida huhusishwa na kuwashwa, uwekundu na uchafu mzito mweupe, lakini dalili hizi hazitoshi kila mara kuthibitisha maambukizi.


Vajinosisi ya bakteria mara nyingi huhusishwa na uchafu mwembamba na harufu ya samaki, wakati trichomoniasis inaweza kusababisha uchafu wenye mabadiliko mbalimbali pamoja na kuwashwa au maumivu.


Kwa hiyo, kutumia Gynazole kila unapopata uchafu kunaweza kusababisha ugonjwa mwingine usitibiwe ipasavyo.


Ni nani anapaswa kumuona daktari kabla ya kutumia Gynazole?

Ni muhimu kupata tathmini ya kitabibu ikiwa:

  • Hujawahi kupata maambukizi ya fangasi hapo awali

  • Dalili ni kali sana

  • Una maumivu makali ya chini ya tumbo

  • Una homa

  • Una harufu kali isiyo ya kawaida ukeni

  • Una damu isiyo ya kawaida ukeni

  • Una vidonda au malengelenge sehemu za siri

  • Una ujauzito

  • Maambukizi yanarudia mara kwa mara

  • Dalili hazipungui baada ya matibabu

  • Dalili zinarudi ndani ya muda mfupi baada ya matibabu


Miongozo inapendekeza wanawake wenye dalili zinazoendelea baada ya kutumia dawa au wanaopata tena dalili ndani ya miezi miwili baada ya matibabu wafanyiwe tathmini ya kitabibu na vipimo inapohitajika.


Je, maambukizi ya fangasi yanaweza kurudia?

Baadhi ya wanawake hupata candidiasis mara kwa mara. Maambukizi yanayorudia yanaweza kuhusishwa na matumizi ya antibiotics, kisukari, au hali nyingine, ingawa wanawake wengi wenye maambukizi yanayorudia hawana sababu moja inayoweza kutambuliwa.


Miongozo hutambua maambukizi ya fangasi kweney vulva na ukeni ya kujirudia kwa kawaida kama vipindi vitatu au zaidi vya maambukizi yenye dalili ndani ya mwaka mmoja.


Ikiwa maambukizi yanarudia, si vizuri kuendelea kununua Gynazole na kujitibu kila mara bila uchunguzi. Inaweza kuwa Kandida aina nyingine, ukinzani wa dawa, au ugonjwa mwingine unaofanana na fangasi.


Je, Gynazole inatibu Kandida aina zote?

Aina mbalimbali za Kandida zinaweza kusababisha maambukizi ya uke. Kandida albicans ndiyo inayohusika na visa vingi, lakini aina nyingine kama Kandida glabrata zinaweza pia kusababisha maambukizi.


Baadhi ya Kandida wasio albicans zinaweza kuwa ngumu zaidi kutibiwa kwa dawa za azole. Kwa maambukizi yanayorudia au yasiyopona, uchunguzi wa maabara kama culture unaweza kusaidia kutambua aina ya Kandida na kuongoza matibabu.


Gynazole na dawa nyingine

Kwa sababu Gynazole hutumika ndani ya uke, mwingiliano wake wa dawa mwilini kwa ujumla huwa mdogo kuliko dawa nyingi za antifungal zinazotumiwa kwa mdomo.


Hata hivyo, mwambie daktari au mfamasia dawa zote unazotumia, hasa ikiwa unatumia dawa nyingine za uke au unaanza matibabu mengine ya maambukizi.


Usitumie dawa nyingi za uke kwa wakati mmoja bila kupewa maelekezo na mtaalamu wa afya.


Ukisahau kutumia Gynazole

Kwa bidhaa ya Gynazole-1 iliyokusudiwa kutumika kama dozi moja, hakuna ratiba ya dozi nyingi za kufidia kama ilivyo kwa dawa zinazotumiwa kila siku.


Ikiwa hujui kama ulitumia dawa ipasavyo au cream ilitoka baada ya kuitumia, usiongeze dozi bila kupata ushauri.


Fuata maelekezo ya kifurushi au wasiliana na mfamasia au daktari.


Je, Gynazole inaweza kutumika kwa watoto?

Gynazole-1 haipaswi kutumiwa kwa mtoto bila tathmini ya daktari.


Kuwashwa au uchafu kwenye sehemu za siri za mtoto unaweza kuwa na sababu tofauti na candidiasis ya uke kwa watu wazima.


Mtoto mwenye dalili za sehemu za siri anapaswa kuchunguzwa ili kutambua chanzo kabla ya kutumia dawa.


Dalili za hatari zinazohitaji kumuona daktari

Usijitibu kwa Gynazole pekee ikiwa una:

  • Homa

  • Maumivu makali ya tumbo la chini

  • Maumivu makali wakati wa kukojoa

  • Kutokwa damu kusiko kawaida

  • Harufu kali sana ya uchafu

  • Vidonda au malengelenge sehemu za siri

  • Maumivu makali wakati wa tendo la ndoa

  • Dalili zinazodumu baada ya matibabu

  • Maambukizi yanayorudia mara kwa mara


Dalili hizi zinaweza kuashiria ugonjwa mwingine ambao hauwezi kutibiwa na Gynazole.


Hitimisho

Gynazole-1 (butoconazole nitrate 2%) ni dawa ya kuua fangasi inayowekwa ndani ya uke na hutumika hasa kutibu maambukizi ya Kandida ukeni. Hufanya kazi kwa kuzuia utengenezaji wa sehemu muhimu ya utando wa seli ya fangasi.


Hata hivyo, si kila uchafu au kuwashwa ukeni ni fangasi. Kutumia Gynazole bila kujua chanzo kunaweza kuchelewesha matibabu ya vajinosisi ya bakteria, trikomoniasisi au maambukizi mengine. Pia, tahadhari ni muhimu wakati wa ujauzito na kwa sababu cream inaweza kudhoofisha kondomu za lateksi na kiwambo.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu Gynazole

1. Gynazole ni dawa ya nini?

Gynazole ni dawa ya kuua fangasi inayotumika kutibu maambukizi ya Kandida kwenye uke. Kiambata chake hai ni butoconazole nitrate 2%.


Husaidia kuondoa fangasi wanaosababisha maambukizi na hivyo kupunguza dalili kama kuwashwa, kuungua na uchafu mzito unaoweza kuambatana na kandidiasisi.


Hata hivyo, haipaswi kutumiwa kutibu kila aina ya uchafu ukeni kwa sababu sababu za uchafu ni nyingi.

2. Je, Gynazole inatibu uchafu mweupe ukeni?

Inaweza kutibu uchafu mweupe unaosababishwa na Kandida, hasa unapokuwa pamoja na kuwashwa, kuungua au uwekundu wa uke.


Lakini uchafu mweupe pekee hauwezi kuthibitisha kwamba una fangasi. Uchafu wa kawaida wa uke unaweza pia kuwa mweupe au wa uwazi bila kuwa ugonjwa.


Ikiwa uchafu una harufu kali, unaambatana na maumivu, homa, damu au dalili nyingine zisizo za kawaida, ni bora kuchunguzwa badala ya kutumia Gynazole pekee.

3. Je, Gynazole inaweza kutumika siku moja tu?

Gynazole-1 yenye butoconazole nitrate 2% imeundwa kwa matumizi ya dozi moja ya gramu 5 ndani ya uke.


Hata hivyo, bidhaa za butoconazole zinaweza kutofautiana katika namna ya kutengenezwa na ratiba ya matumizi.


Kwa hiyo, usitumie ratiba ya bidhaa nyingine ya butoconazole kwa Gynazole-1 bila kuangalia maelekezo ya bidhaa uliyonayo.

4. Je, Gynazole inaweza kutumika wakati wa ujauzito?

Usitumie Gynazole wakati wa ujauzito bila ushauri wa mtaalamu wa afya.


Lebo ya Gynazole-1 inaeleza kwamba usalama na ufanisi wa bidhaa hiyo kwa wanawake wajawazito haujaanzishwa.


Mjamzito mwenye dalili za fangasi anapaswa kupewa dawa inayofaa kwa ujauzito baada ya tathmini ya mtoa huduma wa afya.

5. Je, Gynazole inaweza kutumika pamoja na kondomu?

Tahadhari inahitajika kwa sababu krimu za aina hii zinaweza kuwa na mafuta yanayoweza kudhoofisha lateksi.


Hii inaweza kupunguza ufanisi wa kondomu za latex na diaphragms katika kuzuia mimba au maambukizi.


Soma maelekezo ya bidhaa kuhusu muda unaopaswa kupita kabla ya kutegemea njia hizi za kinga.

6. Je, Gynazole inatibu harufu mbaya ya uke?

Harufu mbaya ya uke inaweza kusababishwa na bacterial vaginosis, trikomoniasisi au sababu nyingine ambazo hazitibiwi na butoconazole.


Kwa hiyo, ikiwa tatizo kuu ni harufu kali bila dalili za kawaida za Kandida, ni bora kutafuta uchunguzi badala ya kutumia Gynazole bila kujua chanzo.

7. Je, mwanaume anaweza kutumia Gynazole?

Gynazole-1 imekusudiwa kutibu candidiasis ya uke kwa wanawake na si dawa ya kawaida ya kutibu maambukizi ya fangasi kwenye uume.


Mwanaume mwenye kuwashwa, uwekundu au uvimbe kwenye kichwa cha uume anapaswa kuchunguzwa ili kuamua dawa inayofaa.


Mwenza wa mwanamke mwenye candidiasis asiye na dalili kwa kawaida hahitaji matibabu.

8. Kwa nini bado ninawashwa baada ya kutumia Gynazole?

Dalili zinaweza kuendelea kwa sababu maambukizi bado hayajapona, kuna maambukizi makali, au chanzo cha dalili si Kandida.


Inawezekana pia kuwa kuna aina ya Kandida ambayo ni ngumu zaidi kutibiwa kwa azole.


Ikiwa dalili zinaendelea au zinarudi ndani ya miezi miwili baada ya matibabu, MiongozoC inapendekeza tathmini ya kitabibu na vipimo inapohitajika.

9. Je, naweza kutumia Gynazole kila ninapopata fangasi?

Si vizuri kufanya hivyo bila kuthibitisha sababu, hasa ikiwa maambukizi yanarudia.


Maambukizi yanayorudia mara kwa mara yanaweza kuhitaji kutafutwa kwa sababu kama kisukari, matumizi ya antibiotics au aina maalumu ya Kandida.


Matumizi ya dawa mara kwa mara bila uchunguzi yanaweza pia kufanya ugonjwa mwingine unaofanana na fangasi usigundulike.

10. Je, Gynazole inaweza kutibu magonjwa ya zinaa?

Hapana. Gynazole hutibu Kandida, si magonjwa mengi ya zinaa.


Haipaswi kutumiwa kama tiba ya kisonono, klamidia, trichomoniasis, kaswende au herpes.


Ikiwa una hatari ya kupata ugonjwa wa zinaa au una dalili kama vidonda, maumivu, damu isiyo ya kawaida au uchafu wenye harufu kali, ni muhimu kupata uchunguzi na vipimo vinavyofaa.


ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha  vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeandikwa:

7 Septemba 2026, 12:21:26

Rejea za mada hii:-

  1. Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1-187.

  2. Centers for Disease Control and Prevention. Vulvovaginal candidiasis [Internet]. Atlanta (GA): CDC; 2021 [cited 2026 Sep 7].

  3. DailyMed. Gynazole-1 (butoconazole nitrate) cream [Internet]. Bethesda (MD): National Library of Medicine; [cited 2026 Sep 7].

  4. Pappas PG, Kauffman CA, Andes DR, Clancy CJ, Marr KA, Ostrosky-Zeichner L, et al. Clinical practice guideline for the management of candidiasis: 2016 update by the Infectious Diseases Society of America. Clin Infect Dis. 2016;62(4):e1-e50.

  5. Sobel JD. Vulvovaginal candidosis. Lancet. 2007;369(9577):1961-1971.

  6. Willems HME, Ahmed SS, Liu J, Xu Z, Peters BM. Vulvovaginal candidiasis: a current understanding and burning questions. J Fungi (Basel). 2020;6(1):27.

bottom of page