top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

Dkt. Sospeter M, MD

Dkt. Lugonda B, MD

27 Agosti 2026, 05:32:40

Dawa Griseofulvin

Dawa Griseofulvin

Griseofulvin ni dawa ya kuua fangasi inayotumika hasa kutibu maambukizi ya fangasi wanaoshambulia ngozi, nywele na kucha, hasa fangasi wa jamii ya dermatophytes. Ni dawa muhimu katika matibabu ya mashilingi ya kichwani kwa jina jingine fangasi wa kichwani (tinea capitis), ambapo dawa za kupaka pekee mara nyingi hazitoshi kwa sababu maambukizi yako ndani ya nywele na kwenye vinyweleo.


Fomu na nguvu za Griseofulvin

Griseofulvin hupatikana katika aina mbalimbali kulingana na mtengenezaji, ikiwa ni pamoja na:

  • Vidonge vya 125 mg

  • Vidonge vya 250 mg

  • Vidonge vya 500 mg

  • Kimiminika cha kunywa katika baadhi ya bidhaa


Muhimu: nguvu ya kidonge na aina ya Griseofulvin—kama ni microsize au ultramicrosize—huathiri namna dozi inavyohesabiwa. Kwa hiyo, si sahihi kubadilisha vidonge au dozi kwa kuangalia idadi ya miligramu pekee bila kuthibitisha aina ya dawa.


Majina yakibiashara ya Griseofulvin

Kwa Griseofulvin, majina ya kibiashara yanayotumika au yanayoweza kupatikana Afrika Mashariki hutofautiana kulingana na nchi na mtengenezaji. Baadhi ya majina yanayojulikana ni:

  • Grisactin

  • Griseofulvin

  • Grisovin

  • Gris-PEG

  • Fulcin

  • Grisoral

  • Grisovin FP

  • Griseofulvin Tablets

  • Griseofulvin Oral Suspension

Kwa Tanzania na Afrika Mashariki, ni muhimu kutambua kwamba jina la kibiashara linaweza kutofautiana kati ya maduka ya dawa na nchi, hivyo mgonjwa anapaswa kuangalia kwenye kifurushi jina la dawa hai (griseofulvin) na nguvu yake, kwa mfano 125 mg, 250 mg au 500 mg, badala ya kutegemea jina la biashara pekee.


Griseofulvin hutibu magonjwa gani?

Griseofulvin hutumika kutibu maambukizi yanayosababishwa na fangasi wa jamii ya dermatophytes, wakiwemo:

  • Mashilingi ya kichwani (tinea capitis)

  • Mashilingi ya mwilini (tinea corporis)

  • Fangasi wa kwenye mapaja/kinena (tinea cruris)

  • Baadhi ya maambukizi ya fangasi kwenye miguu

  • Maambukizi ya fangasi kwenye kucha katika hali zinazofaa

Ufanisi wake hutegemea aina ya fangasi anayesababisha maambukizi. Griseofulvin haitibu maambukizi ya bakteria, na si kila ugonjwa unaoitwa "fangasi" husababishwa na fangasi ambao dawa hii inaweza kuwatibu.


Griseofulvin inavyofanya kazi

Griseofulvin huingilia uwezo wa fangasi kugawanyika na kuzaliana. Dawa hiyo hujikusanya kwenye tishu mpya za keratini, hivyo ngozi, nywele au kucha mpya zinapokua huwa na ulinzi dhidi ya kuendelea kwa maambukizi.


Kwa sababu hiyo, dawa haiwezi kuondoa mara moja sehemu ya nywele au kucha ambayo tayari imeharibika. Mwili huhitaji muda kukuza tishu mpya zilizoathiriwa kidogo au zisizo na fangasi.

Hii ndiyo sababu mtu anaweza kuendelea kuona mabadiliko kwenye nywele au ngozi hata baada ya kuanza kupata nafuu.


Griseofulvin na mashilingi ya kichwani

Mashilingi ya kichwani ni maambukizi ya fangasi kwenye ngozi ya kichwa na nywele. Kwa hali hii, dawa ya kunywa kama Griseofulvin ndiyo tiba muhimu kwa sababu dawa ya kupaka pekee haiwezi kufikia kwa ufanisi sehemu zote zilizoathiriwa ndani ya nywele na vinyweleo.


Muda wa matibabu hutegemea aina ya fangasi, umri, uzito wa mgonjwa, dawa iliyotumika na mwitikio wa mwili. Kwa Griseofulvin, muda wa kawaida uliotajwa katika taarifa za dawa kwa tinea capitis ni takribani wiki 4–6, lakini baadhi ya wagonjwa wanaweza kuhitaji muda tofauti kulingana na tathmini ya mtaalamu.


Dozi ya Griseofulvin

Dozi haiwezi kuamuliwa kwa kusema kila mtu atumie kidonge kimoja au viwili kwa siku. Kwa watoto, dozi mara nyingi huhesabiwa kwa kuzingatia uzito wa mwili na aina ya Griseofulvin.


Kwa mfano, taarifa za dawa za microsize griseofulvin zinaonyesha kuwa kwa watoto wenye umri zaidi ya miaka 2, dozi inaweza kuhesabiwa kwa uzito, huku taarifa za ultramicrosize zikitumia kiwango tofauti kwa sababu dawa hiyo hufyonzwa kwa namna tofauti.


Kwa hiyo, Grisactin-500 haipaswi kutumiwa kwa kuamua tu kwamba "500 mg ni dozi ya kawaida". Daktari au mfamasia anapaswa kuthibitisha aina ya Griseofulvin, umri, uzito na aina ya maambukizi kabla ya kupanga dozi.


Je, Griseofulvin itumike pamoja na chakula?

Griseofulvin inaweza kufyonzwa vizuri zaidi inapochukuliwa pamoja na chakula, hasa chakula chenye mafuta kiasi. Hivyo, ikiwa maelekezo ya bidhaa au mtoa huduma wa afya hayajasema vingine, kuitumia pamoja na chakula inaweza kusaidia ufyonzwaji wa dawa.


Ni muhimu pia kutumia dawa kwa muda uliopangwa. Kuacha dawa mara tu dalili zinapopungua kunaweza kuongeza uwezekano wa maambukizi kurudi. Taarifa za dawa zinasisitiza kuendelea na matibabu hadi maambukizi yatokomee kulingana na tathmini ya kitabibu au vipimo vinavyofaa.


Muda wa kutumia Griseofulvin

Muda unatofautiana kulingana na sehemu iliyoathirika:

Aina ya maambukizi

Muda wa kawaida wa matibabu

Mashilingi ya kichwani

Takribani wiki 4–6

Mashilingi ya mwilini

Takribani wiki 2–4

Fangasi wa miguu

Takribani wiki 4–8

Fangasi wa kucha

Miezi kadhaa, kulingana na aina ya kucha na kasi ya ukuaji

Hii ni mifano ya muda wa matibabu, si maagizo ya kila mgonjwa. Muda unaweza kubadilishwa kulingana na aina ya fangasi na mwitikio wa mgonjwa.


Dawa nyingine zinazoweza kutumika kutibu fangasi

Dawa nyingine za kuua fangasi zinaweza kutumika kulingana na aina na eneo la maambukizi. Mfano ni:

  • Terbinafine

  • Itraconazole

  • Fluconazole

  • Ketoconazole

  • Miconazole

  • Nystatin

  • Clotrimazole

Hata hivyo, dawa hizi hazibadilishani moja kwa moja. Dawa inayofaa hutegemea aina ya fangasi, eneo la maambukizi, umri wa mgonjwa, magonjwa mengine na dawa anazotumia.


Ni nani hapaswi kutumia Griseofulvin?

Griseofulvin haipaswi kutumiwa na mtu mwenye:

  • Mzio unaojulikana kwa Griseofulvin.

  • Ugonjwa mkali wa ini au kushindwa kwa ini kufanya kazi vizuri.

  • Porphyria, kulingana na taarifa za dawa.

Kwa watoto wenye umri wa miaka 2 au chini, usalama na ufanisi wa Griseofulvin haujawekwa vizuri katika baadhi ya taarifa za dawa, hivyo matumizi yanahitaji tathmini maalumu ya mtaalamu.


Griseofulvin wakati wa ujauzito

Griseofulvin haipendekezwi wakati wa ujauzito kwa sababu kuna ushahidi wa hatari kwa kijusi. Mwanamke anayeshuku kuwa ni mjamzito au anayepanga kupata ujauzito anapaswa kumjulisha daktari kabla ya kutumia dawa hii.


Pia, Griseofulvin inaweza kupunguza ufanisi wa baadhi ya vidonge vya uzazi wa mpango vyenye estrogeni. Hivyo, mtu anayetumia uzazi wa mpango wa aina hiyo anapaswa kujadili na mtoa huduma kuhusu njia ya ziada au mbadala ya kuzuia mimba wakati wa matibabu.


Griseofulvin wakati wa kunyonyesha

Haijulikani kwa uhakika kiasi gani cha Griseofulvin kinachoweza kuingia kwenye maziwa ya mama. Kwa hiyo, mama anayenyonyesha anapaswa kumjulisha daktari kabla ya kuanza dawa ili faida na hatari zipimwe kulingana na hali yake.


Madhara ya Griseofulvin

Baadhi ya madhara yanayoweza kutokea ni:

  • Kichefuchefu

  • Kutapika

  • Kuharisha

  • Maumivu ya tumbo

  • Maumivu ya kichwa

  • Kizunguzungu

  • Uchovu

  • Kukosa usingizi

  • Upele au kuwashwa

  • Kuongezeka kwa unyeti wa ngozi kwa mwanga wa jua

Madhara makubwa ni nadra, lakini yameripotiwa, ikiwa ni pamoja na matatizo makubwa ya ngozi na ini. Mtu anayepata manjano ya macho au ngozi, mkojo mweusi, upele mkali, kuvimba uso au shida ya kupumua anapaswa kutafuta huduma ya afya haraka.


Griseofulvin na dawa nyingine

Griseofulvin inaweza kuathiri namna mwili unavyovunja au kutumia baadhi ya dawa. Kwa mfano, inaweza kupunguza ufanisi wa baadhi ya vidonge vya uzazi wa mpango vyenye estrogeni na kupunguza athari za baadhi ya dawa za kuzuia damu kuganda kama warfarin. Inaweza pia kuathiri viwango vya cyclosporine.

Kwa hiyo, mtu anayatumia dawa nyingine kwa muda mrefu anapaswa kumjulisha daktari au mfamasia kabla ya kuanza Griseofulvin.


Griseofulvin na usafi wakati wa kutibu mashilingi

Matibabu hayapaswi kuishia kwenye kumeza dawa pekee. Mashilingi ya kichwani yanaweza kuenea kwa watu wengine kupitia vitu vinavyogusana na nywele au kichwa.

Inashauriwa:

  • Kuepuka kushirikiana masega na brashi.

  • Kuepuka kushirikiana kofia na vitu vingine vinavyogusa kichwa.

  • Kuosha na kutunza vitu vinavyogusa kichwa kwa usafi.

  • Kuwachunguza watu wa karibu wanaoonyesha dalili zinazofanana.

  • Kufuatilia matibabu hadi maambukizi yadhibitiwe.

Hatua hizi husaidia kupunguza uwezekano wa kuambukizwa tena.


Ukisahau dozi ya Griseofulvin

Ukisahau dozi, itumie unapokumbuka ikiwa bado kuna muda wa kutosha kabla ya dozi inayofuata. Ikiwa muda wa dozi inayofuata umekaribia, ruka dozi uliyosahau na endelea na ratiba ya kawaida.

Usitumie dozi mbili kwa wakati mmoja ili kufidia dozi uliyosahau, isipokuwa umeelekezwa tofauti na mtoa huduma wa afya.


Hitimisho

Griseofulvin ni dawa muhimu hasa kwa mashilingi ya kichwani, lakini mafanikio ya matibabu yanategemea utambuzi sahihi, aina ya dawa, dozi inayolingana na mgonjwa na kukamilisha muda unaofaa wa matibabu.


Mtu asiongeze dozi au muda wa Griseofulvin mwenyewe ikiwa mashilingi hayaishi; kutopata nafuu kunaweza kuhitaji kuthibitisha utambuzi, kuchunguza aina ya fangasi au kubadilisha mpango wa matibabu.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu Griseofulvin

1. Nina mashilingi natumia dawa Grisactin-500 za mwezi mmoja, je zitaisha?

Si rahisi kusema kwamba mashilingi yataisha kwa kila mtu baada ya mwezi mmoja. Kwa mashilingi ya kichwani, Griseofulvin mara nyingi hutumika kwa takribani wiki 4–6, lakini muda unaweza kutofautiana kulingana na aina ya fangasi na mwitikio wa mgonjwa.


Pia, jina Grisactin-500 linaonyesha nguvu ya kidonge, lakini halitoshi kuamua kama dozi anayopata mtu ni sahihi. Inahitaji kujulikana kama ni aina gani ya Griseofulvin, pamoja na umri, uzito na aina ya mashilingi.


Ikiwa baada ya mwezi mmoja bado kuna maeneo mapya ya upara, nywele zinazokatika, magamba au kuwashwa, si vizuri kuongeza muda wa dawa mwenyewe. Ni bora kufanyiwa tathmini ili kuhakikisha kwamba kweli ni mashilingi na kwamba dawa inayotumika inafaa.

2. Kwa nini mashilingi yanaweza kuonekana bado yapo wakati dawa inaanza kufanya kazi?

Griseofulvin huua au kuzuia kuendelea kwa fangasi, lakini nywele ambazo tayari zimeharibika haziwezi kurudi kawaida mara moja. Nywele zilizokatika au zilizoharibiwa zinahitaji muda kukua tena.


Kwa hiyo, mwonekano wa kichwa unaweza kubaki na maeneo yenye nywele chache hata baada ya maambukizi kuanza kudhibitiwa. Hili ni tofauti na kuendelea kwa fangasi.


Kinachotia wasiwasi zaidi ni kuendelea kupata maeneo mapya, kuongezeka kwa magamba, kuwashwa au kuendelea kwa nywele kukatika. Hali hiyo inahitaji tathmini ya mtaalamu.

3. Je, mtu anaweza kuwa na mashilingi lakini Griseofulvin isisaidie?

Ndiyo. Neno "mashilingi" hutumiwa na jamii kuelezea hali mbalimbali za ngozi ya kichwa, lakini si kila upara, magamba au kuwashwa kichwani ni mashilingi yanayosababishwa na fangasi.


Ikiwa tatizo si maambukizi ya fangasi wanaoathiriwa na Griseofulvin, dawa inaweza kutotoa matokeo yanayotarajiwa. Pia, aina tofauti za fangasi zinaweza kuitikia dawa za kuua fangasi kwa namna tofauti.


Kwa mtoto ambaye hapati nafuu licha ya kutumia dawa ipasavyo, ni muhimu kuangaliwa upya badala ya kuendelea kubadilisha dawa bila kujua chanzo cha tatizo.

4. Je, nikitumia Griseofulvin kwa mwezi mmoja na mashilingi hayajaisha, ninaweza kuongeza mwezi mwingine?

Usiongeze muda wa matibabu mwenyewe bila tathmini. Kwa baadhi ya wagonjwa, hasa wenye mashilingi ya kichwani, matibabu yanaweza kuhitaji zaidi ya wiki nne, lakini uamuzi huo hutegemea mwitikio wa mgonjwa na tathmini ya mtaalamu.


Kabla ya kuongeza dawa, ni muhimu kujiuliza kama tatizo ni fangasi kweli, kama dozi inalingana na uzito wa mgonjwa na kama dawa inatumika kwa usahihi.


Mtaalamu anaweza pia kuamua kama kuna haja ya uchunguzi wa fangasi au kubadilisha aina ya dawa badala ya kuongeza muda wa Griseofulvin.

5. Je, mtoto anaweza kutumia Griseofulvin kwa mashilingi?

Ndiyo, Griseofulvin hutumika katika matibabu ya mashilingi ya kichwani kwa watoto, lakini dozi ya mtoto huhesabiwa kwa kuzingatia uzito na aina ya Griseofulvin.


Hii ni muhimu kwa sababu kidonge cha 500 mg si lazima kiwe dozi inayofaa kwa kila mtoto. Kumpa mtoto kidonge kizima kwa sababu tu kinaonekana kuwa "cha kawaida" kunaweza kusababisha dozi isiyofaa.


Kwa watoto wadogo sana, hasa walio chini ya miaka 2, matumizi yanahitaji tathmini maalumu kwa sababu usalama na ufanisi haujawekwa vizuri katika baadhi ya taarifa za dawa.

6. Je, nikiona nywele zinaanza kuota tena, naweza kuacha Griseofulvin?

Kuota kwa nywele ni ishara nzuri ya kupona kwa tishu, lakini si uthibitisho wa kwamba fangasi wote wametokomea. Nywele zinaweza kuanza kuonekana vizuri wakati maambukizi bado hayajadhibitiwa kikamilifu.


Kuacha dawa mapema kunaweza kuongeza uwezekano wa maambukizi kuendelea au kurudi. Taarifa za dawa zinaeleza kwamba matibabu yanapaswa kuendelea hadi maambukizi yadhibitiwe kulingana na tathmini inayofaa.


Kwa hiyo, uamuzi wa kuacha dawa unapaswa kuzingatia mpango uliotolewa na mtoa huduma, si kuangalia tu kama nywele zimeanza kuota.

7. Je, mtu mwenye mashilingi anaweza kutumia Griseofulvin pamoja na dawa ya kupaka?

Katika baadhi ya hali, dawa ya kupaka inaweza kutumika kama sehemu ya mpango wa matibabu, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya dawa ya kunywa katika mashilingi ya kichwani. Dawa za kupaka zinaweza kusaidia kupunguza kiasi cha fangasi kwenye uso wa kichwa na kupunguza uwezekano wa kueneza maambukizi.


Hata hivyo, si kila krimu ya fangasi inafaa kupakwa kichwani, na krimu zenye dawa za steroid zinaweza kuwa na matatizo zikitumiwa bila ushauri.


Kwa hiyo, ni vizuri kutumia dawa ya kupaka ikiwa imependekezwa na mtoa huduma na kwa muda ulioshauriwa.

8. Je, Griseofulvin inaweza kusababisha mtoto kuwa na tatizo la ini?

Madhara makubwa ya ini yanaweza kutokea ingawa si ya kawaida. Taarifa za dawa zimeripoti matatizo ya ini na madhara makubwa ya ngozi baada ya matumizi ya Griseofulvin.


Mtoto anayepata manjano ya macho au ngozi, mkojo wenye rangi nyeusi, uchovu usio wa kawaida, kutapika sana au dalili nyingine zinazotia wasiwasi anapaswa kuchunguzwa.


Hii haimaanishi kwamba kila mtoto anayatumia Griseofulvin anahitaji kuogopa uharibifu wa ini. Dawa inapaswa kutumiwa kwa dozi na muda unaofaa, na mtoto afuatiliwe ikiwa ana sababu nyingine zinazoongeza hatari ya matatizo ya ini.

9. Kwa nini mashilingi yanarudi baada ya mtu kumaliza Griseofulvin?

Mashilingi yanaweza kurudi ikiwa maambukizi hayakutokomezwa kikamilifu au mtu ameambukizwa tena kutoka kwa mtu au mazingira yenye fangasi. Taarifa za dawa pia zinasisitiza umuhimu wa hatua za usafi ili kupunguza maambukizi mapya.


Mtoto anaweza pia kuendelea kuwasiliana kwa karibu na mtu mwingine mwenye maambukizi bila kutibiwa, au kushirikiana vitu kama masega na brashi.


Ikiwa mashilingi yanarudi mara kwa mara, ni muhimu kutafuta chanzo cha kuambukizwa tena badala ya kurudia Griseofulvin kila mara bila uchunguzi.

10. Je, Griseofulvin inaweza kutumiwa na mtu anayekunywa vidonge vya uzazi wa mpango?

Griseofulvin inaweza kupunguza ufanisi wa baadhi ya vidonge vya uzazi wa mpango vyenye estrogeni kwa kuongeza uvunjaji wa homoni hizo mwilini. Hivyo, mwanamke anayatumia matibabu haya anapaswa kumjulisha mtoa huduma kuhusu aina ya uzazi wa mpango anaotumia.


Katika hali hiyo, mtoa huduma anaweza kupendekeza njia ya ziada au mbadala ya kuzuia mimba wakati wa matibabu na kulingana na muda unaohitajika.


Pia, ikiwa kuna uwezekano wa ujauzito wakati wa matibabu, ni muhimu kumjulisha daktari kwa sababu Griseofulvin haipendekezwi wakati wa ujauzito kutokana na hatari inayoweza kutokea kwa kijusi.


ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha  vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeandikwa:

9 Agosti 2020, 20:36:05

Rejea za mada hii:-

  1. Griseofulvin. In: StatPearls [Internet]. Treasure Island (FL): StatPearls Publishing; 2024.

  2. Gupta AK, Drummond-Main C, Cooper EA, Brintnell W, Piraccini BM, Tosti A. Systematic review of nondermatophyte mold onychomycosis: diagnosis, treatment and management. J Am Acad Dermatol. 2012;66(4):602-613.

  3. World Health Organization. WHO guidelines on the treatment of skin and oral HIV-associated conditions in children and adults. Geneva: World Health Organization; 2014.

  4. Hay RJ, Ashbee HR. Fungal infections. In: Griffiths CEM, Barker J, Bleiker T, Chalmers R, Creamer D, editors. Rook's Textbook of Dermatology. 9th ed. Chichester: Wiley-Blackwell; 2016.

  5. Bennett JE, Dolin R, Blaser MJ, editors. Mandell, Douglas, and Bennett's Principles and Practice of Infectious Diseases. 10th ed. Philadelphia: Elsevier; 2024.

bottom of page