top of page

Elimu ya magonjwa kwa mjamzito

Sehemu hii utajifunza maelezo ya ziada kuhusu matatizo mbalimbali ya kiafya wakati wa ujauzito. Unashauriwa siku zote kuwasilaina na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile iliyoandikwa humu ili kupata ushauri unaoendana na hali yako ya kiafya.

Kukojoa mara kwa mara kwa mjamzito

Kukojoa mara kwa mara kwa mjamzito

Mara nyingi huwa ni mabadiliko ya kawaida katika ujauzito, yanayohusishwa zaidi na mabadiliko ya utendaji kazi wa figo, homoni na ongezeko la shinikizo la mfuko wa uzazi kwenye kibofu. Ikiwa kuna hisia za maumivu au kuungua wakati wa kukojoa, damu, homa, maumivu ya mgongo au kujisikia mgonjwa, usichukulie hali hiyo kuwa ya kawaida ya ujauzito bila kuchunguzwa.

Mimba wakati wa Kunyonyesha

Mimba wakati wa Kunyonyesha

Inaweza kuingia hata kabla hedhi ya kwanza kurudi kwa sababu yai linaweza kutoka kabla ya hedhi ya kwanza. Kunyonyesha hutoa kinga ya muda tu ikiwa masharti maalumu ya kunyonyesha kikamilifu na mtoto kuwa chini ya miezi sita yametimizwa. Mama anayepata mimba mtoto akiwa na mwezi 1–12 hapaswi kuamua kuitoa kwa sababu ya umri mdogo wa mtoto pekee; anapaswa kupata tathmini ya afya, kuelewa hatari na chaguo zake, kisha kufanya uamuzi wenye taarifa unaoheshimu afya na matakwa yake.

Maambukizi yanayoweza kutoa Mimba

Maambukizi yanayoweza kutoa Mimba

Maambukizi kama kaswende, rubela, toksoplasmosisi, parvovirus B19 na VVU yanaweza kuongeza hatari ya mimba kutoka au matatizo mengine ya ujauzito, kutegemea aina ya maambukizi na muda wa kuambukizwa.
Kupima mapema, kupata matibabu yanayofaa na kufuatiliwa wakati wa ujauzito husaidia kupunguza madhara kwa mama na mtoto.

Maambukizi ya streptokoka kundi B kwa mjamzito

Maambukizi ya streptokoka kundi B kwa mjamzito

Bakteria Streptokoka kundi B mara nyingi hubebwa bila kusababisha ugonjwa kwa mama, lakini wanaweza kumwambukiza mtoto wakati wa kujifungua na kusababisha maambukizi makubwa kama maambukizi ya damu, mapafu au utando unaozunguka ubongo na uti wa mgongo. Upimaji katika wiki 36+0 hadi 37+6 na dawa zinazotolewa wakati wa uchungu kwa wanawake wanaohitaji kinga husaidia kupunguza hatari ya ugonjwa wa mapema kwa mtoto.

Utunzaji wa kidonda cha kuchanwa msamba

Utunzaji wa kidonda cha kuchanwa msamba

Kidonda cha kuchanwa msamba kilichofumuka kinaweza kupona taratibu kwa kukisafisha kwa maji safi, kukiweka katika hali ya usafi na ukavu, pamoja na kufuatiliwa na mhudumu wa afya; si kila kidonda huhitaji kushonwa tena. Hata hivyo, maumivu yanayoongezeka, usaha, harufu mbaya, homa au kidonda kuendelea kufunguka zaidi huhitaji uchunguzi wa mhudumu wa afya ili kubaini tatizo na matibabu yanayofaa.

bottom of page