top of page

Mwandishi:

Mhariri:

ULY CLINIC

DKt. Sospeter B, MD

12 Desemba 2025, 11:26:03

Image-empty-state.png

Kutokwa na Maji ukeni kipindi cha Wiki 25 za Ujauzito: Sababu, Uchunguzi na Tiba

Imeboreshwa:

Kutokwa na maji maji ukeni ni jambo la kawaida kwa wanawake wajawazito kwa sababu ya mabadiliko ya homoni na kuongezeka kwa mtiririko wa damu sehemu za siri. Hata hivyo, katika kipindi cha wiki 25 za ujauzito (Kipindi cha pili cha ujauzito), mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida yanaweza kuashiria maambukizi, hatari ya uchungu wa mapema, au tatizo kwenye shingo ya kizazi (seviksi) au kwenye utando wa mimba (kuta za mimba). Makala hii inalenga kumfafanulia mama mjamzito tofauti kati ya hali ya kawaida na ishara za hatari zinazohitaji matibabu ya haraka.


Ni nini maana ya kutokwa na maji maji ukeni katika ujauzito?

Ni hali ya kutoka majimaji sehemu za siri ambayo yanaweza kuwa ya kawaida yaani ute wa uke unaotoka kama kawaida kwa wanawake au yasiyo ya kawaida yanayoashiria maambukizi au tatizo kwenye mimba. Katika ujumla wake:

  • Majimaji au ute wa kawaida: Huwa ni majimaji au ute mwepesi, usio na harufu kali, mweupe au wazi, usiokuwa na muwasho.

  • Majimaji yasio kawaida: Huwa ni ute au majimaji yenye harufu mbaya, rangi ya njano/kijani/kahawia, yanayoambatana na muwasho, maumivu au joto sehemu za siri.


Dalili zinazohitaji uchunguzi wa haraka


Kutokwa na maji katika wiki 25 kunaweza kuashiria dalili ya tatizo kubwa katika ujauzito. Dalili za hatari ni:


a) Maji kama ya kuvuja bila kukoma – yanaweza kuwa maji ya chupa ya kizazi
  • Kama maji yanayotiririka bila kudhibitika.

  • Hutiririka hadi kwenye mapaja yakiwa mengi

  • Wazi, yasiyo na rangi au yenye harufu isiyo kali.

  • Hatari: uchungu wa mapema, maambukizi kwa mtoto tumboni, kupungua maji ya chupa ya uzazi.


b) Kutokwa na maji yenye harufu mbaya au rangi ya njano/kijani

Inaashiria maambukizi ya uke kama vile vajinosisi ya bakteria, fangasi, trikomoniasisi ambayo yanahatari ya kwenda kwenye mji wa mimba.


c) Kutokwa na maji kwa damu au ute wenye chembe nyekundu

 Inaweza kuwa dalili ya

  • Kondo limejipandikiza sehemu isiyo sahihi- Plasenta previa,

  • Kutoka uchungu wa mapema,

  • Maambukizi ya kizazi au tishu.


d) Muwasho, maumivu, au joto sehemu za siri

Dalili za maambukizi ya fangasi au bakteria ambayo ni hatari kwa ujauzito.


Kwa nini wanawake hutokwa maji maji zaidi kipindi cha wiki 25?

Katika kipindi hiki:


a) Kuongezeka kwa homoni za estrojen

Huchochea tezi za uke kuzalisha ute mwingi kwa ajili ya:

  • Kulinda kijusi dhidi ya maambukizi.

  • Kudhibiti usawa wa bakteria ukeni.


b) Kuongezeka kwa mtiririko wa damu kwenye uke na pelvis

Hufanya ute kuwa mwingi na mwepesi.


c) Ukuaji wa kiunzi cha shingo ya kizazi

Baada ya kutengenezwa kwenye shingo ya kizazi, ute unaweza kuonekana kwa kiasi kidogo ukipenya nje kupitia uke.


Aina za kawaida za maji maji kwenye ujauzito


a. Ute wa kawaida
  • Rangi: mweupe, maziwa au wazi.

  • Muundo: mwembamba au mzito kidogo.

  • Harufu: haitokwi sana au ni laini isiyo kali.

  • Bila maumivu au muwasho.


b. Ute wa kiunzi cha kizazi unayovuja kidogo
  • Mzito, wa utegundo, rangi ya maziwa au mpira kidogo.

  • Haina harufu mbaya.


Sababu za kawaida za kukutwa na maji Maji ukeni wiki 25


1) Leukorrhea

Sababu ya mabadiliko ya homoni, hali hii si hatari.


2) Maambukizi ya fangasi (Kandidiasis)
  • Ute mweupe kama jibini

  • Muwasho mkali

  • Maumivu wakati wa kukojoa au tendo la ndoa


3) Vajinosisi ya bakteria (BV)
  • Ute mweupe/kijivu

  • Harufu ya samaki

  • Hatari: kuzaa kabla ya wakati


4) Trikomoniasis (Ugonjwa wa zinaa)
  • Ute wa kijani/njano

  • Harufu mbaya

  • Muwasho mkali


5) Maambukizi ya mfumo wa mkojo- UTI

Huwa hayatoi maji mengi lakini huambatana na:

  • Maumivu ya chini ya tumbo

  • Kukojoa mara kwa mara


6) Kutoka kwa ute wa kiunzi cha shingo ya kizazi

Kwa kawaida salama ila ikivujia sana inaweza kuashiria shingo ya kizazi kufunguka mapema.


7) Kuvuja kwa maji ya chupa ya uzazi

Hii ndiyo sababhaitari zaidi katika wiki 25.Inahitaji tiba ya haraka hospitalini.


Vipimo vinavyoweza kufanyika hospitalin

  • Uchunguzi wa shingo ya kizazi: Kuangalia kama maji yanatoka shingoni.

  • Kipimo cha Nitrazine: Kuangalia kama ni maji ya mimba.

  • Ultrasound: Kupima kiwango cha maji ya mimba (AFI) na afya ya mtoto.

  • Kuotesha vimela kutoka kwenye ute ukeni: Kubaini bakteria au fangasi.

  • Uchunguzi wa shingo ya kizazi (Urefu wa shingo ya kizazi).


Tiba kutegemea sababu


Leukorrhea ya kawaida

Hakuna dawa. Kujielimisha tu kuhusu ute wa kawaida na kufanya usafi wa uke.


Fangasi

Dawa ya kuingiza ukeni (clotrimazole), salama kama umeshauri wa na daktari kutumia


Vajinosisi ya bakteria (BV)

Metronidazole salama kutumika katika kipindi cha pili cha ujauzito kwa ushauri wa daktari wako.


Trichomoniasis

Matibabu ya mama na mwenza (Dozi yenye mchanganyiko wa metronidazole alama kipindi cha pili cha ujauzito kama ikitumika kwa ushauri wa daktati).


PPROM / Kuvuja kwa maji ya mimba
  • Kulazwa hospitalini

  • Antibayotiki

  • Steroid(kuimarisha mapafu ya mtoto)

  • Kuangaliwa dalili za uchungu na maambukizi

  • Kiwango cha mashauriano na daktari bingwa hutegemea umri wa ujauzito


Namna ya kujikinga na maambukizi

  • Epuka sabuni zenye kemikali kali.

  • Tumia chupi za pamba, badili mara kwa mara.

  • Kaushia mwili vizuri baada ya kuoga.

  • Epuka kuvaa nguo za kubana sana.

  • Kunywa maji ya kutosha.

  • Kuwa mwaminifu kwa mwenza mmoja au tumia kinga.

  • Usitumie dawa za ukeni bila ushauri wa mtaalamu.


Wakati gani ni lazima uende hospitali mara moja?

  • Maji yanaendelea kutoka bila kukoma.

  • Harufu mbaya ya kuvunda.

  • Muwasho mkali au maumivu.

  • Ute wa kijani au njano.

  • Ute wa damu.

  • Kuhisi mtoto anacheza chini ya kawaida.

  • Homa au maumivu makali ya tumbo la chini.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Kutokwa na maji maji ukeni kipindi cha wiki 25 za ujauzito inaweza kuwa ni hatari kwa ujauzito?

Ndiyo. Ingawa mara nyingi ni hali ya kawaida, inaweza kuwa hatari ikiwa maji yanayotoka ni maji ya mimba (PPROM), yanatoka kwa wingi bila kudhibitika, yana harufu mbaya, yana rangi isiyo ya kawaida, au yanahusisha muwasho mkali. Katika wiki 25, kuvujia kwa maji ya mimba kunaongeza hatari ya uchungu wa mapema, kuambukiza mtoto, kupungua maji ya mimba, au matatizo ya ukuaji wa mtoto. Muhimu: tembelea hospitali mara moja.

2. Nitajuwaje kama haya ni maji ya mimba?

Hutiririka kama maji mengi ya wazi, yasiyodhibitika. Mara nyingi hujaa kwenye chupi au kumwagika ghafla. Utaona hayana mnato kama ute wa kawaida.

3. Je, kutokwa na ute mweupe mzito ni kawaida?

Ndiyo, hii mara nyingi ni leukorrhea au ute wa kiunzi (mucus plug) na si hatari kama hakuna muwasho au harufu.

4. Kutokwa na ute wenye harufu ya samaki inamaanisha nini?

Hii ni dalili ya Vajinosisi ya bakteria (BV), maambukizi yanayohitaji dawa na yanaweza kuongeza hatari ya kuzaa kabla ya wakati.

5. Je, ninaweza kutumia dawa za dukani kutibu maambukizi?

Hapana. Wajawazito hawapaswi kutumia dawa za ukeni bila ushauri wa mtaalamu.

6. Fangasi zinaweza kuathiri mtoto?

Kwa ujauzito wa wiki 25 mara nyingi hazidhuru mtoto moja kwa moja, lakini zinahitaji matibabu ili kuzuia usumbufu na kuongezeka kwa maambukizi.

7. Kutokwa maji baada ya tendo la ndoa ni kawaida?

Ndiyo, mara nyingi ni ute uliosukumwa nje au shahawa, lakini kama kuna harufu mbaya au maumivu, pata uchunguzi.

8. Nifanye nini nikiona ute wenye damu?

Nenda hospitali mara moja. Inaweza kuwa ishara ya uchungu mapema, maambukizi au tatizo kwenye kondo la mimba.

9. Je, maji maji yanaweza kuongezeka nikiwa na msongo, uchovu au nikitembea sana?

Ndiyo, shughuli za mwili na msongo huongeza mtiririko wa damu sehemu za siri hivyo ute unaweza kuongezeka.

10. Je, kuna vyakula vinavyoongeza au kupunguza kutokwa na maji?

Hakuna vyakula maalum vinavyobadili kiasi, lakini probiotic foods kama mtindi husaidia kuweka uwiano wa bakteria ukeni.


ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeandikwa:

12 Desemba 2025, 10:33:34

Rejea za dawa

  1. Brown HL, Miller JM. Vaginal discharge in pregnancy: evaluation and management. Obstet Gynecol Clin North Am. 2020;47(1):1–15.

  2. Mercer BM. Preterm premature rupture of the membranes. Obstet Gynecol. 2003;101(1):178–93.

  3. Koumans EH et al. Bacterial vaginosis: risk factors and management. Obstet Gynecol. 2007;109(1):114–22.

  4. Workowski KA, Bachmann LH. Sexually transmitted infections treatment guidelines. CDC. 2021.

  5. ACOG Practice Bulletin No. 217: Prelabor Rupture of Membranes. Obstet Gynecol. 2020;135:e80–97.

  6. Sobel JD. Vulvovaginal candidiasis. Lancet. 2007;369(9577):1961–71.

  7. Lamont RF. Infection in pregnancy and its effect on the fetus. Curr Opin Infect Dis. 2015;28(3):246–52.

bottom of page