Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
25 Oktoba 2025, 12:19:03
Maumivu chini ya kitovu kwa mjamzito
Imeboreshwa:
Maumivu ya chini ya kitovu ( Maumivu ya tumbo la chini) ni malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wajawazito wanaohudhuria kliniki au wanaofika hospitali kutafuta huduma za dharura. Chanzo cha maumivu haya kinaweza kuwa cha kawaida kutokana na mabadiliko ya mwili wakati wa ujauzito, lakini wakati mwingine huashiria matatizo makubwa yanayoweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto. Kwa mama mjamzito, ni muhimu kutambua sababu mbalimbali za maumivu haya na kufanya uchunguzi wa haraka ili kupata matibabu sahihi kwa wakati.
Visababishi vya maumivu ya chini ya kitovu
Kwa ujumla, maumivu haya yanaweza kugawanywa katika makundi mawili: yale yasiyo ya hatari na yale yanayohitaji uingiliaji wa kitabibu wa haraka.
Visababishi visivyo hatari
Mvutiko wa ligamenti duara
Katika hatua ya pili ya ujauzito na kuendelea, kizazi huendelea kukua na kurefuka, na hivyo kupelekea kuvutika kwa ligamenti duara inayoshikilia kizazi(Ligamenti hii hujishikiza katika sehemu ya juu ya kizazi na sehemu ya mbele ya fupanyonga karibu na kibofu cha mkojo). Hii inaweza kusababisha maumivu ya ghafla upande mmoja wa chini ya tumbo, ambayo huchochewa na mabadiliko ya mkao au harakati.
Ujazo wa gesi na kufunga haja kubwa
Pia, kiwango kikubwa cha homoni ya projesteroni hupunguza kasi ya mfumo wa mmeng’enyo, na kusababisha kujaa gesi au kufunga choo, hali inayochangia maumivu ya tumbo.
Ukuaji wa uterasi na shinikizo la viungo vya ndani
Shinikizo kutoka kwa uterasi inayokua linaweza pia kuathiri kibofu cha mkojo, puru, na misuli ya fumbatio, na hivyo kutoa hisia za maumivu au kukosa raha sehemu ya chini ya tumbo bila uwepo wa ugonjwa wowote.
Visababishi vilivyo magonjwa
Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)
Moja ya sababu za kawaida za kitabibu ni maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), ambayo huambatana na maumivu ya suprapubic, kujikojolea mara kwa mara, na hisia ya kuungua wakati wa kukojoa. Ikiwa hayatatibiwa, yanaweza kupelekea maambukizi makubwa zaidi kwenye figo au hata uchungu wa mapema.
Uchungu kabla ya ujauzito kukomaa (Uchungu kabla ya wiki 37)
Uchungu wa leba kabla ya ujuzito kukomaa ni chanzo kingine kikuu. Hali hii hujitokeza kabla ya wiki ya 37 ya ujauzito na huambatana na maumivu ya tumbo ya mara kwa mara, kuongezeka kwa ute ukeni, au kutokwa na damu nyepesi.
Kunyofoka kwa kondo la nyuma
Wakati mwingine, maumivu huashiria kunyofoka kwa kondo la nyuma katika kuta za uzazi, hali inayojitokeza kwa ghafla, ikihusisha maumivu makali, ukakamavu wa fumbatio na kutokwa na damu ukeni. Hali hii huhatarisha maisha ya mama na mtoto na huhitaji uangalizi wa haraka.
Kondo la nyuma kujipandikiza sehemu isiyo sahihi
Mjamzito mwenye kondo lililojipanda sehemu isiyo ya kawaida anaweza kuwa na maumivu ya chini ya tumbo yanayoambatana na kutokwa na damu nyekundu ang’avu bila maumivu makali.
Kutungwa kwa mimba nje ya kizazi
Kwa upande mwingine, ikiwa mimba ipo kwenye hatua ya kwanza ya ujauzito, uwepo wa maumivu ya upande mmoja wa fumbatio pamoja na historia ya kutokwa na damu unaweza kuashiria mimba ya nje ya mfuko wa uzazi.
Kujinyongorota kwa ovari
Kujinyonga au kupasuka kwa uvimbe wa ovari ni hali nyingine inayoweza kusababisha maumivu ya ghafla, makali upande mmoja wa chini ya tumbo na huhitaji uchunguzi wa haraka kwa kutumia ultrasound.
Uchunguzi wa kitabibu
Historia ya tatizo
Historia ya kina ni ya msingi, ikijumuisha muda wa ujauzito, asili ya maumivu, muda wa kuanza, hali zinazoyaongeza au kupunguza, pamoja na dalili zinazofuatana nayo kama homa, kichefuchefu, au kutokwa na damu.
Uchunguzi wa mwili unapaswa kujumuisha vipimo vya dalili muhimu kama vile mapigo ya moyo, hali ya shinikizo la damu, kiwango cha joto la mwili, na hali ya fumbatio.
Vipimo maabara
Vipimo vya maabara kama uchunguzi kamili wa mkojo na kuotesha vimelea kwenye mkojo vinaweza kusaidia kuthibitisha maambukizi ya njia ya mkojo.
Kipimo cha picha kamili ya damu (FBC) hutathmini uwepo wa upungufu wa damu au maambukizi.
Ultrasound ya fumbatio na via vya ndani ya fupanyonga ni muhimu kutathmini hali ya kondo la nyuma, uhai wa kijusi, uwepo wa uvimbe wa ovari au kujinyongorota kwa ovari, pamoja na kuwezesha kubaini mimba ya nje ya mfuko wa uzazi.
Kwa ujauzito wa zaidi ya wiki 28, kipimo kisicho na shinikizo kwa mtoto au cha kuangalia maumbile ya mtoto vinaweza kutumika kutathmini ustawi wa mtoto tumboni.
Wakati gani wa kufika hospitali haraka?
Mjamzito mwenye maumivu ya chini ya kitovu anatakiwa kufika hospitali haraka iwezekanavyo iwapo atakutana na mojawapo ya dalili zifuatazo:
Dalili | Maelezo | Hatua Inayopendekezwa |
Maumivu makali ya ghafla upande mmoja au wote wa chini ya tumbo | Huashiria mimba ya nje ya kizazi, kunyofoka kwa kondo, au kujinyongorota kwa ovari | Fika hospitali mara moja |
Kutokwa na damu ukeni | Inaweza kuashiria hatari kwa mimba kama vile kondo kuachia au kondo kuwa chini | Fika hospitali haraka |
Kupungua au kukoma kwa harakati za mtoto | Inaashiria uwezekano wa shida kwa mtoto tumboni | Nenda hospitali haraka kwa uchunguzi wa hali ya afya ya mtoto |
Maumivu wakati wa kukojoa + kukojoa mara kwa mara | Inaashiria maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) | Fika hospitali kwa uchunguzi wa mkojo na matibabu |
Homa, kutetemeka, joto la mwili kupanda | Inaweza kuashiria maambukizi ya ndani | Nenda hospitali haraka |
Kizunguzungu, udhaifu mwingi, au kupoteza fahamu | Dalili za shinikizo la damu kushuka au upungufu wa damu | Fika hospitali mara moja |
Maumivu ya kichwa, kuona ukungu, kuvimba mwili | Inaweza kuwa preeclampsia au shinikizo la juu la ujauzito | Hudhuria kituo cha afya haraka |
Kutokwa na maji mengi ukeni kabla ya muda | Inaweza kuashiria kupasuka kwa kifuko cha majimaji ya mtoto | Wahi hospitali kwa uangalizi wa leba ya mapema |
Matibabu ya maumivu ya chini ya kitovu kwa mjamzito
Kwa maumivu ya kawaida yanayotokana na kuongezeka kwa kizazi au kunyooshwa kwaligamenti duara, elimu ya hali hiyo na kuhakikisha mjamzito anajifunza mikao bora ya kulala (hasa kulala ubavu wa kushoto), mazoezi mepesi ya kujinyoosha, na ulaji wa vyakula vyenye nyuzinyuzi husaidia kupunguza maumivu hayo.
Kwa sababu za kitabibu, tiba hutegemea chanzo. Maambukizi ya njia ya mkojo hutibiwa kwa antibayotiki salama katika ujauzito kama vile nitrofurantoin au cephalexin. Uchungu wa mapema huweza kudhibitiwa kwa dawa za kuzuia uchungu na kortikosteroid kwa ajili ya kukomaza mapafu ya kijusi. Matatizo ya kondo kama kunyofoka kwa kondo huhitaji uangalizi wa karibu, kuongezewa damu endapo ipo damu inayotoka ni nyingi, na maandalizi ya upasuaji wa haraka pale inapotakiwa. Hali kama kujinyongorota kwa ovari huhitaji upasuaji wa haraka.
Hitimisho
Ni muhimu kwa mjamzito kufahamu tofauti kati ya maumivu ya kawaida na yale yanayoashiria hatari. Kupuuza dalili hizi kunaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto. Wajawazito wote wanapaswa kuelimishwa mapema juu ya dalili hizi hatarishi na kupewa maelekezo ya wazi kuhusu lini kufika hospitali.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara
1. Habari, mimi ni mjamzito wa miezi mitatu bado siku 6 nitimize miezi minne. Napata maumivu chini ya tumbo na nasikia maumivu ukeni, halafu sijui chochote kuhusu ujauzito. Je, hali hii ni ya kawaida?
Jibu: Wakati mimba inakua, kizazi huanza kupanuka na mishipa ya fumbatio hujinyosha, hivyo mjamzito anaweza kuhisi maumivu madogo chini ya tumbo au ukeni. Hii mara nyingi si hatari ikiwa haiambatani na kutokwa damu, homa, au maumivu makali ya upande mmoja. Hata hivyo, kwa kuwa bado unaanza safari ya ujauzito, ni muhimu kuhudhuria kliniki ya wajawazito mara kwa mara ili upate elimu ya hatua za ujauzito, lishe, dalili hatarishi, na lini kufika hospitali.
2. Kwa nini maumivu ya chini ya kitovu hutokea zaidi katika miezi ya pili ya ujauzito?
3. Je, maumivu ya chini ya tumbo yanaweza kutokana na msongo wa mawazo au uchovu?
4. Je, lishe duni inaweza kuongeza hatari ya kupata maumivu ya chini ya tumbo wakati wa ujauzito?
5. Ni mkao upi bora wa kulala kwa mjamzito mwenye maumivu ya chini ya kitovu?
6. Je, ni salama kufanya mazoezi wakati nina maumivu ya chini ya tumbo?
7. Nawezaje kutambua kama maumivu ninayohisi ni kutokana na mimba ya nje ya kizazi?
8. Je, maumivu ya chini ya kitovu yanaweza kuashiria mtoto kukosa hewa tumboni?
9. Nifanye nini nikiwa na maumivu ya chini ya tumbo lakini sina uwezo wa kufika hospitali mara moja?
10. Je, maumivu ya chini ya kitovu yanaweza kuwa dalili ya kuanza leba mapema?
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeandikwa:
30 Mei 2025, 08:02:15
Rejea za dawa
Cunningham FG, Leveno KJ, Bloom SL, et al. Williams Obstetrics. 25th ed. New York: McGraw-Hill Education; 2018.
Kilpatrick SJ, Ecker JL. Severe maternal morbidity: screening and review. Am J Obstet Gynecol. 2016;215(3):B17–22. doi:10.1016/j.ajog.2016.03.042
Malhotra A, Weinberger B. Lower abdominal pain in pregnancy. In: Post TW, editor. UpToDate [Internet]. Waltham (MA): UpToDate; [cited 2025 May 29]. Available from: https://www.uptodate.com
Moore KL, Persaud TVN, Torchia MG. Before We Are Born: Essentials of Embryology and Birth Defects. 10th ed. Philadelphia: Elsevier; 2020.
Rac MW, Revell PA. Ectopic pregnancy: diagnosis and management. Am Fam Physician. 2021;104(3):165–72.
Zloto AE, Gotlieb WH, Gordon N. Ovarian torsion: diagnosis and management. Curr Opin Obstet Gynecol. 2021;33(5):338–44. doi:10.1097/GCO.0000000000000729
RCOG Green-top Guideline No. 72. Care of women presenting with suspected preterm prelabour rupture of membranes from 24+0 weeks of gestation. Royal College of Obstetricians and Gynaecologists; 2022.
Dutta DC. Textbook of Obstetrics. 9th ed. New Delhi: Jaypee Brothers Medical Publishers; 2023.
