Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Salome A, M.D, Dkt. Benjamin L, M.D
28 Julai 2026, 09:09:51
Dalili za uchungu wiki ya 36
Imeboreshwa:
Wiki ya 36 ya ujauzito umbaji wa viungo vya mtoto unakuwa umekamilika na ukuaji wa unaendelea. Uzito wake inakadiliwa kuwa kilo 2.6 na urefu wa nchi 18.7. Mtoto huonekana kama binadamu na Kama dalili za uchungu zitaonekana katika wiki hii utawekwa chini ya uangalizi wa karibu wewe na mtoto tumboni.
Katika wiki hii, mjamzito huendelea kuona dalili na maudhi mbali mbali kama vile kuishiwa pumzi au kushindwa kupumua, maumivu ya nyonga na mgongo, bawasiri, haja ngumu, kuvimba miguu n.k
Je, mtoto anakuwa amekamilika?
Hapana. Mtoto anahitaji wiki chache zaidi ili kukamilisha ukuaji wake wa ubongo, mfumo wa fahamu na mapafu ili kuzuia matatizo yanayoweza kutokea kutokana na kutokomaa kw amifumo hiyo. Licha ya kuwa hajakamilika, anaweza kuzaliwa na kuwa na afya njema.
Dalili za uchungu wiki ya 36
Si kawaida kupata uchungu katika wiki ya 36, endapo itatokea mtoto akizaliwa anaweza kuwa na afya njema hata hivyo atakuwa kwenye uangalizi maalumu kwa siku za awali. Dalili zifuatazo zinaweza kutokea;
Kujongea kwa misuli ya tumbo la chini
Kwenye wiki hii ya 36 unaweza kuhisi dalili hii kama ishara ya awali za uchungu, dalili hii humaanisha uchungu wa uongo kwa mijongeo ya misuli huwa haina mpangilio maalumu na haitokei mara kwa mara kama uchungu wa kweli.
Kuzibuka kwa kifuniko cha shingo ya kizazi
Kutokwa na makamasi mengi ukeni yanayoweza kuwa ya rangi ya maji, pinki, au kuwa na michirizi yad amu. Dalili hii ni kiashiria cha kutoka kwa kifuniko cha shingo ya kizazi ambacho huzuia vimelea kutoka ukeni kuingia kwenye kizazi.
Makamasi yanaweza kutoka kwa dakika chache, masaa au siku kadhaa kabla ya uchungu kuanza. Dalili hii huwa haigunduliwi na wanawake wengi.
Maumivu ya mgongo
Maumivu mara nyingi huwa ya mgongo wa chini yaani katika maeneo ya kiuno, ambayo huwa endelevu na huwa makali ya kutovumilika kwenye hatua za mwisho za uchungu. Maumivu haya yanahusishwa kusababishwa na mgandamizo kwenye via na mishipa ya fahamu ya mfuko wa matumbo(peritoniamu) kutokana na unaoletwa na kukua kwa kizazi.
Hisia za kujisaidia
Ni ishara ya mgandamizo kwenye matumbo na kibofu cha mkojo hivyo kupelekea hisia za kutaka kujisaidia. Hi pia humaanisha mtoto anajongea uelekeo wa kutoka nje ya kizazi kwa jina jingine mtoto kushuka. Mara nyingi hizia hizi huletwa na mgandamizo wa kichwa cha mtoto kwenye maeneo tajwa.
Kupasuka kwa chupa ya uzazi
Kati ya wanawake 10, mjamzito mmoja hupata dalili hii ambayo hutokea sana nyumbani wakati umelala. Baadhi ya nyakati chupa ya uzazi hupasuka kwenye uchungu na wakati mwingine hupasuliwa kwneye hatua ya pili ya uchungu.
Baadhi ya nyakahu huwa ni vigumu kutofautisha kati ya mkojo na maji ya chupa ya uzazi. Hata hivyo kupasuka kwa chupa ya uzazi huambatana na maji mengi yanayochuruzika kwenye mapaja kama mtu amesimama na huwa meupe, hayana harufu na hutoka mengi kwa ghafla au kuendelea kumwagika taratibu.
Kama ukipata dalili hii hakikisha kuwa si mkojo kwa kunusa, na kama ikionekana si mkojo unapaswa kuzingatia utoshiriki ngono au kutumia pedi ya kuchomeka ukeni au kufanya chochote kinachoweza kuingiza bakteria ukeni. Wakati huu onana na mtoa huduma ya afya.
Maji yakiwa na rangi tofauti na maji au harufu huweza kuashiria, maambukizi, au kuchanganyika na choo cha mtoto.
Mabadiliko ya urefu na upana wa shingo ya kizazi
Shingo ya kizazi huwa fupi na nyembamba. Hii ni ishara kwamba sehemu ya chini ya kizazi inajiandaa kwa ajili ya kutoa mtoto kwa kuwa shingo kuwa nyembamba hufanya iweze kutanuka kirahisi Zaidi. Dalili hii hupimwa na mtaalamu wa afya kwa kutia vidole viwili ukeni ili kuifikia shingo ya kizazi.
Ongezeko kipenyo cha shingo ya kizazi
Kuongezeka kwa kipenyo cha shingo ya kizazi ni dalili inayoashiria kufunguka kwa njia ya uzazi ili kichwa cha mtoto. Kizio cha kipimo hiki ni sentimita na kipenyo cha mwisho cha kutanuka ni sentimita 10. Dalili hii huwezi kuifahamu mwenyewe, mtaalamu wa afya hupima shingo ya kizazi kupitia uke kutumia vidole viwili kila baada ya masaa 2 hadi 4 ikitegemea hatua ya uchungu uliyonayo. Hatua za awali za uchungu huweza kuchukua muda kabla ya kwenda kuwa uchungu wa kujifungua
Je, ni salama kujifungua wiki ya 36
Katika kipindi hiki, unakuwa umebakisha wiki 2 hadi 4 kabla ya kujifungua. Ingawa mtoto anakuwa amekamilika uumbaji wa viungo na mifumo mingi, wakati huu mtoto huhitaji kuongezeka uzito zaidi na kuimarika kwa mfumo mfumo wa upumuaji na fahamu. Endapo uchungu utataka kutokea, daktari anaweza kuuruhusu uendelee. Baada ya kujifungua unaweza kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa masaa kadhaa kabla ya kuruhusiwa kwenye nyumbani na mwanao.
Wakati huu kama uchungu haujaanza ni vema kuepuka pia vyakula, dawa au kitu chochote kinachoweza kuamsha uchungu
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara kuhusu ujauzito wa wiki ya 36
1. Je, naweza kujifungua wiki ya 36?
Wiki ya 36 ni kipindi ambacho kujifungua kunawezekana, ingawa bado ujauzito haujafikia muda kamili (full term). Kwa mujibu wa miongozo ya kitabibu, mtoto anayezaliwa kati ya wiki ya 34 na 36 na siku 6 huitwa mtoto aliyezaliwa karibu na muda kamili. Watoto wengi wanaozaliwa katika kipindi hiki huishi na kuwa na afya nzuri, lakini bado wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata matatizo kuliko watoto wanaozaliwa kuanzia wiki ya 39 hadi 40.
Ikiwa uchungu utaanza wiki ya 36, si kila mara madaktari watajaribu kuuzuia. Uamuzi hutegemea sababu ya uchungu kuanza, afya ya mama na hali ya mtoto. Endapo kuendelea na ujauzito kunaweza kuongeza hatari kwa mama au mtoto, kujifungua kunaweza kuruhusiwa kuendelea. Baada ya kuzaliwa, mtoto atafanyiwa uchunguzi wa karibu ili kuhakikisha anapumua vizuri, anaweza kunyonya na kudhibiti joto la mwili.
Ni muhimu pia kufahamu kuwa wanawake wengi wanaopata dalili zinazofanana na uchungu katika wiki ya 36 hawajifungui siku hiyo. Baadhi hupata uchungu wa uongo au dalili za mwili kujiandaa kwa kujifungua, lakini ujauzito unaweza kuendelea kwa wiki mbili au zaidi kabla ya mtoto kuzaliwa.
2. Kama inawezekana kujifungua wiki ya 36, mbona tunaambiwa mimba ni miezi tisa wakati wiki 36 ni miezi tisa?
Swali hili huwachanganya wanawake wengi kwa sababu kuhesabu miezi ya ujauzito si sawa na kuhesabu wiki. Kwa kawaida, ujauzito wa binadamu hudumu wastani wa wiki 40, ambazo ni takribani siku 280 kuanzia siku ya kwanza ya hedhi ya mwisho. Miezi ya kalenda huwa na siku 28 hadi 31, hivyo miezi tisa ya kawaida ni takribani siku 273 hadi 275, ambazo ni chini ya wiki 40.
Ndiyo maana wataalamu wa afya hutumia wiki badala ya miezi kufuatilia ukuaji wa ujauzito, kwa sababu wiki hutoa kipimo sahihi zaidi. Ingawa watu wengi husema "mimba ni miezi tisa", kwa lugha ya kitabibu ujauzito wa muda kamili hufikia karibu miezi tisa na wiki moja. Hivyo, wiki ya 36 bado ni mapema kwa takribani wiki nne kabla ya tarehe inayokadiriwa ya kujifungua.
Kwa hiyo, mwanamke anayejifungua wiki ya 36 hajafikisha muda kamili wa ujauzito, ingawa kwa kuhesabu miezi anaweza kuonekana kuwa amefikisha miezi tisa. Tofauti hii hutokana na namna miezi na wiki zinavyohesabiwa, si kwa sababu kuna makosa katika makadirio ya ujauzito.
3. Mtoto wa wiki ya 36 akizaliwa anaweza kupumua mwenyewe?
Katika wiki ya 36, mapafu ya mtoto huwa yameendelea kukomaa kuliko yalivyokuwa katika wiki za awali, hivyo watoto wengi wanaweza kupumua wenyewe bila msaada wa mashine. Hata hivyo, mfumo wa upumuaji unaweza kuwa bado haujakomaa kikamilifu kwa baadhi ya watoto, hasa kama walizaliwa kutokana na sababu za kiafya zilizolazimisha kujifungua mapema.
Baadhi ya watoto wanaozaliwa wiki ya 36 wanaweza kupata shida ya kupumua kwa muda mfupi baada ya kuzaliwa kutokana na mapafu kutochelewa kuondoa maji yaliyokuwamo ndani yake au kutokomaa kikamilifu. Hali hizi mara nyingi hutambuliwa mapema hospitalini na kutibiwa kwa oksijeni au uangalizi maalumu hadi mtoto atakapokuwa sawa.
Kwa hiyo, ingawa watoto wengi wa wiki ya 36 hupumua wenyewe, kila mtoto huchunguzwa baada ya kuzaliwa ili kuhakikisha mfumo wa upumuaji unafanya kazi vizuri. Uangalizi huu husaidia kugundua matatizo mapema na kuanza matibabu ikiwa yatahitajika.
4. Je, mtoto wa wiki ya 36 lazima alazwe kwenye chumba cha watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (NICU)?
Si kila mtoto anayezaliwa wiki ya 36 hulazwa kwenye chumba cha watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU ya Vichanga- ICUV). Uamuzi wa kumlaza hutegemea hali ya mtoto baada ya kuzaliwa, si umri wa ujauzito pekee. Watoto wengi wanaolia vizuri, wanaopumua kawaida, wanaonyonya vizuri na wanaodhibiti joto la mwili wanaweza kubaki na mama yao wodini.
Hata hivyo, baadhi ya watoto wa wiki ya 36 wanaweza kuhitaji uangalizi maalumu kwa sababu ya uzito mdogo, kushindwa kunyonya vizuri, kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu (haipagaisemia), homa ya manjano ya watoto wachanga (neonatal jaundice) au matatizo ya kupumua. Katika hali hizo, kulazwa ICUV au chumba cha uangalizi maalumu husaidia mtoto kupata matibabu na ufuatiliaji unaohitajika.
Kwa wazazi, kulazwa kwa mtoto ICUV hakumaanishi kuwa mtoto ana tatizo la kudumu. Mara nyingi ni hatua ya kuhakikisha mtoto anaanza maisha katika mazingira salama hadi atakapokuwa tayari kurudi kwa mama na kuendelea na ukuaji wa kawaida.
5. Je, maumivu ya tumbo yanayokatika katika wiki ya 36 ni uchungu wa kweli au wa uongo?
Katika wiki ya 36, wanawake wengi huanza kuhisi tumbo likikaza au maumivu yanayokuja na kupotea. Hata hivyo, si kila maumivu yanamaanisha kuwa uchungu wa kujifungua umeanza. Katika kipindi hiki ni kawaida kupata uchungu wa uongo (Mikazo ya Braxton), ambao ni mikazo ya misuli ya kizazi inayosaidia kuandaa mwili kwa ajili ya kujifungua. Mikazo hii mara nyingi haina mpangilio maalumu, haitokei kwa vipindi vinavyofanana na mara nyingi hupungua ukibadilisha mkao, ukitembea au ukinywa maji.
Kwa upande mwingine, uchungu wa kweli huanza kuwa na mpangilio maalumu. Maumivu huja kwa vipindi vinavyofanana, huongezeka taratibu kwa nguvu na muda wake huwa mrefu zaidi kadiri muda unavyoenda. Tofauti na uchungu wa uongo, maumivu haya hayaishi kwa kubadilisha mkao au kupumzika, na mara nyingi huambatana na mabadiliko ya shingo ya kizazi kama kufupika na kutanuka.
Ikiwa maumivu yanatokea kila dakika 5 hadi 10 kwa zaidi ya saa moja, yanaongezeka kwa nguvu, unaona maji ya chupa ya uzazi yamepasuka au unatokwa na damu nyingi, usisubiri nyumbani. Nenda hospitali au kituo cha afya mara moja ili uchunguzwe na mtaalamu wa afya, kwa sababu dalili hizi zinaweza kuashiria uchungu wa kujifungua umeanza.
6. Mtoto akipungua kucheza wiki ya 36 nifanye nini?
Kadiri ujauzito unavyokaribia mwisho, nafasi ndani ya mfuko wa uzazi hupungua kwa sababu mtoto huwa amekua zaidi. Hivyo, aina ya michezo ya mtoto inaweza kubadilika; badala ya kupiga mateke makubwa unaweza kuhisi kujinyoosha, kujigeuza au kusukuma taratibu. Hata hivyo, idadi ya miondoko haipaswi kupungua sana ghafla.
Ikiwa unaona mtoto hachezi kama kawaida, jaribu kwanza kukaa au kulala ubavu wa kushoto katika sehemu tulivu na uhesabu miondoko yake. Wanawake wengi huhisi angalau miondoko 10 ndani ya saa mbili, ingawa watoto wengine hufikisha idadi hiyo ndani ya muda mfupi zaidi. Pia unaweza kula chakula chepesi au kunywa maji kabla ya kuanza kuhesabu, kwani watoto wengine huongezeka kucheza baada ya mama kula.
Usipoona miondoko ya kutosha au mtoto ameacha kabisa kucheza, usisubiri hadi siku inayofuata. Nenda hospitali siku hiyo hiyo ili afya ya mtoto ichunguzwe. Kupungua kwa miondoko kunaweza kuwa ishara kwamba mtoto anahitaji uchunguzi wa haraka, hata kama mama anajisikia vizuri.
7. Je, ni salama kufanya tendo la ndoa katika wiki ya 36 ya ujauzito?
Kwa wanawake wengi wenye ujauzito unaoendelea kawaida bila matatizo, kufanya tendo la ndoa katika wiki ya 36 kunaweza kuwa salama ikiwa daktari au mtoa huduma wa afya hajakushauri vinginevyo. Tendo la ndoa kwa kawaida halimdhuru mtoto kwa sababu mtoto analindwa na mfuko wa uzazi, maji ya uzazi na mlango wa kizazi ambao hubaki umefungwa kabla ya uchungu kuanza.
Hata hivyo, kuna hali ambazo tendo la ndoa halishauriwi katika kipindi hiki. Mfano ni pale ambapo maji ya chupa ya uzazi yamepasuka, kuna kutokwa na damu ukeni bila sababu inayojulikana, mlango wa kizazi umeanza kufunguka mapema, kuna kondo la nyuma lililofunika mlango wa kizazi (placenta previa), au daktari amekuambia uko kwenye hatari ya kujifungua kabla ya wakati. Katika hali hizi, tendo la ndoa linaweza kuongeza hatari ya maambukizi au matatizo mengine.
Ikiwa baada ya tendo la ndoa utapata maumivu yanayoendelea, kutokwa na damu nyingi, maji mengi kutoka ukeni au kupungua kwa miondoko ya mtoto, unapaswa kufika hospitali haraka kwa uchunguzi. Ikiwa ujauzito wako una matatizo yoyote, ni vyema kumuuliza mtoa huduma wa afya kama ni salama kuendelea na tendo la ndoa katika wiki hii.
8. Je, nikianza kutoka ute mzito wiki ya 36 inamaanisha nitajifungua siku hiyo?
Kutokwa na ute mzito wa ukeni katika wiki ya 36 kunaweza kuwa ishara kwamba kifuniko cha shingo ya kizazi (kamasi nzito ya shingo ya kizazi) kimeanza kutoka. Kifuniko hiki hutengenezwa mapema katika ujauzito na husaidia kuzuia bakteria na vijidudu wengine kuingia ndani ya mfuko wa uzazi. Kinaweza kutoka kwa wakati mmoja au kidogo kidogo, na ute unaweza kuwa wa uwazi, mweupe, wa pinki au wenye michirizi midogo ya damu.
Hata hivyo, kutoka kwa ute huu hakumaanishi kuwa kujifungua kutaanza siku hiyo hiyo. Kwa baadhi ya wanawake, uchungu huanza ndani ya saa chache, lakini kwa wengine unaweza kuanza baada ya siku kadhaa au hata wiki moja au zaidi. Kwa hiyo, ute pekee hauwezi kutumika kutabiri siku halisi ya kujifungua.
Ikiwa ute unaambatana na uchungu wenye mpangilio, kupasuka kwa chupa ya uzazi au kutokwa na damu nyingi kama hedhi, ni muhimu kwenda hospitali kwa uchunguzi. Lakini kama umetoka ute pekee bila dalili nyingine, unaweza kuendelea kufuatilia hali yako huku ukiwa tayari kwa dalili za kujifungua.
9. Je, kusafiri kwa basi au pikipiki katika wiki ya 36 ya ujauzito ni salama?
Katika wiki ya 36, wanawake wengi bado wanaweza kusafiri ikiwa ujauzito unaendelea kawaida na hakuna tatizo la kiafya lililogunduliwa. Hata hivyo, kipindi hiki ni karibu sana na muda wa kujifungua, hivyo safari ndefu zinahitaji tahadhari zaidi kuliko ilivyokuwa katika miezi ya awali ya ujauzito. Kadiri ujauzito unavyokaribia mwisho, uwezekano wa uchungu kuanza au chupa ya uzazi kupasuka huongezeka, hata kama hakukuwa na dalili kabla ya safari.
Safari za muda mrefu kwa basi au gari zinaweza kuongeza uchovu, kuvimba miguu na hatari ya kuganda kwa damu kwenye mishipa ya miguu. Ikiwa ni lazima kusafiri, ni vyema kusimama mara kwa mara ili kutembea kwa dakika chache, kunywa maji ya kutosha na kufunga mkanda wa usalama kwa usahihi, ambapo sehemu ya chini ya mkanda hupita chini ya tumbo na sehemu ya juu ipite kati ya matiti. Kwa upande wa pikipiki, hatari ya ajali ni kubwa zaidi kutokana na mtikisiko na ukosefu wa ulinzi wa kutosha, hivyo si njia inayopendekezwa hasa kwa safari ndefu au kwenye barabara zenye mashimo.
Kama una historia ya kujifungua kabla ya wakati, shinikizo la damu la ujauzito, kutokwa na damu ukeni, kupungua kwa miondoko ya mtoto, mapacha au dalili zozote za uchungu, ni muhimu kuzungumza na mtoa huduma wa afya kabla ya kupanga safari. Ikiwa safari si ya lazima, wanawake wengi hushauriwa kubaki karibu na kituo cha afya katika wiki za mwisho za ujauzito ili waweze kupata huduma haraka endapo uchungu utaanza.
10. Ni dalili zipi katika wiki ya 36 zinahitaji kwenda hospitali mara moja?
Ingawa maumivu madogo ya mgongo, kukaza kwa tumbo mara chache na kuongezeka kwa uchovu ni mambo yanayoweza kutokea kawaida katika wiki ya 36, kuna dalili ambazo hazipaswi kupuuzwa kwa sababu zinaweza kuashiria tatizo linalohitaji matibabu ya haraka. Kutambua dalili hizi mapema kunaweza kusaidia kulinda afya ya mama na mtoto.
Unapaswa kwenda hospitali mara moja ikiwa utapata uchungu wenye mpangilio unaozidi kuongezeka, kupasuka kwa chupa ya uzazi, kutokwa na damu nyingi ukeni, kupungua au kutokuwepo kabisa kwa miondoko ya mtoto, maumivu makali ya tumbo yasiyoisha, homa, au kutokwa na majimaji yenye harufu mbaya. Pia, dalili kama maumivu makali ya kichwa, kuona ukungu au mwanga unaomulika machoni, kuvimba ghafla usoni au mikononi, maumivu makali chini ya mbavu upande wa kulia na kushindwa kupumua vinaweza kuashiria shinikizo la damu la ujauzito (preeclampsia), ambalo ni hali inayohitaji matibabu ya haraka.
Usisubiri kuona kama dalili zitaisha zenyewe ikiwa una mashaka kuhusu afya yako au ya mtoto. Ni salama zaidi kufika hospitali na kukutwa kila kitu kiko sawa kuliko kuchelewa kufika wakati kuna tatizo linalohitaji matibabu ya haraka. Katika wiki ya 36, uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kuzuia madhara makubwa kwa mama na mtoto.
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeandikwa:
21 Julai 2023, 13:45:50
Rejea za dawa
Pregnancy week by week. Week 35. https://www.thebump.com/pregnancy-week-by-week/37-weeks-pregnant. Imechukuliwa 20.07.2023
Hutchison J, et al. Stages of Labor. 2023 Jan 30. In: StatPearls [Internet]. Treasure Island (FL): StatPearls Publishing; 2023 Jan–. PMID: 31335010.
Melzack R, et al. Low-back pain during labor. Am J Obstet Gynecol. 1987 Apr;156(4):901-5. doi: 10.1016/0002-9378(87)90349-8. PMID: 2953242.
Signs and Symptoms of Labor. https://americanpregnancy.org/healthy-pregnancy/labor-and-birth/signs-of-labor/. Imechukuliwa 18.07.2023
William’s Obstetrics Twenty-Second Ed. Cunningham, F. Gary, et al, Ch. 17.
NHS. Pregnancy signs. https://www.nhs.uk/pregnancy/labour-and-birth/signs-of-labour/signs-that-labour-has-begun/. Imechukuliwa 18.07.2023
Cleveland clinic. 8 Signs That Labor Is 24 to 48 Hours Away. https://www.google.com/search?q=labor+symptoms&client. Imechukuliwa 18.07.2023
NCBI. Stages of labor. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK544290/#:. Imechukuliwa 18.07.2023
