Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Sospeter B, MD
9 Julai 2026, 12:39:23
Kujifungua kwa upasuaji: Mwongozo kamili
Imeboreshwa:
Kujifungua kwa upasuaji katika makala hii imetumika kumaanisha neno tiba caesarian delivery, ambacho ni kitendo cha kuchana kuta za tumbo na uzazi ili kutoa mtoto aliye kwenye mji wa mimba. Kitendo hiki hufahamika pia kama kuzaa kwa upasuaji au upasuaji wa kujifungua.
Kuna sababu mbalimbali zinaweza kuchangia mwanamke kujifungua kwa upasuaji, hata hivyo kujifungua kwa njia hii huweza kupangwa kabla ya uchungu kutokea au wakati wa uchungu endapo kuna ishara zimetokea zinazokufanya ushindwe kujifungua kwa njia ya kawaida.
Endapo wewe ni mjamzito unapaswa kufahamu njia za kujifungua ili uweze kufanya maamuzi sahihi wa njia gani sahihi na kwa nini njia hiyo itumike wakati wa kujifungua.
Sababu zinazofanya mtu ajifungue kwa upasuaji;
Zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kupelekea mwanamke akajifungua kwa njia ya upasuaji ambazo ni zimegawanyika katika makundi yafuatayo
1. Sababu zinazotokana na uchungu kutosonga au kuzuiwa
Kutoendelea kwa uchungu
Nyonga ndogo isiyoruhusu mtoto kupita
Kichwa kikubwa cha mtoto (mfano: Kichwa maji)
Kizuizi kwenye njia ya uzazi, kama faibroid kubwa
Plasenta previa (kondo la nyuma kujipandikiza karibu na mlango wa uzazi)
Kondo kunyofoka (abruptio plasentaa)
Kitovu kutangulia
2. Sababu zinazotokana na mtoto
Mtoto kuchoka
Mtoto kulala vibaya (kutanguliza makalio, kulala mshazali, kutanguliza mabega)
Matatizo ya ukuaji wa mtoto, mfano uzito mkubwa kupita kiasi (makadirio ya uzito kuwa mkubwa)
Mimba ya mapacha, hasa kama mtoto wa kwanza hayuko kwenye nafasi sahihi
3. Sababu zinazotokana na mama
Shinikizo la juu la damu linaloelekea kifafa cha mimba (Pre-eklampsia kali)
Kifafa cha mimba (Eklampsia)
Historia ya upasuaji uliopita isiyoruhusu TOLAC/VBAC
Magonjwa ya moyo au kupumua yanayofanya uchungu kuwa hatari
Ujauzito wa kipekee (mtoto wa kipekee) — kulingana na tathmini ya daktari
Ombi la mama — hufanyika baada ya ushauri na tathmini ya kitaalamu
Maelezo zaidi ya kila kisababishi cha kujifungua kwa upasuaji ni yameelezewa hapa chini;
i. Kutoendelea vema kwa uchungu
Kutoendelea au kusimama kwa uchungu ni moja ya sababu kubwa inayopelekea wamama wengi wajifungue kwa upasuaji. Uchungu ukisimama au kutoendelea kama inavyotakiwa hupelekea shingo ya kizazi kutofunguka na hivyo mtoto kutoweza kutoka. Daktari au nesi kwa kawaida huangalia hali ya shingo ya kizazi kila baada ya masaa manne au pungufu yake ikitegemea mwitikio wake dhidi ya uchungu kwa kuingiza vidole viwili kupitia uke. Kwa kufanya hivi huweza kutambua hali yake ikoje na imetanuka kwa sentimita ngapi. Njia hii ni njia mojawapo ya kuangalia maendeleo ya uchungu.
ii. Mtoto kuchoka
Kitiba hufahamika kwa jina la fetal distress, hali hii hugunduliwa endapo mapigo ya moyo ya mtoto yameshuka au yamepanda juu ya kiwango cha kawaida ambacho hupimwa kwa kifaa maalumu kinachowekwa kwenye tumbo. Kiwango cha kawaida cha mapigo ya moyo wa mtoto huwa kati ya midundo 110 hadi 160 kwa dakika (110-160b/min).
iii. Mtoto kulala vibaya kndani ya kizazi
Kwa kawaida mtoto anatakiwa kutanguliza kichwa kabla ya mwezi wa mwisho wa kujifungua. Endapo mtoto ametanguliza matako au mabega au amelala mshazari badala ya kutanguliza kichwa, daktari atakuambia mtoto amelala vibaya hivyo utajifungua kwa upasuaji. Kuna baadhi ya milalo ya mtoto inaweza kufanyiwa kazi ili kufanya mtoto alale kwa kutanguliza kichwa, hata hivyo endapo juhudi zitaferi utatakiw akujifungua kwa upasuaji.
iv. Kuwa na mimba ya mapacha au zaidi
Kuwa na mimba ya mapacha si kigezo pekee cha kujifungua kwa njia ya upasuaji hata hivyo sababu zinazoweza kukufanya ujifungue kwa upasuaji unapokuwa na mimba ya mapacha huwa pamoja na; mtoto wa kwanza kutanguliza makalio au kulala vibaya na kuwa na mimba ya watoto zaidi ya wawili.
v. Kondo la nyuma kujishikiza karibu na kizazi
Kitiba huitwa placenta previa, hii hutokea pale endapo kondo la nyuma limejishikiza karibu na shingo ya kizazi, hutajifungua kwa njia hii kwa sababu mtoto atashindwa kupita vema au atakandamiza kondo hilo. Kondo la nyuma huwa na kazi ya kuingiza virutubisho kwa mtoto, kumpa hewa safi ya oksijen na kuondoa hewa chafu ya carbon dioxyside. Endapo kondo hilo limetangulia au limejishikiza kwenye shingo ya kizazi ni rahisi kunyofoka au kukandamizea wakati wa mtoto anapita na kupelekea mtoto kukosa hewa na kufa.
vi. Kunyofoka kwa kondo la nyuma
Endapo kondo la nyuma limenyofoka lote au sehemu kidogo tu kutoka kwenye ukuta wa kizazi, daktari ataamua ufanyiwe upasuaji haraka ili kuokoa maisha ya mtoto. Sababu ya upasuaji ni ile ile kwamba mtoto huwa anakosa virutubisho na hewa safi ya oksijeni ambayo inamsaidia kuishi. Kuchelewa kufanya upasuaji kutasababisha mtoto kuzaliwa amechoka au kufia tumboni.
vii. Kutangulia kwa kitovu cha mtoto
Endapo kitovu cha mtoto kimetangulia mbele ya uke kabla ya mtoto hii itakuwa ni sababu ya kufanyiwa upasuaji wa kujifungua. Hii ni kwa sababu ya hofu ya mtoto kukandamiza kondo hilo wakati anapita kwenye tundu la uzazi, sababu hii inaweza kupelekea kifo cha mtoto.
viii. Kuwa na nyonga ndogo
Endapo nyonga yako ni ndogo au imekakamaa ikimaanisha haiwezi kufunguka ili kuruhusu mtoto kupita kirahisi, daktari ataamua kukufanyia upasuaji wa kumwondoa mtoto. Hali hii ya kuwa na nyonga ndogo hutambulika kabla ya uchungu kuanza wakati unaenda kuhudhuria kliniki. Hata hivyo endapo umefika wakati wa uchungu, daktari au nesi atakupima kuangalia uwezo wa nyonga yako.
ix. Kizuizi kwenye njia ya uzazi
Endapo kuna kizuizi katika kizazi kinachosababisha mtoto asipite kirahisi, kwa mfano kuwa na fibroid kubwa, au mtoto kuwa na kichwa kikubwa mfano mtoto mwenye kichwa maji, daktari atakushauri ujifungue kwa upasuaji ili kukuokoa wewe na mtoto.
x. Kuwa na historia ya upasuaji kwenye ujauzito uliopita
Unaweza kufanyiwa upasuaji kwa ujauzito wa sasa endapo ujauzito uliopita ulifanyiwa upasuaji endapo sababu iliyosababisha kufanyiwa upasuaji imejirudia au kuwepo kwa sababu zingine ambazo zinaongeza hatari yaw ewe kujifungua kwa upasuaji. Mama aliyejifungua kwa upasuaji ujauzito mmoja uliopita anaweza kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida endapo Hakuna sababu kama ile ya awali,kovu lake limepona vema na sababu zingine endapo zipo vizuri ambazo zimeelezewa kwenye Makala nyingine ndani ya tovuti hii.
xi. Mtoto wa kipekee
Endapo ujauzito huu ni wa kipekee, ikinamaanisha mtoto uliyenaye ndo mtoto wa kwanza na umekuwa ukimtafuta baada ya muda mrefu sana hii inaweza kuwa sababu ya wewe kufanyiwa upasuaji ili kuhakikisha kwamba mama na mtoto hawapati madhara wakati wa kujifungua. Hii hufanyika kwa wanawake wenye mimba ya kwanza kwenye umri mkubwa sana mfano wenye umri Zaidi ya miaka 35, wanawake waliokuwa na matatizo ya mimba kutoka au kuharibika wakati wa kujifungua. Hata hivyo njia hii haishauriwi endapo una mpango wa kuwa na watoto wengi zaidi
xii. Shinikizo la damu linaloelekea kifafa cha mimba
Shinikizo la damu linaloelekea kifafa cha mimba ni hali ambapo mama ana shinikizo la damu lililopanda kupita kiasi pamoja na dalili hatarishi kama kuumwa kichwa kupita kawaida, matatizo ya kuona, maumivu makali ya juu upande wa kulia wa tumbo, au kupungua kwa mkojo. Kwa kuwa hali hii inaweza kuathiri kazi za ini, figo na mtiririko wa damu kwenye kondo la nyuma, daktari anaweza kupendekeza kujifungua kwa upasuaji endapo mama au mtoto yuko katika hatari, au ikiwa shingo ya kizazi haijafunguka na kuruhusu kujifungua kwa njia ya kawaida. Upasuaji husaidia kuzuia madhara makubwa na kuokoa maisha ya mama na mtoto.
xiii. Kifafa cha mimba
Kifafa cha mimba au Eklampsia ni hatua mbaya ya shinikizo la mimba ambapo mama hupata degedege (seizures), na hii ni dharura ya kitabibu. Mshtuko unaweza kuzuia mtiririko wa damu kwenda kwa mtoto na pia kumweka mama kwenye hatari ya kupata kiharusi, kuharibika kwa ini, au kupoteza fahamu. Katika hali hii, upasuaji mara nyingi huwa njia salama zaidi ya kujifungua, hasa pale shingo ya kizazi haijafunguka au mshtuko unaendelea. Lengo ni kumaliza ujauzito haraka na salama ili kulinda afya ya mama na mtoto.
xiv. Ombi la mama
Mama mjamzito anaweza kuomba afanyiwe upasuaji endapo anahitaji kutokana na sababu binafsi. Daktari anaweza kuamua kumsikiliza mgonjwa na kumshauri njia salama kulingana na ombi la mama. Hata hivyo njia hii haishauriwi endapo una mpango wa kuwa na watoto wengi zaidi
Je, kuna sababu zingine za kujifungua kwa upasuaji?
Ndiyo. Mbali na sababu kuu zinazojulikana kama mtoto kulala vibaya, uchungu kusimama, au shinikizo la damu, kuna sababu nyingine za ziada ambazo huweza kumlazimu daktari kupendekeza upasuaji ili kulinda afya ya mama na mtoto. Sababu hizi hutokea kulingana na hali ya ujauzito, magonjwa ya mama, au changamoto za ghafla zinazoibuka wakati wa ujauzito au uchungu. Jedwali 1 linaonyesha kwa ufupi sababu hizi za ziada na namna zinavyoathiri uamuzi wa kitabibu.
Jedwali 1: Sababu za Ziada Zinazoweza Kuletea Upasuaji wa Kujifungua
Sababu ya Ziada | Maelezo Mafupi |
1. Magonjwa makubwa ya moyo au kupumua | Mama hawezi kustahimili msongo wa uchungu, hivyo upasuaji huwa salama zaidi kwake na mtoto. |
2. Maambukizi ya sehemu za siri (mfano: herpes) | Hatari ya mtoto kupata maambukizi makali yakipitia njia ya uke, hivyo upasuaji hupendekezwa. |
3. Uharibifu wa kizazi au nyonga kutokana na upasuaji/ajali | Mfano: upasuaji mkubwa wa faibroidi uliogusa ukuta wa ndani wa kizazi; inaweza kuzuia uchungu wa kawaida. |
4. Kutokwa damu nyingi kabla ya kujifungua | Ni dharura. Upasuaji hufanyika kuokoa maisha ya mama na mtoto. |
5. Maji kidogo sana kwenye chupa ya uzazi (oligohydramnios kali) | Inaweza kusababisha mtoto kuchoka haraka ndani ya tumbo. |
6. Mama mwenye kupooza au matatizo makubwa ya uti wa mgongo | Uchungu unaweza kuongeza ulemavu au kuwazaidia mama kupata maumivu makali yasiyodhibitika. |
7. Mimba kupitiliza muda + dalili za hatari | Mtoto anaweza kuonyesha dalili za kuchoka hivyo upasuaji kuwa salama zaidi. |
Hatari ya kufanyiwa upasuaji ni nini?
Kama ilivyo sawa na upasuaji wa aina nyingine, mama anayefanyiwa upasuaji kwa ajili ya kujifungua huwa kwenye hatari ya matatizo yafuatayo;
Kujeruhiwa wakati wa upasuaji
Ingawa ni kwa nadra sana nja ni kwa bahati mbaya, mama anaweza kujeruhiwa katika sehemu yoyote ya tumbo, mirija ya mikojo. Mtoto pia anaweza kujeruhiwa, kuna baadhi ya watoto huweza kukatwa ngozi sehemu yoyote ya mwili lakini ni kwa nadra sana nah ii hutegemea uzoefu pia wa daktari.
Mtoto kupata matatizo ya upumuaji
Watoto wanaozaliwa kwa njia hii hupata kipindi cha mpito cha kupumua haraka haraka kinachodumu kwa siku chache baada ya kujifungua.
Hatari zingine ni pamoja na;
Mama kupata maambukizi kwenye kuta za kizazi
Kutokwa na damu nyingi baada ya upasuaji
Kuganda kwa damu ndani ya mishipa ya damu haswa kwenye mishipa ya miguu na viungio ndani ya nyonga. Endapo damu iliyoganda itanyofoka na ksuafiri kwenda kwenye mapafu mgonjwa atapata tatizo la pulmonary embolism.
Maambukizi kwenye kidonda cha upasuaji, hutokea endapo kidonda hakitunzwi vema na kutiwa maji
Kupata hatari ya kujifungua kwa upasuaji ujauzito zinazofuata
Kutokwa na damu nyingi
Hatari za muda mrefu ni
Kupata kovu baya kwenye eneo la mshono
Baadhi ya wanawake wanaweza kupata kovu lisiloonekana vizuri katika eneo la mshono wa upasuaji. Hali hii hutegemea jinsi upasuaji ulivyofanyika, mbinu ya daktari aliyetumia kushona kidonda, pamoja na aina ya ngozi ya mama. Watu wenye mwelekeo wa kutengeneza makeloid wana uwezekano mkubwa wa kupata kovu lililoinuka au lililokua zaidi ya kawaida katika eneo hilo.
Kuchanika kwa Kizazi kwenye Ujauzito Unaofuata
Katika ujauzito unaofuata, kuna hatari ndogo ya mshono wa zamani kwenye kizazi kuchanika—hali inayojulikana kitaalamu kama kupasuka kwa kizazi. Hatari hii hutokea zaidi wakati mama anajaribu kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya kufanyiwa upasuaji wa awali. Ndiyo sababu daktari hufuatilia maendeleo ya ujauzito na uchungu kwa umakini ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.
Maandalizi ya kufanya kabla ya kujifungua
Endapo utafanyiwa upasuaji, utakuwa umeandaliwa tayari kwa kuzungumza na mtu wa usingizi kisha kusaini conset form ambayo unaweza kuisaini wewe kama unajitambua au ndugu yako wa karibu endapo hujitambui.
Utafanyiwa pia vipimo vya damu ili kuangaliwa wingi wa damu pamoja na kundi la damu yako ili endapo kutatokea shinda baada ya upasuaji uongezewe damu kiurahisi na hata hivyo kuweza kumsaidia daktari wako kupima kipimo cha kuchunguza wingi wa damu siku kadhaa baada ya kujifungua. Endapo hospitali ina upungufu wa damu unaweza kuombwa kuleta ndugu wa kuchangia damu
Baada ya upasuaji utatakiwa kupata muda wa kupumzika nyumbani kwa wiki kadhaa ili kupona. Hakikisha unafanya maandalizi mapema kupata mtu wa kuweza kukutunza wiki kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Kabla ya kufanyiwa upasuaji nini hufanyika?
Kabla ya kufanyiwa upasuaji utafanyiwa mambo yafuatayo
Utawekewa catheter kwenye mshipa wa damu ili kuongezewa maji kabla au wakati upasuaji uanendelea
Utawekewa mpita wa mkojo ili kukusanya mkojo katika kipindi cha upasuaji na wakati ukiendelea kupona wodini
Utachomwa sindano ya kaputi kisha kulazwa kwenye kitanda cha upasuaji. Wakati mwingine inaweza ikahitajika kuchomwa sindano ya kaputi ambapo utakuwa hutambui nini kinachoendelea mpaka utakapoamka
Utasafishwa tumbo lako katika eneo ambalo litafanyiwa upasuaji kisha
Utavalishwa nguo maalumu kwenye eneo ambalo litafanyiwa upasuaji
Utafanyiwa upasuaji wa kuondoa mtoto na baada ya mtoto kutoka utapewa mtoto umuone jinsia yake na sura kisha kwenda kusafishwa na nesi wakati daktari akiendelea kufunga sehemu aliyochana kutoa mtoto
Baada ya upasuaji kufanyika
Baada ya kufanyiwa upasuaji, utakaa kidogo kwa siku chache (kati ya siku 2 hadi 3) kulingana na utakavyoshauriwa na daktari wako. Utashauriwa pia baada ya madhara ya dawa za usingizi kuisha kuanza kufanya mazoezi, kunywa maji ya kutosha pamoja na kula vyakula laini ili kuzuia kupata haja ngumu na kuganda kwa damu mwilini.
Utafundishwa pia namna ya kunyonyesha mtoto mara moja baada ya kurejea kwenye hali yako nzuri baada ya upasuaji.
Unapokuwa nyumbani nini cha kufanya?
Mara baada ya kufanyiwa upasuaji, utakuwa ukipata maumivu sehemu ya mshono lakini usiwe na hofu unatakiw akufanya mambo yafuatayo
Pumzika na weka vitu ambavyo utakuwa unavihitaji karibu nawe ili usipate kazi ya kuvifikia kwa shida. Usinyanyue vitu vizito kutoka kwenye pozi la kuchuchumaa.
Tumia dawa za maumivu kama ulivyopewa na daktari wako ili kupunguza maumivu, unaweza kujikanda pia kwa chupa ya maji moto.
Usifanye ngono kipindi hiki wakati unasubiria kupona angalau kwa wiki sita toka umefanyiwa upasuaji
Usiendweshe gari kwa kipindi hiki chote mpaka upone
Usifanye mazoezi mazito pia kwa kipindi cha wiki sita au mpaka utakaposhauriwa na daktari wako ili kuepuka mshono kufumuka
Jambo jingine muhimu ni nini?
Endapo utaona dalili zifuatazo hakikisha unawasiliana na daktari wako kwa sababu huwa ni dalili za hatari na zinahitaji maamuzi ya dharura;
Kubadilika rangi kwa kidonda, kuvimba na kutoa usaha au majimaji yasiyo ya kawaida
Kupatwa na homa
Kutokwa na damu nyingi ukeni
Kuongezeka kwa maumivu ya msono
Kutokuwa na furaha, msongo wa mawazo na hisia mbaya dhidi ya mwanao, kutaka kumdhuru mwanao.
Dalili za hatari zinazokupasa uwasilian na Daktari haraka
1. Mabadiliko Yasiyo ya Kawaida kwenye Kidonda cha Upasuaji
Ikiwa utagundua uvimbe, rangi ya zambarau au uwekundu mkali, joto kupita kiasi, upele, au kutoa usaha, hii inaweza kuashiria maambukizi yanayohitaji matibabu ya haraka.
2. Homa au baridi kali
Kupanda kwa joto la mwili baada ya upasuaji kunaweza kuwa ishara ya maambukizi kwenye kizazi, kwenye kidonda, au kwenye mfumo wa mkojo. Ni muhimu kuripoti dalili hizi mapema.
3. Kutokwa na damu nyingi ukeni
Endapo damu itatoka kwa wingi kuliko kawaida, au ikawa na harufu isiyo ya kawaida, hii inaweza kuashiria tatizo kwenye kizazi au kwenye kondo la nyuma.
4. Kuongezeka kwa maumivu badala ya kupungua
Maumivu yanapaswa kupungua kadri unavyopona. Maumivu yanayoendelea kuongezeka yanaweza kuashiria maambukizi au tatizo kwenye mshono wa ndani.
5. Mabadiliko ya hisia na Afya ya Akili
Ikiwa unahisi kutokuwa na furaha, kuwaza mno, kupoteza hamasa, msongo mkali wa mawazo, au kutokuwa karibu na mtoto, inaweza kuwa dalili za Sonona ya uzazi. Hali hii inahitaji ushauri na msaada wa kitaalamu mapema.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Nilijifungua kwa upasuaji miaka miwili iliyopita kutokana na preeklampsia kali. Sasa nina mimba tena. Je, ninaweza kujifungua kawaida, na je presha inaweza kurudi?
Historia ya kufanyiwa upasuaji kutokana na preeklampsia kali haimaanishi moja kwa moja kuwa utahitaji upasuaji tena. Njia ya kujifungua katika ujauzito wa sasa hutegemea mambo mbalimbali, ikiwemo aina ya kovu la upasuaji uliopita, sababu iliyosababisha upasuaji wa kwanza, afya yako kwa sasa, ukuaji wa mtoto, pamoja na hali ya kizazi chako wakati wa uchungu. Wanawake wengi wanaweza kupewa nafasi ya kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya upasuaji (VBAC) ikiwa hakuna sababu zinazoongeza hatari.
Kwa upande wa preeklampsia, ni kweli kuwa mwanamke aliyewahi kuipata ana uwezekano mkubwa zaidi wa kuipata tena kuliko ambaye hajawahi kuugua. Hata hivyo, si kila mwanamke atapata tena. Hatari hutegemea mambo kama umri, uzito, shinikizo la damu kabla ya ujauzito, kisukari, magonjwa ya figo, na muda ambao preeklampsia ilianza katika ujauzito uliopita.
Ni muhimu kuhudhuria kliniki mapema na mara kwa mara ili shinikizo la damu lifuatiliwe, vipimo muhimu vifanyike, na kama inahitajika, daktari anaweza kuanzisha dawa kama aspirin ya dozi ndogo kwa wanawake wenye hatari kubwa. Kufuatilia afya yako kwa karibu husaidia kugundua matatizo mapema na kupanga njia salama zaidi ya kujifungua.
2. Je, kila mwanamke aliyewahi kujifungua kwa upasuaji lazima afanyiwe upasuaji tena?
Hapana. Wanawake wengi waliowahi kujifungua kwa upasuaji wanaweza kujifungua kwa njia ya kawaida katika ujauzito unaofuata ikiwa wanakidhi vigezo vya usalama. Hali hii huitwa kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya upasuaji (VBAC). Uamuzi huu hufanywa na daktari baada ya kutathmini sababu ya upasuaji uliopita, aina ya kovu kwenye kizazi, idadi ya upasuaji uliowahi kufanyiwa, pamoja na maendeleo ya ujauzito wa sasa.
Iwapo sababu ya upasuaji wa kwanza haipo tena, kwa mfano mtoto alikuwa amekaa vibaya au alikuwa mkubwa sana, unaweza kuwa na nafasi nzuri ya kujifungua kawaida. Hata hivyo, kama una makovu mengi kwenye kizazi, kovu lisilo salama, au matatizo mengine ya ujauzito, daktari anaweza kupendekeza upasuaji wa kurudia.
Ni muhimu kutofanya uamuzi huu mwenyewe. Daktari ndiye atakayekueleza faida na hatari za kila njia ya kujifungua kulingana na hali yako binafsi.
3. Upasuaji wa kujifungua huchukua muda gani?
Kwa kawaida upasuaji wa kujifungua huchukua dakika 30 hadi 60, ingawa muda unaweza kutofautiana kulingana na hali ya mama na mtoto. Mara nyingi mtoto hutolewa ndani ya dakika 5 hadi 15 za mwanzo wa upasuaji, huku muda uliobaki ukitumika kushona kizazi, misuli na ngozi kwa usalama.
Iwapo ni upasuaji wa dharura au mama amewahi kufanyiwa upasuaji wa tumbo mara kadhaa, muda unaweza kuongezeka kutokana na uwepo wa makovu au changamoto nyingine zinazohitaji uangalizi zaidi.
Baada ya upasuaji utakaa kwenye chumba cha uangalizi kwa saa chache ili wahudumu wa afya wafuatilie shinikizo la damu, mapigo ya moyo, kiwango cha damu kutoka ukeni, maumivu, na hali ya mtoto kabla ya kurudishwa wodini.
4. Je, kujifungua kwa upasuaji kunaumiza baada ya ganzi kuisha?
Ndiyo. Baada ya dawa ya ganzi kuisha ni kawaida kuhisi maumivu kwenye eneo la mshono na tumbo kwa siku kadhaa. Maumivu haya huwa makali zaidi unapokohoa, kucheka, kusimama au kubeba mtoto, lakini kwa kawaida hupungua taratibu kila siku.
Hospitali hutoa dawa za kupunguza maumivu ili kukusaidia kupona vizuri na kuweza kunyonyesha, kutembea na kumhudumia mtoto bila usumbufu mkubwa. Ni muhimu kutumia dawa kama ulivyoelekezwa badala ya kusubiri maumivu yawe makali.
Iwapo maumivu yanaongezeka badala ya kupungua, mshono unatoa usaha, una harufu mbaya, una wekundu mwingi, au una homa, unapaswa kurudi hospitalini haraka kwa uchunguzi.
5. Ninaweza kuamka na kutembea lini baada ya upasuaji?
Kwa wanawake wengi, kuamka na kuanza kutembea polepole kunashauriwa ndani ya saa 12 hadi 24 baada ya upasuaji, kulingana na hali yao. Wahudumu wa afya watakusaidia kufanya hivyo kwa usalama.
Kutembea mapema husaidia kuboresha mzunguko wa damu, kupunguza hatari ya kuganda kwa damu kwenye miguu, kuchochea utumbo kuanza kufanya kazi tena, na kuharakisha kupona kwa ujumla.
Usijilazimishe kufanya kazi nzito mapema. Ongeza shughuli taratibu kadri mwili unavyopata nafuu, na fuata maelekezo ya wahudumu wa afya kuhusu kuinua vitu vizito na kufanya mazoezi.
6. Je, kujifungua kwa upasuaji kuna hatari zozote kwa mtoto?
Kwa ujumla upasuaji wa kujifungua ni salama na mara nyingi hufanyika ili kulinda afya ya mama au mtoto. Hata hivyo, kama ilivyo kwa njia nyingine za kujifungua, kuna hatari ndogo zinazoweza kutokea.
Baadhi ya watoto wanaweza kupata shida ya kupumua kwa muda mfupi, hasa kama wamezaliwa kabla ya uchungu wa kawaida kuanza. Mara chache sana mtoto anaweza kupata jeraha dogo la ngozi wakati wa kufungua kizazi, lakini hali hii si ya kawaida.
Baada ya kuzaliwa, mtoto atafanyiwa uchunguzi wa kawaida ili kuhakikisha anapumua vizuri, ananyonya vizuri na hana matatizo yanayohitaji matibabu ya ziada.
7. Je, upasuaji wa kujifungua unaweza kuathiri uwezo wangu wa kupata mimba tena?
Kwa wanawake wengi, upasuaji mmoja wa kujifungua hauathiri uwezo wa kupata ujauzito mwingine. Baada ya kupona vizuri, wanawake wengi hupata mimba tena bila matatizo.
Hata hivyo, upasuaji unaweza kuongeza uwezekano wa baadhi ya matatizo katika ujauzito unaofuata, kama vile kondo la nyuma kujishikiza vibaya, kondo kufunika mlango wa kizazi, au mara chache kovu la kizazi kupata changamoto wakati wa uchungu.
Ndiyo maana ni muhimu kumjulisha daktari mapema unapopata ujauzito mwingine ili afuatilie maendeleo ya ujauzito na kupanga huduma zinazofaa.
8. Nina mimba tena lakini nilijifungua kwa upasuaji kwenye mimba iliyopita. Je, kuna madhara yoyote ninayopaswa kuyafahamu?
Kuwa na ujauzito baada ya kufanyiwa upasuaji wa kujifungua si tatizo kwa wanawake wengi, hasa kama mwili ulipata muda wa kupona vizuri. Hata hivyo, ujauzito huu huhitaji ufuatiliaji wa karibu zaidi ili kuhakikisha kovu la kizazi linaendelea kuwa salama na mtoto anakua vizuri.
Daktari atafuatilia eneo la kondo la nyuma, ukuaji wa mtoto, pamoja na dalili zozote zinazoweza kuashiria matatizo ya kovu la kizazi au matatizo mengine ya ujauzito. Pia atakushauri kama unaweza kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida au kama upasuaji mwingine utakuwa salama zaidi.
Nenda hospitali haraka ukipata maumivu makali yasiyoisha ya tumbo, kutokwa na damu ukeni, kupungua kwa mtoto kucheza, kupasuka kwa chupa ya uzazi, au dalili nyingine zozote zisizo za kawaida. Kuhudhuria kliniki zote za wajawazito ni muhimu ili matatizo yagunduliwe mapema.
9. Ninapaswa kusubiri muda gani kabla ya kupata mimba nyingine baada ya kujifungua kwa upasuaji?
Kwa ujumla, wataalamu wengi wa afya hupendekeza kusubiri angalau miezi 18 hadi 24 kabla ya kushika mimba nyingine. Kipindi hiki huruhusu kovu la kizazi na mwili kwa ujumla kupona vizuri, na hupunguza hatari ya matatizo katika ujauzito unaofuata.
Kupata ujauzito mapema sana baada ya upasuaji kunaweza kuongeza uwezekano wa kovu la kizazi kupata changamoto wakati wa ujauzito au wakati wa kujifungua, hasa kama muda kati ya mimba ni mfupi sana.
Ikiwa unapanga kupata mtoto mwingine, zungumza na mtoa huduma za afya kuhusu upangaji uzazi na muda unaofaa zaidi kulingana na afya yako na historia ya ujauzito uliopita.
10. Je, ni kawaida kupata ganzi, kuwashwa au maumivu kwenye mshono hata baada ya miezi kadhaa?
Ndiyo. Baadhi ya wanawake hupata ganzi, kuwashwa, kufa ganzi kwa sehemu ya ngozi, au maumivu madogo karibu na mshono kwa miezi kadhaa baada ya upasuaji. Hii hutokea kwa sababu mishipa midogo ya fahamu hukatwa au kuguswa wakati wa upasuaji na huhitaji muda kupona.
Kwa wanawake wengi, dalili hizi hupungua taratibu ndani ya miezi 6 hadi 12, ingawa kwa baadhi zinaweza kuendelea kwa muda mrefu zaidi bila kuashiria tatizo kubwa.
Ikiwa maumivu ni makali sana, mshono umevimba, unatoa usaha, una harufu mbaya, au una homa, unapaswa kwenda hospitalini haraka kwani huenda kuna maambukizi au tatizo jingine linalohitaji matibabu.
11. Je, upasuaji wa kujifungua unaweza kuathiri uwezo wangu wa kunyonyesha mtoto?
Kwa kawaida hapana. Upasuaji wa kujifungua hauzuii maziwa kutoka wala haupunguzi uwezo wa mama kunyonyesha. Wanawake wengi huanza kunyonyesha ndani ya saa chache baada ya kujifungua mara tu hali yao na ya mtoto inapokuwa nzuri.
Kwa sababu ya maumivu ya mshono, baadhi ya mama wanaweza kupata changamoto ya kupata mkao mzuri wa kunyonyesha. Wahudumu wa afya wanaweza kukusaidia kupata mikao salama, kama kunyonyesha ukiwa umelala ubavuni au kutumia mto kusaidia mtoto ili kupunguza shinikizo kwenye mshono.
Kunyonyesha mapema na mara kwa mara huchochea uzalishaji wa maziwa na humsaidia mtoto kupata lishe bora tangu siku za kwanza za maisha. Ikiwa unapata maumivu makali au mtoto hashiki ziwa vizuri, tafuta msaada wa mtaalamu wa kunyonyesha au mtoa huduma za afya.
12. Je, kujifungua tena kwa upasuaji ndani ya miaka miwili tangu upasuaji uliopita kuna madhara gani?
Kupata ujauzito au kujifungua tena ndani ya kipindi kifupi baada ya upasuaji wa awali, hasa kabla ya kupita miezi 18 hadi 24, kunaweza kuongeza hatari ya baadhi ya matatizo kwa mama na mtoto. Hii ni kwa sababu kovu la kizazi linaweza kuwa bado halijapata muda wa kutosha kupona kikamilifu. Kadiri muda kati ya ujauzito mmoja na mwingine unavyokuwa mfupi, ndivyo uwezekano wa matatizo fulani unavyoweza kuongezeka, ingawa si kila mwanamke atapata matatizo hayo.
Baadhi ya hatari zinazoweza kuongezeka ni pamoja na kuchanika kwa kovu la kizazi wakati wa uchungu wa kujifungua, mtoto kuzaliwa kabla ya wakati, uzito mdogo wa mtoto wakati wa kuzaliwa, pamoja na matatizo ya kondo la nyuma kama kujishikiza vibaya au kufunika mlango wa kizazi. Hata hivyo, wanawake wengi wanaopata ujauzito ndani ya kipindi hiki bado hujifungua salama ikiwa watapata ufuatiliaji mzuri wa kliniki na huduma stahiki za wajawazito.
Ikiwa umepata ujauzito ndani ya miaka miwili baada ya upasuaji wa kujifungua, usiwe na hofu au kukata tamaa. Ni muhimu kuanza kliniki mapema, kuhudhuria miadi yote ya wajawazito, na kufuata maelekezo ya mtoa huduma za afya. Daktari atafuatilia maendeleo ya ujauzito wako, hali ya kovu la kizazi, ukuaji wa mtoto, na atashauri njia salama zaidi ya kujifungua kulingana na hali yako binafsi. Ufuatiliaji wa karibu husaidia kugundua na kushughulikia matatizo mapema, hivyo kuongeza nafasi ya mama na mtoto kuwa salama.
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeandikwa:
23 Februari 2026, 13:33:25
Rejea za dawa
Shepherd A, Cheyne H, Kennedy S. The frequency and reasons for vaginal examinations in labour. Midwifery. 2012;28(6):e804–e810. Available from: https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/22397830/ [Accessed 2021 Jan 10].
Batinelli L, Brunelli R, Di Giovanni A, et al. Improving vaginal examinations performed by midwives. N Am J Med Sci. 2013;5(8):446–450. Available from: https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3749030/ [Accessed 2021 Jan 10].
Freed FC, Raffery ME, Li J, et al. Clinical signs of fetal distress during labor. Am J Obstet Gynecol. 2015. Available from: https://www.ajog.org/article/S0002-9378(15)31746-4/abstract [Accessed 2021 Jan 10].
Berghella V. Cesarean delivery: Preoperative planning and patient preparation. UpToDate. Available from: https://www.uptodate.com/contents/search [Accessed 2021 Jan 10].
Nixon N, et al. Anesthesia for cesarean delivery. UpToDate. Available from: https://www.uptodate.com/contents/search [Accessed 2021 Jan 10].
Berghella V. Cesarean delivery: Surgical technique. UpToDate. Available from: https://www.uptodate.com/contents/search [Accessed 2021 Jan 10].
Berghella V. Cesarean delivery: Postoperative issues. UpToDate. Available from: https://www.uptodate.com/contents/search [Accessed 2021 Jan 10].
American College of Obstetricians and Gynecologists. Postpartum depression. FAQ091. Available from: https://www.acog.org/Patients/FAQs/Postpartum-Depression [Accessed 2021 Jan 10].
American College of Obstetricians and Gynecologists. Cesarean birth (C-section). FAQ006. Available from: https://www.acog.org/Patients/FAQs/Cesarean-Birth-C-Section [Accessed 2021 Jan 10].
Gabbe SG, Niebyl JR, Simpson JL, et al. Obstetrics: Normal and Problem Pregnancies. 7th ed. Philadelphia: Elsevier; 2017. Available from: https://www.clinicalkey.com [Accessed 2021 Jan 10].
Berens P. Overview of the postpartum period: Physiology, complications, and maternal care. UpToDate. Available from: https://www.uptodate.com/contents/search [Accessed 2021 Jan 10].
