top of page

Mwandishi:

Dkt. Peter A, MD

Mhariri:

Dkt. Mangwella Sospeter, MD
Dkt. Adolf Salome, MD

31 Machi 2021 12:10:46

Image-empty-state.png

Pumu kwa mjamzito

Pumu ya kifua ni moja ya tatizo la mfumo wa upumuaji linalofahamika duniani kote, licha ya kutokea kwa watu wa umri na jinsia yoyote, wakati wa ujauzito, tatizo hili linatakiwa kuangaliwa kwa utofauti. Ifahamike kuwa, pumu hutibiwa kwa dawa ambazo zinaweza kudhuru ujauzito, endapo hutazingatia ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya, wewe au mwanao aliye tumboni anaweza kupata madhara. Licha ya pumu kuongeza hatari ya madhara katika ujauzito wako, tatizo hili linaweza kudhibitiwa ipasavyo kwa kujielimisha, kuzingatia ushauri wa daktari na dawa unazotumia. Makala hii imejikita kukupa taarifa nyingi zaidi na muhimu kwako ni matumaini endapo utazingatia, utaweza kuwa na mwisho mwema wa ujauzito wako. Kumbuka kuwasiliana na daktari wako siku zote kwa ushauri zaidi kabla ya kuchukua hatua zozote zile zinazoweza kudhuru afya yako.


Dalili za pumu ya kifua


Pumu ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa upumuaji, dalili za pumu hutokana na kuvimba na kuzalishwa kwa ute mwingi unaopelekea kuziba kwa njia ya hewa na hivyo kuleta dalili ashiria ambazo ni;


 • Kuwa na vipindi vya kujirudia vya kifua kutoa miruzi ya filimbi wakati wa kuvuta hewa na wakati mwingine wakati wa kutoa hewa

 • Kukohoa sana wakati wa asubuhi, wakati wa mazoezi au wakati unacheka

 • Kifua kubanaDalili za shambulio la pumu

Kifua kupiga miruzi wakati wa kupumua, kukohoa na kifua kubana sana bila kuachia kwa muda mrefu

 • Kupumua kwa shida kunakopelekea kushindwa kula, kuongea au kulala

 • Kupumu haraka haraka

 • Mapigo ya moyo kwenda mbio

 • Kusinzia, Kulegea na kizunguzungu

 • Kuwa na rangi ya bluu kwenye vidole vya mikono na midomo

 • Kuzimia au kupoteza fahamu


Vidokezo muhimu kuhusu pumu wakati wa ujauzito


 • Dalili kali za pumu huonekana sana kwa wamama wenye umri wa ujauzito kati ya wiki 29 hadi 36

 • Dalili za pumu huwa si kali katika kipindi cha mwezi wa mwisho kabla ya kujifungua

 • Kujifungua hakusababishi kuongezeka kwa dalili za pumu

 • Wanawake wanaopata nafuu kutoka kwenye dalili kali za pumu, unafuu huo huongezeka kwa jinsi ujauzito unavyokuwa

 • Ukali wa dalili za pumu kwenye ujauzito wa sasa mara nyingi hautatofautiana na ujauzito ujao

 • Dawa za pumu zinazoshauriwa kutumika kipindi cha ujauzito ni zile za kuvuta kwa pumzi badala ya kumeza au kuchoma. Dawa za kunywa hazishauriwi kutumika isipokuwa hakuna njia zingine kwa wakati huo

 • Dawa salama kupita zote kwenye kundi la SABA ('Short Acting Beta-2 Agonist') ni 'Albuterol'. Tafiti nyingi zimefanyika kufuatilia madhara ya dawa kwenye kundi hili na kuonyesha kuwa ,albuterol' ni salama kuliko dawa zingine zilizo kundi hilo.

 • Dawa salama kupita zote kwenye kundi la corticosteroid kutumika kwenye ujauzito ni 'budesonide' ya kuvuta kwa pumzi. Tafiti nyingi zimefanyika na mpaka sasa zinaonyesha kutokuwa na madhara au kuwa na madhara kidogo yasiyo na mashiko.


Viamsha shambulio la pumu


Mambo yanayoamsha shambulio la pumu haswa wakati wa ujauzito bado hayafahamiki vema, hata hivyo shambulio la pumu linalotokea sana katika kipindi cha kwanza na cha pili cha ujauzito, huchangiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuacha kutumia dawa kwa sababu mbalimbali, kama hofu ya mtoto tumboni kupata madhara. Visababishi vingine vinavyoamsha pumu ni vile vile vinavyofahamika kuamsha pumu kwa watu wengine. Viamsha pumu huchokoza mfumo wa kinga kwenye njia ya hewa, kinga ya mwili inapoamka hufanya shambulio ili kuondoa uchafu, kemikali au vimelea vilivyo kwenye mfumo wa upumuaji. Matokeo ya kuamka kwa mfumo wa kinga husababisha dalili za michomo kwenye mfumo wa upumuaji kama vile, kuvimba kwa njia ya hewa na kuongezeka kwa uteute kwenye njia hizo. Matokeo ya shambulio hili ni kuziba kwa njia zinazopitisha hewa na kupelekea kuonekana kwa dalili za pumu.


Baadhi ya viamsha pumu vilivyoorodheshwa kwenye makala hii ni;

 • Poleni za maua

 • Manukato yenye harufu kali

 • Vitu vyenye manukato kama vile sabuni, losheni n.k

 • Kemikali zenye harufu kali

 • Moshi wa sigara au tumbaku

 • Vumbi au kinyesi cha wadudu wanaoishi ndani ya nyumba. Wadudu wadogo wasioonekana kwa macho kama 'dust mite', wadudu wanaoonekana ni kama vile mende n.k

 • Vumbi, kinyesi au manyoya ya wanyama au ndege wanaoishi karibu au ndani ya nyumba kama vile paka, mbwa, kuku, n.k

 • Msongo wa mawazo

 • Mazoezi makali

 • Mabadiliko makubwa ya hali ya hewa


Madhara ya pumu kwa mama mjamzito na mtoto tumboni


Wajawazito wenye pumu wanaonekana kuwa na ongezeko kiasi la hatari ya kupata madhara fulani katika ujauzito ukilinganisha na wanawake wajawazito wasio na pumu, na hakuna sababu za kwanini wanapata madhara hayo. Licha ya kuwa na hatari, wanawake wengi wenye pumu huweza kuwa na mwisho mzuri wa ujauzito bila kupata madhara yaliyo orodheshwa hapa chini. Baadhi ya madhara yanayotokea sana kwa wajawazito wenye pumu ni;


 • Kupata ugonjwa wa shinikizo la juu la damu kipindi cha ujauzito

 • Kupata shinikizo la juu la damu linaloelekea kifafa cha mimba (preeclampsia)

 • Kujifungua kabla ya wakati

 • Kujifungua kwa upasuaji

 • Kujifungua mtoto njiti

Kumbuka: Ili kudhibiti kupata madhara haya, unapaswa kudhibiti pumu kipindi chote cha ujauzito kwa kufuata ushauri ulioelekezwa na daktari wako.


Mambo ya kufahamu kabla ya kutumia dawa za pumu


Kama unasumbuliwa na pumu, ni vema ukafahamu kuhusu dawa zote unazotumia kama zina madhara katika ujauzito kwa kusoma na kuongea na daktari kabla ya kuzitumia. Haijalishi umenunua mwenyewe au umeandikiwa na daktari dawa hizo, mfahamishe daktari wako kuwa una ujauzito ili aweze kupanga matibabu yanayoendana nawe.


Matibabu ya pumu wakati wa ujauzito


Matibabu ya pumu wakati wa ujauzito hufanana na matibabu ya pumu kwa mama asiye mjamzito. Mama unatakiwa kuhudhuria kliniki kuonana na daktari bila kukosa, ili kuweka mwendelezo wa uchunguzi na matibabu. Matibabu ya pumu yatahusisha vitu mbalimbali ambavyo utafanyiwa au kuelekezwa na daktari ambavyo ni; Vipimo na uchunguzi wa kifua

 • Uchunguzi wa maendeleo ya mtoto

 • Kuzuia viamsha pumu

 • Kupewa na kuelimishwa kuhusu dawa za pumu

 • Kupewa elimu zaidi kuhusu pumu

 • Kufundishwa kuhusu matibabu ya pumu nyumbani


Vipimo vya uchunguzi wa kifua


Utakapokuwa unaenda kliniki, daktari atashauri kufanyika kwa vipimo vifuatavyo ili kuchunguza mfumo wako wa hewa na kukushauri inavyotakiwa. Vipimo vilivyozungumziwa hapa vinahusisha; Uchunguzi wa kiwango cha FeNO kuthibitisha kuwa unapumu na

Uchunguzi wa ufanyaji kazi wa mapafu yako


Uchunguzi wa kiwango cha FeNO kuthibitisha pumu


Kipimo cha FeNo hupima kiwango cha gesi ya naitriki oksaidi inayoongezeka kwenye hewa anayopumua mgonjwa wa pumu, haswa pale njia ya mfumo wa upumuaji imeziba. Kipimo hiki pia hufanyika ili kuthibitisha na kufatilia maendeleo ya matibabu ya ugonjwa wa pumu.

Uchunguzi wa ufanyaji kazi wa mapafu


Uchunguzi huu unalenga kupima uwezo wa mapafu kufanya kazi ya upumuaji. Matatizo mbalimbali pia yasiyohusika na pumu huweza kutofautishwa na pumu kwa kipimo hiki. Kipimo cha kutumia vifaa vya 'spirometry na 'peak flow meter' huweza kuchunguza njia ya mfumo wa upumuaji kama imepungua kipenyo au la na kutoa mwangaza wa hali ya pumu na matibabu yanayotakiwa fanyika.


Uchunguzi wa maendeleo ya mtoto tumboni


Uchunguzi wa mtoto hufanyika kwa kila mama mjamzito, kwa kawaida kila mwezi mama anapaswa kwenda kliniki kwa uchunguzi wa ujauzito wake. Viashiria muhimu vya uhai na ukuaji wa mtoto hupimwa kama vile, mapigo ya moyo, urefu kimo cha mimba, mlalo, uchezaji na uzito wa mtoto n.k. Ni muhimu kuhudhuria kliniki kama ulivyokupangia na daktari ili kufanyiwa uchunguzi huu. Endapo mwanao hachezi kama awali, ni vema ukawasiliana na daktari haraka hata kama tarehe yako ya kuhudhuria kliniki bado haijafika. Vifaa tiba vinavyotumika kuchunguza ujauzito na maendeleo ya mtoto ni;


 • Kipimo cha mapigo ya moyo ya mtoto

 • Kipimo cha 'ultrasound' ya tumbo la uzazi


Kipimo cha mapigo ya moyo ya mtoto


Kipimo hiki hutumia kifaa chenye jina la 'fetoscope', hushauriwa kufanyika ili kuchunguza hali ya afya ya mtoto kwa wajawazito wenye pumu na umri wa ujauzito unaozidi wiki 32, na hupendelewa kufanyika kwa wanawake wanaopata shambulio la pumu mara kwa mara. Hali ya mtoto huchukuliwa kuwa nzuri endapo mapigo ya moyo wake yanaongezeka akiwa anacheza ndani ya dakika 2.


Kipimo cha ultrasound ya tumbo la uzazi


Huchunguza maendeleo ya ukuaji (uzito n.k), uchezaji, kiwango cha maji kwenye chupa ya uzazi na upande wa kizazi ambapo kondo limejishikiza. Majibu ya kipimo hiki husaidia sana kufahamu maendeleo ya ukuaji wa mtoto na kupanga njia ya kujifungua.


Kupewa elimu zaidi kuhusu pumu


Elimu zaidi kuhusu pumu itafanya ujiamini na uwe na mpango mzuri wa kukabiliana na pumu. Unapofika kliniki, mbali na kufanyiwa uchunguzi, utapewa elimu zaidi kuhusu;


 • Dalili za pumu

 • Shambulio la pumu na namna ya kujikinga

 • Kujikinga na viamsha shambulio la pumu

 • Kutumia dawa za pumu kama inavyotakiwa(Namna ya kutumia dawa za pumu- dawa za kuvuta kwa pumzi)


Kuzuia viamsha shambulio la pumu


Matokeo ya tafiti na wataalamu wa afya wanashauri njia mbalimbali zitumike kwa pamoja ili kupambana na viamsha pumu ndani na nje ya nyumba yako. Njia mbalimbali zikitumika kwa pamoja zinaongeza ufanisi wa dhana ya kujikinga na viamsha pumu, njia hizo zinajumuisha; Kujikinga dhidi ya viamsha mzio unavyovifahamu au vinavyofahamika mfano vumbi la miili au manyoya au kinyesi cha wadudu, wanyama na ndege iwe nje au ndani ya nyumba unayoishi, nywele, kapeti za manyoya, harufu ya tumbaku au sigara, manukato au mafuta yenye manukato makali na vitu vingine.

Kuacha kuvuta sigara au tumbaku au kuruhusu mtu kuvuta sigara ndani ya nyumba unayokaa au karibu nawe Valisha mto au godoro kava za vitambaa au nailoni ambazo zinathibitishwa kutopitisha vumbi kutoka kwenye mto au godoro. Tumia mbinu mbalimbali za kupambana na wadudu au wanyama wanaoleta mzio kwa binadamu, kama vile kinyesi/miili au manyoya ya panya na mende kwa kutumia njia yoyote ile, kama vile kuweka mitego ya kuwakamata, kutumia sumu au dawa za kuua wadudu au njia yoyote ya kuzuia wasiingie ndani. Tupa mabaki ya chakula kwenye kifaa chenye mfuniko na funika, safisha sehemu ya kupikia na kulia chakula ili kuepuka kupata mende panya au wadudu wengine wanaokula mabaki ya chakula na hivyo kupata kuzaliana. Unga wa chakula ni chakula kizuri cha mende, panya na wadudu wengine, hakikisha unatunza kwenye chombo chenye mfuniko ili kuzuia wasikifikie.

Tafuta watu watakaokusaidia kufanya usafi wa nyumba kwenye sehemu zote ndani ya nyumba mara kwa mara kuondoa wadudu miili yao na kinyesi. Unapokuwa unafua matandiko, tumia maji ya moto au kemikali zinazofahamika kuua vijidudu vya 'dust mit'e. Usitumie kapeti la manyoya ndani ya nyumba yako, na endapo unadhani halikupi shida hakikisha linafanyiwa usafi mara nyingi katika mwezi kwa kuwa hutunza sana vumbi la wadudu n.k Usiishi na wanyama ndani au kuwafuga karibu na nyumba unayokaa. Mfano wa wanyama ni kama vile mbwa, mbuzi, kondoo, ngombe, paka n.k


Endapo una kifaa cha kunyonya vumbi kama vile 'vacuum cleaner', tumia kifaa hicho kuondoa vumbi kwenye kapeti n.k


Kama nyumba ina mfumo wa kutoa nje hewa ya ndani, tumia mfumo huo ili kuhakikisha kuwa ndani ya nyumba yako hakuna vumbi na uchafu unaoamsha mzio.


Endapo umepima kipimo cha mzio na umeonekana huna mzio, utatakiwa kuendelea kufanya usafi ndani ya nyumba na kutumia mbinu mbalimbali za kuepuka vitu vinavyopelekea kuamka kwa mzio, kwa sababu, kipimo hiki wakati mwingine huweza kutoa majibu yasiyo halisia. Kukumbuka: Usishiriki kufanya usafi wa kuondoa viamsha pumu kama ulivyotajwa hapo juu ili kuepuka kuamsha mzio na pumu.


Dawa za pumu wakati wa ujauzito


Dawa zinazotumika kutibu pumu wakati wa ujauzito zinafanana na zile zinazotumika wakati hauna ujauzito, hata hivyo kuna utofauti kidogo wa fomu na dozi inayotakiwa kutumika kwa baadhi ya dawa. Dawa za kuvuta kwa pumzi hushauriwa sana kutumika dhidi ya fomu ya dawa za mishipa, kuchoma kwenye misuli au za kumeza. Mama unapaswa kufahamu kuhusu mabadiliko haya na kuyazingatia ili kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kwako na mtoto aliye tumboni. Licha ya dawa za pumu kutumika kwa muda mrefu sana wakati wa ujauzito, hakuna taarifa zinazotosha kuthibitisha usalama wake kwa mtoto. Taarifa chache zilizopo, zinaonyesha kuwepo na hatari kiasi ya madhaifu ya kiumbaji kwa mtoto tumboni.

Pumu isipotibiwa ipasavyo huongeza hatari zaidi kwa mjamzito zaidi ya madhara ya dawa yanayoweza kujitokeza. Mama unapaswa kuzingatia matibabu ya pumu ili ujiondoe kwenye hatari.

Kupata maelezo zaidi yanayohusu matokeo ya matumizi ya dawa kipindi cha ujauzito, ingia kusoma kwenye sehemu ya 'dawa kipindi cha ujauzito na kunyonysha' ndani ya tovuti ya ULY CLINIC


Makundi ya dawa za pumu wakati wa ujauzito


Makundi mbalimbali ya dawa huweza kutumika katika matibabu ya pumu, dawa hizi hufanya kazi za kuzuia mzio au kufungua njia ya hewa ili uweze kupumua vema. Baadhi ya makundu ya dawa zinazoweza kutumika katika ujauzito ni;


 1. Kundi la Bronchodilator

 2. Kundi la Glucocorticoid (Kundi la Glucocorticoid ya kidonge na Glucocorticoids ya kuvuta kwa pumzi)

 3. Dawa theophylline

 4. Dawa Cromolyn

 5. Dawa kirekebisha Leukotriene

 6. Dawa jamii ya antihistamine

 7. Dawa za kuzibua pua

 8. Dawa za Immunotherapy


Kundi la Bronchodilator


Kundu hili lina makundi mawili madogo ambayo ni;

Bronchodilator zinazofanya kazi kwa muda mfupi mfano ni;


 • Albuterol

 • Levalbuterol

Dawa hizo huonekana kuwa salama kipindi cha ujauzito ukilinganisha na dawa ya kuvuta kwa pumzi jamiii ya epinephrine ambayo husababisha maumivu ya kifua, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kuongezeka kwa shinikizo la damu. Zinazofanya kazi kwa muda mrefu Glucocorticoid ya kuvuta kwa pumzi


Kundi la Glucocorticoid


Dawa kundi la glucocorticoid hutumika kutibu dalili na viashiria vingi vinazosababishwa na pumu. Mfano wa dawa kwenye kundi la glucocorticoid ni;

 • Prednisone

 • Beclomethasone

 • Budesonide, na

 • Fluticasone.

Ili kuongeza ufanisi zaidi wa ufanyaji kazi, dawa za glucocorticoid huunganishwa na dawa zingine kundi la bronchodilator kama zilivyotajwa hapo awali. Glucocorticoid zinapatikana katika fomu mbalimbali zinazotumika kwa kumeza au kuvuta kwa pumzi, maelezo zaidi yamaendikwa kipengele kinachofuata.


Glucocorticoid ya kumeza


Tafiti chache zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko kiasi la hatari ya kupata madhara kwenye ujauzito endapo dawa za kumeza kundi hili zitatumika ukilinganisha na dawa kuvuta kwa pumzi. Madhara yanayoweza jitokeza kwa baadhi ya wajawazito ni kupata mtoto mwenye mdomo sungura, endapo mama alitumia dawa za kumeza haswa katika kipindi cha kwanza cha ujauzito. Madhara mengine ni kuongezeka kwa hatari ya kujifungua kabla ya wakati, kujifungua mtoto njiti, shinikizo la juu la damu na kisukari cha ujauzito. Tafiti zaidi zinatakiwa fanyika ili kuchunguza uhusiano huo kama una mashiko, hata hivyo ni vema kuchukua tahadhari kwa kuacha tumia dawa za kumeza.


Glucocorticoids ya kuvuta kwa pumzi


Taarifa za tafiti kuhusu dawa zilizo kwenye fomu hii zinatoa matumaini ukilinganisha na dawa za kumeza kundi la glucocorticoid. Dawa zinazoweza kutumika bila wasiwasi mkubwa katika kundi hili ni dawa ya kuvuta kwa pumzi yenye jina la budesonide au fluticasone.


Dawa theophylline


Dawa hii imekuwa ikitumika kwa muda mrefu sana katika matibabu ya pumu pasipo kusababisha madhara makubwa, na hivyo inadhaniwa kuwa salama kipindi cha ujauzito. Licha ya kuwa salama, dawa hii kwa sasa haitumiki sana kutokana na kugunduliwa kwa dawa zenye uwezo mkubwa zaidi wa kufanya kazi kama vile dawa kundi la glucocorticoid ya kuvuta kwa pumzi.


Dawa Cromolyn


Kama ilivyo dawa ya theophylline, dawa ya cromolyn inaonekana kuwa salama kipindi cha ujuzito licha ya kutokuwa na matokeo mazuri sana ya kitiba ukilinganisha na dawa dawa kundi la glucocorticoid ya kuvuta kwa pumzi.


Dawa kirekebisha Leukotriene


Baadhi ya dawa kwenye kundi hili zinazotumika katika matibabu ya pumu ni;

 • Montelukast

 • Zafirlukast na

 • Zileuton

Tafiti zinaonyesha wanawake wanaotumia montelukast au zafirlukast hawana hatari la ongezeko la madhara kwa mama au madhaifu ya kiuumbaji kwa mtoto. Kati ya dawa hizi mbili, dawa yenye usalama zaidi ni dawa ya montelukast. Taarifa chache zipo kuhusu usalama wa dawa zileuton kwa wanawake wajawazito, endapo unataka kutumia dawa hii na unapanga kuwa mjamzito, ni vema ukawasiliana na daktari wako kwanza kama dawa hii itakufaa au la.


Dawa jamii ya antihistamine


Kwa kawaida kundi hili la dawa huwa si miongoni mwa dawa zinazotumika katika matibabu ya pumu, hata hivyo dawa hizi ni muhimu na zinaweza kutumika kutibu au kuzuia mzio ambao mara nyingi huambatana na pumu. Dawa zilizo kundi hili baadhi yake ni;


 • Diphenhydramine

 • Chlorpheniramine

 • Loratadine

 • Fexofenadine na

 • Cetirizine


Tafiti za wanyama na binadamu zinaonyesha kuwa, dawa za anthistamine haziongezi hatari ya madhaifu ya kimaumbile kwa kijusi tumboni, na hata kama kuna uwezekano wa kutokea, ni kwa kiasi kidogo saa ambacho hakina mashiko. Kati ya dawa zote za mzio kwenye kundi la antihistamine, dawa ya chlorpheniramine, loratadine na cetirizine ni dawa zinazoonekana kuwa salama zaidi kuliko zingine kutumika kipindi cha ujauzito.


Dawa za kuzibua pua


Dawa hizi pia si miongoni mwa dawa zinazotumika katika matibabu ya pumu, hata hivyo matumizi ya dawa kwenye kundi hili huweza kupunguza dalili za pumu kutokana na mzio kwenye mfumo wa juu wa upumuaji. Mafano wa dawa kwenye kundi hili ni pseudoephedrine. Kuna tafiti chache sana ambazo zimechunguza usalama wa dawa zilio kundi hili kipindi cha ujauzito, taarifa kutoka kwenye tafiti hizo chache hazitoshi kutoa hitimisho kuhusu usalama wake kipindi cha ujauzito. Hivyo kwa sasa ni vema kuepuka kutumia dawa kundi hili mpaka pale taarifa za kujitosheleza zitakapopatikana. Kama kuna ulazima wa mjamzito chini ya wki 13 kutumia dawa kundi hili, dawa za kuvuta kwa pumzi tu zinaweza tumika ila isiwe mara kwa mara au kutumia dozi kubwa.


Dawa za Immunotherapy


Dawa kundi hili zipo katika fomu ya maji kuchoma kwa sindano au vidonge vya kuweka chini ya ulimi. Hufanya kazi kwa kupunguza hatari ya kupata mzio mara kwa mara unaoweza kuamsha pumu kwa kupunguza mwitikio wa kinga ya mwili kwenye viamsha mzio.

Dawa za Immunotherapy hufahaamika kuwa salama kipindi cha ujauzito licha kuwa na hatari kidogo sana ya kuamsha mzio mkubwa wa 'anafailaksis' kwa watumiaji. Hitimisho la usalama ni kwamba, dawa za immunotherapy zinaweza kuwa salama kwa wajawazito ambao waliwahi kuzitumia kabla ya kuwa wajawazito na hivyo wakiendelea nazo hakuna hatari ya kutokea kwa maudhi makubwa. Wanawake ambao hawajawahi kutumia daw akundi hili wanashauriwa kutozitumia ili kuepuka maudhi makubwa yanayoweza kujitokeza. Mfano wa dawa kwenye kundi hili ni;


 • Dupilumab

 • Omalizumab

 • Benralizumab

 • Mepolizumab

 • Reslizumab


Pumu kipindi cha uchungu, kujifungua na baada ya kujifungua


Endapo una pumu katika ujauzito, unapaswa kuongea na daktari kuhusu hali yako ya kiafya pamoja na dawa unazotumia, daktari akifahamishwa huweza kubadili mpango wa matibabu haswa kwenye dawa zinazotumika kipindi cha uchungu, kujifungua na bada ya kujifungua. Dawa ya uchungu oxytocin ni dawa pendekezwa kutumika kwa ajili ya kuongeza uchungu na kuthibiti kuvuja kwa damu nyingi baada ya kujifungua. Uchaguzi wa dawa salama za ganzi utafanyika endapo kuna uhaja wa dawa hizo kutumika haswa unapopangiwa kujifungua kwa upasuaji. Mara nyingi mama hutachomwa dawa za kaputi, mbadala wake utapewa za nusu kaputi. Endapo ni lazima kutumia dawa za kaputi, dawa zinazopendekezwa kutumika ni zile ambazo zinauwezo wa kufungua njia ya hewa.


Wakati wa kunyonyesha


Mama mwenye pumu akinyonyesha mtoto, atapunguza hatari ya mtoto kutoa miruzi ya wakati wa upumuaji kutokana na pumu katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza. Hii inasemekana ni kwa sababu watoto wanaonyonya maziwa ya mama kwa miaka miwili ya mwanzo, huwa hawaugui mara kwa mara magonjwa ya mfumo wa upumuaji.


Je wanawake wenye pumu huweza kujifungua salama?


Ni ngumu kutabiri matokeo ya ujauzito wa mwanamke mwenye pumu utaishia vipi, endapo mama atazingatia ushauri anaopewa na wataalamu wa afya, hatari nyingi za madhara zitapungua na mama atalea vema ujauzito na kujifungua salama.


Matibabu ya nyumbani


Matibabu ya nyumbani huhusisha kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha kwa kuzingatia kanuni mbalimbali za kiafya. Ukiwa nyumbani unaweza kufanya mambo yafuatayo ili kukabiliana na pumu; Tumia kahawa, kahawa hutanua njia ya mfumo wa upumuaji na hivyo kupunguza dalili za pumu, usitumie zaidi ya miligramu 300 kwa siku kwa sababu usalama wa kiwango kilichozidi hapo hakifahamiki kutokana na kutokuwepo kwa tafiti zilizoangalia matumizi ya kiwango kianchozidi hiki pendekezwa. Matumizi ya vyakula vyenye chlorine ambavyo hufanya mwili wako ufanye kazi kama inavyotakiwa, vyakula vyenye choline kwa wingi ni kama vile nyama ya ng'ombe, ini, mayai, nyama ya kuku, samaki, karanga na kabichi ya koliflawa. Fanya mazoezi kuimarisha mfumo wa upumuaji. Mazoezi huweza kupunguza uhitaji wa kutumia dawa za pumu mara kwa mara. Jifunze namna ya kufanya mazoezi ya mfumo wa upumuaji kwenye kurasa za mazoezi kipindi cha ujauzito ndani ya tovuti hii ya ULY CLINIC


Nini unahitaji fahamu zaidi kuhusu pumu?


ULY CLINIC ipo tayari kukusaidia kupata taarifa sahihi za kiafya kuhusu pumu wakati wa ujauzito, uliza swali au toa maoni yako kwenye sehemu ya 'Wasiliana nasi' au kutumia namba ya whatsapp chini ya tovuti hii.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

21 Mei 2023 12:35:30

Rejea za dawa

 1. ULY CLINIC, dawa za kutibu asthma

 2. Dombrowski MP, Schatz M, ACOG Committee on Practice Bulletins-Obstetrics. ACOG practice bulletin: clinical management guidelines for obstetrician-gynecologists number 90, February 2008: asthma in pregnancy. Obstet Gynecol 2008; 111:457. Reaffirmed 2019.

 3. Schatz M, Dombrowski MP. Clinical practice. Asthma in pregnancy. N Engl J Med 2009; 360:1862.

 4. Asthma and alegy foundation of America. Asthma. https://www.aafa.org/asthma.aspx#. Imechukuliwa 30.03.2021 5. Centre for disease control. Asthma. https://www.cdc.gov/asthma/default.htm. Imechukuliwa 30.03.2021

 5. National Heart, Lung, and Blood Institute National Asthma Education and Prevention Program. https://www.nhlbi.nih.gov/sites/default/files/media/docs/EPR-3_Asthma_Full_Report_2007.pdf. Imechukuliwa 30.03.2021

 6. Asthma. https://www.nhlbi.nih.gov/sites/default/files/media/docs/12-5075.pdf. Imechukuliwa 30.03.2021

 7. 2020 Focused Updates to the Asthma Management Guidelines: A Report from The National Asthma Education and Prevention Program Expert Panel Working Group.https://www.nhlbi.nih.gov/asthmaguidelines. Imechukuliwa 30.03.2021

 8. Journal of Allergy and Clinical Immunology. https://www.jacionline.org/article/S0091-6749(20)31404-4/fulltext. Imechukuliwa 30.03.2021

 9. AAAAI ALLERGY & ASTHMA MEDICATION GUIDE. https://www.aaaai.org/conditions-and-treatments/drug-guide/Immunomodulators. Imechukuliwa 31.03.2021 11. Asthma Treatments. https://www.webmd.com/asthma/asthma-treatments. Imechukuliwa 31.03.2021.

 10. Sara Morgan, RPh, et al. Is caffeine consumption safe during pregnancy?. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3625078/#. Imechukuliwa 31.03.2021

bottom of page