Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dr.Sospeter Mangwella, MD
ULY CLINIC
4 Januari 2026, 01:28:28
.jpg)
Damu nyingi mwilini
Damu nyingi ni hufahamika kwa jina jingine la polisaithimia au polycythemia, ni tatizo linalotokea endapo kiwango cha himoglobin ni kingi kuliko kawaida ya umri au jinsia ya mtu. Kwa mtu mzima mwanaume kiwango cha himoglobin kikizidi gramu 16.5 kwa desilita moja ya damu (16.5g/dL) au kuzidi 16g/dL kwa mwanamke, huitwa damu nyingi. Kusoma zaidi kuhusu kiwango cha damu cha kwaida kwa watoto bofya hapa.

Visababishi vya damu nyingi mwilini
Visababishi vya damu nyingi vimegawanyika katika makundi mawili, yenye jina la polisaithemia vera na polisaithemia ya sekondari. Polisaithemia vera huhusianishwa na mabadiliko ya jeni JAK2 kwenye mifupa inayopelekea uzalishaji wa damu kuliko kawaida. Polisaithemia ya sekondari husababishwa na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya dawa za kuongeza uzalishaji damu, magonjwa ya viungo mbalimbali vya mwili, mazingira na mtindo mbaya wa maisha. Kusoma zaidi kuhusu namna gani inatokea bofya hapa.
Dalili za damu nyingi mwilini
Dalili za kuwa na damu nyingi kupita kawaida mwilini ni;
Muwasho
Maumivu ya kichwa
Kizunguzungu
Kupata majeraha kirahisi au kutokwa na damu kirahisi
Kutokwa na jasho zaidi ya kawaida
Maumivu na kuvimba kwa maungio
Kupungua uzito bila sababu
Njano kwenye macho na ngozi
Kuchoka
Maumivu ya tumbo
Alama za zambarau au nyekundu kwenye ngozi
Wakati gani wa kutafuta msaada wa dataktari haraka?
Endapo unatatizo la damu nyingi na unapata dalili zifuatazo, unapaswa kuonana na daktari haraka kwa uchunguzi na tiba;
Kutokwa na damu muda mrefu
Kuvimba endelevu kwa maungio
Kupumua kwa shida
Kuishiwa pumzi
Dalili za kiharusi kama kushindwa kuongea au kuwa dhaifu sehemu moja ya mwili
Matibabu
Matibabu ya hospitali ya damu nyingi
Matibabu ya hospitali kwa tatizo la damu nyingi (polisaithemia) hutegemea aina ya tatizo (Polisaithemia Vera au Polisaithemia ya upili), umri wa mgonjwa, kiwango cha hemoglobini/hematokriti, na uwepo wa matatizo kama vifungo vya damu. Lengo kuu la matibabu ni:
Kupunguza kiwango cha seli nyekundu za damu
Kuzuia kuganda kwa damu
Kupunguza hatari ya kiharusi, mshtuko wa moyo, au DVT
Kupunguza dalili kama maumivu ya kichwa, muwasho, na uchovu
Jedwali 1: Matibabu ya hospitali kwa damu nyingi (Polisaithemia)
Aina ya matibabu | Mfano wa tiba | Namna inavyofanya kazi | Hupendekezwa kwa nani |
1. TIba ya kutoa damu | Kutoa damu 350–500 mL | Kupunguza haraka idadi ya seli nyekundu na msongamano wa damu | Wagonjwa wote wa polisaithemia, hasa kiwango cha chembe zinzobeba oksijeni-hematokriti zikiwa juu sana |
2. Dawa za kupunguza uzalishaji wa damu | Hydroxyurea | Kupunguza uzalishaji wa chembe nyekundu na nyeupe za damu na chembe sahani. | Wagonjwa wenye umri zaidi ya miaka 60 , walio na wenye shida ya kuganda kwa damu, au kiwango cha hemoglobin kinachopanda haraka |
Interferon-alpha | Kurekebisha kinga ili kupunguza uzalishaji wa damu | Wanawake wanaopanga mimba au wajawazito (salama kuliko hydroxyurea) | |
Ruxolitinib (JAK2 inhibitor) | Kuzuia jeni JAK2 linalosababisha uzalishaji kupita kiasi | Wagonjwa wa Polisaithemia Vera wasiostahimili hydroxyurea | |
3. Dawa za kupunguza kuganda kwa damu | Aspirin (75–100 mg) | Kupunguza hatari ya stroke, DVT na heart attack | Karibu wagonjwa wote wa polycythemia |
Warfarin, Apixaban, Rivaroxaban | Kuzuia kuzalika kwa vifundo vya damu (clots) | Wagonjwa wenye historia ya DVT/PE au clots zinazoendelea | |
4. Matibabu ya kisababishi (Kwa Polisaithemia ya upili) | Oksijeni kwa wagonjwa wa magonjwa ya mapafu | Kupunguza upungufu wa oksijeni unaoongeza uzalishaji wa chembe nyekundu za damu | Wagonjwa wenye COPD, asthma kali, nimonia n.k. |
mashine ya CPAP | Kuzuia kushuka kwa oksijeni wakati wa usingizi | Wagonjwa wenye kukosa hewa wakati wa kulala | |
Kufanya upasuaji kuondoa uvimbe unaozalisha homoni EPO inayochochea uzalishaji wa chembe nyekundu za damu | Kuondoa chanzo cha EPO kupita kiasi | Wagonjwa wenye uvimbe kwenye figo au ini | |
Kusitisha tiba ya homoni testosteroni/steroid | Kupunguza kichocheo cha uzalishaji wa chembe nyekundu za damu | Wagonjwa wanaotumia dawa hizi bila uangalizi | |
5. Ufuatiliaji wa tiba | FBC, LFT, KFT, vipimo vya JAK2 | Kuzuia viwango kupanda kupita kiasi na kufuatilia athari za dawa | Wagonjwa wote, kwa vipindi vya wiki hadi miezi |
Ultrasound ya bandama | Kutambua kama bandama inakuwa kubwa (wengu kuongezeka) | Wagonjwa wenye maumivu upande wa kushoto wa tumbo | |
6. Tiba za dalili | Antihistamines | Kupunguza muwasho mkali unaotokana na mzunguko wa damu kuwa mwingi | Wagonjwa wenye muwasho |
NSAIDs maalum | Kutuliza maumivu ya maungio | Kwa uangalizi wa daktari pekee | |
Ruxolitinib kwa bandama lililokuwa | Kupunguza uvimbe wa bandama na dalili zinazohusiana | Wagonjwa ambao bandama limekuwa sana |
Matibabu ya nyumbani
Angalizo muhimu: Matibabu ya polithaisemia hayapaswi kutegemea matibabu ya nyumbani pekee. Njia hizi huweza kusaidia kupunguza hatari ya matatizo wakati mgonjwa anasubiri au anapata matibabu ya daktari.
Jedwali 2: Matibabu ya Nyumbani kwa Damu Nyingi (Polisaithemia)
Aina ya hatua | Mfano wa matibabu ya nyumbani | Jinsi yanavyosaidia | Maelezo muhimu kwa mgonjwa |
Kudhibiti mtindo wa maisha | Kunywa maji ya kutosha (2–3 L kwa siku) | Kupunguza unene wa damu na hatari ya kuganda | Epuka vinywaji vyenye kafeini nyingi au pombe kwani huounguza maji mwilini. |
Mazoezi mepesi (kutembea dakika30 kwa siku) | Kuboresha mzunguko wa damu na kupunguza hatari ya vifungo vya damu | Epuka mazoezi mazito ambayo yanaongeza hitaji la oksijeni kupita kiasi | |
Kuepuka kukaa au kulala muda mrefu katika mkao mmoja | Kuzuia damu kusimama sehemu moja na kupata vifungo | Simama na kunyoosha mwili kila dakika 30–60 | |
Kuboresha afya ya mfumo wa hewa | Epuka kuvuta sigara na moshi wa mazingira | Kupunguza upungufu wa oksijeni unaochochea mwili kuzalisha damu nyingi | Ikiwa unavuta sigara, pata ushauri au dawa za kukusaidia kuacha |
Kulala kwenye chumba chenye hewa safi na ya kutosha | Kuepusha kushuka kwa oksijeni usiku | Hakikisha chumba kina uingizaji hewa wa kutosha | |
Udhibiti wa mazingira | Kuepuka maeneo yenye hewa chafu (barabara zenye magari mengi, viwandani) | Kupunguza hatari ya upungufu wa oksijeni unaosababisha mwili kuzalisha chembe nyekundu za damu kwa wingi. | Tumia barakoa unapolazimika kupita maeneo haya |
Kukaa maeneo karibu na usawa wa bahari inapowezekana (mfano mikoa ambayo ipo karibu na bahari badala ya ile ambayo ipo mbali na usawa wa bahari) | Kuondoa kichocheo cha mwili kuongeza uzalishaji wa chembe nyekundu za damu kutokana na upungufu wa oksijeni milimani | Kama unaishi milimani, zingatia kutumia purifier au kufunga madirisha wakati wa msongamano wa moshi | |
Lishe bora | Kula matunda yenye antioxidants (tufaha, zabibu, kiazi chekundu, tikiti maji) | Kuboresha afya ya mishipa na kupunguza mkusanyiko wa damu | Kula angalau matunda 2–3 kwa siku |
Vyakula vyenye mafuta mazuri (karanga, mbegu, parachichi, samaki) | Kupunguza uvimbe wa mishipa na hatari ya damu kuganda | Epuka mafuta ya kukaanga mara kwa mara | |
Kuepuka vyakula vyenye chuma kingi kupita kiasi (maini, spinach, dagaa kwa wingi sana) ikiwa daktari ameshauri | Kuzuia kuongezeka kwa hemoglobini kupita kiasi | Usiepuke vyakula hivi bila ushauri wa daktari | |
Kuimarisha afya ya mishipa ya damu | Kutumia vitendea kazi vya compression kama soksi za compression ikiwa umeelekezwa | Kusaidia kurudisha mzunguko wa damu kwenye moyo | Usitumie bila ushauri wa daktari wa mishipa |
Kufanya ukandaji-Massage nyepesi kwenye miguu | Kuboreshwa kwa mzunguko wa damu kwenye mishipa ya vena na kupunguza mzio wa damu kusimama | Usifanye massage yenye mgandamizo mkubwa ikiwa una hatari ya kuganda kwa damu katika mishipa ya damu |
Namna ya kujikinga na damu nyingi
Endapo kisababishi ni polisaithemia vera, inaweza kuwa ngumu kujikinga, hata hivyo unaweza kutumia mbinu zifuatazo kujikinga na polisaithemia ya sekondari na kuthibiti polisaithemia vera;
Pata matibabu ya magonjwa ya mapafu na moyo
Acha kuvuta sigara
Jiepushe kukaa muda mrefu kwenye maeneo yenye gesi ya cabonmonoksaidi kama machimboni, kwenye miji yenye magari mengi yanayotumia mafuta ya petrol au dizeli, gereji au kufanya kazi za kurekebisha eksozi ya gari
Ishi mikoa karibu na usawa wa bahari
Fanya uchunguzi wa vinasaba vya polisithimia vera kabla ya kuamua kupata mtoto
Wapi unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu kuwa damu nyingi?
Unaweza kupata taarifa ya kiwango cha damu mwilini kulingana na umri kwa kubofya hapa
Pata taarifa zaidi kuhusu ugonjwa wa damu nyingi au polisaithemia vera kwa kubofya hapa
Wasiliana na daktari wako au daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri zaidi kuhusu dalili na tiba kupitia linki ya 'Mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara
1. Je, damu nyingi inaweza kutokea bila kuonyesha dalili zozote?
Ndiyo. Watu wengi hupatikana na kiwango cha juu cha hemoglobini bila dalili zozote. Mara nyingi huonekana kupitia uchunguzi wa kawaida wa afya. Hii ni hatari kwa sababu damu nzito inaweza kuongeza hatari ya kuganda bila mtu kuhisi dalili.
2. Je, kula vyakula fulani kunaweza kuongeza hemoglobini kupita kawaida?
Kula vyakula vyenye chuma hakusababishi polisaithemia kwa mtu asiye na tatizo. Hata hivyo, kwa watu wenye matatizo ya kurithi kama hemokrromatosis au polysaithemia vera, mwili unaweza kutumia vyakula hivyo kupita kawaida na kuongeza damu.
3. Je, polisaithemia vera ni kansa?
Ndiyo, kwa mujibu wa taksonomia ya magonjwa, polisaithemia vera huainishwa kama aina ya saratani isiyo kali ya uzalishaji damu). Haitokei kwa haraka kama saratani kali lakini huhitaji kufuatiliwa maisha yote.
4. Je, polisaithemia inaweza kuathiri uwezo wa kupata ujauzito?
Ndiyo. Kwa wanawake, damu nyingi inaweza kuathiri utendaji wa ovari na kusababisha hedhi zisizo za kawaida. Pia huongeza hatari ya kuharibika kwa mimba kutokana na damu kuganda kirahisi.
5. Je, mazoezi makali yanaweza kuongeza hemoglobini kupita kawaida?
Ndiyo. Wanariadha na wapanda milima wanaweza kuwa na hemoglobini nyingi kama sehemu ya mwili kuzoea mazingira yenye matumizi makubwa ya oksijeni. Hii si polisaithemia ya ugonjwa, bali ni ya kifiziolojia kutokana na kwa ajili ya kukabiliana namazingira.
6. Je, mwanamke mjamzito anaweza kupata damu nyingi?
Ndiyo, ingawa ni nadra. Mara nyingi ujauzito husababisha kupungua kwa hemoglobini kutokana na kuongezeka kwa maji kwenye damu. Ikiwa hemoglobini ni juu wakati wa ujauzito, daktari hutafuta visababishi vya ukosefu wa oksijeni, maradhi ya mapafu, au matatizo ya kifamilia.
7. Je, kuishi milimani kunaathiri vipimo vya damu?
Ndiyo. Kuishi maeneo ya juu, husababisha mwili kuzalisha hemoglobini nyingi ili kukabiliana na ukosefu wa oksijeni. Hii ni kawaida, lakini inaweza kuficha polycythemia ya ugonjwa kama haitachunguzwa kwa makini.
8. Je, polisaithemia inaweza kupona kabisa?
Polisaithemia vera haiishi kabisa, lakini inaweza kudhibitiwa kwa matibabu ya kudumu kama kupunguza damu kwa kutoa damu, dawa zinazodhibiti uzalishaji wa damu, na ufuatiliaji. Aina ya upili inaweza kupona ikiwa kisababishi chake kimetibiwa.
9. Je, kipimo cha oxygen kinaweza kusaidia kugundua polycythemia?
Kinasaidia sio moja kwa moja kuthibitisha. Ikiwa kiwango cha oksijeni kiko chini kwenye damu, mwili huongeza uzalishaji wa hemoglobini ili kufidia. Hivyo kiwango kidogo kinaweza kuashiria polisaithemia ya upili. Lakini kipimo cha hemoglobin ndicho hutambua tatizo moja kwa moja.
10. Je, kuna hatari gani kubwa zaidi ya damu nyingi kutotibiwa?
Hatari kuu ni:
Kuganda kwa damu katika mishinda ya damu
Kiharusi
Mshtuko wa moyo
Kushindwa kwa moyo
Kupasuka kwa mshipa (kuvuja damu) Kutotafuta matibabu kunaweza kuongeza madhara haya kwa kiwango kikubwa.
Rejea za mada hii
Ayalew Tefferi, et al. Polycythemia vera treatment algorithm 2018. https://www.nature.com/articles/s41408-017-0042-7. Imechukuliwa 02.07.2021
Xiao Lu, et al. Polycythemia Vera. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK557660/. Imechukuliwa 02.07.2021
Anemia in chronic kidney disease. niddk.nih.gov/health-information/kidney-disease/chronic-kidney-disease-ckd/anemia. Imechukuliwa 02.07.2021
Barbui T, et al. Diagnostic impact of the 2016 revised WHO criteria for polycythemia vera. DOI: 10.1002/ajh.24684. Imechukuliwa 02.07.2021
Lung.org. Chronic obstructive pulmonary disease (COPD). lung.org/lung-health-and-diseases/lung-disease-lookup/copd/. Imechukuliwa 02.07.2021
Complete blood count (CBC). labtestsonline.org/tests/complete-blood-count-cbc
Hematocrit. labtestsonline.org/tests/hematocrit. Imechukuliwa 02.07.2021
Hemoglobin. labtestsonline.org/tests/hemoglobin. Imechukuliwa 02.07.2021
Hypothyroidism (underactive thyroid). niddk.nih.gov/health-information/endocrine-diseases/hypothyroidism. Imechukuliwa 02.07.2021
Mayo Clinic Staff. High hemoglobin count. mayoclinic.org/symptoms/high-hemoglobin-count/basics/causes/sym-20050862. Imechukuliwa 02.07.2021
Polycythemia vera in children. stanfordchildrens.org/en/topic/default?id=polycythemia-90-P02398. Imechukuliwa 02.07.2021
Maana ya Marrow. http://www.elimuyetu.co.tz/subjects/arts/eng-swa/m.html. Imechukuliwa 02.07.2021
Arber, D. A. et al. The2016 revision to the World Health Organization classification of myeloid neoplasms and acute leukemia. Blood 127, 2391–2405 (2016)
Marchioli, R. et al. Cardiovascular events and intensity of treatment in polycythemia vera. N. Engl. J. Med. 368, 22–33 (2013)
Landolfi, R. et al. Leukocytosis as a major thrombotic risk factor in patients with polycythemia vera. Blood 109, 2446–2452 (2007)
Chievitz, E. & Thiede, T. Complications and causes of death in polycythaemia vera. Acta Med. Scand. 172, 513–523 (1962)
Imeandikwa:
18 Juni 2025, 15:07:15
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
