Mwandishi:
Dkt. Sospeter B, MD
Mhariri:
Dkt. Salome A, MD
12 Juni 2020, 10:27:06
Kutokwa na damu puani matibabu
Kutokwa na damu ndani ya pua kwa lugha tiba huitwa epistaksizi, huweza kutokea kipindi cha ujana au utotoni kwenye umri fulani. Tatizo hili husababisha hofu kwa mzazi au mtoto, hata hivyo huna haja ya kuogopa kwa sababu tatizo hili mara nyingi huwa si hatari na karibia kila mtu ashapata mara moja katika maisha yake. Hata hivyo endapo unatokwa na damu puani zaidi ya mara moja kwa wiki unatakiwa kupata uchunguzi kutoka kwa daktari.
Wapi unaweza kusoma zaidi kuhusu kutokwa na damu puani?
Soma zaidi kuhusu visababishi kwenye makala za Damu kutoka puani ndani ya tovuti hii ya ULY CLINIC
Huduma ya kwanza ya kutokwa na damu puani
Fanya mambo yafuatayo ili kusimamisha damu isiendelee kutoka;
Peng’a pua ili kuondoa damu iliyoganda, fanya hivi taratibu hii inaweza kuongeza damu kutoka lakini usihofu. Kwa watoto wadogo kufanya hivi si lazima
Pinda mgongo kwa mbele ukiwa umekaa au kusimama. Usilalie mgongo kwa sababu inaweza kusababisha utapike
Bana pua karibu na matundu kwa kutumia vidole viwili vya mikono yako, tumia nguvu sawa kubana matundu yote kwa pamoja
Bana maka kuziba matundu ya pua kwa angalau dakika 5 kwa watoto au 10 hadi 15 kwa mtu mzima. Hakikisha unatumia saa kuhesabu muda huu, watu wengi huacha kubana chini ya muda unaoshauriwa hivyo damu huendelea kutoka.
Endapo unaweza tumia barafu kupaki kweye kuta za pua, hii inasaidia pia mishipa ya damu kusinyaa na kusimamisha damu kutoka lakini si lazima kufanya hivi
Endapo damu inaendelea kutoka ufanye nini?
Endapo umefuata maelezo yaliyoorodheshwa hapo juu na damu bado inaedelea kutoka, rudia upya kwa muda wa dakika 30. Na endapo bado inaendelea kutoka, tafuta msaada kutoka kwa daktari wako haraka au piga simu kuita mtaalamu wa afya kuja kukusaidia.
Namna ya kujikinga na kutokwa damu puani
Tumia Kiyoyozi ili kuongeza unyevu kwenye mazingira yako endapo hewa ni kavu
Tumia dawa ya maji ya chumvi kupulizia kwenye matundu ya pua ili kufanya pua iwe na unyevunyevu
Jizuie kuingiza kidole puani, kama ni lazima kata kucha zako ziwe fupi kuzuia kujiumiza.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasilianane na daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii
Wasiliana na daktari wa ULY clinic kwa kupiga namba za simu au kubonyeza sehemu imeandikwa "Pata tiba" chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
21 Julai 2023, 16:18:21
Rejea za mada hii;
1.Nosebleed patient education. https://www.uptodate.com/contents/nosebleeds-epistaxis-beyond-the-basics. Imechuliwa 12.06.2020
2.Messner AH. Management of epistaxis in children. http://www.uptodate.com/home. Imechuliwa 12.06.2020
3.Messner AH. Epidemiology and etiology of epistaxis in children. http://www.uptodate.com/home. Imechuliwa 12.06.2020
4.Messner AH. Evaluation of epistaxis in children. http://www.uptodate.com/home. Imechuliwa 12.06.2020
5.Ferri FF. Epistaxis. In: Ferri's Clinical Advisor 2015: 5 Books in 1. Philadelphia, Pa.: Mosby Elsevier; 2015. http://www.clinicalkey.com. Imechuliwa 12.06.2020
6.Marx JA, et al. Otolaryngology. In: Rosen's Emergency Medicine: Concepts and Clinical Practice. 8th ed. Philadelphia, Pa.: Mosby Elsevier; 2014. http://www.clinicalkey.com. Imechuliwa 12.06.2020
7.Nosebleeds. American Academy of Otolaryngology — Head and Neck Surgery. http://www.entnet.org/content/nosebleeds. Imechuliwa 12.06.2020