top of page

Dalili na viashiria bonyeza herufi ya kwanza kusoma zaidi

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [#]

Mwandishi:

Dkt. Mercy M, M.D

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

29 Aprili 2020 19:44:51

Matumizi ya barakoa

Matumizi ya barakoa

Matumizi sahihi ya barakoa kujikinga na maambukizi ya COVID 19 au corona


Barakoa nzuri ni ipi?


Barakoa nzuri ni ile yenye uwezo wa


  • Kufunika vema pande zote za mdomo na pua lakini kukuachia uhuru wa kupumua

  • Kushikizwa kwa Kamba au barabendi inayopita nyuma ya sikio au nyuma ya kichwa

  • Iwe na zaidi ya kuta moja ya kitambaa au fabriki

  • Isizuie upumuaji wako

  • Iwe na uwezo wa kusafishwa/kufuliwa na kupigwa pasi bila kuharibika


Inashauriwa na shirika la kimataifa la kupambana na kuzuia magonjwa CDC kuwa, endapo itashindikana kuzuia kujichanganya kwenye mkusanyiko wa watu kama maeneo ya kulia chakula, sokoni, dukani n.k ni vema ukavaa barakoa ya nguo ili kuzuia maambukizi ya corona.


Namna gani ya kuvua barakoa yako


Vua barakoa kwa kushika Kamba nyuma ya sikio, usishike barakoa sehemu ya mbele maana inauwezekano mkubwa wa kuwa na maambukizi. Eneo hili la mbele ndipo hewa chafu, bakteria na virusi wanaweza kuwepo kutoka kwenye hewa, hivyo eneo hili si salama. Shika Kamba nyuma ya sikio kuvua barakoa yako na kisha itupie kwenye ndoo ya maji yenye sabuni au deto na ikae kwa muda wa masaa mawili kabla ya kuifua.


Unatakiwa kubadilisha barakoa mara ngapi kwa siku?


Badilisha barakoa kila mara utakapotaka


  • Kula chakula

  • Kunywa maji

  • Kunywa chai


Kwa kifupi kila utakapotaka kuingiza kitu kinywani ni lazima uvae barakoa mpya. Hii ni kwa sababu kurudia barakoa ile ile inakuweka hatarini kupata maambukizi.


Unatakiwa kuwa na barakoa ngapi?


ULY clinic inashauri uwe na wastani wa barakoa tatu, barakoa ya kwanza itavaliwa wakati unataka kutoka nje kwenda kutafuta mahitaji yako. Unaporejea nyumbani kabla hujaingia ndani vua barakoa kama ilivyoelekezwa hapo juu kwa kushika Kamba iliyo nyuma ya sikio na kisha kuitupa katika chombo maalumu cha kutunzia uchafu. Endapo barakoa yako ni ya kufua, iweke kwenye ndoo ya maji yenye sabuni au deto ambayo utakuwa tayari ulishaiandaa na ipo nje ya nyumba. Funika ndoo na kisha jitakase kwa kunawa mikono yako kwa sabuni na maji tiririka au kwa kutumia vitakasa mikono. Hapa unaweza kufungua mlango na kuingia ndani ya nyumba yako. Unapoingia ndani usiguze chochote wala usiingie na viatu. Elekea bafuni badilisha nguo na oga. Ukimaliza kuoga unaweza kurejea sebleni na kukaa Pamoja na familia yako. Endapo umekuja na vitu kutoka ofisini hakikisha unavifuta maeneo ya juu kwa kitambaa safi kilichochovywa kwenye spiriti au kitakasa mikono. Hii inategemea aina ya vitu ulivyokuja navyo kwani baadhi vinawez akuharibika endapo vitasafishwa kwa vitakasa.


Kwa watu ambao wapo wanaenda makazini, unapoamka na kwenda kazini vaa barakoa yako ya nguo mara unapoondoka nyumbani kwenda ofisini na haikisha unabeba barakoa zingine mbili kwenda nazo. Unapofika ofisini na kufanya shughuli zako hakikisha hushiki barakoa yako sehemu ya mbele. Rekebisha barakoa yako endapo haijakaa vizuri kwa kushika Kamba nyuma ya sikio. Unapotaka kwenda kupata kifungua kinywa, vua barakoa hiyo na kuiweka kwenye ndoo yenye majiya sabuni. Unapomaliza kifungua kinywa vaa barakoa safi, fanya hivi unapotaka kula chakula cha jioni au kunywa maji endapo utatakiwa fanya vitu hivi maeneo ya kazini yenye msongamano wa watu. Hakikisha baada ya masaa mawili unafua barakoa uliyoloweka kwenye ndoo na kuianika kabla ya kuzirudia kuvaa tena.


Vitu ambavyo hutakiwi fanya


  • Kuvua barakoa kisha kuivaa barakoa ile ile kabla ya kufuliwa kweye maji ya sabuni

  • Kushika barakoa maeneo ya mbele

  • Kutunza barakoa iliyotumika kwenye pochi yako ya kutunzia fedha au begi

  • Kurekebisha barakoa ambayo haijakaa vizuri kwa kushika maeneo ya mbele

  • Kuning’iniza barakoa chini au juu ya shingo

  • Kushusha barakoa chini ya pua


Ukifanya hayo yote ni rahisi kujiambukiza endapo kuna virusi au bakteria sehemu ya mbele ya barakoa


Wasiliana na daktari wa uly clinic kwa ushauri wa namna ya kutengeneza barakoa kwa malighafi zilizo karibu na wewe.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasilianane na daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY clinic kwa kupiga namba za simu  au kubonyeza sehemu imeandikwa "Pata tiba" chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

21 Julai 2023 16:18:59

Rejea za mada hii;

1. ULY CLINIC maswali na majibu

2. CDC. https://www.cdc.gov/coronavirus/2019-ncov/prevent-getting-sick/diy-cloth-face-coverings.html. Imechukuliwa 28.06.2020

bottom of page