top of page

Imeandikwa na daktari wa ULYclinic

Ijumaa, 17 Aprili 2020

Estradiol

Estradiol

Utangulizi

Oestradayo (Estradiol) ni homoni yenye nguvu Zaidi na umuhimu katika mfumo wa uzazi wa mwanamke na mwanamme. Homoni ya estradiol hujulikana pia kama Oestradiol au E2 ni moja ya homoni kati ya homoni nne aina ya Estrogen ambazo zingine ni Estrone na Estriol na estetro.

Homoni hii huwa kwa kiwango kikubwa sana kwenye kwa mwanamke na huwa na kazi nyingi ukilinganisha na homoni zingine za estrogen.

Homoni hii huongezeka sana kwenye mfumo wa mzunguko wa hedhi na kusababisha kutolewa kwa yai la kike kutoka kwenye ovary tayari kwa ajili ya kuchavushwa na mbegu ya kiume.

Hufanya kazi ya kukuza ukuta wa kizazi wa endometriamu kwa ajili ya kupokea yai lililorutubishwa, huchochea ukuaji wa tisu za matiti na kuongeza uzito wa mifupa na uimara wake kuwa thabiti

Kiasi cha Estradiol kwa wanawake hupungua kadri mtu anapoongezeka umri kuelekea kipindi cha komahedhi, kipindi hiki tezi za ovari huwa hazifanyi kazi vizuri.

Wakati wa ujauzito homoni hii huzalishwa na plasenta, huongezeka kwa wingi wakati wa ujauzito hadi kufikia wa kujifungua.

Wanaume pia huzalisha Estradiol ila kwa kiasi kidogo kulinganisha na kwa wanawake

Kiwango kidogo cha homoni ya testosterone hubadilishwa na kuwa estradiol ili kusaidia utengenezaji wa manii.

Jinsi uzalishwaji ambavyo huweza kuthibitiwa :

Uzalishwaji wa homoni ya estradiol kwenye ovaria huthibitiwa na tezi ya haipothalamus na pituitari

Haipothalamus hutoa homoni ya Gonadotropin releasing ambayo huchochea tezi ya pituitari kutoa homoni ya Luteinaizing na Follicle stimulating

Homoni ya Luteinaizing na Foliko stimulating huingia kwenye damu na kuchochea ovari kuzalisha homoni ya Estradiol pamoja na kukuza folliko.

Mara baada ya yai kutolewa kwenye ovary, kuta zinazobaki hutengeneza tezi ya kopasi luteamu, tezi hii huanza Kuzalisha homoni ya Estradiol na progesterone. Homoni hizi hufanya kazi ya kuandaa ukuta wa uzazi uwe na mazingira mazuri ya kujipandikiza kwa yai lililorutubishwa na manii.

Kuzidi kwa kiwango cha homoni ya Estradiol Kwa wanawake husababisha dalili za;

• Kuwa na chunusi
• Kuchoka
• Choo kigumu/konstipesheni
• Kukosa hamu ya mapenzi
• Kuwa na hali ya huzuni
• Kuongezeka uzito
• Utasa
• Kiharusi

Kuzidi kwa kiwango cha homoni ya Estradiol kwa wanaume husababisha;

• Matatizo ya kutozalisha manii
• Kuongezeka uzito
• Kuwa na sifa za jinsia ya mwanawake

Wingi wa homoni hii hutokea pale kiasi cha testosterone kinapokuwa chini na hii huweza kupelekea hatari ya kupata saratani ya prostate (tezi dume).

Dalili za upungufu wa homoni ya Estradiol kwa wanawake;

• Kuvunjika mifupa kiurahisi dhidi ya ajali ndogo
• Kuchelewa kubalehe
• Kuchelewa kwa ukuaji wa tisu za matiti
• Kuharibika kwa mzunguko wa hedhi
• Kuwa na hali ya huzuni na kuchoka
• Kutokwa na jasho usiku
• Uke kuwa mkavu

Kwa wale wenye upungufu wa homoni ya striol, wenye saratani ya matiti na tezi dume hupewa dawa homoni ya Estradiol kuthibiti kupata dalili za komahedhi na ukuaji wa saratani.

Kula mboga za majani ,matunda na mboga jamii ya kunde huweza kusaidia katika kuchochea kuzalishwa kwa homoni hii.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliana na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Kwa ushauri zaidi na tiba unaweza kuwasialiana na daktari wa ULY CLINIC kupitia linki ya 'mawasialiano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

17 Aprili 2020 08:35:14

Rejea za mada hii;

bottom of page