top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

Daktari wa ULY Clinic

Daktari wa ULY Clinic

28 Januari 2026, 09:40:40

Glucagon

Glucagon

Glucagon (Glukagon)- Homoni Muhimu ya Kudhibiti Kiwango cha Sukari Kwenye Damu

Glukagon hufahamika kwa lugha nyingine pia kama Glucagon ni homoni muhimu ya mwili inayozalishwa na tezi ya kongosho, hususan katika seli maalum zinazoitwa seli alfa (seli alpha). Homoni hii hufanya kazi kwa karibu sana na homoni ya insulin ili kudhibiti kiwango cha sukari (glukosi) kwenye damu.


Kwa ujumla, glukagon hufanya kazi ya kuongeza kiwango cha glukosi na asidi ya mafuta kwenye damu, hasa pale ambapo mwili unakuwa na upungufu wa sukari au unapohitaji nishati ya haraka.


Glukagon huzalishwa wapi?

Glukagon huzalishwa:

  • Kwenye tezi ya kongosho

  • Ndani ya seli alfa (seli alpha) za kongosho

Baada ya kuzalishwa, huingia kwenye damu na kuelekea hasa kwenye ini, ambako hufanya kazi zake kuu.


Glukagon hutolewa wakati Gani?

Glukagon hutolewa pale ambapo:

  • Kiwango cha sukari kwenye damu kimepungua

  • Mwili unahitaji nishati ya haraka, mfano:

    • Wakati wa njaa

    • Wakati wa kazi ngumu au mazoezi makali

    • Wakati wa msongo wa mwili au tukio la ghafla

Lengo kuu ni kuhakikisha mwili unapata glukosi ya kutosha ili viungo muhimu kama ubongo viendelee kufanya kazi.


Kazi kuu za Homoni ya Glukagon

Glukagon inapokuwa kwenye damu, hufanya kazi zifuatazo:

  • Kuchochea ini kuvunja glailojen kuwa glukosi (glaikojenolisis)

  • Kuchochea glukoneojenesisi, yaani:

    • Kubadilisha amino asidi kuwa glukosi

  • Kuchochea uvunjwaji wa mafuta (lipolisis):

    • Mafuta yaliyohifadhiwa hubadilishwa kuwa asidi ya mafuta kwa ajili ya nishati

Kwa kufanya hivyo, glukagon huhakikisha:

  • Kiwango cha glukosi kwenye damu kinabaki katika hali ya kawaida

  • Shughuli za mwili zinaendelea bila kukosa nishati


Mabadiliko ya kiwango cha Glukagon Kulingana na Lishe

  • Kiwango cha glukagon hupungua:

    • Mtu anapokula vyakula vyenye sukari au wanga kwa wingi

  • Kiwango cha glukagon huongezeka:

    • Mtu anapokula vyakula visivyo na sukari

    • Mtu anapofunga au kuchelewa kula

Kwa wagonjwa wa kisukari:

  • Udhibiti wa glucagon huwa hauko sawa, jambo linalochangia matatizo ya sukari kupanda au kushuka kupita kiasi.


Uhusiano wa Glukagon na Insulin

Glukagon na insulin ni homoni pinzani lakini hufanya kazi kwa ushirikiano:


Baada ya Kula

  • Wanga hubadilishwa kuwa glukosi

  • Kiwango cha glukosi huongezeka kwenye damu

  • Kongosho hutoa insulin

  • Insulin:

    • Hubadilisha glukosi kuwa glaicogen

    • Huihifadhi kwenye ini na misuli


Wakati wa Njaa au Sukari Kushuka

  • Kiwango cha glukosi kinaposhuka

  • Kongosho hutoa glukagon

  • Glukagon:

    • Hubadilisha glycogen kuwa glukosi

    • Huongeza sukari kwenye damu

Kwa pamoja, homoni hizi mbili huhakikisha kiwango cha sukari kwenye damu hakipandi wala kushuka kupita kiasi.


Dalili za Upungufu wa Homoni ya Glukagon

Mtu mwenye kiwango cha chini cha glukagon anaweza kuonyesha dalili zifuatazo:

  • Njaa kali

  • Kutetemeka

  • Woga na wasiwasi

  • Kuchoka haraka

  • Kutokwa na jasho jingi

  • Ngozi kuwa nyeupe

  • Kulala sana

  • Kizunguzungu

Dalili hizi hutokana na upungufu wa sukari kwenye damu (haipoglaisemia).


Dalili za Kuzidi kwa Homoni ya Glukagon

Mtu mwenye kiwango kikubwa cha glukagon anaweza kuwa na dalili kama:

  • Kiu ya maji mara kwa mara

  • Maumivu ya kichwa

  • Kutoona vizuri

  • Kukojoa mara kwa mara

  • Kuchoka na udhaifu wa mwili

  • Kupungua uzito

Kiwango cha juu cha glucagon kwa muda mrefu huweza kuhusishwa na matatizo ya kimetaboliki.


Matibabu ya Upungufu wa Glukagon

Kwa wagonjwa wenye upungufu wa glucagon, hasa wanaopata haipoglaisemia kali:

  • Dawa ya glukagon ya kutengenezwa maabara inaweza kutolewa

  • Hutumika sana kama:

    • Huduma ya dharura kwa wagonjwa wa kisukari

    • Pale ambapo mgonjwa hawezi kumeza sukari kwa mdomo


Umuhimu wa Glukagon katika Afya

Kwa ujumla, glukagon:

  • Ni muhimu kwa udhibiti wa sukari kwenye damu

  • Husaidia mwili kujilinda dhidi ya hypoglycemia

  • Ni homoni muhimu sana kwa:

    • Ubongo

    • Misuli

    • Mfumo wa neva

Bila glukagon, mwili usingeweza kujirekebisha pale sukari inaposhuka.


Hitimisho

Glukcagon ni homoni muhimu inayofanya kazi ya kuongeza kiwango cha sukari kwenye damu pale inapohitajika. Kwa kushirikiana na insulin, homoni hii huhakikisha mwili unapata nishati ya kutosha muda wote. Usawa wa glukagon ni muhimu sana katika afya ya binadamu, hasa kwa wagonjwa wa kisukari na wale wanaopata haipoglaisemia mara kwa mara.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliana na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Kwa ushauri zaidi na tiba unaweza kuwasialiana na daktari wa ULY CLINIC kupitia linki ya 'mawasialiano yetu' chini ya tovuti hii

Imeandikwa;

9 Aprili 2020, 10:46:44

Rejea za mada hii;

  1. Healthline. Insulin and glucagon. Available from: https://www.healthline.com/health/diabetes/insulin-and-glucagon [Accessed 8 Apr 2020].

  2. Mayo Clinic. Glucagon injection. Available from: https://www.mayoclinic.org/drugs-supplements/glucagon-injection-route/description/drg-20064089 [Accessed 8 Apr 2020].

  3. Diabetes UK. Glucagon. Available from: https://www.diabetes.co.uk/body/glucagon.html [Accessed 8 Apr 2020].

  4. Hormone Health Network. Glucagon. Available from: https://www.hormone.org/your-health-and-hormones/glands-and-hormones-a-to-z/hormones/glucagon [Accessed 8 Apr 2020].

  5. Medscape. Glucagon. Available from: https://www.medscape.com/answers/2089114-163731/what-is-glucagon [Accessed 8 Apr 2020].

bottom of page