top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

Daktari wa ULY Clinic

Daktari wa ULY Clinic

28 Januari 2026, 09:40:40

Norepinephrine

Norepinephrine

Norepinephrine, inayojulikana pia kama noradrenaline, ni homoni muhimu inayofanya kazi kama homoni na pia nyurotransimita (mjumbe wa taarifa za mfumo wa fahamu). Homoni hii ina mchango mkubwa katika kurekebisha hali ya moyo, kuongeza umakini, na kusaidia mwili kukabiliana na msongo wa mawazo, hofu na mazoezi.

Norepinephrine hufanya kazi kwa karibu sana na homoni nyingine kama adrenaline ili kuandaa mwili kwa hali ya kupambana au kukimbia (fight or flight).


Norepinephrine Huzalishwa Wapi?

Norepinephrine huzalishwa katika:

  • Tezi ya adreno (adrenal medulla) – sehemu ya ndani ya tezi

  • Mfumo wa neva, hasa kwenye ubongo

Sehemu hii ya tezi ya adreno pia huzalisha homoni nyingine muhimu iitwayo epinephrine (adrenaline).


Familia ya Homoni za Katekolamini

Norepinephrine ipo kwenye kundi la homoni linaloitwa katekolamini, ambalo hujumuisha:

  • Epinephrine (adrenaline)

  • Dopamine


Kazi za Homoni ya Norepinephrine

Norepinephrine ina majukumu mengi muhimu mwilini, yakiwemo:

  • Kuongeza mapigo ya moyo na kusaidia moyo kusukuma damu kwa nguvu

  • Kuongeza shinikizo la damu

  • Kuchochea uvunjaji wa mafuta (lipolysis)

  • Kuongeza sukari kwenye damu na kumpa mtu nguvu zaidi

  • Kwenye ubongo:

    • Kudhibiti mzunguko wa usingizi na kuamka

    • Kuongeza umakini wa kufanya kazi

    • Kuimarisha kumbukumbu

  • Kudhibiti hisia na hali ya moyo

  • Kumpa mtu ujasiri wa kukabiliana na hatari au kukimbia anapokabiliwa na tishio

  • Kutumika kitabibu kuongeza shinikizo la damu endapo litashuka kutokana na dawa au mshtuko (shock)


Upungufu wa Norepinephrine

Kiwango kidogo cha norepinephrine mwilini kinaweza kusababisha:

  • Hali ya huzuni

  • Woga

  • Wasiwasi na msongo wa mawazo

  • Kuishiwa nguvu

  • Kukosa umakini na umakini hafifu


Kuzidi kwa Norepinephrine

Kiwango kikubwa cha norepinephrine kwenye damu kinaweza kupelekea:

  • Hali ya furaha kupita kiasi

  • Kutaharuki

  • Kuongezeka kwa shinikizo la damu


Njia za Asili za Kuongeza Norepinephrine

Baadhi ya njia za asili zinazoweza kusaidia kuongeza kiwango cha norepinephrine ni:

  • Kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara

  • Kulala usingizi wa kutosha

  • Kusikiliza muziki

  • Kupenda na kuhusiana kijamii

  • Kutafakari (meditation)

  • Kula vyakula vinavyoongeza dopamine kama:

    • Chokoleti (kwa kiasi)


Matumizi ya Norepinephrine Kitaalamu

Norepinephrine hutumika kama dawa katika mazingira ya hospitali, hasa kwa:

  • Matibabu ya shoku ya septiki (septic shock) ili kuongeza shinikizo la damu


Dawa na Virutubisho Vinavyoathiri Norepinephrine


Dawa zinazoweza kuongeza norepinephrine:

  • Dawa jamii ya SNRIs, mfano:

    • Duloxetine (Cymbalta)

    • Milnacipran (Savella)

  • Dawa jamii ya amphetamines, mfano:

    • Dextroamphetamine

    • Methylphenidate (Ritalin)


Virutubisho vinavyoweza kusaidia:

  • Rhodiola rosea

  • L-carnitine

  • L-tyrosine

  • L-theanine


Matumizi ya dawa na virutubisho yafanyike chini ya ushauri wa daktari.


Jedwali: Faida na Hasara za Norepinephrine

Faida za Norepinephrine

Hasara za Norepinephrine

Huongeza umakini na nguvu

Kuzidi huongeza shinikizo la damu

Husaidia kukabiliana na msongo wa mawazo

Huchochea kutaharuki

Huimarisha kumbukumbu

Upungufu husababisha huzuni

Huongeza shinikizo la damu wakati wa dharura

Kiwango kisicho sawa huathiri hisia

Muhimu katika fight or flight

Dawa zake huhitaji uangalizi wa kitaalamu


Muhtasari

Norepinephrine (noradrenaline) ni homoni na nyurotransimita muhimu inayodhibiti umakini, shinikizo la damu, hisia na mwitikio wa mwili kwa msongo wa mawazo. Upungufu wake husababisha huzuni na kukosa nguvu, huku kuzidi kwake kukihusishwa na kutaharuki na shinikizo la damu.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliana na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Kwa ushauri zaidi na tiba unaweza kuwasialiana na daktari wa ULY CLINIC kupitia linki ya 'mawasialiano yetu' chini ya tovuti hii

Imeandikwa;

5 Mei 2020, 18:23:27

Rejea za mada hii;

  1. Encyclopaedia Britannica. Norepinephrine. Available from: Encyclopaedia Britannica. Accessed April 14, 2020.

  2. Endocrine Society. Norepinephrine. Available from: Hormone.org. Accessed April 14, 2020.

  3. Everyday Health. Norepinephrine guide. Available from: Everyday Health. Accessed April 14, 2020.

  4. Verywell Health. Norepinephrine: What it does and doesn’t do. Available from: Verywell Health. Accessed April 14, 2020.

  5. Guyton AC, Hall JE. Textbook of Medical Physiology. 14th ed. Philadelphia: Elsevier; 2021.

  6. Katzung BG. Basic & Clinical Pharmacology. 15th ed. New York: McGraw-Hill; 2021.

bottom of page