top of page

Mwandishi;

Mhariri:

Jaza jina na cheo cha mwandishi

Alhamisi, 22 Aprili 2021

Kujifungulia nyumbani- Huduma ya kwanza
Kujifungulia nyumbani- Huduma ya kwanza
Kujifungulia nyumbani- Huduma ya kwanza
Kujifungulia nyumbani- Huduma ya kwanza

Kujifungulia nyumbani- Huduma ya kwanza

Kujifungua nyumbani inatafsiriwa kuwa ni kujifungua eneo lolote nje ya kituo cha afya, na mama hupatiwa huduma kutoka kwa wakunga wa jadi au ndugu na jamaa. Kuna sababu mbalimbali zinazosababisha kujifungu nyumbani hata hivyo kuna athari pia za kujifungulia nyumbani kama vile vifo kwa wajawazito na vichanga hasa katika nchi zinazoendelea.


Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea katika ukanda wa jangwa la sahara yenye vifo vingi vya akina mama na vichanga. Pamoja na juhudi mbalimbali za serikali kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto kupitia mpango mkakati wa Huduma ya Afya ya Mama, Mtoto Mchanga na Mtoto wa mwaka 2016-2020 , bado wakinamama wengi wanajifungua nyumbani na idadi ya vifo vya akina mama na vichanga inaongezeka.


Katika utafiti uliofanyika Dodoma mwaka 2016 ulibaini kuwa asilimia 46.5 ya wajawazito walijifungulia nyumbani bila usaidizi wa mkunga mwenye elimu na uzoefu


Sababu zinazochangia kujifungulia nyumbani

Kutokana na tafiti zilizofanyika hapa Tanzania zifuatazo ni sababu zinazo changia wajawazito kushindwa kujifungua katika vituo vya afya;


Umri wa mama:

Inakadiriwa kuwa wanawake kati ya miaka 20-35 hujifungua nyumbani.


Kiwango cha elimu:

kina mama wasio na elimu na wale wenye elimu ya msingi hujifungua nyumbani ukilinganisha na wenye elimu kwasababu mama aliye elimika hutafuta huduma bora.


Kazi ya mama:

Huchangia sana maamuzi ya sehemu ya kujifungulia, wamama wa nyumbani hujifungua nyumbani ukilinganisha na walio jiajiri na kuajiriwa.


Hali ya ndoa

Kina mama wasioolewa hujifungua nyumbani kwasababu ya kukosa msaada kutoka kwa mume na familia.


Eneo la makazi

Kutokana na miundo mbinu mibovu ya barabara na uhaba wa vituo vya huduma za afya maeneo ya vivijini, wajawazito wengi katika maeneo haya hujifungua nyumbani.


Idadi ya zao

Wanawake wanaobeba ujauzito kwa mara ya kwanza huwa na hofu ya kujifungua, wengi wao hujifungua katika vituo vya afya.Hii ni tofauti na wanawake wenye zao 2 na kuendelea hujiona ni wazoefu na wanaweza kujifungua salama nyumbani, hii hujitokeza sana endapo mama alishawahi kujifungua nyumbani bila kupata madhara yoyote.


Mahudhurio ya kliniki

Wanawake wasiohudhuria kabisa au kuhudhuria kliniki chini ya mara 4 hukosa taarifa muhimu kuhusu mahali pa kujifungulia, hivyo kupelekea kujifungulia nyumbani.


Umbali wa kituo cha afya

Wanawake wanaoishi umbali wa zaidi ya kilomita 5 kutoka kituo cha afya hujifungua nyumbani ukilinganisha na wale waishio karibu.


Mila na desturi

Baadhi ya jamii huwataka wanawake wanao jifungua kwa mara ya kwanza kujifungua nyumbani.


Athari zitokanazo na kujifungulia nyumbani


Zipo athari mbalimbali ambazo kwa ujumla wake hupelekea vifo na madhara mengine kwa mama na vichanga, athari hizo ni ;


Kwa mama

 • Kushindwa kutoka Kondo la nyuma

 • Kupoteza damu nyingi

 • Kuchanika kwa shingo ya mlango wa kizazi

 • Kuchanika msamba (eneo kati ya uke na mlango wa haja kubwa)


Kwa mtoto

 • Kushindwa kupumua vizuri

 • Kuchelewa kulia

 • Kupata maambukizi ya kitovu


Huduma ya kwanza kwa mama aliye au anayetarajia kujifungua nyumbani kwa dharura


Sehemu sahihi na salama ya mama kujifungua ni kituo cha afya au zahanati. Si vema kumsaidia mjamzito kujifungua nyumbani, fanya hivyo endapo tu imetokea kama dharura kutokana na sababu zisizoweza kutatulika kwa wakati. Baada ya huduma ya kwanza hakikisha mama na kichanga wanafika katika kituo cha afya kupatiwa huduma za kitaalamu zaidi.


Hatua za uchungu wa kujifungua (leba)


Hatua ya kwanza

Mama huwa na maumivu ya tumbo la chini yanayosambaa kiunoni, kutokwa na ute ute uliochanganyika na damu, na chupa kuvunjika


Hatua ya pili

Njia yote ya uzazi hufunguka, maumivu huzidi kiwango na mama huhisi kusukuma, kichwa cha mtoto huonekana kwenye uke, na baadae mtoto kuzaliwa


Hatua ya tatu

Kutoka kwa kondo la nyumaMaandalizi


Andaa vifu vifuatavyo kutolea huduma;


 • Kitakasa mikono endapo kinapatikana

 • Maji na sabuni

 • Mipira (glavu) ya kuvaa mikononi kama inapatikana

 • Uzi mnene au kamba ya viatu iliyo safi kwa ajili ya kufunga kitovu

 • Wembe kwa ajili ya kukata kitovu

 • Nguo safi za kumfunikia mtoto

 • Mfuko wa kuwekea kondo la nyumaMambo ya kufanya katika kila hatua za uchungu (leba)


Hatua ya kwanza

 • Mtie moyo na kumuandaa kwa hatua inayofuataHatua ya pili

 • Mlaze mama katika mkao ambao yupo huru kujifungua.

 • Kichwa kinapoanza kuonekana safisha mikono yako na kitakasa mikono au maji yanayotiririka na sabuni, vaa glavu endapo zinapatikana

 • Muhimize mama kusukuma mtoto huku ukiwa umeweka ukinzani eneo la msamba hadi kichwa kitoke chote kikifuatwa na mwili.

 • Mfute mtoto maji maji katika pua na mdomo, hakikisha amelia na anapumua vizuri. Kama anashindwa kupumua mlaze chali na kumsugua sugua kwenye kifua au nyayo, akishindwa kupumua tena mpe hewa kwa njia ya mdomo-kwa mdomo-na-pua. (utahitajika kufanya CPR endapo mtoto atashindwa kupumua, jifunze kwenye kurasa zingine namna ya kufanya CPR ndani ya tovuti hii)

 • Mfute mwili kisha mfunike na mlaze kifuani mwa mama na aanze kumnyonyesha.

 • Funga kitovu sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni umbali wa inchi 4 kutoka kwa mtoto na sehemu ya pili ni umbali wa inchi 2 hadi 4 kutoka ulipofunga kamba ya kwanza kisha kata katikati.

 • Kumbuka kuandika muda mototo alipozaliwaHatua ya tatu

 • Kondo hutoka baada ya muda mfupi, endapo limetoka, hakikisha unaliweka katika mfuko pamoja na damu itakayotoka.

 • Usijaribu kulivuta kwasababu itapelekea kukatika na kuwa vigumu kulitoa au kupelekea mama kupoteza damu nyingi.

 • Muhimize mama kunyonyesha pia umkande kande kizazi kupitia tumbo la chini ili kuzuia damu nyingi kutoka.


Viashiria vya hatari vinavyohitaji msaada wa dharura kutoka kwa wataalamu wa afya


Endapo mama ataonesha viashiria hivi apelekwe hospitali mara moja

 • Kuwa kwenye leba zaidi ya masaa 12

 • Kutokwa na damu kabla mtoto kuzaliwa

 • Kupata degedege

 • Chupa kupasuka na kutoa maji ya rangi ya kijani au maji ya kunde

 • Kitangulizi katika hatua ya pili kuwa ni sehemu zingine za mwili na wala sio kisogo cha mtoto kwa mfano kitovu, uso miguu nk

 • Kondo la nyuma kushindwa kutoka

 • Kutokwa na damu nyingi baada ya kondo kutoka


ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa elimu na ushauri zaidi kabla ya kuchukua thatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa suhauri zaidi kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba'  chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

1 Oktoba 2021 08:12:08

Rejea za mada:

 1. Fabiola Moshi , et al. Prevalence and Factors Associated with Home Childbirth with Unskilled Birth Assistance in Dodoma-Tanzania: A Cross Sectional Study. https://www.researchgate.net/publication/342588657_Prevalence_and_Factors_Associated_with_Home_Childbirth_with_Unskilled birth assistance in Dodoma-Tanzania. Imechukuliwa 20.04.2021

 2. Situ Muhunzi1, et al. Prevalence, predictors and reasons for home delivery amongst womenof childbearing age in Dodoma Municipality in central Tanzania. Inapatikna. https://www.ajol.info/index.php/ahs/article/view/202365/190822. Imechukuliwa 20.04.2021.

 3. Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey 2015-2016.

 4. Fabiola V. Moshi, et al. Determinants for choice of home birth over health facility birth among women of reproductive age in Tanzania: an analysis of data from the 2015-16 Tanzania demographic and health survey and malaria indicator survey. https://bmcpregnancychildbirth.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12884-020-03266-3#ref-CR2. Imechukuliwa 20.04.2021.

 5. Eveline T. Konje, et al. Is it home delivery or health facility? Community perceptions on place of childbirth in rural Northwest Tanzania using a qualitative approach. https://bmcpregnancychildbirth.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12884-020-02967-z. Imechukuliwa 20.04.2021.

 6. Nancy A Scott, et al. Factors affecting home delivery among women living in remote areas of rural Zambia: a cross-sectional, mixed-methods analysis. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6181475/. Imechukuliwa 20.04.2021.

 7. Deneke Delibo, et al. Status of Home Delivery and Its Associated Factors among Women Who Gave Birth within the Last 12 Months in East Badawacho District, Hadiya Zone, Southern Ethiopia. https://www.hindawi.com/journals/bmri/2020/4916421/. Imechukuliwa 20.04.2021.

 8. H Tuladhar etal. Complications of home delivery: a retrospective analysis. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/16554861/. Imechukuliwa 20.04.2021.

 9. Hesperian health guide. A Health Handbook for Women with Disabilities:Danger signs during labor. https://en.hesperian.org/hhg/A_Health_Handbook_for_Women_with_Disabilities:Danger_signs_during_labor. Imechukuliwa 20.04.2021.

bottom of page