Mwandishi;
Mhariri:
Jaza jina na cheo cha mwandishi
Jumanne, 13 Aprili 2021
Kutapika na kuharisha- Huduma ya kwanza
Kuharisha na kutapika ni miongoni mwa dalili zinazoonekana na huashiria magonjwa ya mfumo wa tumbo, au kushiria shida katika mifumo mingine ya mwili. Kuharisha na kutapika husababisha mwili kupoteza maji na chumvi chumvi muhimu za sodium , potassium, bicarbonate na chloride. Watoto na wazee huwa katika hatari zaidi ya kupungukiwa na maji kuliko watu wazima.
Lengo la kutoa huduma ya kwanza kwa mtu anayetapika na kuharisha ni kuzuia kupotea kwa maji na chumvi chumvi. Baada ya huduma ya kwanza unapaswa kumpeleka mgonjwa hospitali kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
Kusoma zaidi kuhusu kuharisha na kutapika rejea katika Makala zingine ndani ya tovuti hii ya ULY CLINIC
Dalili za kupungukiwa na maji kwa watoto zaidi ya miaka mitano na watu wazima
Dalili ashiria huonekana endapo kuna upotevu mkubwa wa madini na chumvi mwilini, hata hivyo, viashiria hutofautiana kulingana na kiwango cha maji na chumvi kilichopotea. Kuna makundi mawili ya dalili ambayo ni
Dalili za kupoteza kiwango kidogo na cha wastani
Dalili za kupoteza kiwango kikubwa kilichopitiliza
Dalili za kupoteza kiwango kidogo na cha wastani cha maji na chumvi mwilinii kutokana na kuharisha na kutapika
Huwa na viashiria vifuatavyo;
Hisia ya kiu
Kukauka midomo
Kupata mkojo kidogo au kukojoa mara chache isivyo kawaida
Kukauka kwa ngozi
Maumivu ya kichwa
Maumivu ya misuli
Dalili za kupoteza kiwango kikubwa kilichopitiliza cha maji na chumvi mwilinii kutokana na kuharisha na kutapika
Kutokea kwa dalili hizi huashiria uhitaji wa kupata matibabu ya dharura, matibabu yake huhusisha kuongezewa maji kwa njia ya mishipa ya damu.
Kama mgonjwa ana viashiria vifuatavyo mpeleke hospitali haraka bila kusubiria au piga namba za simu za dharura ili uje kupatiwa huduma ya dharura;
Kukojoa mkojo kidogo wenye rangi ya manjano-nyeusi, wenye harufu au kukosa mkojo kabisa
Ngozi kukauka sana
Kuhisi kizunguzungu
Mapigo ya moyo kwenda mbio
Kupumua haraka haraka
Kuishiwa nguvu, kuchanganyikwa au kuwa mkali na hasira
Kukauka sana midomo
Kwa watoto kutotoa machozi wakati analia
Macho kudumbukia ndani
Kuzirai
Namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mtoto/mtu anayetapika na kuharisha
Maji ya kunywa yaliyo safi na salama
Kwa mtu mzima mpatie maji ya kutosha na vimiminika kama juisi, soda nk. Epuka kumpa maziwa au vyakula vyenye maziwa, pombe, juisi ya tufaa na vinywaji vyenye kafeini kwani huzidisha kuharisha
Mpatie mtoto maji na anywe kidogo kidogo mara nyingi, akiendelea kutapika na kuharisha mpe maji yenye mchanganyiko wa sukari na chumvi kama vile ORS
Iwapo huna ORS tengeneza kwa kuchanganya vijiko 6 vya sukari vyenye mfuto na kijiko 1 cha chumvi nusu mfuto (tumia kijiko cha chai kupima) kwenye lita moja ya maji ya kunywa kisha koroga na hifadhi katika chombo safi. Mpe anywe kila mara kadri awezavyo hii itamsaidia kuzuia kupotea kwa madini kwenye damu. Maji haya huweza kutumika kwa mtu mzima pia
Hakikisha anapata kiasi kikubwa cha maji kuliko anachopoteza kwa kutapika au kuharisha
Muda wa kupumzika
Hakikisha anapumzika vya kutosha. Muwekee chombo karibu iwapo anatapika au kuharisha mara kwa mara.
Chakula
Mpatie mtoto chakula ambacho kina uwezowa wa kumeng’enywa kwa urahisi mfano mayai, ndizi, wali mweupe, na samaki.
Kwa mtu mzima mpatie chakula laini na chenye kiwango kidogo cha nyuzi nyuzi, mfano tikiti, tango, papai, karoti, juisi ya matunda iliyochujwa n.k.
Epuka kumpa chakula chenye viungo, mafuta mengi au vyakula vyenye asili ya mafuta kwani huzidisha kuharisha.
Mpeleke mgonjwa hospitali haraka endapo
Anaonesha dalili za kupoteza kiwango kikubwa kilichopitiliza cha maji na chumvi
Ni mtoto mchanga
Anaharisha au kutapika damu
ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa elimu na ushauri zaidi kabla ya kuchukua thatua yoyote baada ya kusoma makala hii
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa suhauri zaidi kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba' chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
1 Oktoba 2021 08:12:09
Rejea za mada:
11 foods that are easy to digest. https://www.medicalnewstoday.com/articles/319947#rice. Imechukuliwa 13.04.2021
Diarrhea Treatment. https://www.webmd.com/first-aid/diarrhea-treatment. Imechukuliwa 13.04.2021
Family doctor. Vomiting and Diarrhea. https://familydoctor.org/condition/vomiting-and-diarrhea/amp/. Imechukuliwa 13.04.2021
Luis Tello, et al. Fluid and Electrolyte Therapy During Vomiting and Diarrhea. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC7185384/. Imechukuliwa 13.04.2021
Dehydration. https://www.nhs.uk/conditions/dehydration/. Imechukuliwa 13.04.2021
British Red Cross. Learn first aid for a baby or child who is vomiting and has diarrhoea. https://www.redcross.org.uk/first-aid/learn-first-aid-for-babies-and-children/vomiting-and-diarrhoea. Imechukuliwa 13.04.2021
What is Dehydration? What Causes It?. https://www.webmd.com/a-to-z-guides/dehydration-adults. Imechukuliwa 13.04.2021
Rehydration project. How do I prepare an Oral Rehydration Salts ORS solution at home?. https://rehydrate.org/faq/how-to-prepare-ors.htm. Imechukuliwa 13.04.2021