top of page

Mwandishi;

Mhariri:

Imeboreshwa

ULY CLINIC

ULY CLINIC

23 Agosti 2026, 11:48:02

Namna ya kufanya CPR
Namna ya kufanya CPR
Namna ya kufanya CPR
Namna ya kufanya CPR

Namna ya kufanya CPR

CPR, yaani ufufuaji wa moyo na mapafu, ni hatua za dharura zinazofanywa kwa mtu aliyepoteza fahamu na ambaye hapumui kawaida, ili kuendeleza mzunguko wa damu na oksijeni kwenda kwenye ubongo na viungo muhimu wakati akisubiri huduma ya kitaalamu. CPR inapaswa kuanza haraka inaposhukiwa kuwa mtu amepata mshtuko wa moyo na amesimama kupumua kawaida.


Kwa mtu mzima anayepatikana akiwa hajitambui na hapumui kawaida, usichelewe kuanza CPR kwa sababu ya kuogopa kumuumiza. Kupumua kwa kushtuka-shtuka, kwa nguvu au kwa vipindi visivyo vya kawaida hakuchukuliwi kuwa kupumua kawaida katika hali hii na kunaweza kutokea wakati wa mshtuko wa moyo.

Muhimu: Makala hii inaeleza huduma ya kwanza kwa mtu mzima. CPR kwa mtoto na mtoto mchanga ina tofauti muhimu, hivyo inapaswa kujifunzwa kwa mwongozo maalumu.

CPR inahitajika wakati gani?

Mtu anaweza kuhitaji CPR ikiwa:

  • Ameanguka au amezimia ghafla na hajibu unapomuita au kumgusa.

  • Hapumui kabisa.

  • Anapumua kwa kushtuka-shtuka, kwa kukoroma au kwa namna isiyo ya kawaida.

  • Haonyeshi dalili nyingine za kawaida za uhai kama kupumua kawaida, kufungua macho, kuongea, kusogea kwa makusudi au kuitikia anapoitwa au kuguswa.

Usitumie muda mrefu kujaribu kutambua mapigo ya moyo ikiwa wewe si mtaalamu wa afya. Kwa mtu asiyejibu na anayepumua isivyo kawaida, chukulia hali hiyo kama dharura ya mshtuko wa moyo na anza CPR.


Hatua za kwanza kabla ya kuanza CPR


1. Hakikisha eneo ni salama

Kabla ya kumfikia mtu, angalia kama kuna hatari kwako, kwake au kwa watu wengine, kama umeme, moto, magari au mazingira mengine hatari.


Usijitie kwenye hatari ili kumsaidia mtu kwa sababu unaweza kuwa mhanga wa pili.


2. Angalia kama anaitika

Mkaribie na umguse begani kwa upole huku ukimwita kwa sauti, kwa mfano:

“Unaendelea vizuri? Unanisikia?”

Ikiwa hajibu, chukulia kuwa amepoteza fahamu.


3. Omba msaada mara moja

Mwambie mtu mwingine:

“Piga simu 112 na ulete AED kama ipo.”

Ikiwa uko peke yako, piga huduma ya dharura na tumia kipaza sauti cha simu ili uweze kuendelea kusaidiwa kwa maelekezo wakati unaanza CPR. Mtoa huduma wa dharura anaweza pia kukuelekeza hatua za kufanya.


Angalia upumuaji

Angalia kifua na tumbo kuona kama vinapanda na kushuka kwa namna ya kawaida.


Usipoteze muda mwingi ukichunguza upumuaji. Ikiwa mtu hajitambui na hapumui kawaida, anahitaji CPR. Kupumua kwa kushtuka-shtuka au kwa nguvu zisizo za kawaida hakumaanishi kwamba mtu anapumua kawaida.


Ikiwa anaendelea kupumua kawaida lakini hajitambui, hali hiyo si sawa na mshtuko wa moyo; mweke katika pozi la kupona na endelea kumfuatilia wakati msaada wa kitaalamu ukiitwa.


Namna ya kufanya CPR kwa mtu mzima

Ikiwa mtu hajitambui na hapumui kawaida, anza CPR mara moja. CPR inahusisha migandamizo ya kifua na, kwa mtu aliyefundishwa na aliye tayari kufanya hivyo, pumzi za uokoaji za mdomo kwa mdomo.

Namna ya kufanya CPR kuokoa maisha
Namna ya kufanya CPR kuokoa maisha

Hatua ya 1: Mlaze kwenye sehemu inayofaa

Mlaze chali kwenye sehemu tambarare na imara ikiwezekana.

Ikiwa tayari amelala kwenye kitanda au sehemu nyingine ambayo si rahisi kumhamisha, usicheleweshe CPR kwa kujaribu kumhamisha bila sababu; anza migandamizo mara moja.


Hatua ya 2: Weka mikono katikati ya kifua

  • Kaa au piga magoti pembeni yake.

  • Weka kisigino cha kiganja cha mkono mmoja katikati ya kifua, kwenye sehemu ya chini ya mfupa wa kifua.

  • Weka mkono mwingine juu ya mkono wa kwanza.

  • Ingisha vidole vya mikono miwili ili visiweke shinikizo kwenye mbavu.

  • Weka mabega yako moja kwa moja juu ya mikono yako.

  • Nyosha mikono kwenye viwiko.


Hatua ya 3: Kandamiza kifua

Kandamiza kifua:

  • Kwa kina cha sentimita 5–6.

  • Kwa kasi ya migandamizo 100–120 kwa dakika.

  • Tumia uzito wa mwili wako badala ya kutumia nguvu za mikono pekee.

  • Ruhusu kifua kirudi kikamilifu baada ya kila mbano.

  • Epuka kuegemeza uzito wako kwenye kifua kati ya migandamizo.

  • Punguza kusitisha migandamizo kadiri iwezekanavyo.

Kasi ya migandamizo inaweza kukumbukwa kama takribani migandamizo2 kwa sekunde.


Hatua ya 4: Mpe pumzi za uokoaji

Ikiwa umejifunza CPR na uko tayari kutoa pumzi za uokoaji, baada ya kufanya migandamizo 30 ya kifua, mpe pumzi 2 za mdomo kwa mdomo.

Fanya hivi:

  1. Fungua njia ya hewa kwa kuinua kidevu na kusukuma kichwa nyuma kwa upole.

  2. Bana pua yake kwa vidole vyako.

  3. Funika mdomo wake wote kwa mdomo wako ili hewa isitoke.

  4. Puliza hewa kwa takribani sekunde 1, kiasi cha kutosha kuona kifua kikianza kuinuka.

  5. Ondoa mdomo wako na uruhusu hewa itoke.

  6. Mpe pumzi ya pili kwa namna hiyo.

  7. Endelea na migandamizo 30 ikifuatiwa na pumzi 2.


Usipulize hewa nyingi au kwa nguvu kupita kiasi, kwa sababu hewa inaweza kwenda tumboni na kusababisha kutapika au matatizo mengine.


Ikiwa hujafundishwa kutoa pumzi za uokoaji, huwezi au hutaki kufanya pumzi za mdomo kwa mdomo, usicheleweshe CPR. Endelea na migandamizo ya kifua pekee huku ukisubiri msaada wa kitaalamu. Pumzi za uokoaji ni muhimu, lakini kuchelewesha kuanza migandamizo kwa sababu huwezi kutoa pumzi kunaweza kuwa hatari.


Mpangilio rahisi wa kukumbuka

migandamizo 30 → pumzi 2 → migandamizo 30 → pumzi 2 → endelea.

Endelea CPR hadi mtu aanze kupumua kawaida, kufungua macho, kuongea au kufanya harakati zenye maana, au hadi msaada wa kitaalamu ufike.


Kwa nini ni muhimu kuachia kifua kirudi?

Baada ya kukandamiza kifua, usiendelee kukiegemezea uzito wako. Ruhusu kifua kirudi kwenye nafasi yake ya kawaida huku ukiacha mikono yako ikiwa kwenye kifua.

Hii husaidia moyo kujazwa tena na damu kabla ya mbano unaofuata. Kwa hiyo CPR bora si “kandamiza tu”, bali ni kandamiza na kuachia kikamilifu kwa mpangilio unaoendelea.


CPR ya mikono pekee

Ikiwa hujafundishwa CPR kamili au huwezi kufanya pumzi za uokoaji, unaweza kufanya CPR ya mikono pekee kwa mtu mzima:


Kandamiza katikati ya kifua kwa nguvu na kwa kasi ya migandamizo 100–120 kwa dakika bila kuacha, huku ukiomba msaada wa dharura na kifaa cha umme cha kuamsha moyo yaani AED.


Hii ni muhimu kwa mtu ambaye hajafundishwa kutoa pumzi za uokoaji, au ambaye hataki kufanya pumzi za mdomo kwa mdomo. Jambo muhimu zaidi ni kutochelewesha kuanza migandamizoya kifua.


CPR yenye pumzi za uokoaji

Mtu aliyefundishwa CPR anaweza kufanya: Migandamizo30 → pumzi 2 → migandamizo 30 → pumzi 2

na kuendelea na mzunguko huo. Kila pumzi ya uokoaji inapaswa kudumu takribani sekunde moja na kuwa kiasi cha kutosha kufanya kifua kianze kuinuka. Epuka kupuliza hewa nyingi kupita kiasi.


Ikiwa hujafundishwa au huwezi kutoa pumzi za uokoaji, endelea na CPR ya mikono pekee badala ya kutofanya chochote.


Tumia kifaa cha umeme cha kuamsha moyo(AED) ikiwa inapatikana

AED ni kifaa kinachoweza kutambua baadhi ya aina za mapigo hatari ya moyo na kutoa mshtuko wa umeme inapohitajika.

Ikiwa AED ipo:

  1. Mwambie mtu alete AED bila kuchelewa.

  2. Endelea na CPR wakati kifaa kinaletwa.

  3. Washa AED.

  4. Bandika pedi zake kwenye kifua kama maelekezo ya kifaa yanavyoonyesha.

  5. Fuata maelekezo ya sauti au picha ya AED.

  6. Hakikisha hakuna anayemgusa mtu wakati AED inapochambua mapigo au inapotoa mshtuko.

  7. Anza tena CPR mara moja baada ya kifaa kuruhusu kuendelea.

Mtu wa kawaida anaweza kutumia AED; si lazima awe mtaalamu wa afya au awe na mafunzo ya hali ya juu.


Unaendelea CPR mpaka lini?

Endelea kutoa CPR hadi:

  • Mtu aanze kuonyesha dalili za kuamka au kusogea.

  • Aanze kupumua kawaida.

  • Mtaalamu wa afya achukue jukumu.

  • AED au mtaalamu akuambie usimamishe.

  • Uwe umechoka kiasi kwamba huwezi kuendelea.

  • Eneo liwe hatari na si salama kuendelea.

Ikiwa kuna waokoaji wawili au zaidi waliofunzwa, wanaweza kubadilishana anayefanya migandamizo ili kupunguza uchovu na kusaidia kudumisha ubora wa CPR.


Mambo usiyofanya wakati wa CPR

  • Usichelewe kuanza CPR kwa kusubiri mtaalamu afike.

  • Usikatishe migandamizo mara kwa mara bila sababu.

  • Usikandamize upande wa mbavu badala ya katikati ya kifua.

  • Usiegemee kifua baada ya kila mbano; kiruhusu kirudi kikamilifu.

  • Usitumie kasi ya juu kupita kiasi.

  • Usipulize hewa nyingi wakati wa pumzi za uokoaji.

  • Usimpe mtu aliyepoteza fahamu chakula, maji au dawa kwa mdomo.

  • Usisimamishe CPR kwa sababu unaogopa kuvunja mbavu ikiwa mtu hana dalili za uhai; kuanza CPR kwa wakati ni muhimu zaidi.


CPR inaweza kuvunja mbavu?

Ndiyo, jeraha la mbavu linaweza kutokea wakati wa CPR, hasa kwa sababu migandamizo inapaswa kuwa na nguvu na kufikia kina kinachohitajika.


Hata hivyo, hofu ya kusababisha jeraha haipaswi kukuzuia kuanza CPR kwa mtu ambaye hajitambui na hapumui kawaida. Bila CPR, mtu aliyepata mshtuko wa moyo anaweza kufariki ndani ya muda mfupi. Miongozo ya sasa inasisitiza kwamba hatari ya kutofanya CPR ni kubwa zaidi kuliko hofu ya kusababisha jeraha kutokana na CPR.


Ikiwa mtu anapata degedege wakati wa kupoteza fahamu

Usijaribu kumshikilia kwa nguvu au kuweka kitu mdomoni. Baada ya degedege kuisha, tathmini kama anapumua kawaida na kama anaitika.

Ikiwa hajitambui na hapumui kawaida, fuata hatua za CPR. Ikiwa anapumua kawaida lakini bado hajitambui, mfuatilie na mweke katika hali inayosaidia kuweka njia ya hewa wazi huku ukisubiri msaada wa kitaalamu.


Ikiwa mtu amezama kwenye maji

Mtu aliyezama anaweza kuwa amepata tatizo la kupumua kabla moyo kusimama. Katika hali hiyo, huduma ya haraka ya uokoaji, kufungua njia ya hewa na CPR ni muhimu.

Usijiweke hatarini wakati wa kumuokoa mtu aliyezama. Ikiwa tayari amefikishwa sehemu salama na hajitambui na hapumui kawaida, anza CPR na omba huduma ya dharura mara moja.


Hitimisho

Mtu mzima asiyetambua na asiyepumua kawaida anahitaji msaada wa haraka: omba huduma ya dharura, anza migandamizo ya kifua katikati ya kifua kwa kina cha sentimita 5–6 na kasi ya 100–120 kwa dakika, huku ukiruhusu kifua kirudi kikamilifu baada ya kila mbano.


Ikiwa umefundishwa, ongeza pumzi za uokoaji kwa uwiano wa migandamizo 30 na pumzi 2; ikiwa huwezi kutoa pumzi za uokoaji, endelea na CPR ya mikono pekee na tumia kifaa cha umeme cha kuamsha moyo haraka kinapopatikana. Usichelewe kuanza CPR kwa kuogopa kumuumiza mtu—kutofanya chochote wakati wa mshtuko wa moyo ni hatari zaidi. 


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu CPR

1. Kwa nini mtu anayepumua kwa kushtuka-shtuka anapaswa kupewa CPR?

Kupumua kwa kushtuka-shtuka, kukoroma au kuvuta pumzi kwa vipindi visivyo vya kawaida kunaweza kutokea katika dakika za mwanzo baada ya moyo kusimama. Hii si sawa na kupumua kawaida, hata kama mtu anaonekana kama anavuta hewa.


Tatizo ni kwamba mtu wa kawaida anaweza kudhani kuwa bado anapumua na hivyo kuchelewesha CPR. Katika mshtuko wa moyo, moyo hauzungushi damu kwa ufanisi kwenda kwenye ubongo na viungo vingine, hivyo kila dakika bila msaada inaweza kuwa muhimu.


Kwa hiyo, ikiwa mtu hajitambui na upumuaji wake unaonekana wa ajabu au usio wa kawaida, usisubiri kuona kama utapona wenyewe. Omba msaada wa dharura na anza hatua za CPR huku ukifuata maelekezo ya mhudumu wa dharura.

2. Kwa nini mtu anaweza kufa ikiwa CPR haijaanzishwa mapema?

Moyo unaposhindwa kusukuma damu, ubongo na viungo vingine muhimu havipati oksijeni ya kutosha. CPR hairejeshi kila mara moyo katika hali ya kawaida, lakini migandamizo ya kifua inaweza kusaidia kuendeleza mtiririko wa damu kwa muda wakati msaada mwingine kama AED na matibabu ya kitaalamu yakisubiriwa.


Ndiyo maana CPR ya mtu aliyepata mshtuko wa moyo inapaswa kuanza mapema iwezekanavyo. Kuomba ambulance pekee bila kuanza CPR kunaweza kuacha ubongo na viungo vingine bila mzunguko wa damu unaohitajika.


Kwa upande mwingine, CPR pamoja na matumizi ya AED inapopatikana inaweza kuongeza nafasi ya kuishi. Miongozo ya sasa inasisitiza umuhimu wa kutambua mshtuko wa moyo mapema, kuomba msaada na kuanza CPR bila kuchelewa.

3. Je, mtu anaweza kuanza CPR bila kujua kama moyo wake umesimama kweli?

Mtu asiye mtaalamu wa afya hapaswi kupoteza muda mrefu akijaribu kuthibitisha mapigo ya moyo. Ikiwa mtu hajitambui na hapumui kawaida, hali hiyo inapaswa kuchukuliwa kama mshtuko wa moyo na CPR ianze.


Hii ni kwa sababu kutambua mapigo ya moyo kwa kugusa kunaweza kuwa kugumu kwa mtu ambaye hajafundishwa. Pia, kuchelewa kuanza CPR kunaweza kuwa na madhara makubwa kuliko kuanza CPR kwa mtu ambaye hatimaye atagundulika kuwa hakuwa katika mshtuko wa moyo.


Kwa hiyo, kwa mtoa huduma wa kwanza, kanuni rahisi ni: hajitambui + hapumui kawaida = omba msaada na anza CPR. Ikiwa mhudumu wa dharura yuko kwenye simu, fuata maelekezo yake.

4. Kwa nini kina cha migandamizo kinapaswa kuwa sentimita 5 hadi 6?

Migandamizo inapaswa kuwa na kina cha kutosha ili kubadilisha shinikizo ndani ya kifua na kusaidia damu kusukumwa kwenda kwenye viungo muhimu. Migandamizo ya juu juu sana inaweza isiwe na ufanisi wa kutosha.


Kwa mtu mzima, miongozo ya sasa inapendekeza kina cha angalau sentimita 5 lakini kisizidi sentimita 6. Hii ndiyo sababu si sahihi kufanya migandamizo myepesi kwa kuogopa kumuumiza mtu.


Hata hivyo, kusukuma kwa nguvu kupita kiasi si lengo. Migandamizo inapaswa kuwa katika kina kinachopendekezwa, kwa kasi sahihi, na kifua kiruhusiwe kurudi kikamilifu baada ya kila mbano.

5. Kwa nini kasi ya CPR ni 100–120 kwa dakika?

Kasi hii husaidia kupata uwiano unaofaa kati ya kusukuma damu mara kwa mara na kutoa muda wa moyo kujazwa tena kati ya migandamizo. Kasi ya chini sana inaweza kupunguza idadi ya migandamizo inayopatikana kwa muda, wakati kasi ya juu sana inaweza kuathiri kina na ubora wa migandamizo.


Kwa mtu anayefanya CPR, kukumbuka takribani migandamizo miwili kwa sekunde kunaweza kusaidia kupata kasi inayokaribia kiwango kinachopendekezwa.


Mtoa huduma hapaswi kujikita kwenye kuhesabu kwa ukamilifu kiasi cha kusababisha kusita au kuchelewesha CPR. Ubora wa migandamizo, kina kinachofaa na kupunguza mapumziko ni muhimu pia.

6. Kwa nini pumzi za uokoaji zinaweza kuwa changamoto kwa mtu ambaye hajafundishwa?

Pumzi za uokoaji zinahitaji kufungua njia ya hewa, kufunga mdomo vizuri na kutoa kiasi kinachofaa cha hewa. Mtu ambaye hajafundishwa anaweza kuogopa, kushindwa kufanya mbinu hiyo vizuri au kuchelewesha migandamizo ya kifua.


Ndiyo maana kwa mtu mzima aliyepata mshtuko wa moyo, CPR ya mikono pekee ni chaguo muhimu kwa mtu ambaye hajafundishwa CPR kamili au hawezi kutoa pumzi za uokoaji.


Hata hivyo, mtu aliyefundishwa CPR anaweza kufanya migandamizo pamoja na pumzi za uokoaji. Jambo la msingi ni kutoruhusu kutoweza kutoa pumzi za uokoaji kukuzuie kufanya chochote.

7. Kwa nini AED inapaswa kutumika mapema inapopatikana?

Baadhi ya mishtuko ya moyo husababishwa na mabadiliko hatari ya mfumo wa umeme wa moyo ambayo yanaweza kurekebishwa kwa mshtuko wa umeme. AED inaweza kuchambua mapigo ya moyo na kuamua ikiwa mshtuko wa umeme unahitajika.


AED haipaswi kutumiwa bila kufuata maelekezo yake. Kifaa hutoa maelekezo ya hatua kwa hatua na humwelekeza mtumiaji wakati wa kutomgusa mgonjwa.


CPR na AED hufanya kazi kwa pamoja: CPR husaidia kudumisha mzunguko wa damu wakati msaada unasubiriwa, huku AED ikitoa matibabu ya umeme inapofaa. Kwa hiyo, mtu mwingine anapaswa kupewa jukumu la kutafuta AED wakati mtu mwingine akiendelea na CPR.

8. Kwa nini mtu aliyefufuka baada ya CPR bado anahitaji hospitali?

Kuanza kupumua au kuonyesha dalili za kuamka baada ya CPR ni jambo la kutia moyo, lakini haimaanishi kwamba chanzo cha tatizo kimekwisha.


Mshtuko wa moyo unaweza kuwa umetokana na tatizo kubwa kama ugonjwa wa moyo, tatizo la mpangilio wa mapigo ya moyo, kuzama, tatizo la upumuaji au sababu nyingine. Pia, ubongo na viungo vingine vinaweza kuwa vimeathiriwa na ukosefu wa oksijeni.


Kwa hiyo, mtu aliyerudisha fahamu baada ya CPR anahitaji tathmini ya kitabibu hata kama anaonekana ameimarika. Usimwache aende nyumbani bila tathmini baada ya tukio kubwa kama hilo.

9. Je, CPR inaweza kufanywa na mtu ambaye hajawahi kuhudhuria mafunzo?

Mtu ambaye hajawahi kufanya mafunzo anaweza kuanza CPR ya mikono pekee kwa mtu mzima ambaye hajitambui na hapumui kawaida. Miongozo inasisitiza kwamba kila mtu anaweza kujifunza CPR na kwamba hofu ya kumuumiza mtu isiwe sababu ya kutofanya chochote.


Hata hivyo, kusoma maelekezo pekee hakufanyi mtu awe na ujuzi wa vitendo sawa na mtu aliyefanya mafunzo. CPR ni ujuzi unaoboreshwa sana kwa kufanya mazoezi kwenye kifaa maalumu cha mafunzo.


Kwa hiyo, watu wanashauriwa kuhudhuria mafunzo ya CPR yanayojumuisha mazoezi ya vitendo. Hii huongeza uwezo wa kuweka mikono sehemu sahihi, kutumia kina kinachofaa na kufanya CPR kwa utulivu wakati wa dharura.

10. Nifanye nini ikiwa nimeanza CPR lakini nachoka?

CPR inaweza kuchosha sana kwa sababu inahitaji kutumia nguvu na kudumisha kasi ya migandamizo kwa muda. Ikiwa kuna mtu mwingine aliyefundishwa, mnaweza kubadilishana anayefanya migandamizo ili kudumisha ubora wa CPR.


Mabadiliko yanapaswa kufanyika kwa haraka ili kupunguza muda ambao migandamizo imesimama. Mtu mwingine anaweza pia kupewa jukumu la kuwasiliana na huduma ya dharura, kutafuta kifaa cha umeme cha kuamsha moyo au kufuatilia maelekezo ya mhudumu wa dharura.


Ikiwa uko peke yako na umechoka sana kiasi kwamba huwezi kuendelea, endelea kadiri unavyoweza huku ukifuata maelekezo ya huduma za dharura. Usisimamishe CPR kwa sababu tu huoni mabadiliko ya haraka, kwa sababu mtu anaweza kuhitaji CPR kwa muda kabla ya kurejesha dalili za uhai.


ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa elimu na ushauri zaidi kabla ya kuchukua thatua yoyote baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa suhauri zaidi kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba'  chini ya tovuti hii

Imeandikwa;

23 Agosti 2026, 11:33:56

Rejea za mada:

  1. Smith CM, Rogers J, Klaassen B, Perkins G, Scott M, Thomas L, et al. Adult basic life support guidelines. London: Resuscitation Council UK; 2025 [cited 2026 Aug 23]. Available from: Resuscitation Council UK

  2. American Heart Association. 2025 AHA guidelines for CPR and ECC: adult basic life support algorithm for health care professionals [Internet]. Dallas (TX): American Heart Association; 2025 [cited 2026 Aug 23]. Available from: American Heart Association

  3. American Heart Association. Treatment of cardiac arrest [Internet]. Dallas (TX): American Heart Association; 2025 [cited 2026 Aug 23]. Available from: American Heart Association

  4. American Heart Association. Highlights of the 2025 American Heart Association guidelines for CPR and emergency cardiovascular care [Internet]. Dallas (TX): American Heart Association; 2025 [cited 2026 Aug 23]. Available from: American Heart Association

  5. Perkins G, Benson Clarke A. Executive summary of the main changes since the 2021 guidelines. London: Resuscitation Council UK; 2025 [cited 2026 Aug 23]. Available from: Resuscitation Council UK

  6. Djarv T, Rogers J, Semeraro F, Brädde L, Cassan P, Cimpoesu D, et al. European Resuscitation Council guidelines 2025: first aid. Resuscitation. 2025;215(Suppl 1):110752. doi:10.1016/j.resuscitation.2025.110752. Available from: Resuscitation Council UK

  7. Smyth MA, van Goor S, Hansen CM, Fijačko N, Nakagawa NK, Raffay V, et al. European Resuscitation Council guidelines 2025: adult basic life support. Resuscitation. 2025;215(Suppl 1):110771. Available from: Resuscitation Council UK

  8. Soar J, Böttiger BW, Carli P, Carmona Jiménez F, Cimpoesu D, Cole G, et al. European Resuscitation Council guidelines 2025: adult advanced life support. Resuscitation. 2025;215(Suppl 1):110769. Available from: Resuscitation Council UK

bottom of page