Mwandishi;
Mhariri:
Imeboreshwa
Dkt. Sospeter B, MD
Dkt. Salome A, MD
2 Aprili 2026, 12:09:07

Tiba ya kuvia damu kutokana na majeraha
Kwa kawaida, kuvia kwa damu chini ya ngozi huisha bila matibabu ndani ya siku 10 hadi 14 kwa mtu mwenye afya njema. Baadhi ya watu, damu iliyovia huweza kuendelea kwa muda mrefu hata kama wana afya njema.
Kuvia damu chini ya ngozi kutokana na majeraha mbalimbali kama kuanguka, kupigwa au madhara ya matibabu huweza harakiswa uponyaji wake kwa dawa, upasuaji au matibabu ya nyumbani. Hata hivyo baadhi ya sehemu za mwili zinaweza kubaki na alama endapo damu iliyovia ni nyingi
Nini cha kufanya ili kuharakisha damu iliyovia kupotea?
Muda mfupi baada ya kupata majeraha kwenye ngozi, mwili huamsha mfumo wa kinga ili kufanya kazi yake ya kufyonza na kuondoa damu hiyo mara moja. Mchakato huu huchukua muda mrefu hivyo damu iliyovia huchelewa kuisha.
Endapo mwathirika wa tatizo hili atapata matibabu mapema zaidi, anaweza kupunguza muda wa kupotea kwa damu iliyovia.
Kupata matibabu kwa njia zifuatazo ndani ya masaa 48 kufuatia kuvia kwa damu chini ya ngozi huharakisha kutokea kwa uponyaji;
Kukanda eneo lililovia damu kwa barafu- hufanya mishipa ya damu isinyae na hivyo damu kutoendelea kuvia
Endapo muda umepita zaidi ya masaa 48 tumia maji ya moto kukanda eneo lenye mvio wa damu- kufanya hivyohusaidia kuongeza mzunguko wa damu ambao utaondoa damu iliyovia.
Kupaka mafuta ya vitamin K
Matumizi ya bromelain
Kama huwezi pata dawa zakuvia damu ufanyaje?
Endapo huwezi pata dawa zilizoorodheshwa hapo juu unaweza kutumia vitu mbadala kama;
Kupaka mafuta ya arnica angalau mara mbili kwa siku au
Paka maji ya alovera yaliyoandaliwa muda si mrefu. Paka mara mbili hadi tatu kwa siku kwenye eneo lenye mvio wa damu
Kunywa vidonge vya vitamin C. Kunywa vidonge au kupaka krimu au mafuta yenye vitamin C husaidia kuondoa michomo kutokana na kinga ya mwili hivyo kuharakisha uponyaji
Kula nanasi kwa wingi katika mlo wako au paka maji yake. Dawa bromelain imetengenezwa kutoka kwenye kiini cha nanasi ambayo huharakisha uponyaji kwa kuzuia michomo inayotokana na kinga za mwili.
Kula matunda na mboga za majani kwa wingi ili kupata virutubisho vingine muhimu kwa ajili ya mwili wako kufanya kazi vema ya kuondoa majeraha.
Usisahau kutumia vya kula jamii ya protini ambayo ni muhimu kurejesha tishu zilizokufa kwa majeraha. Tumia protini kutoka kwenye nyama nyeupe kama inavyoshauriwa kwenye tafiti mbalimbali.
Matibabu ya uvimbe wa kuvia damu
Kuvia damu nyingi kuliko kawaida husababisha uvimbe chini ya ngozi wenye jina la hematoma. Hematoma huonekana kama uvimbe wenye rangi nyeusi au zambarau chini ya ngozi wenye uwezo wa kuleta mgandamizo sehemu ulipotokea. Matibabu ya hematoma hufanywa na mtaalamu wa afya kwa kufyonzwa damu iliyovia kwa kutumia sindano.
Wakati gani uonane na daktari endpo umevia damu kwenye ngozi?
Kama umevia damu kutokana na majeraha ya kuanguka, kupigwa au matibabu, onana na daktari wako haraka endapo;
Kudumu kwa maumivu licha ya kupat amajeraha kidogo
Uvimbe umetokea kwenye eneo lililovia damu
Unapata mkojo wenye damu
Unapata kinyesi cheusi au chenye damu
Unapata maumivu ya kichwa au umepoteza fahamu ndani ya masaa 24
ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa elimu na ushauri zaidi kabla ya kuchukua thatua yoyote baada ya kusoma makala hii
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa suhauri zaidi kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba' chini ya tovuti hii
Imeandikwa;
2 Aprili 2026, 12:09:07
