Kamusi Tiba ya ULY CLINIC
Kiwango cha chini cha kolestero nyepesi kwenye damu
Pia kama kiwango cha chini cha lehemu nyepesi ni hali ambapo kiwango cha LDL (lipoproteini yenye msongamano mdogo) katika damu huwa chini kuliko kiwango kinachotarajiwa. LDL hubeba kolestero kutoka kwenye ini kwenda kwenye sehemu mbalimbali za mwili.
Upungufu wa protini mwilini
Ni hali ambapo kiwango cha protini, hasa alibumini, huwa chini kuliko kiwango kinachotarajiwa katika damu. Alibumini husaidia kushikilia majimaji ndani ya mishipa ya damu, hivyo kiwango chake kinapopungua, majimaji yanaweza kutoka kwenye mishipa na kujikusanya kwenye tishu na kusababisha idima.
Idima
Ni hali ya mkusanyiko usio wa kawaida wa majimaji kwenye tishu za mwili, hasa katika nafasi zilizopo kati ya seli. Hali hii husababisha sehemu ya mwili kuvimba na inaweza kutokea eneo moja au sehemu mbalimbali za mwili. Huonekana mara nyingi kwenye vifundo vya miguu, miguu, mikono na uso, lakini inaweza pia kutokea ndani ya mwili, kama vile kwenye mapafu au tumboni.
Mkusanyiko wa maji kwenye tishu
Ni hali ambapo majimaji mengi yanakusanyika ndani ya tishu za mwili, hasa kwenye nafasi iliyopo kati ya seli. Hali hii kitaalamu huitwa idima. Hali hii inaweza kutokea sehemu moja ya mwili, kama miguu, vifundo vya miguu au mikono, au inaweza kuenea sehemu mbalimbali za mwili.
