top of page

Imeandikwa na daktari wa ULY-Clinic

​

19 Juni, 2018

​

Kipanda Uso

 

 

Kipanda uso  kwa lugha ya tiba migraine, ni tatizo ambalo halifahamiki mpaka leo kisababishi chake halisi, linapotokea husababisha maumivu ya upande mmoja wa kichwa.

​

Mara nyingi sana, maumivu ya migraine hutanguliwa na dalili kwenye macho au masikio zinazojulikana kama viashiria vya migraine au  Aura za migraine. Viashiria vya migrainepia huweza tokea baada ya maumivu ya kichwa.

 

Tatizo la kipanda uso hutokea sana kwa wanawake na huonekana kurithiwa kwenye familia kupitia jeni zilizo kwenye chembe za binadamu.

 

 

Nini husababisha maumivu haya ya migraine?

 

Hapo zamani ilifahamika kuwa, kipanda uso kinasababishwa na mabadiliko yanayotokea katika mishipa ya damu ya kichwa, inaelezewa kuwa kuna wakati mishipa ya damu inasinyaa  kwa muda na baadae hufuatiwa na kipindi cha kutanuka kwa mishipa hiyo hivo kuleta maumivu wakati wa kitendo hiki kinapotokea.

 

Kwa sasa kuna maelezo yajulikanayo kama 'maelezo ya nyurovasikula' ambayo yanasema kwamba kipanda uso husababishwa na matatizo/mabadiliko yanayotokea katika mfumo wa fahamu na matatizo hayo yanatokana na kupungua kwa usafirishaji wa virutubisho kutoka kwenye mishipa ya damu kwenda kwenye chembe za ubongo. Kitendo hiki husababsisha michomo kwenye mishipa ya fahamu kutokana na kukosa virutubisho hivyo.

 

Kuhusianishwa kwa vinasaba huonyesha kuwa asilimia 70 ya watu wenye kipanda uso wana ndugu wa tumbo moja wenye tatizo hili, hata hivyo mambo mengi ya kimazingira huchangia kuamka kwa dalili za kipanda uso kwa mtu aliyerithi ugonjwa huu.

 

 

Mgonjwa wa kipanda uso anapata dalili zipi?

 

 

Dalili za kipanda uso zinapotokea au kabla hazijatokea huwa na dalili za awali au viashiria, viashiria hivyo vimewekwa katika makundi manne kitaalamu ambayo ni prodromu, aura, maumivu ya kichwa na na postdromu

 

Prodromu

 

Dalili hii hutokea siku moja au mbili kabla mtu hajashikwa na kipanda uso, huwa na dalili kati ya zifuatazo;

  • Haja kubwa ngumu au kukosa haja kabisa

  • Sonona ( kuwa na hali ya chini ya moyo)

  • Njaa kali

  • Kutotulia kimawazo au matendo

  • Kukereka na vitu vidogo ( kulia lia kwa mtoto akishikwa)

  • Kukakamaa kwa shingo

  • Kupata miayo mingi isiyozuilika

 

Aura

 

Kipindi hiki kinaweza kutokea kabla au baada ya mshiko wa kipanda uso . Aura hutokea kutokana na mabadiliko kwenye mfumo wa fahamu na huja na dalili zinazodhuru mfumo wa hisia kama vile kuona unamulikwa na mwanga mkali wakati hakuna mwanga, kuhisi umeguswa mwilini wakati hujaguswa.

 

Mabadiliko mengine ni kwenye mgonjeo wa mwili na mfumo wa maongezi. Watu wengi wanapata kipanda uso pasipo kupata aura. Dalili za aura hutokea polepole na kuongezeka jinsi muda unavyokwenda na huweza dumu kwa dakika 20 hadi 60. Mifano ya aura imeorodheshwa hapa chini;

​

  • Matatizo ya kuona maumbo, mwanga mkali au miale ya mwanga inamulika machoni wakati haipo

  • Kupoteza uwezo wa kuona

  • Kuhisi michomo ya pini au sindano kwenye mwili

  • Kushindwa kufanya maongezi kama vile kushindwa kueleweka unachoongea au kutamka maneno isivyosahihi

  • Kwa mara chache sana aura inaweza kutokea na ganzi miguuni au kupoeza fahamu kwa miguu

 

Maumivu ya kichwa

 

Kama maumivu haya yasipotibiwa hukaa kwa masaa 4 hadi 72, lakini idadi ya maumivu kujirudiarudia na ukali wa maumivu hutegemea au hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Baadhi ya watu hupata kipanda uso mara nyingi katika mwezi au mara chache zaidi. Mtu akiwa anapata kipanda uso anaweza kupata dalili zifuatazo;

  • Maumivu upande mmoja au pande zote za kichwa

  • Maumivu ya kichwa kupwita pwita

  • Kupata maumivu zaidi unapokuwa kwenye mwanga wowote

  • Kichefuchefu na kutapika

  • Kufifia kwa vitu vinavyokuzunguka

  • Kizunguzungu kinachofuatiwa mara nyingine na kuzimia

 

Postdromu

 

Hiki ni Kipindi cha mwisho cha kipanda uso, hutokea baada ya kupata maumivu ya kichwa ya kiopanda uso kama yalivyoelezewa hapo juu. Kipindi hiki mwathirika wa kipanda uso anaweza kuhisi  mtupu ingawa watu wengine wanaweza kuhisi wanafuraha ya uongo

 

Nini huchochea tatizo la kipanda uso?

 

Vitu/sababu zozote zinazoweza kusabaisha maumivu ya kichwa huamsha kipanda uso. Mambo mengi yanayoweza kuamsha kipanda uso ni;

 

  • Mabadiliko ya vichochezi mwili-homoni kwa mwanamke. Mabadiliko ya kichochezi mwili cha estrogen huamsha kipanda uso kama inavyoonekana kwa wanawake wengi wanaopata kipanda uso, wanawake wanaopata maumivu ya kichwa ya kipanda uso huripoti kwamba wametoka au wapo kwenye kipindi cha hedhi ambapo homoni hii ya estrogeni huwa imeshuka kwa kipindi hiki. Wanawake mengine wanapata maumivu haya wakati wa ujauzito au wanawake wanapokuwa kwenye kipindi cha kukoma kwa mzunguko wa hedhi(menopause) madawa ya homoni  kama madawa ya mpango wa uzazi huamsha kipanda uso ingawa baadhi ya wanawake huweza kupata nafuu wanapopata awa hizi

  • Chakula. Vyakula vilivyochacha, vyenye chumvi nyingi na vyakula vya kusindikwa huweza kuamsha kipanda uso. Kifunga au kuruka mlo kunaweza kuamsha kipanda uso pia

  • Msongo wa mawazo

  • Kulala sana au kidogo

  • Madawa ya kutanua mishipa ya damu (vasodilators)

  • Kuvuta sigara

  • Kukaa kwenye mwanga mkali

  • harufu kali kama ya pafume madawa ya meno na petroli

  • Jeraha kichwani

  • Baridi kama barafu

  • Kutofanya mazoezi

  • Kunywa wine nyekundu (red wine)

 

Baadhi ya vyakula vinavyosemekana kuamsha kipanda uso ni;

 

  • Vinywaji vyenye kafeini

  • vinywaji vyenye sukari isiyo asili kama juis kola n.k

  • matunda aina ya citrus kama machungwa ndimu n.k

  • vyakula vyenye kemikali aina ya tyramine kama cheese zilizaokaa muda mrefu n.k

  • nyama yenye kemikali ya nitrates 

 

Matibabu ya kipanda uso

 

 

Matibabu ya kipanda uso huwa ya aina mbili, kuondoa dalili na matibabu ya kuzuia kupata vipindi vya maumivu ya kichwa.Kwa wagonjwa ambao wanapata kipanda uso mara kwa mara wanatakiwa kujifunza kujizuia kutoka kwenye mambo au vitu vinavyowasababishia kupata dalili hizo.

 

Mgonjwa wa Kipanda uso anatakiwa kupimwa na kuangaliwa kama anavihatarishi vya ugonjwa wa moyo, kama anavyo matibabu ya haraka yanatakiwa kufanyika ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea na ikiwa anakuwa na vipindi vya Aura anatakiwa kupewa elimu juu ya hatari ya kupata kiharusi na wale ambao wanavuta sigara ni vema wakaambiwa madhara ya sigara katika tatizo walionalo

 

Matibabu ya dawa

 

  • Dawa za maumivu kama mgonjwa anapata maumivu ya kichwa

  • Dawa za kuzuia kipanda uso kutokea mara kwa mara

  • Dawa za kuondoa dalili kama kichefuchefu au kutapika

 

Matibabu ya kuzuia kupata kipanda uso

 

Mgojwa anatakiwa ajifunze vitu/tabia gani zinazosababisha kuamka kwa kipanda uso, endapo anamatumizi ya dawa zinazoamsha kipanda uso basi anatakiwa kuacha

 

Matibabu mengine anayoweza kupata ni yale dawa za kuzuia kupata dalili ya maumivu ya kichwa mara anapokuwa katika kipindi cha migraine na pia kuna dawa mgonjwa anaweza kupata kila baada ya muda flani kupita kwa ajili ya kuzuia kupata vipindi vingi vya kipanda uso. 

 

 

Madhara yatokanayo na kipanda uso 

 

  • Maumivu sugu ya kichwa au chronic migraine

  • Kifafa

  • Kiharusi

  • Kupata Aura endelevu dakika 30 hadi 60)

 

Kiharusi cha kutokana na kipanda uso ni nadra sana kutokea, lakini kinapotokea huwa na madhara makubwa yatokanayo na kipanda uso. Katika kipindi cha aura na maumivu ya kichwa ,mivilio ya damu huweza kutokea ndani ya ubongo lakini vilevile ni nadra.

 

Vihatarishi vya kupata kiharusi kwa mtu anayepata kipanda uso ni hivi vifuatavyo 

 

  • Maumivu ya kichwa yanayofuatiwa na kipindi cha aura

  • Kuwa na jinsia ya kike

  • Uvutaji wa sigara

  • Matumizi ya hormoni ya estrogen kama kwa wanawake wanaotumia vidonge vya majira

​

​

ULY CLINIC inakushauri siku zote upate ushauri na Tiba kutoka kwa daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile inayodhuru afya yako.

 

Wasilina na daktari wa ULY CLINIC kwa suhauri zaidi na Tiba kupitia namba za simu au bonyeza Pata Tiba chini ya tovuti hii.

 

​

Imeboreshwa, , 03.07.2021

​

Rejea za mada hii,

​

  1. Migraine information page. NINDS. https://www.ninds.nih.gov/Disorders/All-Disorders/Migraine-Information-Page. Imechukuliwa 3.07.2021

  2. Uptodate. Acute treatment of migraine in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 3.07.2021

  3. ABC's of headache trigger management. American Migraine Foundation. https://americanmigrainefoundation.org/resource-library/abcs-of-headache-trigger-management/. Imechukuliwa 3.07.2021

  4. Headache: Hope through research. National Institute of Neurological Disorders and Stroke. https://www.ninds.nih.gov/Disorders/Patient-Caregiver-Education/Hope-Through-Research/Headache-Hope-Through-Research. Imechukuliwa 3.07.2020

  5. Uptodate. Preventive treatment of migraine in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 3.07.2021

  6. FDA approves new treatment for patients with migraine. U.S. Food and Drug Administration. https://www.fda.gov/news-events/press-announcements/fda-approves-new-treatment-patients-migraine. Imechukuliwa 3.07.2021

  7. FDA approves new treatment for patients with migraine. U.S. Food and Drug Administration. https://www.fda.gov/news-events/press-announcements/fda-approves-new-treatment-adults-migraine. Imechukuliwa 3.07.2021

bottom of page