Magonjwa na saratani mbalimbali
Sehemu hii utasoma kuhusu hali na magonjwa mbalimbali

Vipele vya jasho
Ni vipele vidogo vinavyotokea pale mirija ya jasho inapoziba, hasa wakati wa joto na unyevunyevu mwingi, na kwa kawaida si ugonjwa wa kuambukiza wala hatari. Kuweka mwili katika hali ya ubaridi, kuvaa nguo nyepesi zinazopitisha hewa na kuepuka joto na unyevunyevu husaidia kuondoa upele na kuzuia usijirudie.

Siriangoma
Ni vijivimbe vidogo visivyo vya saratani vinavyotokana na tezi za jasho, na mara nyingi huonekana usoni hasa kuzunguka macho, haviambukizi wala kusababishwa na uchafu wa ngozi. Kwa kawaida havihitaji matibabu, lakini vinaweza kuondolewa kwa njia za kitaalamu kama laser au upasuaji mdogo ikiwa vinasumbua muonekano, huku kuepuka kujikamua au kutumia kemikali kali nyumbani.

Ugonjwa wa Seli mundu
Ni ugonjwa wa kurithi unaosababishwa na mabadiliko ya umbile la chembe nyekundu za damu. Unaweza kusababisha upungufu wa damu, maumivu makali na kuathiri viungo mbalimbali vya mwili. Uchunguzi wa mapema, ufuatiliaji wa kitabibu, chanjo, matumizi sahihi ya dawa na kuepuka vichochezi vya mashambulio husaidia kupunguza madhara na kuboresha maisha ya mtu mwenye seli mundu.

Kiharusi
Ni hali ya ghafla inayoweza kuathiri uwezo wa kuongea, kutembea, kuona au kutumia upande mmoja wa mwili, na matibabu ya mapema husaidia kupunguza madhara. Kudhibiti shinikizo la damu, kisukari na cholesterol, kuacha sigara, kufanya mazoezi na kula vizuri husaidia kupunguza hatari ya kupata kiharusi.
