Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Imeboreshwa:
8 Machi 2026, 07:08:09

Bawasiri: Visababishi, Dalili, Uchunguzi, Matibabu na Kinga
Bawasiri, ambayo pia huitwa pile, ni hali ya kuvimba au kutanuka kwa mishipa ya damu (vena) inayopatikana katika sehemu ya mwisho ya utumbo mpana karibu na tundu la haja kubwa. Mishipa hii inapopanuka au kujaa damu kupita kiasi hutengeneza uvimbe au vinundu vinavyojulikana kama bawasiri.
Bawasiri ni mojawapo ya matatizo ya kawaida ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Tafiti zinaonyesha kuwa karibu asilimia 50 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50 huwa wamewahi kupata dalili za bawasiri katika maisha yao.
Ingawa bawasiri mara nyingi si ugonjwa hatari, inaweza kusababisha usumbufu mkubwa kama vile maumivu, kuwasha, kutokwa damu wakati wa kujisaidia na uvimbe kwenye njia ya haja kubwa.
2. Pathofiziolojia (Jinsi Bawasiri hutokea)
Katika sehemu ya mwisho ya utumbo mpana kuna mtandao wa mishipa ya damu unaosaidia kudhibiti ufunguaji na kufungwa kwa mlango wa haja kubwa wakati wa kutoa haja kubwa.
Wakati shinikizo ndani ya mishipa hii linaongezeka kwa muda mrefu, mishipa hiyo:
Hutanuka
Hujaa damu
Hupoteza uimara wake
Matokeo yake mishipa hiyo huvimba na kutengeneza bawasiri. Shinikizo hilo linaweza kuongezeka kutokana na:
Kukenya sana wakati wa kujisaidia
Choo kigumu
Kukaa muda mrefu chooni
Ujauzito
Uzito mkubwa
Kuhara kwa muda mrefu
Kadiri umri unavyoongezeka, kuta za mishipa hupoteza nguvu na kunyumbulika, jambo linaloongeza uwezekano wa kupata bawasiri.
3. Aina za Bawasiri
Bawasiri hugawanyika katika aina kuu mbili kulingana na mahali zinapotokea.
3.1 Bawasiri ya ndani
Hutokea ndani ya njia ya haja kubwa (puru). Kwa kawaida:
Halionekani kwa macho
Mara nyingi halisababishi maumivu
Dalili kuu ni:
Kutokwa damu nyekundu wakati wa kujisaidia
Bawasiri kuchomoza nje wakati wa kujisaidia
Madaraja ya Bawasiri ya Ndani
Bawasiri ya ndani inaweza kugawanywa katika madaraja yafuatayo:
Daraja la kwanza-Bawasiri ipo ndani ya mkundu na halichomoki nje.
Daraja la pili-Bawasiri huchomoza wakati wa kujisaidia lakini hurudi ndani yenyewe.
Daraja la tatu-Bawasiri huchomoza na hulazimika kurudishwa ndani kwa mkono.
Daraja la nne-Bawasiri hubaki nje ya njia ya haja kubwa na haiwezi kurudishwa ndani.
3.2 Bawasiri yanje
Hutokea chini ya ngozi inayozunguka mlango wa haja kubwa.
Dalili zake ni pamoja na:
Maumivu
Kuwasha
Kuvimba
Uvimbe unaoonekana karibu na mkundu
Kutokwa damu
Wakati mwingine damu inaweza kuganda ndani ya bawasiri na kusababisha hali inayoitwa bawasili iliyoganda, ambayo huleta maumivu makali.
4. Dalili za Bawasiri
Dalili hutegemea aina ya bawasiri na ukubwa wake.
Dalili zinazoweza kuonekana ni pamoja na:
Kutokwa na damu nyekundu wakati wa kujisaidia
Damu kwenye kinyesi au karatasi ya chooni
Kuwasha kwenye mkundu
Maumivu wakati wa kukaa au kujisaidia
Kuvimba karibu na mkundu
Uvimbe unaochomoza nje ya mkundu
Hisia ya kutokukamilisha haja kubwa
Kutokwa na ute kwenye mkundu
Ni muhimu kufahamu kuwa kutokwa damu wakati wa kujisaidia si lazima iwe bawasiri pekee, kwani inaweza pia kusababishwa na magonjwa mengine kama saratani ya utumbo.
5. Sababu na vihatarishi vya bawasiri
Sababu zinazoweza kuongeza uwezekano wa kupata bawasiri ni pamoja na:
Kukenya sana wakati wa kujisaidia
Kukaa muda mrefu chooni
Choo kigumu
Kuhara kwa muda mrefu
Uzito mkubwa kupita kiasi
Ujauzito
Kutokula chakula chenye nyuzilishe
Kuingiliwa kinyume na maumbile
Kukaa sana bila kufanya mazoezi
Kuzeeka
6. Madhara ya Bawasiri
Ingawa hutokea mara chache, madhara ya bawasiri yanaweza kujumuisha:
6.1 Upungufu wa damu (Anemia)
Kutokwa damu kwa muda mrefu kunaweza kupunguza kiwango cha chembe nyekundu za damu na kusababisha:
Uchovu
Kizunguzungu
Mwili kukosa nguvu
6.2 Kuganda kwa damu kwenye bawasiri (Thrombosisi)
Damu inaweza kuganda ndani ya bawasiri la nje na kusababisha:
Maumivu makali
Uvimbe mkubwa
Ngozi kuwa ya rangi ya zambarau
6.3 Kujisokota kwa Bawasiri kujinyonga
Hii hutokea pale bawasiri linapokosa damu ya kulilisha na kusababisha maumivu makali na kifo cha tishu zake.
7. Uchunguzi wa Bawasiri
Daktari anaweza kufanya uchunguzi kwa njia zifuatazo:
7.1 Uchunguzi wa mwili
Daktari huangalia eneo la mkundu ili kuona kama kuna uvimbe au bawasiri la nje.
7.2 Uchunguzi wa njia ya haja kubwa kwa vidole
Daktari huingiza kidole kilichovaa glavu kwenye mkundu ili kuhisi kama kuna uvimbe au kitu kisicho cha kawaida.
7.3 Anoskopi au kolonoskopi
Hivi ni vipimo vinavyotumia kamera ndogo kuangalia ndani ya njia ya haja kubwa au utumbo mpana.
Vipimo hivi vinaweza kufanyika kama:
Mgonjwa ana zaidi ya miaka 50
Kuna dalili zisizoeleweka vizuri
Kuna hatari ya saratani ya utumbo
8. Matibabu ya Bawasiri
Matibabu hutegemea ukubwa wa tatizo na dalili alizonazo mgonjwa.
8.1 Matibabu ya nyumbani
Mabadiliko ya mfumo wa maisha yanaweza kusaidia sana:
Jedwali: Matibabu ya Nyumbani ya Bawasiri
Njia ya Matibabu | Maelezo | Faida zake |
Kula vyakula vyenye nyuzilishe nyingi | Kula matunda, mboga za majani, nafaka zisizokobolewa, maharage na dengu. | Hufanya kinyesi kiwe laini na kupunguza kukenya wakati wa kujisaidia. |
Kunywa maji mengi | Kunywa angalau glasi 6–8 za maji kila siku. | Husaidia kulainisha kinyesi na kuzuia choo kigumu. |
Kukalia maji ya uvuguvugu | Kukaa kwenye maji ya uvuguvugu kwa dakika 10–15 mara kadhaa kwa siku. | Hupunguza maumivu, kuwasha na uvimbe kwenye njia ya haja kubwa. |
Kutumia krimu au mafuta ya bawasiri | Krimu au mafuta hupakwa kwenye eneo la mkundu ili kupunguza dalili. | Hupunguza muwasho, maumivu na uvimbe kwa muda. |
Kuepuka kukenya wakati wa kujisaidia | Usitumie nguvu nyingi kusukuma kinyesi. | Hupunguza shinikizo kwenye mishipa ya mkundu. |
Kwenda chooni mara unapohisi haja | Usizuie haja kubwa kwa muda mrefu. | Huzuia kinyesi kuwa kigumu na kupunguza maumivu wakati wa kujisaidia. |
Kufanya mazoezi mara kwa mara | Kutembea, kukimbia kidogo au kufanya mazoezi mepesi kila siku. | Husaidia mmeng’enyo wa chakula na kuzuia choo kigumu. |
Kuepuka kukaa muda mrefu | Epuka kukaa muda mrefu hasa chooni au kwenye kiti. | Hupunguza shinikizo kwenye mishipa ya mkundu. |
8.2 Matumizi ya dawa
Dawa zinazoweza kutumika ni:
Krimu za kupaka mkunduni
Mafuta ya kupunguza muwasho
Padi za matibabu
Dawa zenye hydrocortisone
Dawa hizi hupunguza:
Maumivu
Kuwasha
Uvimbe
Lakini hazipaswi kutumiwa kwa muda mrefu bila ushauri wa daktari.
8.3 Matibabu ya upasuaji mdogo
Kufunga kwa rababendi
Daktari huweka raba bendi kwenye bawasiri ili kukata mzunguko wa damu. Baada ya siku chache bawasiri hukauka na kuanguka.
Sklerotherapi
Kemikali maalum huchomwa kwenye bawasiri ili kusababisha mishipa yake kusinyaa.
Kugandisha kwa mwanga
Mwanga maalum hutumika kugandisha damu kwenye bawasiri na kusababisha mishipa kusinyaa.
8.4 Upasuaji mkubwa (Upasuaji wa kukata bawasili)
Katika hali kali sana, bawasiri inaweza kuondolewa kwa upasuaji.
Upasuaji huu hufanywa ikiwa:
Bawasiri ni kubwa sana
Matibabu mengine hayajasaidia
Dalili ni kali sana
9. Jinsi ya kuzuia Bawasiri
Njia bora ya kuzuia bawasiri ni kuhakikisha kinyesi kinakuwa laini na rahisi kupita.
Hatua za kujikinga ni pamoja na:
Kula matunda mengi
Kula mboga za majani
Kula nafaka zisizokobolewa
Kunywa maji glasi 6–8 kwa siku
Kufanya mazoezi mara kwa mara
Kwenda chooni mara unapohisi haja
Kuepuka kukaa muda mrefu chooni
Wanawake wanahitaji takribani gramu 25 za nyuzilishe kwa siku, na wanaume gramu 38 kwa siku.
10.0 Elimu kwa Mgonjwa
Mgonjwa anapaswa kufahamu kwamba:
Bawasiri ni tatizo la kawaida na linaweza kutibiwa
Dalili nyingi hupungua kwa kubadili mfumo wa maisha
Kutokwa damu mara kwa mara kunahitaji uchunguzi wa daktari
Matibabu ya mapema huzuia madhara makubwa
10.1 Wakati gani wa kumwona Daktari
Unapaswa kumwona daktari haraka kama:
Unatoka damu mara kwa mara unapojisaidia
Damu ni nyingi
Bawasiri lina maumivu makali
Dalili haziponi baada ya matibabu ya nyumbani
Kinyesi ni cheusi
Kuna damu iliyoganda au damu iliyochanganyika kwenye kinyesi
Dalili hizi zinaweza pia kuashiria magonjwa mengine kama saratani ya utumbo mpana au saratani ya puru.
11. Hitimisho
Bawasiri ni ugonjwa wa kawaida unaosababishwa na kuvimba kwa mishipa ya damu karibu na mkundu. Ingawa mara nyingi si hatari, unaweza kusababisha usumbufu mkubwa kwa mgonjwa.
Kwa kubadili mfumo wa maisha kama:
kula chakula chenye nyuzilishe,
kunywa maji ya kutosha,
kufanya mazoezi,
inawezekana kuzuia au kupunguza dalili za bawasiri kwa kiwango kikubwa.
Ikiwa dalili zinaendelea au zinazidi kuwa mbaya, ni muhimu kumwona daktari kwa uchunguzi na matibabu sahihi.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake ya kina kuhusu bawasiri
1. Bawasiri ni nini?
Bawasiri ni hali ya kuvimba au kutanuka kwa mishipa ya damu (vena) inayopatikana karibu na tundu la haja kubwa (mkundu)Â au ndani ya njia ya haja kubwa (rectum). Mishipa hii inapovimba huunda vinundu vinavyojulikana kama bawasiri.
Kuna aina mbili kuu za bawasiri:
Bawasiri ya ndani – hutokea ndani ya njia ya haja kubwa na mara nyingi halisababishi maumivu makali.
Bawasiri ya nje – hutokea chini ya ngozi inayozunguka mkundu na linaweza kusababisha maumivu, kuwasha na uvimbe.
Bawasiri ni tatizo la kawaida sana, hasa kwa watu wazima na wazee, na mara nyingi husababishwa na shinikizo kubwa kwenye mishipa ya mkundu.
2. Dalili za bawasiri ni zipi?
Dalili za bawasiri hutegemea aina na ukubwa wa bawasiri aliyonayo mtu. Dalili zinazojitokeza mara nyingi ni:
Kutokwa na damu nyekundu wakati wa kujisaidia
Kuona damu kwenye kinyesi au karatasi ya chooni
Kuwasha kwenye mkundu
Maumivu wakati wa kukaa au kujisaidia
Kuvimba karibu na mkundu
Uvimbe au kinundu kinachochomoza nje ya mkundu
Hisia ya kutokukamilisha haja kubwa
Ikiwa damu inatoka mara kwa mara au kwa kiasi kikubwa, ni muhimu kumwona daktari mapema kwa uchunguzi zaidi.
3. Nini husababisha bawasiri?
Bawasiri hutokea wakati mishipa ya damu inayozunguka mkundu inapopata shinikizo kubwa kwa muda mrefu na hivyo kuvimba.
Sababu kuu zinazoweza kusababisha bawasiri ni:
Kukenya sana wakati wa kujisaidia
Choo kigumu (constipation)
Kukaa muda mrefu chooni
Kuhara kwa muda mrefu
Uzito mkubwa kupita kiasi
Ujauzito
Kutokula chakula chenye nyuzinyuzi
Kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi
Kuzeeka
Kubadili mfumo wa maisha kunaweza kupunguza hatari ya kupata bawasiri.
4. Je, bawasiri linaweza kupona lenyewe?
Ndiyo, bawasiri ndogo mara nyingi huweza kupona au kupungua dalili zake bila upasuaji, hasa kama mtu atafanya mabadiliko katika maisha yake.
Hatua zinazoweza kusaidia ni pamoja na:
Kula chakula chenye nyuzinyuzi nyingi
Kunywa maji mengi
Kufanya mazoezi
Kuepuka kukenya wakati wa kujisaidia
Kutokaa muda mrefu chooni
Hata hivyo, ikiwa dalili zinaendelea au zinaongezeka, ni muhimu kutafuta matibabu ya daktari.
5. Bawasiri linaweza kutibiwa nyumbani?
Ndiyo, katika hatua za mwanzo bawasiri linaweza kutibiwa nyumbani kwa kufanya mambo yafuatayo:
Kula matunda na mboga nyingi
Kunywa maji glasi 6–8 kwa siku
Kuoga kwa maji ya uvuguvugu (sitz bath)
Kutumia krimu au mafuta ya bawasiri
Kuepuka kukaa muda mrefu
Njia hizi husaidia kupunguza:
Maumivu
Kuwasha
Uvimbe
Lakini ikiwa dalili ni kali au hazipungui, ni muhimu kumwona daktari kwa matibabu zaidi.
6. Ni wakati gani mtu anapaswa kumwona daktari kwa bawasiri?
Ni muhimu kumwona daktari kama:
Unatoka damu mara kwa mara unapojisaidia
Maumivu ni makali sana
Bawasiri linachomoza nje na haliingii tena
Dalili haziponi baada ya matibabu ya nyumbani
Kinyesi ni cheusi au kina damu iliyochanganyika ndani yake
Dalili hizi zinaweza pia kuashiria magonjwa mengine ya utumbo kama saratani ya utumbo mpana, hivyo uchunguzi wa daktari ni muhimu.
7. Je, bawasiri linaweza kusababisha saratani?
Hapana. Bawasiri halisababishi saratani.
Hata hivyo, dalili za bawasiri kama kutokwa damu wakati wa kujisaidia zinaweza kufanana na dalili za saratani ya utumbo mpana.
Kwa hiyo, kama damu inatoka mara kwa mara au kuna dalili zisizoeleweka vizuri, ni muhimu kufanya uchunguzi wa kitabibu ili kuhakikisha tatizo halisababishwi na ugonjwa mwingine.
8. Ni chakula gani kinasaidia kuzuia au kutibu bawasiri?
Chakula chenye nyuzilishe nyingi husaidia sana kuzuia bawasiri kwa kufanya kinyesi kiwe laini na rahisi kupita.
Vyakula vinavyoshauriwa ni:
Matunda kama papai, parachichi na ndizi
Mboga za majani kama mchicha na matembele
Nafaka zisizokobolewa
Maharage na dengu
Mbegu na karanga
Pia ni muhimu kunywa maji ya kutosha ili kusaidia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kufanya kazi vizuri.
9. Je, upasuaji wa bawasiri ni lazima?
Upasuaji si lazima kwa watu wote wenye bawasiri.
Kwa watu wengi, dalili hupungua kwa:
kubadili mfumo wa maisha,
kutumia dawa,
au kufanya matibabu madogo kama kufunga kwa rababendi.
Upasuaji hufanyika tu ikiwa:
bawasiri ni kubwa sana,
linachomoza nje mara kwa mara,
au matibabu mengine hayajasaidia.
10. Bawasiri linaweza kuzuiwa vipi?
Njia bora ya kuzuia bawasiri ni kuzuia choo kigumu na kupunguza shinikizo kwenye mishipa ya mkundu.
Hatua muhimu za kujikinga ni:
Kula chakula chenye nyuzilishe nyingi
Kunywa maji ya kutosha kila siku
Kufanya mazoezi mara kwa mara
Kuepuka kukenya wakati wa kujisaidia
Kwenda chooni mara unapohisi haja
Kuepuka kukaa muda mrefu chooni
Kufuata hatua hizi kunaweza kupunguza sana hatari ya kupata bawasiri.
Rejea za mada hii:
Davis BR, et al. Clinical practice guidelines for the management of hemorrhoids. Diseases of the Colon & Rectum.
National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases (NIDDK). Hemorrhoids.
The American Society of Colon and Rectal Surgeons. Hemorrhoids information guide.
Kellerman RD. Conn's Current Therapy. Elsevier.
Bleday R. Management of symptomatic hemorrhoids. UpToDate.
