Mwandishi:
Mhhariri
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
ULY CLINIC
22 Agosti 2026, 17:44:08

Fangasi kwenye damu
Fangasi kwenye damu, kitabibu huitwa kandidemia, ni hali ambapo fangasi wa aina ya kandida huingia na kuenea kwenye mfumo wa damu. Ni aina ya maambukizi makubwa ambayo inaweza kuathiri viungo vingine vya mwili na kusababisha hali hatari kama sepsis ikiwa haitatambuliwa na kutibiwa mapema. Aina zinazohusika mara nyingi ni Candida albicans, C. glabrata, C. tropicalis, C. parapsilosis na C. krusei.
Ni muhimu kutofautisha fangasi kwenye damu na fangasi wa kawaida wa uke, mdomo au ngozi. Kuwa na fangasi ukeni au kwenye ngozi hakumaanishi kwamba fangasi wameingia kwenye damu. Kandidemia ni maambukizi ya ndani zaidi na kwa kawaida huhusishwa na wagonjwa wenye sababu maalumu za hatari, hasa waliolazwa hospitalini.
Fangasi huingiaje kwenye damu?
Fangasi wanaweza kuwepo mwilini bila kusababisha ugonjwa, hasa kwenye ngozi, mdomo, njia ya chakula na uke. Tatizo hutokea pale mazingira yanaporuhusu fangasi kuvuka sehemu zinazowazuia na kuingia kwenye damu.
Hii inaweza kutokea baada ya upasuaji mkubwa, uharibifu wa utando wa njia ya chakula, au maambukizi kutoka sehemu nyingine za mwili. Kwa wagonjwa walio hospitalini, mirija ya kuingiza dawa au maji kwenye mishipa inaweza pia kuwa chanzo cha maambukizi.
Baada ya kuingia kwenye damu, fangasi wanaweza kusafiri hadi kwenye viungo mbalimbali, ikiwemo macho, moyo, figo, ini, wengu, mifupa na mfumo wa fahamu. Ndiyo sababu kandidemia huhitaji matibabu ya kimfumo na ufuatiliaji wa karibu.
Nani yuko katika hatari kubwa ya kupata fangasi kwenye damu?
Hatari huwa kubwa zaidi kwa mtu mwenye moja au zaidi ya hali zifuatazo:
Kulazwa hospitalini kwa muda mrefu.
Kuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Kutumia catheter ya mshipa kwa muda.
Kufanyiwa upasuaji mkubwa, hasa wa tumbo.
Kutumia antibiotics zenye wigo mpana kwa muda mrefu.
Kupokea lishe kupitia mshipa.
Kuwa na kinga ya mwili iliyopungua.
Kuwa na neutropenia.
Kuwa na baadhi ya saratani.
Kupata maambukizi makubwa au sepsis.
Kuwa na ugonjwa mkali unaohitaji matibabu ya hospitalini kwa muda mrefu.
Hata hivyo, kuwa na sababu moja ya hatari hakumaanishi kwamba mtu ana fangasi kwenye damu. Uchunguzi unahitajika kuthibitisha maambukizi.
Dalili za fangasi kwenye damu
Kandidemia haina dalili moja maalumu inayoweza kutumiwa kuitambua. Mara nyingi mgonjwa huwa na dalili zinazofanana na maambukizi makubwa ya bakteria.
Dalili zinaweza kujumuisha:
Homa.
Baridi au kutetemeka.
Udhaifu mkubwa.
Uchovu.
Mapigo ya moyo kwenda haraka.
Kupumua kwa kasi.
Shinikizo la damu kushuka.
Kuchanganyikiwa au kupungua kwa fahamu.
Maumivu mbalimbali mwilini.
Dalili za kushindwa kufanya kazi kwa viungo katika maambukizi makali.
Kwa baadhi ya wagonjwa, homa inaweza kuendelea licha ya matumizi ya antibiotics, jambo linaloweza kumfanya daktari kufikiria uwezekano wa maambukizi ya fangasi, hasa kama kuna sababu za hatari.
Je, fangasi kwenye damu husababisha kuwashwa mwili?
Inawezekana kupata mabadiliko kwenye ngozi wakati wa maambukizi ya fangasi, lakini kuwashwa mwili pekee si dalili maalumu ya fangasi kwenye damu.
Mtu mwenye kandidemia anaweza kuwa na dalili za jumla za maambukizi bila kuwa na upele au kuwashwa kabisa. Kwa hiyo, mtu anayewashwa mwili bila dalili nyingine za maambukizi hapaswi kudhani moja kwa moja kwamba ana fangasi kwenye damu.
Sababu nyingi zaidi za kuwashwa ni pamoja na magonjwa ya ngozi, mzio, dawa, ukavu wa ngozi, baadhi ya magonjwa ya ini au figo na hali nyingine mbalimbali.
Je, fangasi wa uke wanaweza kuingia kwenye damu?
Kwa mtu mwenye afya nzuri, fangasi wa uke kwa kawaida hubaki kwenye eneo hilo na hauingii kwenye damu. Kandidemia hutokea zaidi kwa watu wenye sababu maalumu zinazorahisisha maambukizi ya ndani, hasa wagonjwa wenye hali mbaya au wanaotumia vifaa vya kimatibabu.
Hivyo, kuwa na candidiasis ya uke mara kwa mara hakumaanishi kwamba mtu ana kandidemia. Fangasi wa uke pia hutibiwa kwa njia tofauti na kandidemia.
Ikiwa mwanamke mwenye fangasi wa uke pia ana homa kali, kutetemeka, udhaifu mkubwa au dalili za maambukizi makubwa, anapaswa kufanyiwa tathmini badala ya kudhani kwamba ni fangasi wa uke pekee.
Je, fangasi kwenye damu wanaweza kusababisha sepsis?
Ndiyo. Fangasi wakisababisha maambukizi makubwa kwenye damu inaweza kusababisha sepsisi, ambapo mwitikio mkali wa mwili kwa maambukizi huanza kuathiri viungo.
Sepsis inaweza kusababisha shinikizo la damu kushuka, matatizo ya kupumua, kuchanganyikiwa, figo kushindwa kufanya kazi na matatizo ya viungo vingine. Kandidemia yenye mshituko wa usumu wa fangasi ni hali ya dharura inayohitaji matibabu ya haraka.
Kwa hiyo, mgonjwa mwenye kandidemia anayekuwa na kuchanganyikiwa, kupumua kwa shida, shinikizo la damu kushuka, mkojo kupungua au hali ya mwili kuzorota anahitaji huduma ya dharura.
Fangasi kwenye damu hugunduliwaje?
Uchunguzi muhimu zaidi ni kipimo cha kuotesha fangasi kwenye damu, ambapo sampuli ya damu huchukuliwa na kupelekwa maabara kutafuta ukuaji wa fangasi.
Baada ya fangasi kupatikana, maabara inaweza kutambua aina ya kandida na kufanya vipimo vya kuangalia kama fangasi anahusika na usugu wa dawa za kuua fangasi. Hii ni muhimu kwa sababu aina mbalimbali za Kandida zinaweza kuwa na mwitikio tofauti kwa dawa.
Vipimo vingine vinaweza kutumika kusaidia uchunguzi katika mazingira maalumu, lakini havichukui nafasi ya tathmini nzima ya mgonjwa. Daktari anaweza pia kufanya vipimo vya damu, figo, ini na uchunguzi wa viungo vingine kulingana na dalili.
Je, kipimo cha damu kikionyesha fangasi ni lazima kutibiwa?
Ikiwa fangasi imepatikana kwenye kipimo cha kuotesha fangasi kwenye damu, hali hiyo inachukuliwa kwa uzito na kwa kawaida huhitaji matibabu ya antifungal. Hii ni tofauti na kupata fangasi kwenye sehemu kama mkojo, makohozi au ngozi, ambapo uwepo wake unaweza wakati mwingine kumaanisha colonization badala ya maambukizi ya ndani.
Kwa kandidemia, daktari huangalia aina ya fangasi, hali ya mgonjwa, dawa alizotumia hapo awali na matokeo ya vipimo vya usikivu wa dawa.
Matibabu ya fangasi kwenye damu
Kandidemia hutibiwa kwa dawa za antifungal za kimfumo, mara nyingi zikianza kwa dawa zinazotolewa kupitia mshipa kwa wagonjwa wenye hali kali.
Kwa wagonjwa wengi ambao si neutropenic, kundi la dawa linaloitwa echinocandins hutumika kama matibabu ya awali. Dawa kama caspofungin, micafungin au anidulafungin ni mifano ya kundi hili. Fluconazole inaweza kuwa chaguo kwa baadhi ya wagonjwa walio katika hali nzuri na ambao aina ya fangasi inayohusika ina uwezekano wa kuitikia dawa hiyo.
Matibabu hubadilishwa kulingana na majibu ya mgonjwa na matokeo ya maabara. Kwa mgonjwa aliyeimarika, mwenye fangasi anayejulikana kuwa anaitikia fluconazole na ambaye blood cultures zimekuwa negative, daktari anaweza kubadili kutoka echinocandin kwenda fluconazole.
Je, fluconazole inatibu fangasi kwenye damu?
Fluconazole inaweza kutumika kutibu baadhi ya kandidemia, lakini si sahihi kusema kwamba ndiyo dawa inayofaa kwa kila mgonjwa.
Aina fulani za fangasi zinaweza kuwa na usugu dhidi ya fluconazole. Kwa hiyo, uchaguzi wa dawa unatakiwa kuzingatia aina ya fangasi, hali ya mgonjwa na matokeo ya susceptibility testing inapopatikana.
Muda wa matibabu ni siku ngapi?
Kwa kandidemia ambayo haina matatizo ya kuenea kwenye viungo vingine, matibabu kwa kawaida huendelea angalau wiki mbili baada ya kuthibitishwa kwa kuondoka kwa fangasi kwenye damu na baada ya dalili zinazohusishwa na kandidemia kuisha.
Hii ndiyo sababu mgonjwa hapaswi kuacha dawa mara tu anapohisi nafuu. Daktari anaweza kuagiza kipimo cha uoteshaji wa fangasi wa damu za kufuatilia ili kujua ni lini damu imekuwa huru kwenye maambukizi.
Ikiwa fangasi umeenea kwenye moyo, macho, mifupa, mfumo wa fahamu au kiungo kingine, muda wa matibabu unaweza kuwa mrefu zaidi na matibabu maalumu yanaweza kuhitajika.
Kwa nini kipimo cha uoteshaji fangasi kwenye damu hurudiwa?
Baada ya kandidemia kuthibitishwa, uoteshaji wa fangasi kwenye damu hurudiwa ili kujua kama fangasi ameondoka kwenye damu.
Matokeo haya husaidia daktari kujua kama dawa inafanya kazi na kuamua muda wa kuendelea na matibabu. IDSA inapendekeza blood cultures za ufuatiliaji kila siku au kila baada ya siku moja hadi kuonyesha kwamba kandidemia imeondoka.
Ikiwa blood culture inaendelea kuwa positive, daktari hutafuta chanzo cha maambukizi na matatizo yanayoweza kuwa yamejitokeza kwenye viungo vingine.
Je, catheter inaweza kuwa chanzo cha fangasi kwenye damu?
Ndiyo. Mrija wa mshipa, hasa mrija wa mishipa ya kati ya damu, inaweza kuwa chanzo cha kandidemia katika baadhi ya wagonjwa.
Ikiwa catheter inadhaniwa kuwa chanzo cha maambukizi, daktari anaweza kuamua kuiondoa mapema ikiwa kufanya hivyo ni salama. Uamuzi huo hutegemea hali ya mgonjwa na sababu ya catheter kuwekwa.
Hii ni muhimu kwa sababu kutibu fangasi kwa dawa pekee bila kudhibiti chanzo cha maambukizi kunaweza kufanya maambukizi yaendelee.
Fangasi kwenye damu wanaweza kuathiri macho?
Ndiyo. Fangasi wanaweza kusambaa kutoka kwenye damu hadi kwenye jicho na kusababisha maambukizi ya ndani ya jicho, ikiwa ni pamoja na endophthalmitisi.
Kwa sababu hiyo, wagonjwa wenye kandidemia wanaweza kuhitaji uchunguzi wa macho unaopanua mboni ili kutafuta dalili za maambukizi ya fangasi wenye jicho. IDSA inapendekeza uchunguzi huo ndani ya wiki ya kwanza kwa wagonjwa wasio na neutropenia.
Mgonjwa anayepata kuona ukungu, maumivu ya jicho, mwanga kumuumiza au mabadiliko mengine ya kuona wakati wa kandidemia anapaswa kumjulisha daktari mara moja.
Je, fangasi kwenye damu wanaweza kupona kabisa?
Ndiyo, kandidemia inaweza kutibiwa na mgonjwa kupona, hasa ikiwa maambukizi yanatambuliwa mapema, dawa inayofaa inatumika na chanzo cha maambukizi kinadhibitiwa.
Hata hivyo, kandidemia ni maambukizi makubwa na hatari yake hutegemea umri, kinga ya mwili, hali ya viungo, aina ya fangasi, uwepo wa sepsis na kama maambukizi yameenea kwenye viungo vingine.
Ndiyo maana mtu anayeshukiwa kuwa na fangasi kwenye damu hapaswi kujitibu kwa dawa za kawaida za fangasi za ngozi au uke. Anahitaji uchunguzi wa hospitali na dawa maalumu za antifungal.
Je, fangasi kwenye damu unaweza kuambukizwa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine?
Kwa ujumla, kandidemia si ugonjwa unaoenea kwa urahisi kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kama mafua au COVID-19. Mara nyingi hutokea kutokana na fangasi ambayo tayari ipo mwilini au kupitia mazingira maalumu ya matibabu.
Hata hivyo, hospitalini kuna aina fulani za fangasi zenye usugu mkubwa wa dawa, kama Candida auris, ambazo zinaweza kuenea kati ya wagonjwa kupitia mazingira au vifaa vilivyochafuliwa. Hii ndiyo sababu udhibiti wa maambukizi hospitalini ni muhimu.
Wakati gani mtu mwenye dalili anapaswa kwenda hospitali?
Nenda hospitali haraka ikiwa una:
Homa kali inayoendelea.
Kutetemeka sana au baridi kali.
Kupumua kwa shida.
Kuchanganyikiwa.
Kuzimia au udhaifu mkubwa.
Mapigo ya moyo kwenda haraka sana.
Shinikizo la damu kushuka.
Mkojo kupungua sana.
Hali ya mwili kuzorota haraka.
Dalili hizi zinaweza kuashiria sepsisi, ambayo ni dharura ya kitabibu.
Tofauti kati ya fangasi wa kawaida na fangasi kwenye damu
Hali | Maana |
Fangasi wa uke | Maambukizi ya fangasi kwenye uke |
Fangasi wa mdomo | Fangasi kwenye mdomo au koo |
Fangasi wa ngozi | Maambukizi kwenye ngozi |
Kandidemia | Fangasi wameingia kwenye damu |
Invasive candidiasis | Fangasi wameingia kwenye tishu au viungo vya ndani |
Kwa hiyo, kuwa na fangasi ukeni, mdomoni au kwenye ngozi hakumaanishi una fangasi kwenye damu. Kandidemia ni hali tofauti na inahitaji uchunguzi na matibabu ya hospitalini.
Hitimisho
Fangasi kwenye damu (kandidemia) ni maambukizi makubwa yanayosababishwa na fangasikuingia kwenye mfumo wa damu na yanaweza kuenea hadi kwenye viungo vingine. Mara nyingi huonekana zaidi kwa wagonjwa wenye sababu za hatari kama kulazwa ICU, matumizi ya catheter ya mshipa, upasuaji mkubwa, antibiotics za muda mrefu au kinga dhaifu.
Dalili zake si maalumu, hivyo kipimo cha kuotesha fangasi na tathmini ya kitabibu ni muhimu katika kuthibitisha ugonjwa. Matibabu huhusisha dawa maalumu za antifungal, ufuatiliaji wa blood cultures na wakati mwingine kuondoa chanzo kama catheter iliyoambukizwa.
Fangasi wa uke, ngozi au mdomo si sawa na fangasi kwenye damu. Mtu mwenye homa kali, kutetemeka, kupumua kwa shida, kuchanganyikiwa, shinikizo la damu kushuka au hali kuzorota haraka anapaswa kupata huduma ya hospitali bila kuchelewa.
Maswali 10 yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu fangasi kwenye damu
1. Je, mtu anaweza kuwa na fangasi kwenye damu bila kuwa na dalili?
Ndiyo, inawezekana hasa mwanzoni mwa maambukizi au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa mwingine unaoficha dalili. Hata hivyo, kandidemia kwa kawaida huleta mabadiliko fulani katika hali ya mgonjwa, kama homa inayoendelea, udhaifu au kuzorota kwa afya kwa ujumla. Kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini, dalili hizi zinaweza kuchanganywa na maambukizi mengine, hivyo uchunguzi wa maabara huwa muhimu.
Mtu anayekuwa katika hatari kubwa, kwa mfano mwenye catheter ya mshipa au kinga dhaifu, anaweza kufuatiliwa kwa karibu hata kama dalili hazionekani wazi. Hii haimaanishi kwamba kila mtu mwenye sababu ya hatari anahitaji kupimwa fangasi mara kwa mara; daktari huamua kulingana na hali ya mgonjwa na dalili.
Kwa hiyo, kutokuwa na dalili hakutoshi kusema kwamba hakuna kandidemia, lakini pia hakuna sababu ya kudhani una fangasi kwenye damu bila ushahidi wa kitabibu au wa maabara.
2. Je, mtu mwenye fangasi wa uke wa muda mrefu anaweza kupata fangasi kwenye damu?
Fangasi wa uke mara nyingi hubaki kwenye eneo la uke na kwa mtu mwenye afya kwa ujumla hauendi kwenye damu. Hata ugonjwa wa fangasi inayojirudia mara kwa mara haiwezi, kwa yenyewe, kuthibitisha kwamba fangasi umeingia kwenye damu.
Kandidemia huonekana zaidi katika mazingira yanayorahisisha Fangasi kuvuka kinga za mwili, kama upasuaji mkubwa, matumizi ya vifaa vya mshipa, kinga dhaifu au ugonjwa mkali. Kwa hiyo, historia ya fangasi wa uke pekee haitoshi kumfanya mtu afikiri ana kandidemia.
Hata hivyo, mwanamke mwenye fangasi wa uke ambaye pia ana homa isiyoelezeka, kutetemeka, udhaifu mkubwa au hali ya afya kuzorota anapaswa kuchunguzwa kwa sababu dalili hizo zinaweza kuashiria tatizo jingine linalohitaji matibabu.
3. Je, vipimo vya kawaida vya damu vinaweza kuonyesha fangasi kwenye damu?
Vipimo vya kawaida kama hesabu kamili ya damu (FBC)Â vinaweza kuonyesha kwamba mwili unapambana na maambukizi, lakini kwa kawaida haviwezi kuthibitisha kwamba maambukizi hayo yamesababishwa na Fangasi. Kwa mfano, mabadiliko katika chembe nyeupe za damu yanaweza kutokea katika maambukizi mengi ya bakteria, virusi au fangasi.
Kipimo muhimu zaidi cha kuthibitisha kandidemia ni kipimo cha kuotesha fangasi kwenye damu, ambapo damu huwekwa kwenye mazingira maalumu ya maabara ili kuona kama fangasi wanakua. Baada ya kupatikana, maabara inaweza kutambua aina ya fangasi na wakati mwingine kupima mwitikio wake kwa dawa.
Kwa hiyo, mtu hawezi kuhitimisha kuwa ana fangasi kwenye damu kwa kuangalia tu FBC, ESR, CRP au kipimo kingine cha kawaida cha damu. Vipimo hivyo vinaweza kusaidia kutathmini hali ya mgonjwa, lakini si uthibitisho wa kandidemia.
4. Je, fangasi kwenye mkojo inamaanisha fangasi wapo pia kwenye damu?
Si lazima. Fangasi wnaweza kupatikana kwenye mkojo bila kuwa imeingia kwenye damu, hasa kwa watu wenye mpira wa mkojo au matatizo fulani ya njia ya mkojo. Hali hii inaweza kuwakilisha uwepo wa fangasi bila maambukizi makubwa ya mwili mzima.
Kwa upande mwingine, katika baadhi ya wagonjwa, fangasi kwenye mkojo inaweza kuhusishwa na maambukizi ya njia ya mkojo au, mara chache, kuhusishwa na maambukizi yanayoanzia sehemu nyingine. Hivyo matokeo haya yanahitaji kutafsiriwa pamoja na dalili na hali ya mgonjwa.
Kwa hiyo, Fangasi kwenye mkojo si sawa na kandidemia. Daktari anaweza kuhitaji kufanya vipimo vingine, ikiwa ni pamoja na blood culture, endapo kuna sababu za kushuku maambukizi ya damu.
5. Je, mtu anaweza kujua mwenyewe kwamba ana fangasi kwenye damu kwa kuangalia rangi ya damu au dalili za mwili?
Damu yenye fangasi haiwezi kutambulika kwa macho kwa kuangalia rangi yake. Pia hakuna dalili ya nje ya mwili ambayo inaweza kuthibitisha kandidemia kwa uhakika.
Dalili kama uchovu, kutokwa jasho, kuwashwa, kupungua uzito, ulimi kuwa mweupe au maumivu ya mwili zinaweza kusababishwa na hali nyingi tofauti. Kuzihusisha moja kwa moja na fangasi kwenye damu kunaweza kuchelewesha kutambua ugonjwa halisi.
Ndiyo maana kandidemia inahitaji tathmini ya kitabibu na vipimo vinavyofaa. Hakuna kipimo cha nyumbani kinachoweza kuthibitisha fangasi kwenye damu kwa kutazama dalili pekee.
6. Kwa nini mtu anaweza kuendelea kuwa na homa licha ya kutumia antibayotiki?
Antibayotiki hutibu bakteria, si fangasi. Ikiwa homa inasababishwa na kandidemia, kutumia antibiotic pekee kunaweza kutofanya homa iishe kwa sababu chanzo cha maambukizi bado hakijatibiwa.
Hata hivyo, homa inayoendelea wakati wa antibiotics haimaanishi moja kwa moja kwamba mtu ana fangasi. Inaweza kusababishwa na bakteria ambao dawa haijawafaa, maambukizi ya virusi, ugonjwa mwingine usio wa maambukizi au chanzo kingine cha homa.
Kwa mgonjwa mwenye sababu za hatari za kandidemia ambaye homa inaendelea licha ya matibabu, daktari anaweza kufanya uchunguzi mpana zaidi, ikiwa ni pamoja na blood cultures na vipimo vingine, badala ya kuanza dawa za antifungal bila uthibitisho.
7. Je, mtu mwenye kandidemia anaweza kutibiwa nyumbani?
Mara nyingi kandidemia huhitaji tathmini na matibabu ya hospitalini, hasa mwanzoni, kwa sababu dawa zinazotumika mara nyingi hutolewa kwa njia ya mshipa na mgonjwa anahitaji kufuatiliwa kwa karibu.
Hospitalini pia kunaweza kufanyika blood cultures za ufuatiliaji, vipimo vya figo na ini, pamoja na uchunguzi wa kutafuta kama maambukizi yameenea kwenye viungo vingine. Hii ni tofauti na fangasi wa kawaida wa ngozi au uke ambao mara nyingi unaweza kutibiwa bila kulazwa.
Baada ya hali ya mgonjwa kuwa imara na vigezo vya kitabibu kutimizwa, daktari anaweza kubadilisha aina ya dawa au njia ya kuitoa. Uamuzi huo unategemea majibu ya vipimo na hali ya mgonjwa, si kwa kujisikia nafuu pekee.
8. Je, kandidemia inaweza kurudi baada ya mtu kupona?
Ndiyo, inaweza kutokea, hasa kama sababu iliyochangia maambukizi haijaondolewa au mgonjwa bado ana sababu kubwa za hatari. Kwa mfano, mtu anayehitaji catheter ya mshipa kwa muda mrefu au ambaye kinga yake iko chini anaweza kubaki katika hatari.
Kurudi kwa homa baada ya matibabu hakumaanishi moja kwa moja kwamba fangasi umerudi. Kunaweza kuwa na maambukizi mengine au tatizo tofauti kabisa. Ndiyo maana mgonjwa aliyewahi kupata kandidemia anapaswa kuchunguzwa ikiwa dalili zinarudi.
Kukamilisha matibabu kama alivyoelekezwa, kuhudhuria ufuatiliaji na kudhibiti chanzo cha maambukizi ni muhimu katika kupunguza uwezekano wa kurudia.
9. Je, kandidemia inaweza kuathiri uwezo wa kupata watoto baadaye?
Kandidemia yenyewe si sababu ya kawaida ya utasa. Maambukizi haya huathiri zaidi mfumo wa damu na yanaweza kuathiri viungo vingine, lakini si kawaida kusababisha uharibifu wa moja kwa moja wa mayai, mbegu za kiume au mfumo wa uzazi.
Hata hivyo, ikiwa maambukizi makali yamesababisha ugonjwa mkubwa wa mwili au yameenea kwenye kiungo fulani cha uzazi, hali hiyo inaweza kuwa tofauti. Athari pia zinaweza kutegemea ugonjwa uliosababisha au kuambatana na kandidemia.
Kwa hiyo, mtu aliyewahi kutibiwa kandidemia na baadaye akapata changamoto ya kupata ujauzito hapaswi kudhani moja kwa moja kwamba chanzo ni fangasi kwenye damu. Uchunguzi wa sababu nyingine za utasa unahitajika.
10. Baada ya kutibiwa fangasi kwenye damu, ni dalili gani zinapaswa kunifanya nirudi hospitali?
Mtu aliyewahi kuwa na kandidemia anapaswa kutafuta matibabu ikiwa anapata tena homa, kutetemeka, udhaifu mkubwa au hali ya afya kuzorota. Dalili mpya pia zinaweza kuonyesha kwamba maambukizi hayajaondoka kabisa, yamerudi au kuna tatizo jingine.
Mabadiliko ya kuona, maumivu makali ya macho, kuchanganyikiwa, kupumua kwa shida, maumivu makali ya kifua au tumbo, kupungua sana kwa mkojo au kuzimia ni dalili zinazohitaji tathmini ya haraka.
Muhimu zaidi, usiache dawa za antifungal kwa sababu tu umeanza kujisikia vizuri. Muda wa matibabu huamuliwa kulingana na blood cultures, dalili, aina ya kandida na kama kuna maambukizi katika viungo vingine.
Imeandikwa:
22 Agosti 2026, 17:44:08
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba, au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii
Rejea za mada hii:
Pappas PG, Kauffman CA, Andes DR, Clancy CJ, Marr KA, Ostrosky-Zeichner L, et al. Clinical practice guideline for the management of candidiasis: 2016 update by the Infectious Diseases Society of America. Clin Infect Dis. 2016;62(4):e1-e50. doi:10.1093/cid/civ933.
Kullberg BJ, Arendrup MC. Invasive candidiasis. N Engl J Med. 2015;373(15):1445-1456. doi:10.1056/NEJMra1315399.
Pappas PG, Lionakis MS, Arendrup MC, Ostrosky-Zeichner L, Kullberg BJ. Invasive candidiasis. Nat Rev Dis Primers. 2018;4:18026. doi:10.1038/nrdp.2018.26.
Clancy CJ, Nguyen MH. Diagnosing invasive candidiasis. J Clin Microbiol. 2018;56(5):e01909-17. doi:10.1128/JCM.01909-17.
Kett DH, Azoulay E, Echeverria PM, Vincent JL; Extended Prevalence of Infection in ICU Study Group of the European Society of Intensive Care Medicine. Candida bloodstream infections in intensive care units: analysis of the extended prevalence of infection in intensive care unit study. Crit Care Med. 2011;39(4):665-670. doi:10.1097/CCM.0b013e318206c3ca.
Guinea J. Global trends in the distribution of Candida species causing candidemia. Clin Microbiol Infect. 2014;20 Suppl 6:5-10. doi:10.1111/1469-0691.12539.
Arendrup MC, Patterson TF. Multidrug-resistant Candida: epidemiology, molecular mechanisms, and treatment. J Infect Dis. 2017;216(suppl_3):S445-S451. doi:10.1093/infdis/jix131.
Kauffman CA. Candiduria. Clin Infect Dis. 2005;41 Suppl 6:S371-S376. doi:10.1086/430918.
