Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin L, MD
Jumanne, 26 Oktoba 2021

Fangasi ukeni kwenye ujauzito
Maambukizi ya fangasi ukeni ni husababisha kutokwa na uchafu usio wa kawaida wakati wa ujauzito. Tatizo hili huwapata wanawake wengi haswa kwenye kipindi cha pili cha ujauzito yani wiki ya 13 hadi 27 ya ujauzito.
Nini husabaisha maambukizi ya fangasi wakati wa ujauzito
Wakati wa ujauzito kuna mabadiliko ya homoni yanayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kupata maambukizi ya fangasi ukeni, tafiti zinaonyesha kuwa maambukizi ukeni hutokea sana kipindi hiki kutokana na mabadiliko ya utindikali wa uke unaosababishwa na mabadiliko ya homoni.
Dalili za fangasi ukeni kwenye ujauzito
Dalili za fangasi ukeni wakati wa ujauzito ni;
Ongezeko la ute unaotoka ukeni unaoambatana na sifa zifuatazo;
Kuwa mweupe kama pamba au kama maziwa mgando
Ute usio na harufu mara nyingi, hata hivyo unapokuwa na harufu hunuka kama mkate
Kuwashwa maeneo yanayozunguka tundu la na mashavu ya uke
Vihatarishi
Mambo yafuatayo yanaongeza hatari ya kupata fangasi ukeni kwenye ujauzito;
Matumizi ya dawa za uzazi wa mpango
Matumizi ya antibayotiki au dawa jamii ya steroid
Kuwa na kiwango cha juu cha sukari kama kwa wagonjwa wa kisukari
Kushiriki ngono
Kujisafisha na kemikali au sabuni ukeni
Kutumia marashi ya kuweka ukeni
Damu ukeni au kuwa na shahawa kutokana na kutojisafisha
Magonjwa mengine yanayosababisha uchafu ukeni kwenye ujauzito
Magonjwa mengine yanayoweza kuleta dalili kama hizi ni;
Maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama kisonono, kaswende n.k
Vipimo na utambuzi
Mara nyingi daktari atatambua kwa kutumia historia ya tatizo lako baada ya kukuulzia maswali, endapo atataka kutofautisha na magonjwa mengine au kuthibitisha, ataagiza vipimo vifuatavyo kufanyika;
Kipimo cha culture ya majimaji kutoka ukeni
Kipimo cha syphilis
Ni dawa gani unapaswa kutumia wakati wa ujauzito kutibu fangasi ukeni?
Si dawa zaote unapaswa kutumia wakati wa ujauzito kwa matibabu ya fangasi ukeni. Dawa nyingi zinazotumika ni zile za kuweka ukeni au kupaka. Dawa za kumeza za fangasi hazishauriwi kutumika, wasiliana na daktari wako kwa ushauri zaidi wa dawa gani inakufaa. Unaweza kusoma 'dawa za kutibu fangasi ukeni' kwenye makala zingine ndani ya tovuti hii.
Wakati gani uwasiliane na daktari?
Unapaswa kuhofu kuwa una maambukizi ukeni au tatizo la kufanyiwa uchungnzi wa haraka endapo uchafu au ute wenye sifa zifuatazo unatoka ukeni;
Ute wenye rangi ya njano
Ute wa kijani
Ute wa kijivu
Ute wenye harufu kali au ya kuoza
Ute mweupe mzito kama maziwa mgando
Ute wenye rangi nyekundu ( damu mbichi)
Ute unaoambatana na muwasho, wekundu au kuvimba kwa mashavu ya uke
Ute unaoambatana na harufu kali au kama ya samaki
Ute unaoambatana na maumivu ya tumbo la chini au wakati wa kukojoa
Ukitokwa na ute au uchafu wenye rangi na sifa zilizotajwa hapo juu kwenye ujauzito wasiliana na daktari wako kwa uchuguzi na tiba.
Kinga ya maambukizi ya fangasi ukeni kwenye ujauzito
Ili kujikinga na maambukizi ya fangasi kwenye ujauzito, fanya mambo yafuatayo
Vaa nguo zisiyobana na inayoruhusu hewa kuingia mwilini
Tumia nguo za ndani zenye pamba
Kausha maeneo ya uke baada ya kuoga au kufanya mazoezi
Kula vyakula vya maziwa mgando na ingine vilivyochachushwa ili kufanya bakteria walinzi waongezeke ukeni
Usitumie manukato ya kuweka ukeni
Jisafishe uke kutoka mbele kwenda nyuma badala ya nyuma kwenda mbele kuepuka kutia uchafu au majimaji ya njia ya haja kubwa ukeni
Sehemu gani nyingine unaweza kupata taarifa zaidi?
Pata taarifa zaidi kuhusu ute unaotoka ukeni, rangi ya kawaida na isiyo ya kawaida na maana yake kiafya kwa kubofya linki inayofuata.
1. https://www.ulyclinic.com/post/rangi-ya-majimaji-ukeni-na-maana-zake-kiafya-uly-clinic
Majina mengine ya tatizo la fangasi ukeni kwenye ujauzito
Baadhi ya watu hufahamu tatizo hili kama;
Kutokwa na maziwa ukeni wakati wa ujauzito
Uchafu mweupe mzito ukeni wakati wa ujauzito
Kuwashwa ukeni wakati wa ujauzito
Kutokwa na maji yasiyo ya kawaida ukeni wakati wa ujauzito