top of page

Mwandishi:

Mhhariri

Dkt. Benjamin L, MD

Dkt. Salome A, MD

Jumanne, 31 Mei 2022

Gono

Gono

Utangulizi


Gono ni moja ya ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria anayeitwa Neisseria gonorrhoeae. Kimelea huyu mara nyingi huathiri mrija wa mkojo wenye jina la urethra pamoja na shingo ya kizazi kwa wanawake.


Dalili mara nyingi huwa hazionekani na endapo zitaonekana kwa kawaida huwa pamoja na maumivu wakati wa kukojoa na kutokwa uchafu kwenye mrija wa mkojo.


Ugonjwa huu hutibiwa kwa dawa jamii ya antibayotiki. Matibabu huhusisha pande mbili yaani mtu na mpenzi wake.


Kama mgonjwa akipata matibabu mapema, huzuia kupata madhara ya muda mrefu kama makovu kwenye njia ya mkojo na utasa.


Dalili za Gono


Mara nyingi Gono haisababishi dalili yoyote ile na endapo zitaonekana huwa pamoja na;

 • Maumivu kama ya kuungua wakati wa kukojoa

 • Kutokwa na uchafu au usaha sehemu za siri

 • Maumivu wakati wa kumwaga manii

 • Kuvimba korodani

 • Kutokwa damu ukeni baada ya kujamiiana

 • Kutokwa na damu katikati ya vipindi vya hedhi

 • Maumivu chini y kitovu


Dalili zingine za Gono


Kama maambukizi yamesambaa sehemu nyingine ya mwili mbali na mfumo wa uzazi, dalili zinaweza kujumuisha:


 • Maumivu ya koo

 • Maumivu wakati wa kutoa haja kubwa

 • Kutokwa na uchafu kwenye haja kubwa

 • Maumivu ya jicho

 • Maumivu ya koo


Unaweza kusoma zaidi kuhusu dalili za Gono kwa wanaume na wanawake katika makala zingine ndani ya tovuti ya ULY CLINIC


Vihatarishi vya kupata Gono


Gono mara nyingi huwaata watu walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 35 na huambukizwa kwa njia ya kujamiiana na mtu mwenye maambukizi pasipo kutumia kinga, ngono inaweza kuwa ya uke kwa kinywa, uume kwa kinywa, uume kwa njia ya haja kubwa au uume kwa uke au uke kwa uke. Watoto wachanga pia wanaweza kupata maambukizi kutoka kwa wazazi wao wakati wa kuzaliwa.


Vipimo


Mara nyingi vipimo huwa havihitajiki kugundua ugonjwa huu, na ugonjwa hutibiwa kwa kutumia dalili pamoja na uchunguzi wa mwili unaofanywa na daktari.

Kama vipimo vitahitajika huhusisha kipimo cha bacteria culture na sensitivity kinachoangalia uwepo wa bakteria kwenye majimaji ya sehemu iliyoathirika na dawa gani yenye uwezo wa kuua vimelea hao.


Matibabu ya Gono


Gono hutibiwa kwa dawa jamii ya antibayotiki. Matibabu huhusisha pia kutibu mpenzi au wapenzi unaoshiriki ngono ili kuzuia mwendelezo wa maambukizi. Endapo unaoshiriki nao ngono hawajapata tiba, unaweza kupata maambukizi mara moja baada ya kushiriki nao.


Kinga maambukizi ya Gono


Gono huepukwa mara nyingi kwa kutumia kondomu kwa kila tendo moja. Ni muhimu pia kupima kabla ya kushiriki ngono na endapo mmoja wenu ana maambukizi, mnapaswa kutibiwa wote ili kuvinja mwendelezo wa maambukizi.


Madhara ya Gono


Kama Gono isipotibiwa, mara nyingi huweza kusababisha madhara yafuatayo:

 • Makovu kwenye mrija urethra na falopia

 • Kusinyaa kwa mrija wa urethra na falopia

 • Maumivu sugu ya mrija wa urethra au uume

 • Utasa

 • Maambukizi kwenye via vya uzazi (PID)

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

8 Mei 2023 15:20:56

Rejea za mada hii:

1. CDC fact sheet (detailed version). Gonorrhea. Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/std/gonorrhea/stdfact-gonorrhea.htm. Imechukuliwa 28.05.2022

2. Ghanem KG. Clinical manifestations and diagnosis of Neisseria gonorrhoeae infection in adults and adolescents. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 28.05.2022

3. Office on Women's Health. Gonorrhea. . https://www.womenshealth.gov/a-z-topics/gonorrhea. Imechukuliwa 28.05.2022

4. Merck Manual Professional Version. Gonorrhea. https://www.merckmanuals.com/professional/infectious-diseases/sexually-transmitted-diseases-stds/gonorrhea. Imechukuliwa 28.05.2022

5. Chlamydia, gonorrhea, and nongonococcal urethritis. Mayo Clinic; 2019.
Speer ME. Gonococcal infection in the newborn. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 28.05.2022

bottom of page