Mwandishi:
Mhhariri
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
ULY CLINIC
8 Agosti 2026, 12:56:29

Hidradenaitisi supurativa
Hidradenaitisi supurativa: Vipele sugu vinavyorudia kwenye ngozi
Hidradenaitisi supurativa (Hidradenitis suppurativa, HS)Â ni ugonjwa sugu wa ngozi unaosababisha vinundu vya ndani ya ngozi, uvimbe wenye maumivu, majipu yanayorudia, vidonda vinavyoweza kutoa usaha au damu, na makovu. Mara nyingi huathiri maeneo ambayo ngozi hugusana au kuna vinyweleo na msuguano, kama kwapani, kinena, mapaja ya ndani, chini ya matiti na makalioni.
Tatizo hili mara nyingi huanza kama vipele au vinundu vinavyofanana na chunusi au jipu, hivyo baadhi ya watu hutumia dawa za kawaida kwa muda mrefu bila kupata nafuu ya kudumu. Hidradenaitisi suppurativa si ugonjwa wa zinaa, si ugonjwa unaotokana na uchafu, na hauambukizwi kutoka mtu mmoja kwenda mwingine.
Hidradenaitisi supurativa huonekanaje kwenye ngozi?
Mwonekano unaweza kutofautiana sana kulingana na hatua ya ugonjwa na pia rangi ya ngozi ya mtu. Hili ni jambo muhimu kwa watu wenye ngozi nyeusi au ya kahawia kwa sababu uchochezi wa ngozi hauonekani kila mara kama wekundu unaoonekana kwa urahisi kwenye ngozi nyeupe.
Kwa mtu mwenye ngozi nyeupe, eneo lililoathirika linaweza kuonekana kuwa jekundu, nyekundu iliyokolea au zambarau.
Kwa mtu mwenye ngozi nyeusi au ya rangi ya kunde, vipele hivyo vinaweza kuonekana vya zambarau, kahawia, kahawia iliyokolea au karibu nyeusi, hasa wakati kuna uchochezi au baada ya kupona na kuacha mabadiliko ya rangi. Kwa hiyo, kutokuwepo kwa rangi nyekundu hakumaanishi kwamba hakuna uchochezikinga.
Hidradenaitisi suppurativa inaweza kuonekana kama:
Vinundu vilivyo ndani ya ngozi na kuuma
Vipele vinavyofanana na majipu
Uvimbe unaojirudia katika eneo lilelile
Vinundu vyenye usaha
Vidonda vinavyopasuka na kutoa usaha au damu
Matundu au njia chini ya ngozi zinazounganisha vinundu
Makovu magumu au yaliyojikunja
Mabadiliko ya rangi ya ngozi baada ya vipele kupona
Baada ya muda, vinundu vinavyorudia vinaweza kusababisha makovu na njia/mifereji chini ya ngozi. Hii ni moja ya sifa muhimu zinazosaidia kuitofautisha hidradenaitisi suppurativa na majipu ya kawaida.
Kwa nini hidradenaitisi supurativa hutokea?
Chanzo kamili cha hidradenaitisi suppurativa hakijaeleweka kikamilifu. Hata hivyo, ugonjwa huo unahusishwa sana na kuziba kwa vinyweleo na uchochezi wa ndani wa ngozi. Baadaye, uvimbe huo unaweza kuendelea na kusababisha vinundu, majipu, njia chini ya ngozi na makovu.
Kwa hiyo, si sahihi kueleza ugonjwa huu kama maambukizi ya kawaida ya bakteria pekee. Bakteria wanaweza kuwepo kwenye vidonda au maambukizi ya pili yanaweza kutokea, lakini msingi wa hidradenaitisi suppurativa ni mchakato sugu wa uchochezi wa ngozi.
Vitu vinavyoweza kuongeza hatari au kuchochea tatizo
Baadhi ya mambo yamehusishwa na uwezekano mkubwa wa kupata au kuwa na hidradenaitisi suppurativa, ingawa si kila mtu mwenye moja ya mambo haya atapata ugonjwa huo.
Msuguano wa ngozi
Msuguano wa mara kwa mara katika maeneo kama makalio, mapaja ya ndani, kinena na kwapa unaweza kuongeza usumbufu wa ngozi.
Jasho na joto
Joto na unyevunyevu vinaweza kufanya ngozi iwe rahisi kuwashwa na kuchochea vipindi vya tatizo kwa baadhi ya watu.
Uzito mkubwa
Uzito mkubwa unaweza kuongeza msuguano na mikunjo ya ngozi. Pia umehusishwa na ugonjwa huu.
Uvutaji wa sigara
Uvutaji sigara umehusishwa kwa kiasi kikubwa na hidradenaitisi suppurativa na unaweza kufanya ugonjwa uwe mgumu zaidi kudhibiti.
Historia ya familia
Baadhi ya watu wenye hidradenaitisi suppurativa huwa na mtu mwingine wa familia mwenye tatizo kama hilo, jambo linaloonyesha kuwa kuna mchango wa vinasaba kwa baadhi ya wagonjwa.
Mabadiliko ya homoni
Kwa baadhi ya wanawake, vipindi vya ugonjwa vinaweza kuhusiana na mabadiliko ya homoni na wakati mwingine dalili huongezeka karibu na hedhi.
Dalili za hidradenaitisi supurativa
Dalili hutofautiana kulingana na hatua ya ugonjwa. Dalili za kawaida ni:

Vinundu vyenye maumivu:Â Huonekana ndani ya ngozi na vinaweza kuhisiwa kama mpira au uvimbe mgumu chini ya ngozi.
Majipu yanayorudia:Â Tofauti na jipu moja linalotokea mara moja, hidradenaitisi suppurativa inaweza kusababisha vinundu vipya katika eneo lilelile mara kwa mara.
Usaha:Â Baadhi ya vinundu hujaa usaha na hatimaye kupasuka.
Kutokwa na damu:Â Vidonda vilivyofunguka vinaweza kutoa mchanganyiko wa usaha na damu.
Harufu:Â Vidonda vinapotoa majimaji mara kwa mara vinaweza kuwa na harufu isiyopendeza.
Makovu:Â Baada ya vipindi vingi vya uchochezi, makovu yanaweza kubaki na ngozi inaweza kuwa ngumu au kubadilika umbo.
Mabadiliko ya rangi:Â Kwa ngozi nyeusi au ya kunde, maeneo yaliyowahi kuathirika yanaweza kubaki na rangi ya kahawia iliyokolea, zambarau au nyeusi baada ya uchochezi kupungua.
Hidradenaitisi supurativa ya makalioni
Ingawa watu wengi huifahamu Hidradenaitisi supurativa kwa vipele vya kwapani au kinena, inaweza pia kutokea kwenye makalio na maeneo yanayozunguka makalio.
Mtu anaweza kuanza kuona vinundu vidogo kwenye makalio ambavyo huonekana kama vimeumwa na mdudu au kama chunusi. Baada ya muda vinaweza kuvimba, kuuma na kutoa usaha. Kipele kinaweza kukauka, lakini baada ya siku au wiki vinundu vingine vinaweza kutokea tena.
Ikiwa hali hii imeendelea kwa miaka, inaweza kuacha makovu na njia chini ya ngozi. Hivyo, mtu mwenye vipele vinavyorudia sehemu ileile kwa muda mrefu, hasa vinavyouma au kutoa usaha, anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa hidradenaitisi supurativa.
Je, hidradenaitisi supurativa ni ugonjwa wa zinaa?
Hapana. Hidradenaitisi supurativa si ugonjwa wa zinaa na haiambukizwi kwa kufanya ngono. Pia si ugonjwa unaosababishwa na kutofanya usafi.
Hata hivyo, kwa sababu baadhi ya vidonda vinaweza kuwa karibu na sehemu za siri, vinaweza kuchanganywa na magonjwa ya zinaa. Mtaalamu wa afya anaweza kufanya uchunguzi na vipimo vya magonjwa ya zinaa ikiwa historia na dalili zinaonyesha uwezekano huo.
Je, hidradenaitisi supurativa husababishwa na uchafu?
Hapana. Hili ni jambo muhimu sana kueleweka. Mtu anaweza kuoga vizuri, kuvaa nguo safi na kutunza ngozi yake ipasavyo lakini bado akapata hidradenaitisi supurativa. Kwa hiyo, kumwambia mtu mwenye Hidradenaitisi supurativakwamba ana vipele kwa sababu haogi vizuri kunaweza kumfanya ajisikie vibaya na pia kuchelewesha kupata matibabu sahihi.
Usafi wa ngozi bado ni muhimu kwa ajili ya kupunguza jasho, uchafu na maambukizi ya pili, lakini usafi hauondoi chanzo cha Hidradenaitisi supurativa.
Uchunguzi wa hidradenaitisi supurativa
Kwa kawaida, utambuzi wa hidradenaitisi supurativa hufanywa zaidi kwa kutumia historia ya mgonjwa na uchunguzi wa ngozi. Hakuna kipimo kimoja cha damu kinachoweza kuthibitisha Hidradenaitisi supurativa.
Mtaalamu wa afya anaweza kuuliza:
Tatizo lilianza lini?
Vinundu vinatokea mara ngapi?
Huonekana sehemu gani?
Huuma?
Hutoa usaha au damu?
Hupona na kurudi tena?
Kuna makovu?
Kuna mtu mwingine wa familia mwenye tatizo kama hilo?
Je, dalili huongezeka wakati fulani wa mzunguko wa hedhi?
Je, mtu anavuta sigara?
Je, kuna magonjwa mengine kama kisukari au psoriasis?
Wakati wa kuchunguza ngozi, mtaalamu hutafuta vinundu, majipu, vidonda, makovu na njia zinazounganisha sehemu mbalimbali chini ya ngozi.
Vipimo vinavyoweza kufanyika
Hakuna kipimo cha damu kinachothibitisha moja kwa moja hidradenaitisi supurativa. Vipimo huchaguliwa kulingana na hali ya mgonjwa.
Swab au uchunguzi wa usaha
Ikiwa kidonda kinatoa majimaji, sampuli inaweza kuchukuliwa ili kutafuta bakteria au maambukizi mengine. Hii inaweza kuwa muhimu hasa ikiwa kuna mashaka ya maambukizi ya pili.
Vipimo vya damu
Vipimo vinaweza kufanywa kutathmini afya kwa ujumla au kutafuta hali zinazoweza kuambatana na ugonjwa, lakini havithibitishi Hidradenaitisi supurativa yenyewe.
Ultrasound ya ngozi
Katika baadhi ya wagonjwa, ultrasound inaweza kusaidia kuonyesha vinundu vya ndani na njia zilizo chini ya ngozi ambazo huenda zisionekane vizuri juu ya ngozi.
Bayopsi ya ngozi
Si kila mgonjwa huhitaji biopsy. Inaweza kuzingatiwa ikiwa utambuzi haueleweki au kuna haja ya kuondoa uwezekano wa ugonjwa mwingine wa ngozi.
Differential diagnosis ya hidradenaitisi suppurativa
Kwa sababu Hidradenaitisi supurativa inaweza kufanana na magonjwa mengine, mtoa huduma anapaswa kutofautisha na hali mbalimbali.
Majipu ya kawaida
Majipu husababishwa na maambukizi ya vinyweleo na tishu zinazozunguka. Hidradenaitisi supurativa, kwa upande mwingine, huwa na tabia ya kurudia katika maeneo yale yale na kusababisha makovu na njia chini ya ngozi.
Folikulaitisi
Folikulaitisi kwa kawaida huonekana kama vipele vidogo vinavyohusiana na vinyweleo. Mara nyingi huwa juu zaidi kwenye ngozi kuliko vinundu virefu vya Hidradenaitisi supurativa.
Chunusi za vulgarisi
Chunusi zinaweza kuwa na vinundu na usaha, lakini Hidradenaitisi supurativa kwa kawaida huathiri maeneo maalum kama kwapa, kinena, mapaja ya ndani na makalioni na huwa na historia ya kurudia, vidonda na makovu.
Kifukomaji(sisti)
Kifukomaji kinaweza kuonekana kama uvimbe mmoja chini ya ngozi na inaweza kuvimba au kuambukizwa. Hata hivyo, kifukomaji kimoja si sawa na Hidradenaitisi supurativa inayosababisha vidonda vinavyorudia na njia nyingi chini ya ngozi.
Ugonjwa wa Pilonido
Hali hii huathiri zaidi sehemu ya juu ya mpasuko wa makalio karibu na mfupa wa mkia. Inaweza kutoa usaha na kuonekana kama jipu, hivyo inaweza kuchanganywa na Hidradenaitisi supurativa.
Magonjwa ya zinaa
Herpes inaweza kusababisha malengelenge na vidonda vinavyouma, wakati kaswende inaweza kusababisha vidonda au vipele katika hatua mbalimbali. Uchunguzi wa historia na vipimo husaidia kutofautisha hali hizi.
Hatua za hidradenaitisi supurativa
Hidradenaitisi supurativa inaweza kugawanywa kwa hatua kulingana na ukubwa na kina cha ugonjwa.
Hatua ya kwanza
Kuna vinundu au majipu yanayorudia lakini bado hakuna njia kubwa chini ya ngozi wala makovu mengi.
Hatua ya pili
Vinundu vinakuwa vya mara kwa mara zaidi na vinaweza kuanza kuunda njia chini ya ngozi pamoja na makovu.
Hatua ya tatu
Kuna maeneo mengi yaliyounganishwa na njia nyingi chini ya ngozi, vidonda vinavyorudia na makovu makubwa. Hatua hii inaweza kuathiri uwezo wa mtu kutembea, kukaa au kufanya shughuli za kawaida. Mojawapo ya mifumo inayotumika sana kitabibu ni Hatua za Hurley.
Matibabu ya hidradenaitisi supurativa
Matibabu hutegemea ukali wa ugonjwa, eneo lililoathirika, idadi ya vidonda, uwepo wa njia chini ya ngozi na jinsi ugonjwa unavyoathiri maisha ya mgonjwa. Lengo ni kupunguza vipindi vya ugonjwa, kupunguza maumivu, kuzuia vidonda vipya, kudhibiti uchochezi na kuzuia makovu na njia zaidi kutokea.
Huduma ya ngozi
Mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia bidhaa laini za kusafisha ngozi na kuepuka vitu vinavyokera ngozi. Baadhi ya wagonjwa wanaweza kufaidika na dawa za kuosha zenye uwezo wa kupunguza bakteria kwenye ngozi.
Epuka kubinya vipele
Kubinya au kutumbua vinundu vya Hidradenaitisi supurativa kunaweza kujeruhi ngozi na kuzidisha uchochezi.
Antibayotiki
Antibiotiki zinaweza kutumika katika baadhi ya wagonjwa, hasa kwa kupunguza uchochezi au kutibu maambukizi yanayoambatana na vidonda. Dawa na muda wa matumizi hutegemea hali ya mgonjwa na zinapaswa kuongozwa na mtaalamu wa afya.
Dawa za kupaka
Kwa Hidradenaitisi supurativa isiyo kali, clindamycin ya kupaka inaweza kutumika kwa baadhi ya wagonjwa. Matibabu mengine ya kupaka yanaweza kuchaguliwa kulingana na aina ya vidonda.
Sindano ya steroidi kwenye kidonda
Kwa baadhi ya vinundu vyenye maumivu makali lakini visivyo na maambukizi, mtaalamu anaweza kutumia corticosteroid ndani ya kidonda ili kupunguza uchochezi. Hii haiwezi kutibu njia zilizo chini ya ngozi.
Matibabu ya homoni
Kwa baadhi ya wanawake, hasa pale ambapo kuna uhusiano kati ya dalili na mabadiliko ya homoni, matibabu kama spironolactone au baadhi ya njia za uzazi wa mpango yanaweza kuzingatiwa na daktari.
Dawa za kibaolojia
Kwa Hidradenaitisi supurativaya wastani hadi kali, dawa za kibaolojia zinaweza kuhitajika. Mifano ni adalimumab na secukinumab, kulingana na upatikanaji, vigezo vya mgonjwa na mwongozo wa mtaalamu.
Upasuaji na taratibu maalum
Kwa vidonda vinavyorudia au njia zilizo chini ya ngozi, taratibu kama kuondoa sehemu iliyoathirika, deroofing au upasuaji mwingine zinaweza kuhitajika. Matibabu ya upasuaji mara nyingi huunganishwa na matibabu ya dawa ili kudhibiti ugonjwa kwa ujumla.
Kutoa usaha pekee kwa kuchoma na kufungua jipu kunaweza kupunguza shinikizo kwa muda lakini hakutibu mchakato wote wa Hidradenaitisi supurativa, hivyo vidonda vinaweza kurudi.
Utunzaji wa ngozi nyumbani
Mtu mwenye Hidradenaitisi supurativa anaweza kusaidia ngozi yake kwa:
Kuosha ngozi kwa upole
Kukausha vizuri baada ya kuoga
Kuepuka kubinya au kutumbua vipele
Kuepuka kusugua ngozi kwa nguvu
Kupunguza msuguano
Kuvaa nguo zisizobana
Kubadilisha nguo zenye jasho
Kuepuka bidhaa zinazokera ngozi
Kutumia dawa alizoelekezwa na mtaalamu
Kutafuta matibabu mapema ikiwa vipele vinaendelea kurudia
Kwa baadhi ya watu, kupunguza uzito ikiwa wana uzito mkubwa na kuacha sigara kunaweza kuwa sehemu ya mpango wa kudhibiti Hidradenaitisi supurativa. Hata hivyo, Hidradenaitisi supurativa inaweza kutokea pia kwa mtu asiye na uzito mkubwa na asiyevuta sigara.
Je, polyester na nailoni zinaweza kuathiri Hidradenaitisi supurativa?
Polyester na nailoni ni nyuzi za sintetiki na si sababu ya moja kwa moja ya hidradenaitisi supurativa. Hata hivyo, nguo zinazobana au zinazohifadhi joto na unyevunyevu zinaweza kuongeza msuguano, jasho na muwasho kwa baadhi ya watu.
Mtu mwenye Hidradenaitisi supurativa anaweza kujaribu kuvaa nguo zisizobana na zinazopitisha hewa vizuri, hasa kama anatambua kwamba aina fulani ya nguo hufanya dalili ziwe mbaya zaidi. Lengo si kusema kwamba polyester au nailoni ni marufuku, bali kupunguza mazingira yanayoweza kuchochea usumbufu wa ngozi.
Hidradenaitisi supurativa na magonjwa mengine
Hidradenaitisi supurativa inaweza kuambatana na matatizo mengine ya kiafya, ndiyo maana uchunguzi wa mgonjwa mzima ni muhimu. Hali zinazoweza kuhusishwa nayo ni pamoja na uzito mkubwa, kisukari, baadhi ya magonjwa ya moyo, arthraitisi na soriasis.
Kwa wagonjwa wenye Hidradenaitisi supurativa ya muda mrefu, hasa yenye vidonda sugu katika eneo la kinena au karibu na njia ya haja kubwa, mtaalamu anaweza pia kuangalia mabadiliko yasiyo ya kawaida ya vidonda kwa sababusaratani ya chembe squamous imehusishwa kwa nadra na Hidradenaitisi supurativa ya muda mrefu.
Madhara yanayoweza kutokea
Hidradenaitisi supurativa isipotibiwa au ikiwa ni kali inaweza kusababisha:
Maumivu ya muda mrefu
Vidonda vinavyotoa usaha mara kwa mara
Makovu
Njia chini ya ngozi
Harufu kutokana na majimaji ya vidonda
Ugumu wa kutembea au kukaa
Maambukizi ya pili
Athari kwenye kazi na shughuli za kila siku
Msongo wa mawazo, huzuni au aibu
Kwa nadra, saratani ya ngozi aina ya squamous cell carcinoma kwenye maeneo yenye Hidradenaitisi supurativa ya muda mrefu.
Wakati gani mtu amuone daktari?
Mtu anapaswa kutafuta uchunguzi ikiwa:
Vipele vinaendelea kurudia katika eneo lilelile
Vinundu vinauma na kuwa vya ndani ya ngozi
Vipele vinatoa usaha au damu
Kuna makovu yanayoongezeka
Kuna matundu au njia chini ya ngozi
Tatizo limeendelea kwa miezi au miaka
Matibabu ya kawaida ya majipu hayasaidii
Kuna vidonda vinavyopona polepole sana
Kuna homa au dalili za maambukizi makubwa
Tatizo linaanza kuathiri kukaa, kutembea, kufanya kazi au maisha ya kawaida
Uchunguzi wa mapema ni muhimu, kwa sababu Hidradenaitisi supurativa inaweza kuwa rahisi zaidi kudhibiti kabla haijafikia hatua ya kutengeneza njia nyingi chini ya ngozi na makovu makubwa.
Hitimisho
Hidradenaitisi supurativa ni ugonjwa sugu wa ngozi unaoweza kuonekana kama chunusi, majipu au vipele vinavyorudia, lakini huwa na tabia ya kurudia, kutoa usaha, kutengeneza makovu na wakati mwingine njia chini ya ngozi. Si ugonjwa wa zinaa, hauambukizwi na haukusababishwi na uchafu.
Kwa watu wenye ngozi nyeusi au ya kunde, Hidradenaitisi supurativa inaweza kuonekana ya zambarau, kahawia, kahawia iliyokolea au nyeusi badala ya wekundu unaoonekana zaidi kwenye ngozi nyeupe; hivyo rangi ya kipele pekee haitoshi kuamua kama kuna uchochezi. Utambuzi na matibabu ya mapema vinaweza kusaidia kupunguza maumivu, vidonda vipya, makovu na madhara ya muda mrefu.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu hidradenaitisi supurativa
1. Je, hidradenaitisi supurativa inaweza kupona kabisa?
Hidradenaitisi supurativa ni ugonjwa sugu, hivyo kwa watu wengi lengo la matibabu ni kudhibiti ugonjwa badala ya kutegemea kwamba utaondoka kabisa bila kurudi. Matibabu yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa vipindi vya vipele, maumivu, usaha na kuendelea kwa makovu.
Baadhi ya watu wanaweza kuwa na vipindi virefu bila dalili, hasa wanapopata mpango sahihi wa matibabu na kutambua mambo yanayochochea dalili zao.
2. Je, hidradenaitisi supurativa inaweza kuanza kwenye makalio pekee?
Ndiyo. Ingawa kwapa na kinena ni maeneo yanayojulikana sana, hidradenaitisi supurativa inaweza kuathiri makalio na maeneo mengine yanayofaa kwa kutokea kwa ugonjwa huu.
Kwa hiyo, mtu mwenye vipele vya muda mrefu makalioni hapaswi kuhitimisha kwamba ni majipu ya kawaida kwa sababu tu hana vipele kwapani au kinena.
3. Kwa nini kipele kinatokea, kinapona, halafu kingine kinatokea karibu na hapo?
Hii ni tabia inayoweza kuonekana katika hidradenaitisi supurativa. Ugonjwa unaweza kuendelea ndani ya ngozi hata baada ya kipele kimoja kupungua. Vinundu vipya vinaweza kutokea katika eneo lilelile na baada ya muda vinaweza kuungana kupitia njia zilizo chini ya ngozi.
Ndiyo maana historia ya kurudia kwa vipele katika eneo moja ni taarifa muhimu sana wakati wa uchunguzi.
4. Je, mtu mwenye hidradenaitisi supurativa anaweza kufanya mazoezi?
Ndiyo, lakini aina ya mazoezi inaweza kuhitaji kubadilishwa kulingana na eneo na ukali wa vidonda. Mazoezi yanayoongeza sana msuguano au jasho yanaweza kuwa yasiyofaa wakati wa kipindi cha ugonjwa.
Mtu anaweza kuchagua shughuli zinazomletea msuguano mdogo na kubadilisha nguo zenye jasho baada ya mazoezi. Ikiwa mazoezi fulani yanaonekana kuchochea vidonda kila mara, hilo linapaswa kujadiliwa na mtaalamu wa afya.
5. Je, hidradenaitisi supurativa inaweza kusababisha utasa?
Kwa kawaida, hidradenaitisi supurativa yenyewe haimaanishi kwamba mtu hawezi kupata watoto. Hata hivyo, ugonjwa mkali unaoathiri sana maeneo ya kinena, maumivu, msongo wa mawazo au baadhi ya magonjwa yanayoambatana nao yanaweza kuathiri maisha ya ngono na ustawi wa mtu.
Mtu anayepata maumivu au changamoto katika tendo la ndoa kwa sababu ya hidradenaitisi supurativa anapaswa kuzungumza na mtaalamu wa afya badala ya kudhani kwamba ugonjwa huo umesababisha utasa.
6. Je, mtoto anaweza kurithi hidradenaitisi supurativa kutoka kwa mzazi?
Kuna ushahidi wa mchango wa vinasaba kwa baadhi ya watu, na historia ya familia inaweza kuongeza uwezekano wa hidradenaitisi supurativa. Hata hivyo, kuwa na mzazi mwenye Hidradenaitisi supurativa hakumaanishi kwamba mtoto lazima apate ugonjwa huo.
Kwa hiyo, historia ya familia ni sababu ya kuongeza tahadhari, si utabiri wa uhakika kwamba mtoto atapata hidradenaitisi supurativa.
7. Je, hidradenaitisi supurativa inaweza kuchanganywa na jipu?
Ndiyo, hasa wakati ugonjwa umeanza. Zote zinaweza kuonekana kama uvimbe wenye maumivu na usaha.
Kinachosaidia zaidi ni historia ya ugonjwa. Hidradenaitisi supurativa huwa na tabia ya kurudia, kutokea katika maeneo maalum, kuacha makovu na kutengeneza njia chini ya ngozi, wakati jipu la kawaida linaweza kuwa tukio moja linalotokana na maambukizi.
8. Kwa nini watu wenye ngozi nyeusi wanaweza kuonekana kama hawana wekundu?
Rangi ya ngozi huathiri namna uchochezi unavyoonekana. Katika ngozi yenye melanin nyingi, uchochezi unaweza kuonekana zaidi kama zambarau, kahawia, kahawia iliyokolea au nyeusi, badala ya wekundu unaoonekana kwa urahisi kwenye ngozi nyeupe.
Kwa hiyo, wakati wa kuchunguza Hidradenaitisi supurativa kwa mtu mwenye ngozi nyeusi, ni muhimu kuangalia pia joto la ngozi, uvimbe, maumivu, kubadilika kwa rangi, unene wa ngozi, usaha na makovu, si kutafuta wekundu pekee.
9. Je, Hidradenaitisi supurativa inaweza kuathiri afya ya akili?
Ndiyo. Maumivu ya mara kwa mara, harufu ya vidonda, usaha, makovu, aibu na hofu ya watu wengine kuona vidonda vinaweza kuathiri kujiamini na maisha ya kijamii.
Mtu mwenye Hidradenaitisi supurativa anayepata huzuni ya muda mrefu, kujitenga na watu au kupoteza hamu ya shughuli alizokuwa akipenda anapaswa kuzungumza na mtaalamu wa afya. Matibabu ya Hidradenaitisi supurativa yanapaswa kuangalia pia athari zake kwenye maisha ya mtu, si ngozi pekee.
10. Je, mtu mwenye Hidradenaitisi supurativa anapaswa kutoboa jipu ili kutoa usaha?
Kwa kawaida hapana, si vizuri kulibinya au kulitoboa mwenyewe. Kufanya hivyo kunaweza kujeruhi ngozi na kuongeza uchochezi.
Ikiwa kuna uvimbe mkubwa wenye maumivu au usaha mwingi, mtaalamu wa afya anaweza kuamua kama kuna haja ya kufanya utaratibu maalum wa kutoa yaliyomo au kuondoa sehemu iliyoathirika. Hii ni tofauti na kutoboa kidonda nyumbani.
Imeandikwa:
8 Agosti 2026, 12:56:13
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba, au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii
Rejea za mada hii:
Goldburg SR, Strober BE, Payette MJ. Hidradenitis suppurativa: epidemiology, clinical presentation, and pathogenesis. J Am Acad Dermatol. 2020;82(5):1045-1058. doi:10.1016/j.jaad.2019.08.090.
Preda-Naumescu A, Ahmed HN, Mayo TT, Yusuf N. Hidradenitis suppurativa: pathogenesis, clinical presentation, epidemiology, and comorbid associations. Int J Dermatol. 2021;60(11):e449-e458. doi:10.1111/ijd.15579.
Saunte DML, Jemec GBE. Hidradenitis suppurativa: advances in diagnosis and treatment. JAMA. 2017;318(20):2019-2032.
van der Zee HH, Jemec GBE. New insights into the diagnosis of hidradenitis suppurativa: clinical presentations and phenotypes. J Am Acad Dermatol. 2015;73(5 Suppl 1):S23-S26. doi:10.1016/j.jaad.2015.07.047.
Byrd AS, Rosenberg AZ, Shipman WD, Okoh UJ, Mazhar M, Okoye GA, et al. Hidradenitis suppurativa in Black and White patients: a clinical study. Eur Rev Med Pharmacol Sci. 2023;27(3 Suppl):92-98. doi:10.26355/eurrev_202304_31325.
Okeke CAV, Perry JD, Simmonds FC, Erskine AE, Shipman WD, Seltzer JA, et al. Clinical trials and skin of color: the example of hidradenitis suppurativa. Dermatology. 2022;238(1):180-184. doi:10.1159/000516467.
Okoye GA, et al. Hidradenitis suppurativa: racial and socioeconomic considerations in management. Int J Dermatol. 2022;61. doi:10.1111/ijd.16163.
Robinson I, Lee L, Cotton C. The impact of racial differences on treatment strategies in hidradenitis suppurativa: a retrospective review. J Drugs Dermatol. 2022;21(3):270-275. doi:10.36849/JDD.6446.
Vlassova N, Kuhn D, Okoye GA. Hidradenitis suppurativa disproportionately affects African Americans: a single-center retrospective analysis. Acta Derm Venereol. 2015;95(8):990-991.
Yang JH, Moon J, Kye YC, Kim KJ, Kim MN, Ro YS, et al. Demographic and clinical features of hidradenitis suppurativa in Korea. J Dermatol. 2018;45(12):1389-1395. doi:10.1111/1346-8138.14656.
Nguyen TV, Damiani G, Orenstein LAV, Hamzavi I, Jemec GBE, et al. Hidradenitis suppurativa: an update on epidemiology, phenotypes, diagnosis, pathogenesis, comorbidities and quality of life. J Eur Acad Dermatol Venereol. 2021;35(1):50-61.
Elbuluk N, et al. Variations in genetics, biology, and phenotype of cutaneous disorders in skin of color. Part II: differences in clinical presentation and disparities in cutaneous disorders in skin of color. J Am Acad Dermatol. 2022;87(1):S1-S?. [Review].
Choi J, Rookwood R, Yoon I, Campton K, Kobets K. Disparities in hidradenitis suppurativa clinical trials: an updated review of ClinicalTrials.gov from 2020 to 2024. J Drugs Dermatol. 2025;24(12):1203-1207. doi:10.36849/JDD.9066.
