Mwandishi:
Mhhariri
Imeboreshwa:
Dkt. Salome A, MD
Dkt. Benjamin L, MD
27 Agosti 2026, 09:23:41

Kiharusi
Dalili, sababu, vipimo, matibabu, kinga na maisha baada ya kiharusi
Kiharusi, ambacho pia huitwa stroku, ni hali inayotokea pale mtiririko wa damu kwenda sehemu ya ubongo unapozuiwa au mshipa wa damu unapopasuka na kusababisha damu kuvuja ndani au kuzunguka ubongo. Kwa sababu seli za ubongo huhitaji oksijeni na virutubisho vinavyofikishwa na damu, kukatizwa kwa mtiririko huo kunaweza kuharibu sehemu ya ubongo na kusababisha ulemavu au kifo.
Kiharusi ni dharura ya kitabibu. Matibabu ya haraka yanaweza kupunguza uharibifu wa ubongo na kuongeza uwezekano wa mtu kupona vizuri. Kwa hiyo, mtu anayepata dalili zinazoweza kuashiria kiharusi anapaswa kupelekwa hospitali haraka, hata kama dalili zinaanza kupungua au kuisha.
Kiharusi hutokea kwa namna gani?
Kuna aina kuu mbili za kiharusi:
1. Kiharusi cha kuziba kwa mshipa wa damu
Hii ndiyo aina inayotokea mara nyingi zaidi. Hutokea pale gando la damu au mabonge ya mafuta yanapoziba mshipa unaopeleka damu kwenye ubongo. Sehemu ya ubongo iliyo nyuma ya mshipa huo hukosa damu na oksijeni.
Gando linaweza kutengenezwa kwenye mshipa wenyewe au kutoka sehemu nyingine ya mwili, kwa mfano kwenye moyo, kisha kusafiri hadi kwenye ubongo na kuziba mshipa. Aina hii huitwa kiharusi cha isikemia.
2. Kiharusi cha kuvuja damu
Hutokea pale mshipa wa damu unapopasuka na damu kuvuja ndani ya ubongo au kwenye maeneo yanayouzunguka. Damu hiyo inaweza kuharibu seli za ubongo na kuongeza shinikizo ndani ya fuvu.
Shinikizo la damu lisilodhibitiwa ni mojawapo ya vihatarishi muhimu vya aina hii ya kiharusi, ingawa kuna visababishi vingine pia.
Kiharusi cha mpito (TIA) ni nini?
Kiharusi cha mpito (Transient Ischemic Attack-TIA) ni hali ambapo mtiririko wa damu kwenda sehemu ya ubongo huzuiwa kwa muda na dalili zinazofanana na kiharusi hutokea, lakini dalili hizo huisha. Hata hivyo, mtu hawezi kutofautisha TIA na kiharusi halisi kwa kuangalia dalili pekee.
Kwa hiyo, dalili zinapoisha si sababu ya kupuuza hali hiyo. Kiharusi cha mpito kinaweza kuwa ishara kwamba mtu yuko katika hatari ya kupata kiharusi na anahitaji uchunguzi wa haraka ili chanzo kitambuliwe na hatua za kuzuia kiharusi zichukuliwe.
Dalili za kiharusi ni zipi?
Dalili hutegemea sehemu ya ubongo iliyoathirika, lakini mara nyingi huanza ghafla. Dalili muhimu ni:
Uso kupinda upande mmoja au kushindwa kutabasamu vizuri
Mkono mmoja au mguu mmoja kuwa dhaifu au kufa ganzi
Kushindwa kuinua mkono mmoja au yote mawili vizuri
Maneno kuwa mazito, kuvurugika au kushindwa kuzungumza
Kushindwa kuelewa anachoambiwa
Kuona kwa shida, kuona mara mbili au kupoteza uwezo wa kuona
Kupoteza uwiano au kushindwa kutembea vizuri
Kizunguzungu kikali kilichoanza ghafla
Maumivu makali ya kichwa yaliyoanza ghafla, hasa katika kiharusi cha kuvuja damu
Kuchanganyikiwa au kupoteza fahamu katika baadhi ya wagonjwa
Njia rahisi ya kukumbuka dalili: SUMKOMAOMU
SU – Sura: Angalia kama uso umepinda upande mmoja. MKO – Mkono: Muombe mtu anyanyue mikono yote miwili; mmoja unaweza kushindwa kuinuka au kushuka. MAO – Maongezi: Sikiliza kama anaongea kwa shida au maneno yamevurugika. MU – Muda: Usipoteze muda; tafuta huduma ya dharura mara moja.
Dalili zikionekana, andika muda zilipoanza, kwa sababu taarifa hiyo inaweza kuwa muhimu katika kuamua matibabu.

Nani yuko katika hatari zaidi ya kupata kiharusi?
Kiharusi kinaweza kumpata mtu wa umri wowote, lakini hatari huongezeka kadiri umri unavyoongezeka. Vihatarishi vingine vinaweza kudhibitiwa na vingine haviwezi.
Vihatarishi muhimu ni:
Shinikizo la damu
Kisukari
Uvutaji wa sigara au tumbaku
Kiwango kikubwa cha kolestro LDL
Uzito kupita kiasi
Kutofanya mazoezi
Lishe yenye chumvi, mafuta yasiyofaa na sukari nyingi
Matumizi hatarishi ya pombe
Mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, hasa atrial fibrillation
Baadhi ya magonjwa ya moyo
Ugonjwa wa figo
Historia ya TIA au kiharusi cha awali
Umri mkubwa
Historia ya familia ya kiharusi
Shinikizo la damu ni mojawapo ya vihatarishi vinavyoweza kudhibitiwa kwa ufanisi, na WHO inaeleza kuwa udhibiti wake pamoja na mtindo bora wa maisha unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kiharusi.
Vipimo na uchunguzi wa kiharusi
Mtu anayeshukiwa kuwa na kiharusi huchunguzwa haraka ili kujua kama kuna kiharusi, aina gani ya kiharusi na sehemu gani ya ubongo imeathirika.
Uchunguzi unaweza kujumuisha:
Uchunguzi wa mfumo wa fahamu: Kuangalia nguvu za mikono na miguu, uwezo wa kuongea, kuona, kuhisi mguso, kutembea na uratibu wa mwili.
Kipimo cha sukari kwenye damu: Sukari kushuka sana inaweza wakati mwingine kuiga baadhi ya dalili za kiharusi na inahitaji kutengwa.
CT scan ya ubongo: Husaidia kutafuta kuvuja kwa damu na mambo mengine muhimu katika hatua za awali.
MRI ya ubongo: Inaweza kutoa taarifa za kina kuhusu eneo la ubongo lililoathirika.
ECG: Husaidia kutafuta matatizo ya mpangilio wa mapigo ya moyo kama atrial fibrillation.
Vipimo vya damu: Huenda vikafanyika kulingana na hali ya mgonjwa na matibabu yanayopangwa.
Uchunguzi wa mishipa ya shingo na ubongo: Kama ultrasound ya carotid, CT angiography au MR angiography inapohitajika.
Matibabu ya kiharusi
Matibabu hutegemea aina ya kiharusi. Ndiyo maana ni muhimu kufanya picha ya ubongo kabla ya kuamua baadhi ya dawa.
Matibabu ya kiharusi cha kuziba mshipa
Lengo ni kurejesha mtiririko wa damu kwenye eneo la ubongo lililoathirika haraka iwezekanavyo.
Kwa wagonjwa wanaokidhi vigezo, dawa za kuyeyusha mgando wa damu kama alteplase au tenecteplase zinaweza kutumika katika muda unaofaa baada ya dalili kuanza. Kwa baadhi ya wagonjwa wenye mshipa mkubwa ulioziba, upasuaji wa thrombektomi, yaani upasuaji wa kuondoa gando kwa kutumia kifaa kupitia mshipa wa damu, inaweza kufanyika.
Matibabu ya kiharusi cha kuvuja damu
Aina hii haitibiwi kwa dawa za kuvunja gando. Matibabu hulenga kudhibiti kuvuja damu, shinikizo ndani ya fuvu na chanzo cha kuvuja damu. Baadhi ya wagonjwa wanaweza kuhitaji upasuaji au utaratibu maalumu wa kuziba mshipa unaovuja, kulingana na aina na eneo la damu iliyovuja.
Matibabu baada ya hali kutengemaa
Mgonjwa anaweza kuhitaji dawa za kuzuia kuganda kwa damu au dawa nyingine za kupunguza hatari ya kiharusi kingine, kulingana na chanzo cha kiharusi. Pia matibabu yanaweza kujumuisha udhibiti wa shinikizo la damu, kisukari na lehemu(kolestro).
Usitumie aspirin, anticoagulants au dawa nyingine za “kupunguza damu” mwenyewe wakati unashuku kiharusi, kwa sababu ikiwa ni kiharusi cha kuvuja damu, dawa hizo zinaweza kuwa hatari.
Maisha baada ya kiharusi
Madhara ya kiharusi hutegemea sehemu ya ubongo iliyoathirika na ukubwa wa uharibifu. Baadhi ya watu hupona kwa kiasi kikubwa, wakati wengine hubaki na matatizo ya muda mrefu.
Madhara yanaweza kujumuisha:
Udhaifu au kupooza upande mmoja wa mwili
Matatizo ya kutembea na uwiano
Matatizo ya kuongea au kuelewa lugha
Matatizo ya kumeza
Mabadiliko ya kumbukumbu na uwezo wa kufikiri
Mabadiliko ya hisia au tabia
Matatizo ya kuona
Msongo wa mawazo au huzuni baada ya kiharusi
Ukarabati baada ya kiharusi
Ukarabati huanza kulingana na hali ya mgonjwa na unaweza kuhusisha wataalamu mbalimbali, kama:
Daktari
Muuguzi
Mtaalamu wa mazoezi ya viungo
Mtaalamu wa tiba ya kazi
Mtaalamu wa usemi na kumeza
Mtaalamu wa afya ya akili
Mtaalamu wa lishe
Lengo ni kumsaidia mgonjwa kurejesha uwezo aliopoteza, kujitegemea katika shughuli za kila siku na kuzuia matatizo mengine.
Je, kiharusi kinaweza kuzuiwa?
Ndiyo. Hatari ya kiharusi inaweza kupunguzwa kwa kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kubadilishwa. WHO inaeleza kuwa udhibiti wa shinikizo la damu, kuacha tumbaku, kula lishe bora, kufanya mazoezi, kudhibiti kisukari na cholesterol na kupunguza matumizi hatarishi ya pombe ni hatua muhimu za kinga.
Hatua muhimu ni:
Pima na dhibiti shinikizo la damu
Dhibiti kisukari
Pima na dhibiti cholesterol inapohitajika
Acha kuvuta sigara na kutumia tumbaku
Fanya mazoezi mara kwa mara
Kula mboga, matunda, nafaka zisizokobolewa na vyakula vingine vyenye lishe bora
Punguza chumvi, mafuta yaliyojaa na sukari nyingi
Dumisha uzito unaofaa
Punguza au epuka matumizi hatarishi ya pombe
Tumia dawa ulizoandikiwa kwa usahihi
Ikiwa una atrial fibrillation au ugonjwa mwingine wa moyo, fuata matibabu na ufuatiliaji uliopendekezwa
Mtu aliyewahi kupata TIA au kiharusi anahitaji mpango maalumu wa kuzuia kiharusi kingine, kwa sababu historia hiyo huongeza hatari ya kupata kiharusi kingine.
Wakati gani wa kwenda hospitali?
Usisubiri ikiwa mtu ameanza ghafla kupata:
Uso kupinda
Udhaifu au ganzi ya mkono au mguu, hasa upande mmoja
Kushindwa kuongea au kuelewa
Kuona mara mbili au kupoteza uwezo wa kuona
Kushindwa kutembea au kupoteza uwiano ghafla
Kizunguzungu kikali kilichoanza ghafla pamoja na dalili nyingine za mfumo wa fahamu
Maumivu makali ya kichwa yaliyoanza ghafla
Kupoteza fahamu
Hata kama dalili zitaisha baada ya dakika chache, mtu bado anapaswa kutathminiwa haraka kwa sababu inaweza kuwa TIA.
Hitimisho
Kiharusi ni hali inayohitaji kutambuliwa na kutibiwa mapema, lakini hatari yake inaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa kudhibiti shinikizo la damu, kisukari na cholesterol, kuacha sigara, kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora. Kutambua dalili za ghafla na kuwahi hospitali kunaweza kusaidia kupunguza madhara na kuongeza nafasi ya kupona.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu kiharusi
1. Je, mtu anaweza kupata kiharusi akiwa kijana?
Ndiyo. Ingawa hatari ya kiharusi huongezeka kadiri umri unavyoongezeka, kiharusi kinaweza kutokea hata kwa mtu kijana. Kwa watu vijana, daktari anaweza kuangalia pia visababishi tofauti na vile vinavyoonekana zaidi kwa wazee, kulingana na historia ya mtu.
Miongoni mwa mambo yanayoweza kuhusika ni baadhi ya magonjwa ya moyo, matatizo ya kuganda kwa damu, matumizi ya tumbaku, dawa fulani za kulevya, magonjwa yanayoathiri mishipa ya damu na baadhi ya hali za kurithi. Hii haimaanishi kwamba kila kijana mwenye kizunguzungu au ganzi ana kiharusi.
Cha muhimu ni kutazama mwanzo wa dalili na mabadiliko ya ghafla. Udhaifu wa ghafla wa upande mmoja, matatizo ya kuongea au kuona na kupoteza uwiano ghafla vinahitaji tathmini ya haraka bila kujali umri.
2. Je, kiharusi kinaweza kutokea bila mtu kupoteza fahamu?
Ndiyo. Kupoteza fahamu si lazima kuwepo katika kiharusi. Mtu anaweza kuwa macho kabisa lakini akawa na udhaifu wa upande mmoja, uso kupinda au kushindwa kuongea.
Hii ndiyo sababu wakati mwingine watu wanaweza kuchelewa kutafuta huduma kwa sababu wanafikiri kiharusi lazima mtu aanguke na kupoteza fahamu. Kwa kweli, dalili ndogo zinazoanza ghafla zinaweza pia kuwa ishara muhimu.
Ikiwa mtu ana dalili zinazofanana na kiharusi, usisubiri mpaka apoteze fahamu. Muda ambao dalili zilianza ni muhimu kwa timu ya matibabu kuamua hatua inayofuata.
3. Je, mtu aliyepata TIA anaweza kupona na asiwe na tatizo tena?
Dalili za TIA zinaweza kuisha kabisa, lakini hilo halimaanishi kwamba tatizo limekwisha bila haja ya uchunguzi. TIA inaweza kuwa ishara kwamba kuna chanzo kinachoweza kusababisha kiharusi baadaye.
Baada ya TIA, daktari anaweza kutafuta sababu kama shinikizo la damu, ugonjwa wa mishipa ya shingo, atrial fibrillation, cholesterol au sababu nyingine. Matokeo ya uchunguzi yanaweza kusaidia kuchagua njia ya kuzuia kiharusi.
Kwa hiyo, mtu aliyepata dalili za TIA anapaswa kwenda hospitali hata kama sasa anajisikia vizuri. Kutoweka kwa dalili hakutoshi kuthibitisha kwamba hakuna tatizo linalohitaji matibabu.
4. Je, mtu aliyepata kiharusi anaweza kupona kabisa?
Ndiyo, baadhi ya watu hupata nafuu kubwa na wengine wanaweza kurejesha sehemu kubwa ya uwezo waliopoteza. Kiwango cha kupona hutegemea eneo la ubongo lililoathirika, ukubwa wa kiharusi, kasi ya matibabu na afya ya mtu kwa ujumla.
Ukarabati una jukumu muhimu. Mazoezi ya viungo, tiba ya kazi, tiba ya usemi na mbinu nyingine zinaweza kusaidia mtu kujifunza tena au kuboresha uwezo wa kutembea, kuzungumza, kula na kufanya shughuli za kila siku.
Mchakato wa kupona unaweza kuchukua muda na hutofautiana sana kati ya watu. Kwa hiyo, kutokupata nafuu haraka katika siku za mwanzo hakumaanishi kwamba hakuna uwezekano wa kuendelea kuboreka.
5. Je, mtu aliyewahi kupata kiharusi anaweza kupata kiharusi kingine?
Ndiyo, mtu aliyewahi kupata kiharusi yuko katika hatari kubwa zaidi ya kupata kingine. Ndiyo maana baada ya kiharusi ni muhimu kutafuta chanzo chake na kudhibiti vihatarishi.
Daktari anaweza kumpa mgonjwa dawa kulingana na aina na chanzo cha kiharusi, pamoja na mpango wa kudhibiti shinikizo la damu, cholesterol, kisukari au matatizo ya moyo. Aina ya dawa hutegemea hali ya mtu; si kila mgonjwa anahitaji dawa sawa.
Mgonjwa pia anapaswa kufuata miadi ya ufuatiliaji na kuepuka kuacha dawa mwenyewe. Udhibiti wa vihatarishi na matumizi sahihi ya matibabu yanaweza kusaidia kupunguza uwezekano wa kiharusi kingine.
6. Je, shinikizo la damu linaweza kusababisha kiharusi hata kama mtu hajisikii?
Ndiyo. Shinikizo la damu mara nyingi linaweza kuwepo bila dalili zinazoonekana. Mtu anaweza kujisikia mzima kabisa lakini akawa na shinikizo la damu kwa muda mrefu.
Shinikizo la damu lisilodhibitiwa huongeza hatari ya magonjwa ya mishipa ya damu na kiharusi. Ndiyo maana kupima shinikizo la damu mara kwa mara ni muhimu hata kwa mtu ambaye hajisikii mgonjwa.
Ikiwa mtu amegundulika kuwa na shinikizo la damu, anapaswa kufuata mpango wa matibabu aliopewa. Mabadiliko ya lishe, mazoezi, kupunguza chumvi, kuacha sigara na kutumia dawa inapohitajika vinaweza kusaidia kudhibiti hatari.
7. Je, mtu akipata dalili za kiharusi anaweza kupewa aspirin nyumbani?
Si salama kumpa mtu aspirin kwa kujiamulia wakati ana dalili mpya zinazoweza kuwa kiharusi. Sababu ni kwamba kuna aina ya kiharusi inayosababishwa na kuvuja damu, na dawa zinazozuia kuganda kwa damu zinaweza kuongeza tatizo hilo.
Hospitalini, picha ya ubongo hutumiwa kusaidia kutofautisha aina ya kiharusi kabla ya kuamua matibabu fulani. Kwa kiharusi cha ischemia, aspirin inaweza kuwa sehemu ya matibabu baada ya kuvuja damu kutengwa kwa picha ya ubongo, kulingana na tathmini ya kitabibu.
Kwa hiyo, hatua muhimu zaidi nyumbani ni kutafuta huduma ya dharura haraka, si kujaribu kutibu kiharusi kwa dawa bila uchunguzi. Pia usimpe mgonjwa chakula au kinywaji kama ana shida ya kumeza, kwa sababu anaweza kukabwa.
8. Je, kiharusi kinaweza kusababisha matatizo ya kuongea na kuelewa?
Ndiyo. Kiharusi kinapoharibu sehemu za ubongo zinazohusika na lugha, mtu anaweza kushindwa kutamka maneno, kupata maneno sahihi, kuzungumza kwa ufasaha au kuelewa anachoambiwa.
Tatizo la kuongea linaweza kuwa la aina mbalimbali. Mtu anaweza kuwa anajua anachotaka kusema lakini ashindwe kukitamka vizuri, au anaweza kuzungumza lakini akawa na shida ya kuelewa lugha. Uchunguzi wa mtaalamu wa usemi husaidia kutambua aina ya tatizo.
Ukarabati unaweza kusaidia. Mtaalamu wa usemi na lugha anaweza kufanya mazoezi yanayolenga mawasiliano, lugha na wakati mwingine matatizo ya kumeza. Familia pia inaweza kusaidia kwa kumpa mgonjwa muda wa kuzungumza na kutomkatisha haraka.
9. Je, chakula kinaweza kuzuia kiharusi?
Hakuna chakula kimoja kinachoweza kuhakikisha kwamba mtu hatapata kiharusi. Hata hivyo, lishe bora inaweza kusaidia kupunguza vihatarishi kama shinikizo la damu, cholesterol, uzito kupita kiasi na kisukari.
Mlo wenye mboga, matunda, nafaka zisizokobolewa, kunde na vyanzo vinavyofaa vya protini, pamoja na kupunguza chumvi, sukari nyingi na mafuta yaliyojaa, unaweza kuwa sehemu ya kinga ya muda mrefu. Mlo unapaswa pia kuendana na hali ya mtu kama ana kisukari, ugonjwa wa figo au shinikizo la damu.
Kwa hiyo, usitegemee chakula maalumu, juisi au dawa ya asili kama kinga ya pekee dhidi ya kiharusi. Kinga bora inahusisha mchanganyiko wa lishe bora, mazoezi, kutovuta sigara, kudhibiti magonjwa na kutumia dawa zilizoandikwa ipasavyo.
10. Je, kiharusi kinaweza kutokea tena baada ya miaka mingi?
Ndiyo. Historia ya kiharusi inaendelea kuwa jambo muhimu katika kutathmini hatari ya kiharusi kingine, hata kama mtu amekuwa vizuri kwa miaka kadhaa.
Ndiyo maana mtu aliyewahi kupata kiharusi hapaswi kuacha ufuatiliaji au dawa bila ushauri wa daktari kwa sababu tu amekuwa akijisikia vizuri. Vihatarishi kama shinikizo la damu, cholesterol, kisukari, sigara na matatizo ya moyo vinaendelea kuhitaji kudhibitiwa.
Pia, dalili mpya za ghafla zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito sawa na mara ya kwanza. Ikiwa uso unapinda, mkono unadhoofika, maneno yanavurugika, kuona kunabadilika au uwiano unapotea ghafla, tafuta huduma ya haraka badala ya kusubiri kuona kama dalili zitaisha.
Imeandikwa:
27 Agosti 2026, 08:26:44
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba, au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii
Rejea za mada hii:
Campbell BCV, De Silva DA, Macleod MR, Coutts SB, Schwamm LH, Davis SM, et al. Ischaemic stroke. Nat Rev Dis Primers. 2019;5(1):70.
Powers WJ, Rabinstein AA, Ackerson T, Adeoye OM, Bambakidis NC, Becker K, et al. Guidelines for the early management of patients with acute ischemic stroke: 2019 update to the 2018 guidelines. Stroke. 2019;50(12):e344-e418.
Kleindorfer DO, Towfighi A, Chaturvedi S, Cockroft KM, Gutierrez J, Lombardi-Hill D, et al. 2021 guideline for the prevention of stroke in patients with stroke and transient ischemic attack. Stroke. 2021;52(7):e364-e467.
Sacco RL, Kasner SE, Broderick JP, Caplan LR, Connors JJB, Culebras A, et al. An updated definition of stroke for the 21st century: a statement for healthcare professionals from the American Heart Association/American Stroke Association. Stroke. 2013;44(7):2064-89.
Feigin VL, Brainin M, Norrving B, Martins S, Sacco RL, Hacke W, et al. World Stroke Organization (WSO): global stroke fact sheet 2022. Int J Stroke. 2022;17(1):18-29.
Campbell BCV, Khatri P. Stroke. Lancet. 2020;396(10244):129-42.
Powers WJ, Rabinstein AA, Ackerson T, Adeoye OM, Bambakidis NC, Becker K, et al. 2018 guidelines for the early management of patients with acute ischemic stroke. Stroke. 2018;49(3):e46-e110.
Hemphill JC 3rd, Greenberg SM, Anderson CS, Becker K, Bendok BR, Cushman M, et al. Guidelines for the management of spontaneous intracerebral hemorrhage. Stroke. 2015;46(7):2032-60.
Hankey GJ. Stroke. Lancet. 2017;389(10069):641-54.
World Health Organization. Global status report on physical activity 2022. Geneva: World Health Organization; 2022.
