Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Lugonda S, MD
Imeboreshwa:
24 Julai 2026, 05:46:34

Kuvimba tezi tonses (tonsil): Dalili, sababu, matibabu na wakati wa kumuona daktari
Kuvimba tezi tonses
Kuvimba tezi tonses (pia huitwa kuvimba tezi tonsil, tonsilitis au tonsilaitisi) ni hali inayotokea pale tezi tonses zinapopata maambukizi au kuvimba kutokana na sababu mbalimbali. Kwa hiyo, tezi tonses na tezi tonsil ni kitu kimoja; tofauti ni namna ya kutamka au kutumia neno, lakini zote zinamaanisha tezi zilezile zilizopo pande zote mbili za nyuma ya koo.
Ugonjwa huu ni wa kawaida zaidi kwa watoto wenye umri wa miaka 3 hadi 15, lakini unaweza pia kuwapata vijana na watu wazima. Mara nyingi husababishwa na virusi, ingawa wakati mwingine husababishwa na bakteria, hasa bakteria aina ya Streptococcus pyogenes.
Kwa watu wengi, ugonjwa huu hupona ndani ya siku chache kwa matibabu sahihi na kupumzika. Hata hivyo, kwa baadhi ya watu maambukizi yanaweza kujirudia mara kwa mara, kuwa sugu au kusababisha madhara yanayohitaji upasuaji wa kuondoa tezi tonses.
Tezi tonses ni nini?
Tezi tonses ni mkusanyiko wa tishu za mfumo wa kinga zilizopo pande zote mbili za nyuma ya koo. Ni sehemu ya mfumo wa mwili unaoitwa bangiri ya Waldeyer's , ambao pia unajumuisha:
Tezi za adenoidi (zilizopo nyuma ya pua)
Tonses za ulimi
Tonses za pembeni mwa koo
Tishu nyingine za kinga zinazozunguka njia ya hewa ya juu.
Tezi hizi zina chembe nyingi nyeupe za damu zinazotambua na kupambana na bakteria, virusi na vijidudu vingine vinavyoingia kupitia mdomo na pua.
Kazi za tezi tonses
Ingawa watu wengi huzifahamu tu zinapovimba, kwa kawaida tezi hizi zina kazi muhimu katika mfumo wa kinga, hasa kipindi cha utotoni. Kazi zake ni pamoja na:
Kutambua vijidudu vinavyoingia mwilini kupitia chakula na hewa.
Kuzalisha kingamwili zinazosaidia mwili kupambana na maambukizi.
Kuchochea mfumo wa kinga kujifunza kutambua vijidudu mbalimbali.
Kupunguza uwezekano wa maambukizi kufika kwenye njia ya hewa ya chini.
Kazi hizi huwa kubwa zaidi utotoni, hasa kati ya miaka 3 hadi 10. Kadiri mtu anavyokua, mfumo mzima wa kinga huendelea kukomaa na umuhimu wa tezi hizi hupungua.
Ndiyo sababu kuondolewa kwa tezi za tonses kwa wagonjwa wanaostahili upasuaji hakusababishi kushuka kwa kinga ya mwili kwa kiwango kinachosababisha mtu kuwa mgonjwa mara kwa mara, kwani viungo vingine vya mfumo wa kinga huendelea kufanya kazi zake.
Sababu za kuvimba tezi tonses
Sababu ya kawaida ni maambukizi ya vijidudu.
1. Maambukizi ya virusi
Zaidi ya nusu ya wagonjwa hupata ugonjwa huu kutokana na virusi kama vile:
Rhinovirus
Adenovirus
Influenza
Parainfluenza
Coronavirus
Epstein-Barr virus (husababisha mononucleosis)
Enterovirus
Virusi hivi kwa kawaida husababisha dalili za mafua pamoja na koo kuuma.
2. Maambukizi ya bakteria
Bakteria anayesababisha ugonjwa huu mara nyingi ni Streptococcus pyogenes ( Streptococcus kundi A).
Bakteria wengine wanaoweza kusababisha ni:
Staphylococcus aureus
Haemophilus influenzae
Moraxella catarrhalis
Fusobacterium necrophorum (hasa vijana na watu wazima)
Maambukizi ya bakteria yanaweza kuhitaji dawa za antibayotiki baada ya kuthibitishwa au pale daktari anapokuwa na ushahidi mkubwa wa kitabibu.
3. Maambukizi ya fangasi
Fangasi si sababu ya kawaida. Huonekana zaidi kwa:
Watu wenye VVU wasiotumia dawa vizuri,
Wagonjwa wa saratani,
Wanaotumia dawa zinazopunguza kinga,
Wagonjwa wa kisukari kisichodhibitiwa,
Watoto wachanga,
Watu waliotumia antibayotiki kwa muda mrefu.
Jinsi maambukizi yanavyoenea
Vijidudu vinaweza kuenea kupitia:
Mate,
Kukohoa,
Kupiga chafya,
Kushiriki vijiko au vikombe,
Kushikana mikono na kugusa mdomo au pua.
Mtoto mmoja mwenye maambukizi anaweza kuambukiza watoto wengine kwa urahisi shuleni au nyumbani.
Vihatarishi
Mtu anaweza kuwa kwenye hatari zaidi iwapo:
Ni mtoto wa shule,
Hukaa sehemu zenye msongamano,
Ana kinga ya mwili iliyo dhaifu,
Ana mzio wa mara kwa mara,
Huvuta sigara au kuvuta moshi wa sigara,
Ana usafi duni wa kinywa,
Hupata maambukizi ya koo mara kwa mara.
Dalili za kuvimba tezi tonses

Dalili hutegemea chanzo cha ugonjwa na ukali wa maambukizi.
Dalili zinazoweza kujitokeza ni:
Koo kuuma ghafla,
Maumivu wakati wa kumeza,
Kushindwa kumeza vizuri,
Homa,
Kutetemeka,
Sauti kubadilika,
Harufu mbaya mdomoni,
Maumivu ya kichwa,
Maumivu ya mwili,
Uchovu,
Kupungua hamu ya kula,
Mate kutoka mengi kwa watoto,
Mtoto kukataa kula,
Maumivu ya masikio,
Kuvimba tezi za limfu shingoni.
Mgonjwa akifungua mdomo anaweza kuonekana:
Tezi zimevimba,
Zina rangi nyekundu,
Zina usaha mweupe au wa njano,
Koo limevimba.
Dalili za hatari
Mgonjwa anapaswa kufikishwa hospitali haraka endapo atapata zalili za:
Kushindwa kupumua,
Kushindwa kufungua mdomo,
Kushindwa kumeza mate,
Kutoa mate muda wote,
Sauti kubadilika sana,
Uvimbe mkubwa upande mmoja wa koo,
Maumivu makali yanayozidi haraka,
Homa kali isiyoshuka.
Dalili hizi zinaweza kuashiria jipu karibu na tonses au maambukizi makubwa yanayohitaji matibabu ya haraka.
Kuvimba upande mmoja wa tonses
Watu wengi huvimba tonses zote mbili. Hata hivyo, ikiwa tezi moja pekee imevimba kwa muda mrefu, hasa kwa mtu mzima, daktari anaweza kufikiria sababu nyingine kama:
Jipu,
Uvimbe usio wa saratani,
Saratani ya eneo la koo,
limfoma.
Kwa hiyo uvimbe wa upande mmoja unaodumu kwa wiki kadhaa unahitaji uchunguzi wa daktari bingwa wa masikio, pua na koo.
Maambukizi sugu ya tezi tonses
Maambukizi husemwa kuwa sugu pale ambapo:
Yanajirudia mara nyingi,
Dalili haziponi kabisa,
Mgonjwa hupata maumivu ya koo mara kwa mara,
Kuna harufu mbaya ya mdomo inayodumu,
Kuna mabaki meupe yanayojikusanya kwenye mashimo ya tonses.
Mara nyingi bakteria wanaohusika huishi kwa pamoja katika tabaka maalumu linaloitwa biofilm, jambo linalofanya antibayotiki zisifanye kazi vizuri kama ilivyo kwenye maambukizi ya kawaida.
Tonsilithi (mawe kwenye tonses)
Baadhi ya watu hupata chembe ngumu nyeupe au njano zinazojikusanya kwenye mashimo ya tonses. Hizi huitwa tonsilithi au mawe kwenye tonses.
Hazimaanishi kila wakati kuna maambukizi, lakini zinaweza kusababisha:
Harufu mbaya ya mdomo,
Hisia ya kitu kukwama kooni,
Maumivu madogo wakati wa kumeza,
Kukohoa mara kwa mara.
Tonsilithi kubwa au zinazojirudia zinaweza kuhitaji matibabu ya daktari.
Je, kuvimba tonses kunaambukiza?
Ikiwa sababu ni virusi au bakteria, mgonjwa anaweza kuwaambukiza wengine kupitia mate au matone ya hewa yanayotoka wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza kwa karibu. Kunawa mikono mara kwa mara, kufunika mdomo unapokohoa na kutoshirikiana vyombo vya chakula husaidia kupunguza maambukizi.
Uchunguzi wa kuvimba tezi tonses
Daktari huanza kwa kusikiliza historia ya mgonjwa na kufanya uchunguzi wa mwili. Mara nyingi utambuzi unaweza kufanyika kwa kuangalia koo na kutathmini dalili alizonazo mgonjwa. Wakati wa uchunguzi, daktari huangalia:
Ukubwa wa tezi za tonses.
Rangi ya tezi na koo.
Uwepo wa usaha au utando mweupe.
Kuvimba kwa tezi limfu shingoni.
Hali ya kupumua na uwezo wa kumeza.
Dalili za jipu karibu na tonses au maambukizi mengine.
Kwa watoto, daktari pia huangalia kama tonses zimekuwa kubwa kiasi cha kuzuia njia ya hewa au kusababisha mtoto kushindwa kupumua vizuri.
Vipimo vinavyoweza kufanyika
Si kila mgonjwa huhitaji vipimo. Wagonjwa wengi hupata utambuzi kwa historia ya ugonjwa na uchunguzi wa daktari pekee. Hata hivyo, vipimo vinaweza kuhitajika katika baadhi ya wagonjwa ambavyo ni;
1. Kipimo cha Streptococcus (Kipimo cha haraka cha trep)
Hiki ni kipimo kinachofanyika kwa kuchukua sampuli kutoka kwenye tonses kwa kutumia kifaa maalumu.
Matokeo hupatikana ndani ya dakika chache na husaidia kubaini kama maambukizi yanasababishwa na bakteria aina ya Streptococcus kundi A.
2. Kukuza vimelea (Kuotesha vimelea)
Iwapo majibu ya kipimo cha haraka hayako wazi au daktari bado anashuku maambukizi ya bakteria, sampuli inaweza kupelekwa maabara ili kukuza vimelea. Hiki ndicho kipimo chenye usahihi mkubwa zaidi katika kuthibitisha bakteria wa streptococcus.
3. Vipimo vya damu
Vipimo vya damu vinaweza kuhitajika ikiwa:
Ugonjwa unaonekana kuwa mkali,
Daktari anashuku mononucleosis,
Kuna dalili za maambukizi yaliyosambaa mwilini,
Kuna sababu nyingine zinazoweza kufanana na tonsilitis.
4. Vipimo vingine
Kwa wagonjwa wenye uvimbe wa upande mmoja unaodumu kwa muda mrefu au wanaoshukiwa kuwa na saratani, daktari anaweza kupendekeza:
Kipimo cha CT Scan,
MRI,
Ultrasound ya shingo,
Kuchukua kipande cha tishu (bayopsi).
Matibabu ya kuvimba tezi tonses
Matibabu hutegemea chanzo cha ugonjwa, si wagonjwa wote wanahitaji antibayotiki. Kwa wagonjwa wengi wenye maambukizi ya virusi, matibabu hulenga kupunguza dalili wakati mwili ukipambana na maambukizi.
Matibabu ya nyumbani
Wagonjwa wengi hupata nafuu kwa kufanya yafuatayo:
Kupumzika vya kutosha.
Kunywa maji mengi.
Kula vyakula laini visivyokera koo.
Kuepuka sigara na moshi wa sigara.
Kusukutua maji ya uvuguvugu yenye chumvi mara kadhaa kwa siku (kwa watoto wakubwa na watu wazima wanaoweza kusukutua bila kumeza maji).
Kutumia dawa za kupunguza maumivu au homa kama alivyoelekeza daktari.
Kwa watoto wadogo, ni muhimu kuhakikisha wanaendelea kunywa maji ili kuzuia upungufu wa maji mwilini.
Je, antibayotiki zinahitajika kila wakati?
Hili ni kosa ambalo watu wengi hulifanya, kwa kuwa maambukizi mengi ya tonses husababishwa na virusi, antibayotiki hazitasaidia na zinaweza kuongeza usugu wa bakteria dhidi ya dawa pamoja na kusababisha madhara yasiyo ya lazima. Antibayotiki hutolewa pale ambapo:
Maambukizi ya bakteria yamethibitishwa kwa kipimo,
Au daktari ana ushahidi mkubwa wa kitabibu kuwa chanzo ni bakteria.
Ni muhimu kutumia antibayotiki kama ulivyoelekezwa na kumaliza dozi yote hata kama dalili zimeanza kupungua.
Dawa za kupunguza maumivu
Daktari anaweza kupendekeza dawa za kupunguza maumivu na homa kulingana na umri na hali ya mgonjwa.
Kwa watoto, dawa zinapaswa kutolewa kwa kufuata uzito wa mtoto na ushauri wa mtaalamu wa afya.
Epuka kumpa mtoto aspirini bila ushauri wa daktari kwa sababu inaweza kuhusishwa na matatizo makubwa ya afya katika baadhi ya watoto.
Maambukizi sugu ya tonses
Kwa wagonjwa wenye maambukizi yanayojirudia mara kwa mara, daktari hufanya tathmini ya kina ili kubaini sababu. Wakati mwingine tatizo linaweza kuhusishwa na:
Bakteria wanaounda biofilm,
Tonsilithi,
Ukuaji mkubwa wa tonses,
Matatizo ya kinga,
Au sababu nyingine zinazofanana na tonsilitis.
Matibabu hutegemea chanzo kilichobainika.
Je, tonses zinaweza kuondolewa kwa upasuaji?
Upasuaji wa kuondoa tonses unaoitwa tonsilektomi siku hizi haufanywi kwa kila mgonjwa mwenye koo kuuma. Hufanyika pale ambapo faida zake ni kubwa kuliko hatari zinazoweza kutokea.
Ni nani anaweza kuhitaji upasuaji?
Daktari anaweza kupendekeza upasuaji iwapo mgonjwa ana:
Maambukizi yanayojirudia mara kwa mara licha ya matibabu sahihi;
Tonses kubwa zinazozuia kupumua au kumeza;
Kushindwa kupumua wakati wa usingizi (kukosa pumzi usingizini kwa kuziba kwa njia za hewa) kutokana na tonses kubwa;
Jipu la tonses linalojirudia;
Uvimbe unaoshukiwa kuwa saratani au ugonjwa mwingine unaohitaji uchunguzi wa tishu.
Uamuzi wa kufanya upasuaji hutolewa baada ya tathmini ya kina ya daktari bingwa wa masikio, pua na koo.
Baada ya upasuaji
Baada ya kuondolewa tonses, mgonjwa anaweza kupata:
Maumivu ya koo kwa siku kadhaa;
Maumivu yanayosambaa hadi masikioni;
Ugumu wa kula kwa muda mfupi;
Haja ya kunywa maji mengi na kula vyakula laini.
Watu wengi hupona vizuri ndani ya wiki moja hadi mbili. Hata hivyo, damu kutoka kooni baada ya upasuaji ni hali ya dharura na mgonjwa anatakiwa kurejea hospitali mara moja.
Madhara yanayoweza kutokea ikiwa ugonjwa hautatibiwa
Ingawa wagonjwa wengi hupona bila matatizo, baadhi wanaweza kupata madhara kama:
Kuota kwa jipu karibu na tonses;
Maambukizi kusambaa kwenye tishu za shingo;
kushindwa kupumua kutokana na kuziba kwa njia ya hewa;
Homa ya baridi yabisi (homa ya rheumatiki) baada ya maambukizi ya streptococcus yasiyotibiwa ipasavyo;
Kuvimba kwa figo baada ya maambukizi ya streptococcus (Glomerulanephraitisi ya maambukizi ya streptococcal), ingawa ni nadra.
Matatizo haya ni sababu muhimu ya kutafuta matibabu mapema.
Jinsi ya kujikinga
Hakuna njia inayoweza kuzuia kabisa kuvimba kwa tonses, lakini unaweza kupunguza hatari kwa:
Kunawa mikono kwa sabuni mara kwa mara;
Kuepuka kushiriki vijiko, vikombe au chupa za maji;
Kufunika mdomo na pua unapokohoa au kupiga chafya;
Kutovuta sigara na kuepuka moshi wa sigara;
Kudumisha usafi wa kinywa kwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku;
Kula lishe bora na kupata usingizi wa kutosha ili kuimarisha kinga ya mwili;
Kuwapeleka watoto hospitali mapema wanapopata homa na koo kuuma kali.
Wakati wa kumuona daktari
Muone daktari haraka ikiwa:
Koo linauma sana kwa zaidi ya siku tatu hadi tano bila nafuu;
Una homa kali;
Unashindwa kumeza mate;
Unashindwa kupumua vizuri;
Tonses zimevimba sana;
Uvimbe uko upande mmoja tu na unaendelea kuongezeka;
Unapata maambukizi ya tonses mara kwa mara;
Mtoto anakataa kabisa kula au kunywa.
Mambo muhimu ya kukumbuka
Tezi tonses na tezi tonsil ni kitu kimoja.
Maambukizi mengi husababishwa na virusi, hivyo si kila mgonjwa anahitaji antibayotiki.
Maambukizi ya bakteria yanahitaji tathmini ya daktari ili kubaini kama antibayotiki zinahitajika.
Maambukizi yanayojirudia mara kwa mara yanaweza kuhitaji uchunguzi zaidi au upasuaji.
Kushindwa kupumua au kumeza ni dalili za dharura zinazohitaji matibabu ya haraka.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu kuvimba tezi tonses na majibu yake ya kina
​1. Je, mtu anaweza kuvimba tezi tonses mara nyingi ndani ya mwaka mmoja?
Watu wengine hupata maambukizi ya tonses mara kwa mara kuliko wengine. Hali hii huonekana zaidi kwa watoto wanaokwenda shule kwa sababu hukutana na watoto wengi na hivyo kuongeza uwezekano wa kuambukizana virusi na bakteria. Kwa watu wazima, maambukizi yanayojirudia yanaweza kuhusishwa na mazingira ya kazi, uvutaji sigara, mzio wa muda mrefu au magonjwa yanayopunguza kinga ya mwili.
Ikiwa maambukizi yanajirudia mara kwa mara, daktari atataka kujua idadi ya vipindi vilivyotokea ndani ya mwaka mmoja, kama vilithibitishwa na uchunguzi wa kitabibu na kama vilihitaji antibayotiki au kulazwa hospitali. Historia hii husaidia kutathmini kama mgonjwa anaweza kufaidika na matibabu mengine, ikiwemo upasuaji wa kuondoa tonses.
Ni muhimu kutofautisha maambukizi mapya na hali nyingine zinazoweza kufanana na tonsilitis, kama vile mzio, kucheua tinfikali (GERD), mawe kwenye tonses (tonsilithi) au maambukizi ya muda mrefu ya koo. Ndiyo maana kujitibu kila mara bila uchunguzi wa daktari si jambo linaloshauriwa.
2. Je, mtoto mwenye tonses kubwa lazima afanyiwe upasuaji?
Tonses kubwa pekee hazimaanishi kuwa mtoto anahitaji kuondolewa tezi hizo. Kwa watoto wengi, tonses huwa kubwa zaidi katika umri wa utotoni kwa sababu mfumo wa kinga bado unakua, na baadaye hupungua ukubwa kadiri mtoto anavyokua.
Daktari huzingatia kama tonses hizo zinasababisha matatizo ya kiafya. Kwa mfano, mtoto anayekoroma sana kila usiku, anayesimama kupumua wakati wa usingizi, anayopata usingizi usio mzuri au anayeshindwa kula vizuri kutokana na tonses kubwa anaweza kuhitaji tathmini ya kina zaidi.
Uamuzi wa kufanya upasuaji hutegemea dalili, athari kwa afya ya mtoto na matokeo ya uchunguzi, si ukubwa wa tonses pekee. Hivyo wazazi hawapaswi kuogopa wanapoambiwa mtoto ana tonses kubwa, bali wanapaswa kufuata ushauri wa daktari.
3. Je, kuondoa tezi tonses hupunguza kinga ya mwili?
Hili ni swali linaloulizwa mara nyingi sana. Ingawa tonses ni sehemu ya mfumo wa kinga, tafiti nyingi zimeonyesha kuwa kwa wagonjwa wanaochaguliwa vizuri kwa upasuaji, kuondolewa kwa tonses hakusababishi kushuka kwa kinga ya mwili kwa kiwango kinachoongeza maambukizi kwa muda mrefu.
Sababu ni kwamba mwili una viungo vingi vinavyoshiriki kazi za kinga, kama vile tezi za limfu, uboho, wengu, adenoidi na tishu nyingine za mfumo wa limfu. Viungo hivi vinaendelea kufanya kazi hata baada ya tonses kuondolewa.
Hata hivyo, upasuaji hufanywa tu pale unapokuwa na sababu za kitabibu. Tonses haziondolewi kwa kila mtu mwenye koo kuuma, kwa sababu kila upasuaji una faida na hatari zake ambazo lazima zipimwe kwa makini.
4. Je, mtu aliyekwishafanyiwa upasuaji wa kuondoa tonses anaweza bado kupata koo kuuma?
Kuondolewa kwa tonses hakumaanishi kwamba mtu hatapata tena maumivu ya koo. Koo linaweza kuathiriwa na virusi, bakteria, mzio, moshi wa sigara, hewa kavu au asidi inayopanda kutoka tumboni.
Tofauti ni kwamba mtu aliyefanyiwa tonsilektomi hatapata tena maambukizi yanayotokana na tezi za tonses kwa sababu tezi hizo zimeondolewa. Hata hivyo, sehemu nyingine za koo bado zinaweza kuvimba au kuambukizwa.
Kwa hiyo, mtu aliyefanyiwa upasuaji akipata koo kuuma mara kwa mara, ni muhimu kutafuta chanzo halisi badala ya kudhani kuwa upasuaji haukufanikiwa.
5. Je, vyakula au vinywaji vya baridi husababisha kuvimba tezi tonses?
Hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa kula barafu, kunywa maji baridi au kutumia vinywaji vya baridi husababisha tonsilaitisi(kuvimba tonses) moja kwa moja. Maambukizi ya tonses husababishwa na vijidudu kama virusi au bakteria, si joto au baridi ya chakula.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanaweza kuhisi koo linauma zaidi wanapokunywa vitu vya baridi sana au vya moto sana, hasa kama tayari wana maambukizi au uvimbe. Hilo ni suala la kuongeza usumbufu wa dalili, si sababu ya ugonjwa.
Kwa baadhi ya wagonjwa, hasa baada ya upasuaji wa tonses, vyakula vya baridi vinaweza hata kusaidia kupunguza maumivu na uvimbe. Hivyo hakuna sababu ya kuepuka vinywaji vya baridi ikiwa haviongezi usumbufu wako.
6. Je, kuvimba tezi tonses kunaweza kusababisha kukoroma au kushindwa kupumua wakati wa usingizi?
Tonses zinapokuwa kubwa sana, hasa kwa watoto, zinaweza kupunguza nafasi ya kupita kwa hewa kwenye koo. Hali hii inaweza kusababisha mtoto au mtu mzima kukoroma kwa nguvu, kulala kwa mdomo wazi au hata kusimama kupumua kwa sekunde chache wakati wa usingizi. Tatizo hili huitwa Kukosa pumzi usingizini kwa kuziba kwa njia za hewa (OSA).
Watoto wenye tatizo hili wanaweza kuonekana kama wanalala sana lakini usingizi wao unakuwa wa kukatika. Wanaweza kuamka mara kwa mara usiku, kutokwa na jasho wakati wa kulala, kukojoa kitandani, kuwa na usingizi mchana au kushindwa kuzingatia masomo. Kwa baadhi ya watoto, dalili kuu si usingizi bali kuwa na hasira, kutotulia au kufanya vibaya shuleni kutokana na kukosa usingizi wa kutosha.
Iwapo mtoto au mtu mzima anakoroma kila usiku, anasimama kupumua wakati wa usingizi au anaonekana kusongwa na hewa akiwa amelala, ni muhimu kufikishwa kwa daktari kwa uchunguzi. Endapo tatizo linasababishwa na tonses kubwa, matibabu yanaweza kuboresha kwa kiasi kikubwa ubora wa usingizi, ukuaji wa mtoto na afya kwa ujumla.
7. Je, kuvimba tezi tonses kunaweza kuathiri kula, kunywa au ukuaji wa mtoto?
Watoto wenye maambukizi ya mara kwa mara au tonses kubwa wanaweza kushindwa kula vizuri kwa sababu ya maumivu wakati wa kumeza au kutokana na kuziba kwa sehemu ya koo. Hali hii inaweza kufanya mtoto ale chakula kidogo kuliko kawaida na kunywa maji kwa shida.
Tatizo likiendelea kwa muda mrefu, baadhi ya watoto wanaweza kushindwa kuongeza uzito kama inavyotarajiwa au kuchelewa kukua. Hata hivyo, si kila mtoto mwenye tonses kubwa atapata matatizo ya ukuaji. Daktari hutathmini uzito, urefu, historia ya kula na dalili nyingine kabla ya kuhitimisha kuwa tonses ndiyo chanzo.
Wazazi wanapaswa kufuatilia kama mtoto anakataa kula kwa muda mrefu, anapungua uzito, anakunywa maji machache au anaonekana mchovu kila wakati. Dalili hizi zinahitaji uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini sababu na kupanga matibabu yanayofaa.
8. Je, kuvimba tezi tonses kunaweza kuhusiana na harufu mbaya ya mdomo?
Harufu mbaya ya mdomo (halitosisi) inaweza kuwa moja ya dalili za kuvimba kwa tezi tonses, hasa pale maambukizi yanapodumu kwa muda mrefu au kunapokuwa na tonsilithi (mawe kwenye tonses). Mabaki ya chakula, seli zilizokufa na bakteria vinaweza kujikusanya kwenye mashimo madogo ya tonses na kutoa harufu isiyopendeza.
Hata hivyo, si kila harufu mbaya ya mdomo hutokana na tonses. Sababu nyingine zinazoweza kusababisha hali hii ni pamoja na usafi duni wa kinywa, kuoza kwa meno, magonjwa ya fizi, ukavu wa mdomo, uvutaji sigara na baadhi ya magonjwa ya mfumo wa chakula.
Ikiwa harufu mbaya inaendelea licha ya kupiga mswaki, kusafisha ulimi na kutunza afya ya kinywa, ni vyema kufanyiwa uchunguzi wa daktari au daktari wa meno ili kubaini chanzo halisi.
9. Je, mtu mzima anaweza kupata kuvimba tezi tonses au ni ugonjwa wa watoto pekee?
Ingawa ugonjwa huu huonekana zaidi kwa watoto, watu wazima pia wanaweza kuupata. Kwa watu wazima, maambukizi yanaweza kusababishwa na virusi, bakteria au, kwa nadra, magonjwa mengine yanayoathiri mfumo wa kinga.
Tofauti na watoto, uvimbe wa tonses kwa mtu mzima unaodumu kwa muda mrefu, hasa ukiwa upande mmoja tu, unahitaji uchunguzi wa kina zaidi. Hii ni kwa sababu, ingawa si kawaida, unaweza kuhusishwa na magonjwa mengine kama uvimbe usio wa kawaida au saratani ya koo. Watu wanaovuta sigara, wanaokunywa pombe kupita kiasi au walio na maambukizi ya HPV wako kwenye hatari kubwa zaidi ya baadhi ya saratani za eneo la koo.
Kwa hiyo, mtu mzima anayekuwa na maumivu ya koo yanayorudia mara kwa mara, sauti kubadilika, ugumu wa kumeza au uvimbe wa tonses usiopona anapaswa kumuona daktari wa masikio, pua na koo kwa uchunguzi wa mapema.
10. Je, ni kweli kuwa kila koo linalouma linamaanisha mtu ana tonses?
Koo kuuma ni dalili, si ugonjwa wenyewe. Kuna magonjwa mengi yanayoweza kusababisha koo kuuma bila kuhusisha tezi za tonses. Miongoni mwa sababu hizo ni mafua ya kawaida, mafua makali (influenza), COVID-19, mzio, hewa kavu, kuvuta moshi wa sigara, kutumia sauti kupita kiasi na asidi kutoka tumboni (GERD).
Kwa baadhi ya watu, maumivu ya koo yanaweza pia kutokana na vidonda vya mdomoni, maambukizi ya fangasi, maambukizi ya meno au hata magonjwa ya tezi ya thairoidi. Hivyo, kuona koo linauma pekee hakutoshi kusema kuwa mtu ana tonsilaitisi.
Ndiyo maana daktari huchunguza koo lote, pua, masikio na shingo, na wakati mwingine huomba vipimo ili kubaini chanzo halisi cha dalili kabla ya kuanza matibabu.
11. Je, kuna utofauti kati ya matonses na tezi zinazovimba shingoni?
Kuna utofauti mkubwa. Watu wengi hutumia neno "tezi za shingoni"Â kumaanisha uvimbe wowote unaotokea shingoni, lakini kwa kitabibu kuna aina mbalimbali za tezi na viungo vinavyoweza kuvimba katika eneo hilo. Kutambua tofauti zake husaidia kuelewa chanzo cha tatizo na kupata matibabu sahihi.
Tezi tonses (tonsil)Â zipo ndani ya koo, pande zote mbili za nyuma ya mdomo. Kazi yake ni kushiriki katika mfumo wa kinga kwa kutambua na kupambana na vijidudu vinavyoingia kupitia mdomo na pua. Zinapovimba, mgonjwa hupata dalili kama koo kuuma, maumivu wakati wa kumeza, homa na wakati mwingine usaha kwenye tonses.
Kwa upande mwingine, tezi za limfu zipo sehemu mbalimbali za shingo, chini ya taya, nyuma ya masikio, nyuma ya shingo na maeneo mengine ya mwili. Kazi yake ni kuchuja maji ya limfu na kusaidia kupambana na maambukizi. Tezi hizi zinaweza kuvimba kutokana na maambukizi ya koo, meno, ngozi, masikio, kifua kikuu, magonjwa ya mfumo wa kinga au hata baadhi ya saratani. Mara nyingi mtu huhisi kama kuna uvimbe au kifundo chini ya ngozi ya shingo.
Aidha, kuna tezi ya thairoidi  ambayo ipo mbele ya shingo, chini kidogo ya kidaka tonge. Tezi hii haitumiki kupambana na maambukizi bali huzalisha homoni zinazodhibiti kasi ya matumizi ya nishati mwilini (umetaboli), mapigo ya moyo, ukuaji na kazi nyingine nyingi za mwili. Uvimbe wa tezi ya thairoidi unaweza kusababishwa na upungufu wa madini joto, magonjwa ya kinga ya mwili, uvimbe usio wa saratani au saratani, na mara nyingi hauambatani na maumivu ya koo kama ilivyo kwa tonsilaitisi.
Pia kuna tezi za mate kama tezi ya parotidi, submandibulari na sublinguali, ambazo huzalisha mate. Tezi hizi zinaweza kuvimba kutokana na maambukizi, kuziba kwa mirija ya mate au magonjwa ya kinga ya mwili. Uvimbe wake huonekana pembeni mwa uso au chini ya taya na mara nyingi huongezeka wakati wa kula.
Kwa hiyo, si kila uvimbe wa shingo ni "tonses." Eneo lilipo uvimbe, dalili zinazoambatana nao, muda uliokuwepo na matokeo ya uchunguzi wa daktari ndivyo vinavyosaidia kubaini ni tezi gani imeathirika na chanzo chake. Ikiwa uvimbe wa shingo unaendelea zaidi ya wiki mbili hadi tatu, unaongezeka ukubwa, ni mgumu, hauumi au unaambatana na kupungua uzito, jasho la usiku au homa ya muda mrefu, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa haraka ili kuondoa uwezekano wa magonjwa makubwa kama kifua kikuu au saratani.
12. Ugonjwa wa matezi unasababishwa na nini?
Neno "matezi" ni mojawapo ya maneno yanayotumiwa sana na jamii, lakini kwa upande wa kitabibu halimaanishi ugonjwa mmoja maalumu. Mara nyingi watu wanaposema "nina matezi" huwa wanamaanisha kuna tezi fulani zimevimba, bila kujua ni tezi zipi hasa. Hivyo, "matezi" ni jina la jumla linaloweza kumaanisha uvimbe wa tezi za limfu, tezi za tonses (tonsils), tezi ya thairoidi, tezi za mate au hata tezi nyingine zilizopo mwilini. Kwa hiyo, mtu hawezi kutibiwa "matezi" bila kwanza kubaini ni tezi gani zimeathirika na sababu ya kuvimba kwake.
Sababu za kuvimba kwa tezi hutegemea aina ya tezi iliyoathirika. Tezi za limfu huvimba mara nyingi kutokana na maambukizi ya bakteria au virusi, maambukizi ya meno, koo, masikio, ngozi, kifua kikuu, magonjwa ya kinga ya mwili au baadhi ya saratani. Tezi za tonses huvimba kutokana na maambukizi ya virusi au bakteria yanayosababisha tonsilitis. Tezi ya thairoidi inaweza kuvimba kutokana na upungufu wa madini joto, magonjwa ya kinga ya mwili, uvimbe usio wa saratani au saratani. Vilevile, tezi za mate zinaweza kuvimba kutokana na maambukizi, mawe yanayoziba mirija ya mate au magonjwa ya kinga ya mwili.
Kwa sababu sababu za kuvimba kwa tezi ni nyingi, matibabu hutegemea chanzo kilichobainika. Si kila uvimbe wa tezi huhitaji antibiotiki, na si kila uvimbe ni dalili ya saratani. Mtu mwenye uvimbe wa tezi unaodumu zaidi ya wiki mbili hadi tatu, unaoongezeka ukubwa, ni mgumu, hauumi, unaambatana na homa ya muda mrefu, jasho la usiku, kupungua uzito au ugumu wa kupumua au kumeza anapaswa kufika hospitali mapema kwa uchunguzi. Kutambua mapema aina ya tezi iliyoathirika na chanzo chake husaidia kupata matibabu sahihi na kuzuia madhara yanayoweza kutokea.
