Mwandishi:
Mhhariri
Dkt. MangwellaS, MD
Dkt. Lugonda B, MD
Imeboreshwa:
16 Januari 2026, 09:50:13

Kuvunjika fupakola
Kuvunjika kwa fupakola ni aina ya jeraha linalotokea sana kwa watoto na vijana wadogo. Fupakola ni mfupa unaounga mkono kwenye sehemu ya juu ya fupatiti.
Miongoni mwa visababishi vikuu vya kuvunjika kwa fupakola ni ajali ya kunguka wakati umesambaza mikono, kuangukia bega au kupata ajali ya gari.
Vichanga mara nyingi huvunjika fupakola wakati kuzaliwa endapo njia ya uzazi ni ndogo, mtoto ni mkubwa sana, kujifungua kwa kuvutwa na vifaa au kukwama kwa bega la mtoto wakati wa kujifungua.
Unapaswa kutafuta msaada wa huduma za afya mara upatwapo na tatizo hili. Hata hivyo mara nyingi mfupakola uliovunjika hupona wenyewe bila kufanyiwa matibabu endapo hautajongeshwa na kuupa subira.
Utatakiwa kuukanda kwa barafu na kutumia dawa za maumivu au kuufunga mkono ili usijongee kuharakisha uponyaji.
Kama mfupa umevunjika vibaya, utahitaji upasuaji ili kuufanya uunge haraka na katika anatomia yake ya kawaida.
Kuvunji kwa fupakola hufahamika kwa majina mengine ya 'Kuvunjika clavicle' na 'Kuvunjika kwa klaviko'
Dalili
Dalili za kuvunjika kwa fupa kola ni pamoja na;
Maumivu ya mkono yanayoongezeka wakati wa kujongea kwa bega
Uvimbe
Maumivu sehemu iliyovunjika endapo pataguswa
Kuvia kwa damu sehemu mfupa ulipo
Kuhisi sauti ya kusagana kwa mifupa wakati wa bega linajongea
Kupoteza uwezo wa kujongesha bega
Kukakamaa kwa bega
Kwa vichanga kushindwa kujongea kwa mkono siku kadhaa baada ya kuzaliwa
Kichanga kulia anapoguswa mkono uliovunjika
Wakati gani uonane na daktari haraka?
Ukiona dalili yoyote ya kuvunjika fupakola unapaswa kawasiliana na daktari au kufika kituo cha kutolea huduma za afya kwa ushauri na tiba mara moja.
Visababishi
Visababishi vikuu vya kuvunjika fupakola ni;
Kuangukia bega au kuangukia mkono uliosambaa nje
Kupigwa na kitu kwenye bega
Ajali ya gari, pikipiki au baiskeli
Majeraha wakati wa kichanga anapita kwenye njia ya uzazi( kwa vichanga)
Vihatarishi
Vihatarishi vya kuvunjika fupa kola ni;
Kuwa na umri chini ya miaka 20
Kuwa mzee
Fupakola hukomaa mara nyingi mtu anapofikia umri wa miaka 20, hii ndio maana watoto na vijana wadogo wapo kwenye hatari ya kuvunjika mfupa huu. Baada ya kuvuka umri wa miaka 20, hatari hupungua lakini huongezeka tena wakati wa uzeeni.
Madhara
Fupakola mara nyingi hupona bila madhara yoyote kwa watu wengi, hata hivyo baadhi ya watu wanaweza kupata madhara yafuatayo;
Majeraha ya mishipa ya damu na fahamu
Kuunga vibaya au kuchelewa kuunga
Uvimbe kwenye bega
Michomo kinga kwenye maungio ya fupakola
Majeraha ya mishipa ya damu na fahamu
Sehemu zilizochongoka za mfupa uliovunjika zinaweza kutoboa au kukata mishipa ya damu na fahamu hivyo kuleta dalili mbalimbali za kuhisi baridi, ganzi kwenye mkono au kuvilia kwa damu ndani ya bega.
Kuunga vibaya au kuchelewa kuunga
Kama mfupa umevunjika vibaya, unaweza kuchelewa kuunga au kuunga vibaya. Kuunga vibaya kunaweza kuleta mwonekano tofauti wa anatomia ya bega mfano mfupa kuwa mfupi kuliko ulewa mkono mwingine.
Uvimbe wa bega
Uvimbe hutokea sehemu ambayo vipande vya mifupa vimeungana, hii ni moja ya hatua za kuunga kwa mfupa. Baada ya miaka kadhaa, uvimbe huu unaweza kuisha kabisa kwa watu walio wengi au kubakia kwa baadhi ya watu.
Michomo kinga kwenye maungio ya fupakola
Hii hutokea sana kama fupakola umevunjika maeneo ya karibu unapounganika na fupatiti au fupabapa (skapula). Michomo hii huambatana na maumivu makali ya maungio ya bega wakati wa kujongea mkono na uvimbe.
Vipimo na utambuzi
Baada ya kufika hospitali, utachukuliwa historia ya tatizo na kufanyia uchunguzi wa mwili kwenye bega lililoathirika kisha utafanyiwa vipimo kati ya;
X-ray ya bega
CT scan
Matibabu
Msingi wa matibabu ya fupakola uliovunjika ni kupunguza mjongeo wa bega lililovunjika, kufanya hivi huzuia kutonesha, kuharibu harakati za uponyaji na huharakisha mfupa kuunga. Unaweza kufungwa na kitambaa au kupewa kivalo maalumu cha kushikiria mkono wako ili kupunguza mjongeo.
Kwa vichanga ambao wamevunjika wakati wa kuzaliwa, mara nyingi hawavalishwi chochote, mzazi unatakiwa kuwa makini tu na mkono uliovunjika na kudhibiti maumivu tu.
Ni kwa muda gani utatakiwa kutojongesha mkono uliovunjika?
Muda wa kutojongesha mkono au kuvaa kivalo cha kubeba mkono hutegemea aina na ukubwa wa jeraha la kuvunjika. Hata hivyo mara nyingi kwa watoto fupakola huunga baada ya wiki tatu hadi 6 , wakati watu wazima huchukua wiki 6 hadi 12. Baada ya fupakola kuunga unaweza kuacha kutumia kivalo cha kushikiria mkono.
Matibabu ya dawa
Ili kupunguza maumivu na uvimbe, daktari anaweza kukupa dawa za kupunguza maumivu jamii ya nakotiki kwa muda wa siku chache tu. Kisha utaendelea kusubiria mkono upone wenywe. Utahitajika kupunguza mijongeo ya mkono ulioathirika ili kupunguza maumivu. Dawa jamii ya NSAIDS kama Diclofenac, aspirin hazitumiki mara nyingi kwa kuwa huongeza hatari ya kuvia kwa damu kwenye mishipa iliyopasuka.
Mfano wa dawa jamii ya nakotiki ni;
Codeine
Oxycodone
Hydrocodone
Tramadol
Morphine
Hydromorphone
Fentanyl
Carfentanil
Matibabu kwa vichanga na watoto wadogo
Mara nyingi vjichanga hawahitaji kufanyiwa chochote kile na mdupa hupona ndani ya wiki 3 hadi 6. Unaweza kufundishwa kubana mkono uliovunjika kwa kitambaa au nguo aliyovaa mbele ya mwili ili kuzuia kujongea sana wakati unasubiri mfupa upone wenywe (Angalia kwenye picha namba tatu kwa mfano)
Epuka mambo yafuatayo mpaka baada ya wiki 4 hadi 6
Kunyanyua mkono wenye shida juu ya usawa wa bega
Kuweka mgandamizo au mjongeo kwenye bega lililovunjika
Kubebesha uzito kwenye mkono wa bega lililovunjika
Tiba upasuaji
Kama fupakola umevunjika na kuchomoza nje ya mwili au vipande vimetengena sana au umevunjika kwenye vipande vingi, utahitaji upasuaji ili kuondoa vipande, kukutanisha mifupa kwa kuwekewa vyuma ndani au nje ya mfupa.
Tiba mazoezi
Baada ya kupata matibabu ya awali, unaweza kufundishwa mazoezi madogo ya kufanya ili kuzuia kukakamaa kwa mkono. Mazoezi mengine pia utafundishwa kuyafanya wakati mfupa umeshaunga. Unashaurwa usifanye mazoezi ambayo yanaongeza mjongeo kwenye mfupa uliovunjika hivyo kuchelewesha kupona.
Matibabu ya nyumbani
Wakati upo nyumbani unaweza kufanya mambo yafutayao ili kupunguza uvimbe na maumivu pasipo dawa na kuharakisha mfupa kupona;
Kukanda eneo lililoathirika kwa barafu kwa muda wa dakika 20 hadi 30siku mbili hadi 3 za kwanza toka mfupa umevunjika
Kula mlo kamili kutoka kwenye makundi matano ya chakula
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Je, kila mtu anayevunjika fupakola lazima afanyiwe upasuaji?
Hapana. Wagonjwa wengi hupona bila upasuaji, hasa pale ambapo vipande vya mfupa havijatengana sana na mfupa haujachomoza nje ya ngozi. Upasuaji huangaliwa pale tu ambapo kuna hatari ya kupona vibaya, majeraha ya mishipa ya damu/fahamu, au kuvunjika kwa vipande vingi.
2. Kwa nini fupakola hupona vizuri hata bila kufungwa plasta?
Fupakola ina mtiririko mzuri wa damu na misuli inayosaidia kushikilia vipande vya mfupa karibu wakati wa kupona. Kwa watoto hasa, mifupa ina uwezo mkubwa wa kujirekebisha (bone remodeling), hivyo hata kama kuna mkengeuko mdogo, hujirekebisha kadri mtoto anavyokua.
3. Je, ni salama mtoto au mtu mzima kulala upande wa mfupa uliovunjika?
Hapendekezwi katika wiki za mwanzo. Kulala juu ya mfupa uliovunjika kunaweza kuongeza maumivu, kuhamisha vipande vya mfupa, au kuchelewesha kuunga. Ni bora kulala chali au upande wa mkono mzima ukiungwa mkono kwa mto.
4. Ni dalili zipi zinaashiria hatari baada ya kuvunjika fupakola?
Dalili hatarishi ni pamoja na:
Mkono kuwa baridi au ganzi
Kubadilika kwa rangi ya mkono (kuwa bluu au mweupe)
Maumivu makali yasiyopungua hata baada ya dawa
Kuvimba sana au damu kujaa haraka
Dalili hizi zinaweza kuashiria tatizo kwenye mishipa ya damu au fahamu na zinahitaji huduma ya haraka.
5. Je, mtoto anaweza kurudi kucheza au kufanya michezo lini baada ya kupona?
Kwa watoto wengi, michezo mepesi huruhusiwa baada ya wiki 6–8 endapo mfupa umeunganika vizuri. Michezo yenye kugongana (mf. mpira wa miguu, rugby) inashauriwa kusubiri angalau wiki 10–12 ili kuepuka kuvunjika tena.
6. Mwanangu amevunjika fupakola nimeenda hospitali wakaniambia avae arm sling (arm lift) kwa mwezi mmoja kisha wafanye X-ray nyingine. Je, hii ni sahihi?
Ndiyo, hii ni hatua sahihi na ya kitaalamu kabisa.Kuvaa arm sling kwa wiki 4–6:
Hupunguza mjongeo wa bega
Husaidia vipande vya mfupa kuanza kuunganika
Hupunguza maumivuKufanya X-ray ya pili baada ya muda huo husaidia daktari kuthibitisha kama mfupa unaungana vizuri kabla ya kuruhusu matumizi ya kawaida ya mkono.
7. Je, kuna uwezekano mfupa kuunganika lakini mkono ukaonekana mfupi au umepinda?
Ndiyo, inaweza kutokea hasa kama mfupa uliunganika vibaya. Kwa watoto wadogo hili mara nyingi hujirekebisha lenyewe kadri wanavyokua. Kwa watu wazima, kama mkengeuko ni mkubwa na unasababisha maumivu au upungufu wa uwezo wa mkono, upasuaji wa kurekebisha unaweza kuzingatiwa.
8. Je, chakula kina mchango wowote katika kupona kwa fupakola?
Ndiyo. Lishe yenye:
Protini (samaki, mayai, maharage)
Madini ya calcium (maziwa, dagaa)
Vitamin Dhusaidia kuharakisha kuunga kwa mfupa. Upungufu wa lishe bora unaweza kuchelewesha uponyaji.
9. Je, kuvunjika fupakola kunaweza kutokea tena baada ya kupona?
Inawezekana, hasa endapo:
Mfupa haukupona vizuri
Mtu alirudi mapema kwenye michezo au kazi nzito
Kuna ajali nyingineNdiyo maana ni muhimu kufuata muda uliopendekezwa wa mapumziko na maelekezo ya daktari.
10. Je, kuna athari za muda mrefu baada ya kuvunjika fupakola?
Watu wengi hupona kabisa bila tatizo la kudumu. Hata hivyo kwa wachache, kunaweza kubaki:
Maumivu ya mara kwa mara
Uvimbe mdogo wa kudumu
Kukakamaa kwa bega
Tiba ya mazoezi (fiziotherapia) husaidia sana kupunguza athari hizi.
Rejea za mada hii:
Andreas F, Mavrogenis et al. Birth fracture of the clavicle. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/22123402/. Imechukuliwa 18.07.2021.
American Academy of Orthopaedic Surgeons. Clavicle fracture (broken collarbone). http://orthoinfo.aaos.org/topic.cfm?topic=A00072. Imechukuliwa 18.07.2021.
B Kaplan, et al. Fracture of the clavicle in the newborn following normal labor and delivery. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/9849706/. Imechukuliwa 18.07.2021.
Hatch RL, et al. Clavicle fractures. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 18.07.2021.
McKee-Garrett TM. Neonatal birth injuries. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 18.07.2021.
Peters MDJ. Surgical versus conservative interventions for treating broken collarbones in adolescents and adults. Orthop Nurs. 2014;33:171.
The Big List of Narcotic Drugs. https://americanaddictioncenters.org/the-big-list-of-narcotic-drugs. Imechukuliwa 18.07.2021.
