top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

Ijumaa, 27 Novemba 2020

Maambukizi ya Helicobacter pylori

Maambukizi ya Helicobacter pylori

Helicobacter pylori (H. pylori) ni maambukizi ya bakteria katika mfumo wa tumbo, kwa kawaida maambukizi hutokea wakati wa utotoni. Bakteria huyu huwa na tabia ya kusababisha sana vidonda vya tumbo, na takribani nusu ya watu duniani wana maambukizi haya licha ya kutoonyesha dalili yoyote au kuumwa.


Endapo utapata dalili za maambukizi haya ambazo huwa ni dalili za vidonda vya tumbo, daktari wako atakuagiza ufanye vipimo vya kutambua H. pylori.


Dalili za maambukizi ya H. pylori


Licha ya kundi kubwa la watu wenye maambukizi ya H.pylori huwa hawana dalili kutokana na uimara wa miiili yao dhidi ya bakteria hawa, baadhi ya watu huweza kuonyesha dalili ambazo zimeorodheshwa hapa chini;


  • Maumivu ya kuungua na moto tumboni

  • Maumivu ya kuungua na moto nyuma ya mgongo

  • Maumivu ya tumbo ambayo huwa makalai wakati unakula au wakati tumbo likiwa halina kitu

  • Kichefuchefu

  • Kukosa hamu ya kula

  • Kubeua mara kwa mara

  • Hisia za tumbo limejaa au umeshiba

  • Kupoteza uzito bila sababu

  • Kuishiwa damu

  • Kuchoka mwili bila sababu


Wakati gani wa kumwona daktari


Mwone daktari endapo unapata dalili zifuatazo


  • Maumivu ya tumbo makali au yanayoendelea

  • Kushindwa kumeza chakula

  • Kupata haja nyeusi au yenye damu

  • Kutapika damu au vitu vyenye rangi kama unga wa kahawa


Vihatarishi


Maambukizi ya H.pylori hutokea kupitia kuingia kinwani kwa mate, matapishi au kinyesi cha mtu mwenye maambukizi haya. Hata hivyo vyakula vilivyopikwa au kuoshwa na maji yaliyochanganyika na vimelea kutoka kwenye vyanzo vilivyotajwa awali huweza kuwa chanzo cha maambukizi pia. Vihatarishi vya kupata maambukizi haya ni;


  • Kuishi makazi yenye mkusanyiko wa watu wengi

  • Kuishi maeneo ambayo hayana chanzo cha kueleweka cha maji

  • Kuishi mazingira ambayo hayazingatii usafi wa mazingira haswa kwenye swala la usafi wa vyoo na utunzaji wa kinyesi

  • Kuishi na mtu mwenye maambukizi ya H.pylori


Madhara ya maambukizi ya H.pyroli


  • Vidonda vya tumbo- asilimia 10 tu ya watu walioambukizwa H.pylori hupata vidonda vya tumbo

  • Kuvia damu ndani ya tumbo

  • Kutoboka kwa tumbo na utumbo

  • Michomo kwenye kuta za tumbo na kusababisha ugonjwa wa gastritis

  • Hatari ya kupata saratani ya tumbo


Vipimo vya H.pylori


Vipo vipimo mbalimbali ambavyo hutumika katika kupima maambukizi ya H.prlori, vipimo hivyo vimeorodheshwa hapa chini. Kwa maelezo bonyeza kipimo husika kusoma Zaidi.


Kupima urea kwenye pumzi

Utapewa kidonge maalumu au maji yenye molecule za kaboni kasha hewa inayotoka kwenye kinywa chako itapimwa na kifaa maalumu kuangalia uwepo wa kabon molecules kwenye hewa.


Kipimo cha damu

Utachukliwa damu kwenye mishipa ya damu kasha itaenda maabara kupimwa uwepo wa protini maalumu zinazoitwa antibody za bakteria huyu kwenye damu. Antibody hizi huweza kuonaekana pia wiki kadhaa baada ya kupata maambukizi na huweza kudumu mwilini pia kwa miezi kadhaa hata baada ya kutibiwa na kupona. Kwa sababu hiyo huwa hakifanyiki chenyewe, ni vema ukafanya hiki na kingine cha kinyesi ambacho kimeelezewa hapo chini.


Kipimo cha kupiga antijeni

Kipimo hiki hutumia sampuli ya kinyesi ili kuangalia uwepo wa H.pylori kwenye mfumo wako wa chakula. Huwa ni kipimo kizuri kwa sababu kinaonyesha maambukizi yanayoendelea, kipimo hiki mara nyingi huweza kufanyika pamoja na kipimo cha hapo juu, lakini pia kinajitosheleza chenyewe kuangalia maambukizi hayo.


Kipimo cha kamera- endoscopy

Hiki ni kipimo kinachotumia mrija maalumu wenye kamera ili kuangalia njia ya mfumo wa chakula. Utapewa dawa ya usingizi kukulewesha kabla ya kuingiziwa kipimo hiki. Daktari ataona njia ya mfumo wa chakula na tumbo kasha atachukua sampuli kidogo ya nyama kutoka kwenye tumbo lako kwa ajili ya kufanya kipimo cha kuangalia uwepo wa bakteria H.pylori. kipimo hiki si lazima kuwa cha kwanza kufanyika wakati mwingi ukilinganisha na vipimo vilivyoorodheshwa hapo juu kwa sababu huwa cha gharama na kina hatua nyingi.


Kipimo cha culture

Sampuli ya kipimo hiki hutokea kwenye kinyama kilichokatwa kutoka kwenye tumbo baada ya kufanyiwa kipimo cha endoscopy


Baadhi ya vitu au mambo yinavyoweza kusababisha majibu yako ya kipimo cha antijeni na antibody yasiwe sahihi ni matumizi ya baadhi ya dawa kama dawa za jamii ya Proton pump Inhibitor, dawa ya bismuth subsalicylate, na dawa za antibayotiki. Utatakiwa kuacha tumia dawa hizi kwa wiki moja au mbili kabla ya kupima vipimo hivi.


Matibabu ya H.pyrol

​

Mara baada ya kupimwa na kukutwa na maambukizi ya H.pylori utatakiwa kuanza kutumia dawa za kupambana na maambukizi hayo pamoja na zile za kuzuia uharibifu unaoendelea kusababishwa na bacteria huyu. Utapewa da kutoka kwenye makundi matatu hadi manne. Tafiti zinaonyesha baadhi ya dawa zinazotumika sana na watu zimeshakuwa na usugu hivyo ni vema ukafahamu katika eneo lako bakteria hawa wanaitikia kwenye dawa gani. Makundi ya dawa hizo huwa ni;


  • Dawa jamii ya proton pump inhibitor (PPI)- mfano wake ni omeprazole. Pantoprazole n.k

  • Dawa kundi la histamine, mfano ni cimetidine n.k (endapo mgonjwa kama mbadala wa dawa za PPI)

  • Dawa kundi la antibayotiki- mfano wake ni clindamycin, fluoroquinolones n.k

  • Dawa za kurejesha ute kwenye tumbo mfano wake ni Dawa ya bismuth subcyclate


Je baada ya kupona ninaweza kupata maambukizi mengine?


Kupata tiba ya H.Pylori huwa haitoi kinga kupata maambukizi mengine unatakiwa kuzingatia njia za kujikinga kupata maambukizi mapya. Hata hivyo ukipata maambukizi mengine utatibiwa kama ilivyoandikwa hapo juu


Kinga


Unaweza kujikinga na mambukizi ya H.Pylori kwa kufanya mambo yafuatayo;


  • Kwenye maeneo ambayo maambukizi ya H.pylori ni makubwa hakikisha huli au kunywa vitu vilivyoandaliwa bila kuzingatia usafi na kanuni za kiafya

  • Hakikisha kama una familia mmepima maambukizi ya H.pylori na endapo kuna watu wamegundulika nao basi wapate tiba

  • Tumia maji ya kunywa au kuoshea matunda yaliyochemshwa na kupoa

  • Hakikisha unanawa mikono kwa sabuni kila unapotoka chooni au unapotoka safari

  • Usitumie vyomba pamoja na mtu mwenye maambukizi mpaka apate tiba

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

13 Aprili 2022 20:41:45

Rejea za mada hii:

1.Peptic ulcer. Centers for Disease Control and Prevention. http://www.cdc.gov/ulcer/keytocure.htm. Imechukuliwa 25.11.2020

2.National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases. Peptic ulcers (stomach ulcers).. https://www.niddk.nih.gov/health-information/digestive-diseases/peptic-ulcers-stomach-ulcers/all-content. Imechukuliwa 25.11.2020

3.Papadakis MA, et al. Gastrointestinal disorders. In: Current Medical Diagnosis & Treatment 2017. The McGraw-Hill Companies; 2017. http://www.accessmedicine.com. Imechukuliwa 25.11.2020

4.Merck Manual Professional Version .Helicobacter pylori infection. https://www.merckmanuals.com/professional/gastrointestinal-disorders/gastritis-and-peptic-ulcer-disease/helicobacter-pylori-infection. Imechukuliwa 25.11.2020

5.University of Arizona. H. Pylori Transmission and Spread of Infection. https://publichealth.arizona.edu/outreach/health-literacy-awareness/hpylori/transmission. Imechukuliwa 25.11.2020

6.NCI. Helicobacter pylori and Cancer. https://www.cancer.gov/about-cancer/causes-prevention/risk/infectious-agents/h-pylori-fact-sheet. Imechukuliwa 25.11.2020

7.Carolyn J. Hildreth, MD etal. Helicobacter pylori. https://jamanetwork.com/article.aspx?doi=10.1001/jama.300.11.1374. Imechukuliwa

bottom of page