Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Salome A, MD
Jumapili, 13 Julai 2025

Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI
Virusi vya Ukimwi (VVU) ni vimelea vinavyoshambulia kinga ya mwili. Maambukizi haya, yakiachwa bila matibabu, husababisha UKIMWI (Upungufu wa Kinga Mwilini). Hali hii huufanya mwili kuwa dhaifu na kuathirika kirahisi na magonjwa mbalimbali, yanayojulikana kama magonjwa nyemelezi.
Dalili za VVU
Dalili hutegemea hatua ya maambukizi:
1. Hatua ya mwanzo (Siku 2–6 baada ya maambukizi)
Homa ya ghafla
Maumivu ya kichwa na koo
Kikohozi kikavu
Kuvimba tezi za shingo, kwapani au mapajani
Upele mwilini
Kuharisha au kichefuchefu
Uchovu usioelezeka
Dalili hizi huisha ndani ya wiki 2–4, na mara nyingi huhisiwa kama mafua au malaria.
2. Hatua tulivu (Miaka 2–10 bila dalili)
Mwili huonekana mzima lakini virusi huendelea kuzaliana kimyakimya na kuharibu seli za kinga (CD4).
3. Hatua ya UKIMWI (Mwisho wa mchakato wa maambukizi)
Dalili nyingi huonenaka kutokana na upungufu wa kinga mwilini, baadhi yake zinaweza kuhusisha;
Kupungua uzito kwa kasi
Kuharisha sugu
Kikohozi kisichoisha
Kelele au maambukizi ya mara kwa mara ya kinywa au uke
Magonjwa nyemelezi kama kifua kikuu, nimonia sugu, kansa aina ya Kaposi, nk.
Njia za maambukizi ya VVU
VVU huambukizwa kupitia:
Ngono isiyo salama (bila kondomu)
Kushirikiana vitu vyenye damu kama sindano au wembe
Mama kwenda kwa mtoto (ujauzito, wakati wa kujifungua au kunyonyesha)
Damu au bidhaa za damu zilizo na VVU
Hatari ya kuambukizwa huongezeka ikiwa:
Unajamiiana na mtu mwenye maambukizi bila kutumia kinga
Unatumia dawa za kulevya kwa sindano
Unapata magonjwa ya zinaa
Una vidonda sehemu za siri
Upimaji na Utambuzi wa VVU
Upimaji wa VVU ni njia pekee ya kuthibitisha kama mtu ameambukizwa:
Unaweza kupima VVU katika vituo vya afya au kwa kutumia self-test kit
Vipimo huchukua dakika 15–30 kutoa majibu
Umuhimu wa CD4
CD4 ni aina ya seli nyeupe zinazosaidia mwili kupambana na maambukizi. Kupungua kwa CD4 huashiria kushuka kwa kinga ya mwili:
CD4 ya kawaida: 500–1600/mm³
Hatari huanza chini ya 350/mm³
CD4 chini ya 200 = UKIMWI
Matibabu ya VVU
Wakati wa kuanza dawa za ARV
Watu wote wanaogundulika na VVU wanashauriwa kuanza dawa mara moja bila kusubiri CD4 kushuka (Treat All Approach).
Makundi ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV)
NRTIs (Nucleoside Reverse Transcriptase Inhibitors) – Zidovudine, Lamivudine
NNRTIs (Non-Nucleoside RTIs) – Efavirenz, Nevirapine
Integrase inhibitors – Dolutegravir (DTG)
Faida za matibabu ya ARV
Kupunguza kiasi cha virusi (viral load)
Kuzuia uambukizaji kwa wengine
Kurejesha kinga ya mwili
Kuboresha maisha na maisha marefu
Tiba ya magonjwa nyemelezi
Wagonjwa waliochelewa kupata tiba huathirika na magonjwa kama:
Kifua kikuu
Fangasi ya mdomoni na ukeni
Saratani ya Kaposi
Matibabu hutegemea ugonjwa uliopo sambamba na dawa za ARV.
Kinga ya UKIMWI
Namna ya kuzuia maambukizi ya VVU ni kwa kutumia mbinu zifuatazo
Tumia kondomu kila tendo la ndoa
Epuka kushiriki sindano au vifaa vya kuchoma ngozi
Pima VVU mara kwa mara wewe na mwenza
Tumia dawa za kuzuia maambukizi kabla au baada ya hatari (PrEP na PEP)
Wanawake wajawazito wapate ushauri na tiba ya kuzuia maambukizi kwa mtoto
Dawa za kuzuia maambukizi
1. PrEP (Kinga kabla ya kujianika)
Dawa za kumeza kila siku kabla ya kuwa kwenye hatari
Inafaa kwa watu wasio na VVU lakini wapo kwenye mazingira ya hatari
2. PEP (Kinga baada ya kujianika)
Dawa zinazotolewa ndani ya saa 72 baada ya tukio la hatari (mfano kujamii ana bila kinga au ajali ya sindano)
Humezwa kwa siku 28 mfululizo
Hitimisho
VVU ni ugonjwa unaoweza kudhibitika iwapo utagunduliwa mapema na kuanza matibabu sahihi. Kinga ni bora kuliko tiba – fanya maamuzi sahihi ya kiafya na epuka hatari zisizo za lazima.
Maswali ya mara kwa mara kuhusu VVU/UKIMWI
Je, mtu mwenye VVU anaweza kuishi maisha marefu?
Ndiyo. Kwa kutumia ARV kikamilifu, mtu anaweza kuishi miaka mingi bila kuugua UKIMWI.
Nifanyeje kama nimejamiiana bila kondomu?
Je, punyeto husababisha VVU?
Naweza kupata VVU kwa kumbusu mtu?
Je, kuna tiba ya VVU?
Rejea za mada hii
Tanzania Ministry of Health. National Guidelines for the Management of HIV and AIDS. Dar es Salaam: Ministry of Health; 2023.
World Health Organization (WHO). Consolidated Guidelines on HIV Prevention, Testing, Treatment, Service Delivery and Monitoring. Geneva: WHO; 2023.
Centers for Disease Control and Prevention (CDC). HIV Basics [Internet]. Atlanta: CDC; Updated 2024 [cited 2025 Jul 13]. Available from: https://www.cdc.gov/hiv
UNAIDS. Global HIV & AIDS Statistics – Fact Sheet. Geneva: UNAIDS; 2024.
PEPFAR Tanzania. Country Operational Plan (COP) 2023 – Strategic Direction Summary [Internet]. Washington, DC: U.S. Department of State; 2023 [cited 2025 Jul 13]. Available from: https://www.state.gov/pepfar
National AIDS Control Programme (NACP), Tanzania. HIV/AIDS Epidemiological Factsheet – Tanzania Mainland. Dar es Salaam: NACP; 2023 [cited 2025 Jul 13]. Available from: https://www.nacp.go.tz
Medscape. HIV Infection: Practice Essentials, Background, Pathophysiology [Internet]. Updated 2024 [cited 2025 Jul 13]. Available from: https://emedicine.medscape.com/article/211873-overview
British HIV Association (BHIVA). Guidelines for the Treatment of HIV-1 Positive Adults with Antiretroviral Therapy. London: BHIVA; 2023. Available from: https://www.bhiva.org/guidelines
AVERT. Global Information and Education on HIV and AIDS [Internet]. Accessed 2024 [cited 2025 Jul 13]. Available from: https://www.avert.org
Johns Hopkins University. HIV Clinical Guidelines [Internet]. Updated 2024 [cited 2025 Jul 13]. Available from: https://www.hopkinsguides.com