top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

Imeboreshwa:

13 Desemba 2025, 14:03:28

Maumivu ya korodani kutokana na Epididimaitis

Maumivu ya korodani kutokana na Epididimaitis

Epididimaitis ni neno tiba lenye maana ya uvimbe wa mirija ya epididimis kutokana na mwitikio wa chembe hai za mwili dhidi ya maambukizi au kitu kigeni kwenye mirija hiyo. Mirija ya epididimis huwa ipo nyuma ya korodani ambayo huwa na sura ya kujizungusha kama koili. Kazi za mirija hii ni kutunza shahawa.


Ni nini husababisha Epididimaitis

Kisababishi kukuu kwa vijana wenye umwi chini ya miaka 35 huwa ni maambukizi ya magonjwa ya zinaa ambayo ni

  • Kisonono

  • Chlamydia

Hata hivyo maambukizi ya UTI (Escherichia coli) yanaweza kusambaa kutoka kwenye tezi dume kuja kwenye mirija hii na kuleta maambukizi


Visababishi vingine vya epididimaitis kwa vijana wa umri wa miaka 35 au zaidi

  • Maambukizi kutoka kwenye tezi dume

  • Mkojo kuingia kwenye mirija ya epidydimis

  • Kupata jeraha kwenye korodani

  • Maambukizi ya TB kwenye korodani

  • Maambukizi ya virusi na fangasi kwa wagonjwa wenye kinga za chini na wenye UKIMWI/Kisukari

  • Sababu zisizojulikana


Dalili za Epididimaitis


Dalili za epididimaitis huwa kati ya zifuatazo;

  • Kuvimba na kubadilika rangi kwa pumbu

  • Maumivu ya korodani zikishikwa, mara nyingi huwa upande mmoja tu na maumivu huanza taratibu

  • Maumivu wakati wa kukojoa au kupata hamu ya kukojoa ghafla

  • Kutokwa na uchafu kwenye uume

  • Maumivu ya tumbo la chini au kwenye nyonga

  • Kutokwa na damu kwenye shahawa

  • Kwa nadra sana unaweza pata homa


Kumbuka

Dalili hutegemea hatua ya ugonjwa, hivyo unaweza kuwa na dalili mbili au zaidi ili kusemekana kuwa una maambukizi haya.


Vihatarishi vya ugonjwa wa epididimaitis

Vitu au mambo yafuatayo yanakuweka kwenye hatari ya kupata maambukizi haya

  • Kuwa na wapenzi wengi

  • Kutotumia kodomu wakati wa kufanya ngono

  • Kuwa na historia ya kuumwa magonjwa ya zinaa

  • Historia ya maambukizi kwenye tezi dume(prostatitis) au UTI

  • Kufanyiwa upasuaji kwenye njia ya mkojo

  • Kuwekewa mrija wa mkojo kwenye uume

  • Kutotahiliwa

  • Kukua kwa tezi dume


Vipimo vya kutambua ugonjwa wa epididimaitis

Mara utakapofika hospitali utaulizwa maswali mbalimbali yanayolega kufahamu visababishi kama vilivyoandikwa hapo juu kisha daktari ataagiza vipimo kulingana na nini ameona ni shida. Vipimo huhusisha;

  • Kuchukuliwa ute kutoka ndani ya uume wako kwa ajili ya kipimo cha magonjwa ya zinaa

  • Kipimo cha urine culture

  • Kipimo cha damu kuangalia kama kuna shida yoyote

  • Kipimo cha mkojo kuangalia kama kuna shida yoyote kwenye mkojo

  • Kipimo cha ultrasound kuangalia hali ya mirija ya epidydimis pamoja na korodani na kutofautisha tatizo hili na magonjwa mengine kama kujisokota kwa moroja ya korodani n.k


Madhara ya ugonjwa wa epididimaitis
  • Madhara yafuatayo yanawez akutokea endapo matibabu hayajafanyika kwa wakati

  • Kujaa kwa usaha ndani ya pumbu

  • Kupata ugonjwa wa epidydimo-orchitis

  • Ugumba


Wakati gani mgonjwa wa epididimaitis amwone daktari?

Ni vema mara baada ya kuanza kuhisi maumivu ya korodani kumwona daktari wako haraka ili kufanyiwa uchunguzi na tiba kabla ya tatizo kuwa kubwa. Kumbuka korodani ni kitu cha muhimu sana.


Matibabu ya ugonjwa wa epididimaitis

Matibabu husisha;

  • Dawa

  • Upasuaji


Dawa

Dawa za kutibu magojwa ya zinaa au UTI, mpenzi wako pia atahitaji matibabu ili kuondoa kihatarishi cha kupata maambukizi kutoka kwake kwa mara nyingine. Utapswa kumaliza dozi uliyopewa hatakama zitapotea kabla ya kumaliza dozi


Endapo una maumivu, tumia dawa za kuondoa maumivu kama parasetamo.


Upasuaji

Hufanyika kwa watu wenye usaha kwenye korodani, upasuaji hufanyika kuondoa usaha kwenye korodani na kufanya zipone haraka. Baadhi ya wakati itahitajika kuondoa sehemu ya mirija ya epididimis.


Matibabu ya upasuaji wa kuondoa mrija(mirija) ya epididimis huweza hitajika fanyika kwa wagonjwa ambao wanapata maambukizi kujirudia kwenye tezi dume(prostataitis) au mrija wa urethra (urethraitis)


Namna ya kujikinga na ugonjwa wa epididimaitis

Fanya mambo yafuatayo ili kujikinga na tatizo hili;

  • Tumia kondomu unaposhiriki ngono

  • Pata matibabu sahihi ya UTI ya kujirudia na kwa wakati


Matibabu ya nyumbani ya ugonjwa wa epididimaitis

Endapo una tatizo hili fanya mambo yafuatayo kupunguza dalili

  • Pumzika kwa kulala kitandani huku korodani zikiwa juu

  • Tumia barafu kukanda eneo lenye maumivu ya korodani jinsi unavyoweza

  • Usinyanyue mizigo mizito

  • Usishiriki mapenzi mpaka upone kabisa


Maswali yanayoulizwa Mara kwa Mara Kuhusu Epididimaitis

1. Je, epididimaitis ni sawa na maambukizi ya korodani?

La, si sawa kabisa. Epididimaitis ni maambukizi ya mirija ya epididimis (iliyopo nyuma ya korodani), lakini inaweza kuambatana na maambukizi ya korodani na kuitwa epididymo-orchitis.

2. Je, epididimaitis ni ugonjwa wa zinaa?

 Si mara zote. Kwa vijana chini ya miaka 35, mara nyingi husababishwa na magonjwa ya zinaa kama kisonono au chlamydia. Lakini kwa wazee au watu waliofanyiwa upasuaji, inaweza kutokana na maambukizi ya njia ya mkojo.

3. Je, epididimaitis inaweza kuambukizwa kwa mwenza wangu?

Ikiwa imesababishwa na magonjwa ya zinaa, basi ndiyo, mwenza wako pia yuko hatarini. Wote wawili mnahitaji matibabu.

4. Je, epididimaitis inaweza kupona bila dawa?

Hapana. Inahitaji matibabu ya dawa sahihi (antibiotics). Kuchelewa kutibiwa kunaweza kusababisha madhara kama usaha au ugumba.

5. Naweza kuendelea kushiriki tendo la ndoa nikiwa na epididimaitis?

Hapana. Inashauriwa usishiriki tendo la ndoa mpaka utakapopona kabisa ili kuepuka maambukizi zaidi na kumwambukiza mwenza.

 6. Je, epididymitis inaweza kurudi tena baada ya kutibiwa?

Ndiyo, hasa kama chanzo cha maambukizi hakijatibiwa ipasavyo au kama ni matokeo ya matatizo ya muda mrefu kama prostatitis au UTI za kurudia.

7. Je, epididimaitis inaweza kuathiri uwezo wa kupata watoto?

Ndiyo. Ikiwa haitatibiwa kwa wakati, inaweza kuharibu mirija ya shahawa na kusababisha ugumba.

8. Nitatambua vipi kama nina epididymitis au ni tatizo lingine kwenye korodani?

Ni vigumu kujitambua mwenyewe. Huhitaji vipimo kama ultrasound, mkojo, na damu ili daktari atofautishe na matatizo mengine kama korodani kujisokota.

9. Je, barafu inaweza kusaidia kutuliza maumivu ya epididimaitis?

Ndiyo. Kuweka barafu kwenye eneo la maumivu kwa muda mfupi husaidia kupunguza uvimbe na maumivu.

10. Nitapona kabisa baada ya matibabu?

Kwa wagonjwa wengi, tiba ya mapema na sahihi huleta nafuu kamili bila madhara ya muda mrefu. Ni muhimu kumaliza dozi na kufuata ushauri wa daktari.

11. Je, Maumivu ya Korodani Moja Wakati wa Kutembea Sana Yanamaanisha Nini?

Ikiwa unapata maumivu ya korodani moja kila unapotembea sana, hii inaweza kuwa ishara ya shinikizo lisilo la kawaida au kuvimba kwenye mirija ya epididimis, hasa kama maumivu yanarudia au kuongezeka polepole.


Visababishi vinazowezekana ni pamoja na:
  • Epididimaitis ya hatua ya awali, ambayo bado haijatoa dalili kamili

  • Uvimbe au mkazo kwenye korodani au mirija ya shahawa kutokana na shughuli nyingi au msuguano

  • Henia (ngiri) – ambapo utumbo mdogo huingia kwenye mfuko wa korodani

  • Varikosili – mishipa ya damu kujaa kwenye korodani, huleta hisia ya uvutaji au maumivu ya kuvuta

  • Korodani kujisokota – ingawa ni ya dharura, mara nyingine huanza polepole kabla ya kuwa kali


Nini cha Kufanya?

Ikiwa una maumivu ya mara kwa mara ya korodani moja unapokuwa umesimama kwa muda mrefu au unapotembea sana, ni muhimu kufika hospitali kwa uchunguzi. Daktari anaweza kupendekeza:

  • Ultrasound ya korodani – kuangalia hali ya ndani

  • Vipimo vya mkojo na damu – kuangalia maambukizi

  • Uchunguzi wa mwili – kuchunguza uwepo wa ngiri au varikosili


Usisite kutafuta msaada wa kitaalamu mapema, hasa kama maumivu yanaendelea, yanaongezeka au yanaambatana na uvimbe au mabadiliko ya rangi ya korodani.


Rejea za mada hii:
  1. Arap MA. Varicocele and male infertility: current concepts and future perspectives. Clinics (Sao Paulo). 2022;77:100035. doi:10.1016/j.clinsp.2022.100035.

  2. Brady JD, Schaeffer AJ. Acute epididymitis and orchitis: diagnosis, management, and complications. Urol Clin North Am. 2018;45(3):485–497.

  3. CDC. Epididymitis. https://www.cdc.gov/std/tg2015/epididymitis.htm. Imechukuliwa 1.12.2020.

  4. CDC. Epididymitis tables of evidence. https://www.cdc.gov/std/tg2015/evidence-tables/epididymitistableevidence-2015.pdf. Imechukuliwa 1.12.2020.

  5. Cummings JM, Boullier JA. Differential diagnosis of scrotal pain. Emerg Med Clin North Am. 2011;29(3):469–484.

  6. Eyre RC. Evaluation of acute scrotal pain in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 1.12.2020.

  7. Eyre RC. Evaluation of nonacute scrotal conditions in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 1.12.2020.

  8. Merck Manual Professional Version. Epididymitis. https://www.merckmanuals.com/professional/genitourinary-disorders/penile-and-scrotal-disorders/epididymitis. Imechukuliwa 1.12.2020.

  9. Nickel JC. Prostatitis and related conditions, orchitis, and epididymitis. In: Litwin MS, Saigal CS, eds. Urologic Diseases in America. US Department of Health and Human Services; 2012:385–409.

  10. Patrick J. Shenot, MD, et al. Epididymitis. https://www.msdmanuals.com/professional/genitourinary-disorders/penile-and-scrotal-disorders/epididymitis. Imechukuliwa 1.12.2020.

  11. Pilatz A, Wagenlehner FME, Weidner W. Acute epididymitis in adults. Dtsch Arztebl Int. 2012;109(33–34):546–552. doi:10.3238/arztebl.2012.0546.

  12. Redmond EJ, et al. Epididymitis. In: Wein AJ, Kavoussi LR, Partin AW, Peters CA, eds. Campbell-Walsh Urology. 12th ed. Philadelphia: Elsevier; 2020:886–890.

  13. Rupp T, et al. Epididymitis. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK430814/. Imechukuliwa 1.12.2020.

  14. Trojian TH, Lishnak TS, Heiman D. Epididymitis and orchitis: an overview. Am Fam Physician. 2009;79(7):583–587.

  15. Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, et al. Sexually Transmitted Infections Treatment Guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187. doi:10.15585/mmwr.rr7004a1.


Imeandikwa:

6 Aprili 2021, 17:49:52

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

bottom of page