Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin L, MD
Jumatano, 10 Novemba 2021

Mawe kwenye figo
Mawe kwenye figo kwa jina jingine hufahamika kama calculi, ni mkusanyiko wa madini ndani ya figo yenye uhuru wa kujongea. Mawe yanayotokea ndani ya njia za mkojo hufahamika pia kama nephrolithiasis au urolithiasis.

Kuwa na mkojo wenye kiasi kikubwa cha calcium, matumizi ya dawa aina fulani na sahani za mifupa huchangia kupata mawe kwenye figo.
Dalili
Dalili na viashiria vya kuwa na mawe kwenye figo ni;
Maumivu makali ya kuchoma kama mshale maeneo ya chini ya mbavu upande wa kushoto au kulia
Maumivu yanayoanzia chini ya mbavu upande mmoja wa mwili na kuelekea chini ya tumbo na kinena
Maumivu yanayokuja na kuondoka na yenye kutofautiana ukali
Hisia za kuungua wakati wa kukojoa
Dalili zingine
Dalili zingine ni;
Kutoa mkojo wenye rangi nyekundu, pinki au kahawia
Kupata mkojo wenye mawingu au unaonuka kama umeoza
Hamu endelevu ya kenda kukojoa
Kukojoa mara kwa mara zaidi ya kawaida au kukojoa mkojo kidogo dogo
Kichefuchefu na kutapika
Homa na kutetemeka
Wakati gani wa kumwona daktari?
Onana na daktari haraka kama una dalili zifuatazo;
Maumivu makali yasiyovumilika
Maumivu yanayoambatana na kichefuchefu na kutapika
Maumivu yanayoambatana na homa na kutetemeka
Kupata mkojo wenye damu
Kushindwa kupitisha mkojo
Visababishi
Kuna sababu mbalimbali ambazo zikikutanika kwa pamoja hupelekea kufanyika kwa mawe ndani ya figo. Mawe kwenye figo hutengenezwa kama kuna mkojo kidogo wenye madini mengi yenye uwezo wa kuganda kama calcium, oxalate na uric. Mkojo mkojo kidogo hushindwa kuzimua kiasi cha madini hayo na hivyo kutengeneza mazingira mazuri ya kufanyika kwa mawe.
Viunda vya mawe kwenye figo
Asilimia 80 ya mawe ya figo hutokana na calcium ambayo hupatikana kama calcium oxalate (CaOx) na calcium phosphate (CaP).
Kiasi kilichobaki (Asilimia 20) cha mawe ya figo hutengenezwa kwa;
Uric acid
Struvite
Cysteine
Dawa mfano indinavir na atazanavir
Melamine ( kampaundi inayotumika kutengeneza vyombo vya plastiki
Vihatarishi
Historia iliyopita
Kuwa na historia ya kupata mawe kwenye figo, au historia ya ndugu wa tumbo mmoja kupata mawe kwenye figo huwa kihatarishi cha kupata mawe ya figo hapo baadae.
Kuishiwa maji
Kutokunywa maji yakutosha kila siku katika kiasi kinachoshauriwa kiafya kulingana na mwili wako hupelekea mkojo kuwa na madini mengi hivyo kuhatarisha kufanyika kwa mawe ndani ya figo. Hata hivyo watu wanaoishi kwenye mazingira ya joto na wanaotokwa na hasho kwa wingi huwa kwenye hatari ya kuishiwa maji na kutengeneza mawe kwenye figo.
Kula aina Fulani ya chakula
Aina Fulani ya chakula kama vile vyakula vyenye chumvi na sukari kwa wingi huongeza hatari ya kufanyika kwa mawe ndani ya figo. Kula kiasi kikubwa cha chumvi (sodium) huongeza kiasi cha calcium kwenye figo.
Obeziti
Kuwa na uwiano mkubwa wa uzito kwa urefu, kuongezeka mwili maeneo ya kiuno na kuongezeka uzito haraka huambatana na ongezeko la hatari ya kufanyika kwa mawe ndani ya figo.
Magonjwa kwenye mfumo wa mmengāenyo wa chakula
Magonjwa kama inflammatori bowel na tatizo sugu la kuhara huweza athiri uwezo wa utumbo kufyonza calcium na maji na hivyo kuongeza hatari ya kufanyika kwa mawe ndani ya figo.
Upasuaji
Kufanyiwa upasuaji wa kuchepuka tumbo (Gastric bypass), huathiri uwezo wa utumbo kufyonza calcium na maji na hivyo kuongeza hatari ya kufanyika kwa mawe ndani ya figo.
Hali na magonjwa mengine
Magonjwa kama renal tubular acidosis, cystinuria, hyperparathyroidism na maambukizi ya njia ya mkojo ya kujirudia rudia ( U.T.I sugu) ni kihatarishi kikubwa cha kupata mawe ndnai ya figo.
Matumizi ya dawa
Matumizi ya viinirishe na dawa aina Fulani huongeza hatari ya kupata mawe kwenye figo. Dawa hizo mfano ni;
Vidonge vya vitamin C
Dawa za kulainisha haja kubwa
Dawa za kuzuia uzalishaji tindikali zenye calcium
Dawa za VVU kama atazanavir na indinavir
Dawa za kutibu kipanda uso na sonona
Matumizi ya kemikali
Matumizi ya vyombo vilivyotengenezwa kwa kemikali kama melamine inayotumika kutengeneza vyombo vingi vya nyumbani kama vile sahani na vikombe vya mifupa, huongeza hatari ya kupata mawe kwenye figo.
Vipimo
Ili kutambua uwepo wa mawe kwenye figo, utaulizwa dalili kasha vipimo vitafuata ambavyo hutumiwa na daktari kuthibitisha kisababishi cha dalili zako. Vipimo hivyo ni;
Vipimo vya damu
Kuangalia kiasi cha calcium na uric acid kwenye damu. Kipimo hiki huweza kutumika kuangalia ufanisi wa matibabu na visababishi vingine vya mawe kwenye figo.
Kipimo cha mkojo
Mkojo wa masaa 24 utakusanywa kisha kupimwa kuangalia kiasi cha madini yanayotengeneza mawe na kiasi cha kemikali zinazozuia ufanyikaji wa mawe kwenye figo.
Vipimo vya kiradiolojia
VIpimo vya kiradiolojia huonyesha sehemu ambapo mawe yamefanyika katika njia za mkojo iwe kwenye figo, kibofu au mrija wa ureta. Vipimo hivyo ni kama X-ray ya tumbo, computerized tomography (CT). X-ray ya tumbo inaweza kutotambua mawe madogo.
Uchunguzu wa mawe
Unaweza kuombwa ukojoe kwenye chombo maalumu ili kuweka kupata mawe kwenye figo kwa ajili ya vipimo vya nini kinachosababisha. Majibu ya kipimo hiki husaidia kukupa ushauri wa nini cha kufanya ili kuepuka mawe kwenye figo.
Matibabu
Matibabu ya mawe kwenye figo yapo ya aina mbili. Matibabu yam awe madogo na matibabu ya mawe makubwa.
Matibabu ya mawe madogo kwenye figo
Mara nyingi mawe madogo kwenye figo huisha pasipo matibabu. Baadhi ya matibabu ambayo hutumika kuondoa mawe madogo kwenye figo ni pamoja na;
Kunywa maji ya kutosha. Angalau lita 2 hadi 3.6 kwa siku ili kufanya mkojo kuwa mwepesi na kuyeyusha mawe madogo. Unatakiwa kushauriwa na daktari wako kama kunywa maji kiasi hiki ni salama kwa afya yako.
Kutumia dawa za maumivu. Kwa sababu kupitisha mawe yenye umbile dogo katika njia za mkojo husababisha maumivu, daktari anaweza kukushauri utumie dawa za maumivu kama ibuprofen au naproxen husaidia kupunguza maumivu
Matibabu ya dawa. Unaweza kuandikiwa dawa za kukusaidia kupitisha kirahisi pasipo maumivu mawe madogo kwenye njia ya mkojo. Dawa hizo zipo kwenye makundi ya alpha blocker (kama tamsulosin) au dutasteride na tamsulosin.
Matibabu ya mawe makubwa ndani ya figo
Mawe makubwa ndani ya figo hayawezi kutoka yenyewe bila matibabu, na huweza kuharibu njia ya mkojo, kusababisha kutokwa na damu na maambukizi ndani ya figo ya kujirudia.
Njia za kuondoa mawe hayo ni pamoja na;
Matumizi ya mawimbi sauti kuvunja mawe
Upasuaji wa kuondoa mawe ndani ya figo
Matumizi ya kifaa chenye kamera kuondoa mawe ndani ya figo
Upasuaji wa kuondoa tezi parathyroid
Dawa za kudhibiti mawe kwenye figo
Unaweza kuandikiwa na daktari wako dawa za kuzuia au kudhibiti ufanyikaji wa mawe kwenye figo kutokana na aina ya mawe kama vile;
Mawe ya calcium. Dawa jamii ya thiazide diuretic au zenye phosphate
Mawe ya uric acid. Dawa kama allopurinol (Zyloprim, Aloprim)
Mawe ya struvite. Kunywa maji ya kutosha
Mawe ya cysteine. Kunyw amaji ya kutosha na kupunguza vyakula vyenye protini ya wanyama na chumvi kwa wingi.
Kinga
Ili kujikinga na kufanyika kwa mawe ndani ya figo unapaswa;
Kunywa maji ya kutoka kama inavyoshauriwa kwa siku
Kama unaishi maeneo yenye joto au unafanya kazi za kukutoa jasho, unapaswa kunywa maji mengi zaidi.
Kula mara chache vyakula vyenye kemikali ya oxalate kwa wingi au kuviepuka kabisa ambavyo ni rhubarb, beets, okra, spinachi, Swiss chard, viazi vitamu, karanga, majani ya chai, chocolate, pilipili manga na vyakula vyenye vinavyotokana na soya.
Kula mlo wenye chumvi na protini kiasi. Chagua protini ambayo haitokani na wanyama kama vile kunde, maharagwe n.k
Endelea kula vyakula vyenye calcium ingawa unabidi kuwa makini na vidonge vyenye madini ya calcium.