top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Benjamin L, MD

Ijumaa, 12 Novemba 2021

Mgongo wazi

Mgongo wazi

Uti wa mgongo ulio wazi au mgongo wazi kwa jina jingine hufahamika kama Spinal bifida ni hali ya mtoto kuzaliwa na uti wa mgongo ulio wazi (mishipa mkubwa wa fahamu unaotoka kwenye ubongo) kutokana na madhaifu ya kutokufunga vizuri kwa mifupa ya uti wa mgongo. Mgongo wazi (spinal bifida) hutokea kwa watoto 3 kati ya watoto 10000 wanaozaliwa.

Uti wa mgongo hutengenezwa mara tu baada ya mimba kutungwa, ikiwa kuna kasoro katika utengenezaji wa uti huu basi sehemu fulani ya uti wa mgongo itabaki bila kuzibwa.

Visababishi


Tatizo la mgongo wazi husababishwa na muunganiko wa mambo mablimbali yakiwemo ya kijeni (mfano kuwa na historia ya tatizo hili kwa ndugu wa damu moja), kilishe (kama vile kuwa upungufu wa folate wakati wa ujauzito) na sababu zingine za kimazingira.


Vihatarishi


Kuna sababu mbalimbali zinapelekea uti wa mgongo kutoziba, ambazo zinaweza zuilika, nazo ni ;


  • Upungufu wa folic acid ( vitamin B9) na vitamin B12 katika kipindi cha kwanza cha ujauzito

  • Matumizi ya dawa za kifafa katika kipindi cha ujauzito kama vile valproic acid

  • Mama mjamzito kupiga X-ray

  • Maambukizi ya baadhi ya virusi wakati wa ujauzito

  • Kisukari

  • Obeziti

  • Ongezeko la joto mwilini

​​

Aina

Zipo aina mbiliza tatizo la tundu katika mgongo ama mgongo wazi ambazo ni;

​

Aina ya kwanza ni occulta ambapo huwa na aina mbili pia, aina ya kwanza ni ile ambapo panakuwa na vinyweleo tu vinavyoonekana nyuma chini ya mgongo bila kuwa na dalili zozote zile, ama kunaweza kujitokeza kwa kuta zinazofunika mishipa ya fahamu tu.

Aina ya pili ni sistica ambapo panakuwa na mwonekano wa uvimbe mithiri ya kifuko ambacho ndani yake huwa na mishipa ya fahamu. Aina hii ni mbaya zaidi kwani inaweza kusababisha mtoto asitembee ama asiweze zuia haja kubwa na ndogo.

Dalili


Dalili huwa kama zifuatazo

​

  • Kuwa na uvimbe unaochomoza mgongoni katika mifupa ya uti wa mgongo

  • Kuwa na vinyweleo sehemu za chini ya mgongo bila kuwa na tatizo kweny mfumo wa fahamu

  • Kushindwa kutembea ama kukosa hisia katika miguu

  • Kushindwa zuzuia haja kubwa ama ndogo kama mishipa yote ya fahamu imeathiriwa

  • Na dalili zingine zinazoambatana kuharibika kwa mishipa ya fahamu

​

Matibabu

​

Upasuaji

Upasuaji ni tiba pekee ya uti wa mgongo ulio wazi(spinal bifida) inayofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa mishipa ya fahamu(neurosurgeons) wanachofanya ni kuziba lile tundu lililowazi.

Dawa na viinirishe

  • Wanawake wengi walio katika kipindi cha kuzaa na wajawazito hawatumii vyakula vyenye vitamin B na folic acid inavyopaswa, vyakula hivyo ni matunda,mboga za majani, mbaazi na choroko.

  • Mwanamke mjamzito akipata lishe yenye virutubisho hivyo pamoja na kunywa vidonge vya folic acid, kwa asilimia 30% inaweza kupunguza hatarishi ya kupata watoto wenye uti wa mgongo ulio wazi.

  • Pia kwa wanawake wajawazito katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo, wanashauriwa kutokupiga X-ray.Inawezekana mwanamke akawa hatambui kama ni mjamzito,kipimo cha mkojo cha ujauzito(UPT-urinary pregnancy test) kifanyike kwa haraka kama mwanamke haelewi vizuri mzunguko wake wa hedhi kabla hajapiga X-ray ikiwa ana tatizo lingine la kiafya,

  • Mwanamke mwenye kifafa akiwa mjamzoto pia yupo kwenye matibabu, awahi haraka kwa daktari kushauriana ni nini zaidi cha kufanya ili kumsaidia.

  • Wanawake wajawazito wanashauriwa kuhudhulia kliniki mapema zaidi ili wapate elimu ya lishe na kuweza kuanza mapema kutumia folic acid kama kinga ya Mgongo wazi.

​

Madhara ya mgongo wazi


Madhara ya mgongo wazi hutegemea ukubwa wa tatizo, inaweza kuleta udhaifu mdogo au mkubwa. Baadhi ya madhara ni;


Kushindwa jongea

Kutokana na kudhurika kwa mishipa ya fahamu chini ya tundu, kama mishipa ya fahamu inayohusika na kutembea imeathirika, mtoto hataweza kutembea kirahisi. Ugonjwa unaweza kuathiri sehemu moja ya mwili pia na hivyo kuleta udhaifu wa upande mmoja.


Madhara ya mifupa na misuli

Watoto wenye mgongo wazi wa myelomeningocele huwa na matatizo mbalimbali miguuni na kwenye mifupa ya uti wa mgongo kutokana na kuwana misuli dhaifu. Aina ya tatizo linalotokea hutegemea tundu la mgongo wazi lilipo, mfano kuwa na kibiyongo, kukua vibaya, kunyofoka kwa fupa paja, magonjwa ya mifupa na maungio yake na kukakamaa kwa misuli.


Kushindwa kudhibiti haja kubwa na ndogo

Mishipa ya fahamu inayolisha kibofu cha mkojo na matumbo mara nyingi hushindwa fanya kazi vema kama mtoto ana mgongo wazi aina ya myelomeningocele, hii ni kwa sababu mishipa hiyo huathirika.


Kichwa maji

Ni tatizo linalotokea kama maji yatakusanyika kwenye ubongo na kusababisha ongezeko la shinikizo ndani ya ubongo. Watoto waliozaliwa na mgongo wazi wa myelomeningocele mara nyingi hupatwa na tatizo hili pia.


Kushindwa fanya kazi njia mbadala za kutoa maji kichwani


Njia mbadala za kutoa maji kichwani zilizotengenezwa ili kukabiliana na tatizo la kichwa maji huweza kukosa ufanisi mzuri kutokana na tatizo la mgongo wazi.


Uharibifu wa Chiari aina ya II.


Uharibifu wa chiari aina ya II ni tatizo la ubongo linalotokea sana kwa watoto wenye mgongo wazi aina ya myelomeningocele. Watoto hawa huwa na shina lefu la ubongo linaloketi chini zaidi ya kawaida na hivyo kupelekea urahisi wa kugandamizwa na kuleta matatizo ya kushindwa kupumua na kumeza.


Maambukizi kwenye kuta inayofunika ubongo

Maambukizi haya hufahamika pia kama homa ya uti wa mgongo. Maambukizi hutokea kirahisi kutokana na kuwa wazi. Maambukizi haya huwa makali na yanatishia maisha ya mtoto.


Kujishikiza kwa mishipa ay fahamu kwenye makovu ya uti wa mgongo

Hutokea kwa watoto waliofanyiwa upasuaji wa kurekebisha mgongo wazi haswa wale wanaokuwa. Mishipa ikijishikiza kwneye makovu ya upasuaji huweza pelekea mtoto kushindwa kuwa vema na kupoteza misuli pamoja na uwezo wa kufanya kazi kwa kibofu cha mkojo.


Madhaifuya kushindwa kulala

Watoto na watu wazima wenye mgongo wazi haswa ule wa myelomeningocele, huweza kupata vipindi vya kusimama kwa upumuaji wakati wamelala au matatizo mengine ya kulala.


Vidonda

Watoto wenye mgongo wazi wanaweza kupata vidonda mara kwa mara kutokana na kutokuwa na hisia maeneo ya kanyagio, miguu, mapaja na matakoni.


Mzio kwenye latex

Watoto wenye mgongo wazi huwa na mzio kwenye kampaundi za latex. Huweza pia kupata mzio mkali wa latex au anafailaksia inayoweza pelekea kupoteza maisha. Inashauriwa usitumie glavu na vitu vingine vilivyotengenezwa kwa latex ili kuepuka kuwasababishia mzio.


Madhaifu mengine

Madhaifu mengine ya mgongo wazi ni pamoja na maambukizi ya kujirudia ya njia mfumo wa mkojo, madhaifu ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na sonona.


Kinga


Ili kujikinga kupata mtoto mwenye tatizo la mgongo wazi ni vema;


Kutumia folic acid. Mama akitumia vidonge vya folic acid kabla ya kupata ujauzito na kipindi chote cha ujuzito haswa kipindi cha kwanza cha ujauzito ambapo uumbaji wa mtotona mfumo wa fahamu hufanyika.


Kupata ujauzito uliopangwa. Hii itazuia kupata mtoto wa mgongo wazi kutokana na upungufu wa folic acid. Ukipanga kupata ujauzito unapaswa kutumia folic acid angalau wiki 4 hadi 8 kabla ya kuwa mjamzito na kipindi choche cha ujauzito.


Kumbuka kwamba

​

Jamii inapaswa kujua kuwa Mgongo wazi haitokani na mambo ya kishirikina bali ni hali ambayo inaweza kuzuilika. Mzazi yeyote mwenye mtoto mwenye Mgongo wazi anashauriwa ampeleke mtoto wake hospitali ili apate maelekezo ni wapi mtoto anaweza kupata matibabu ya upasuaji.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

12 Novemba 2021, 13:40:29

Rejea za mada hii:

1. Bowman RM. Overview of the management of myelomeningocele (spina bifida). https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa12.11.2021

2. Bowman RM. Pathophysiology and clinical manifestations of myelomeningocele (spina bifida). https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa12.11.2021

3. Dietary supplement fact sheet: Folate. Office of Dietary Supplements. https://ods.od.nih.gov/factsheets/folate-HealthProfessional/. Imechukuliwa12.11.2021
4. Dukhovny S, et al. Open neural tube defects: Risk factors, prenatal screening and diagnosis, and pregnancy management. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa12.11.2021

5. Ferri FF. Spina bifida. In: Ferri's Clinical Advisor 2020. Elsevier; 2020. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa12.11.2021

6. Goetzl LM. Folic acid supplementation in pregnancy. https://www.uptodate.com/contents/search Imechukuliwa12.11.2021

7. MAFP1 alpha-fetoprotein (AFP), single marker screen, maternal, serum. Mayo Medical Laboratories. https://www.mayocliniclabs.com/test-catalog/Overview/113382. Imechukuliwa12.11.2021

8. Moise KJ Jr., et al. Current selection criteria and perioperative therapy used for fetal myelomeningocele surgery. Obstetrics and Gynecology. 2016; doi:10.1097/AOG.0000000000001296.

9. Patel DM, et al. Sleep-disordered breathing in patients with myelomeningocele. Journal of Neurosurgery: Pediatrics. 2015; doi:10.3171/2014.11.PEDS14314.

10. Rei J, et al. Endoscopic third ventriculostomy for the treatment of hydrocephalus in a pediatric population with myelomeningocele. World Neurosurgery. 2017; doi:10.1016/j.wneu.2017.05.107.

11. Routh JC, et al. Design and methodological considerations of the Centers for Disease Control and Prevention urologic and renal protocol for the newborn and young child with spina bifida. Journal of Urology. 2016; doi:10.1016/j.juro.2016.07.081.

12. Shepard CL, et al. Pregnancy among mothers with spina bifida. Journal of Pediatric Urology. 2018; doi:10.1016/j.jpurol.2017.08.001.

13. Spina bifida fact sheet. National Institute of Neurological Disorders and Stroke. https://www.ninds.nih.gov/Disorders/Patient-Caregiver-Education/Fact-Sheets/Spina-Bifida-Fact-Sheet. Imechukuliwa12.11.2021

14. Swaroop VT, et al. Orthopedic issues in myelomeningocele (spina bifida). https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa12.11.2021

15. What is spina bifida? Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/ncbddd/spinabifida/facts.html. Imechukuliwa12.11.2021

bottom of page