top of page

Mwandishi:

Mhhariri

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

ULY CLINIC

2 Septemba 2026, 18:12:16

Siriangoma

Siriangoma

Siriangoma ni nini?

Siringoma( kwa kizungu syriangoma) ni uvimbe mdogo unaotokea kutokana na kuongezeka kwa seli zinazohusiana na sehemu ya kutoa jasho ya tezi za eccrine. Uvimbe huu huwa wa usio saratani, maana yake si saratani na kwa kawaida hauenei kwenda sehemu nyingine za mwili.


Kwa kawaida siriangoma huwa na ukubwa mdogo, mara nyingi takribani milimita 1–3, na huonekana kama vijivimbe vilivyojitokeza kidogo juu ya ngozi.


Mara nyingi huonekana kwa makundi badala ya kuwa uvimbe mmoja mkubwa.


Siriangoma huonekana wapi?

Sehemu inayojulikana zaidi ni usoni, hasa:

  • Kwenye kope za chini

  • Chini ya macho

  • Pembeni mwa macho

  • Kwenye sehemu ya juu ya mashavu

  • Karibu na pua

  • Wakati mwingine kwenye paji la uso


Ingawa usoni ndipo huonekana zaidi, siriangoma inaweza pia kutokea kwenye sehemu nyingine za mwili, ikiwemo shingo, kifua au sehemu za siri.


Siriangoma inaonekanaje?

Siriangoma mara nyingi huonekana kama:

  • Vijivimbe vidogo sana vilivyoinuka juu ya ngozi

  • Rangi ya ngozi au nyeupe kidogo

  • Rangi ya njano-kahawia kwa baadhi ya watu

  • Vilivyo na umbo la mviringo au lenye kubapa kidogo

  • Vilivyokusanyika katika eneo moja

  • Vinavyokuwa na ukubwa unaofanana


Mara nyingi haviumi wala kuwasha. Kwa sababu vinaweza kufanana na matatizo mengine ya ngozi, kuangalia picha pekee si mara zote kunatosha kuthibitisha kuwa uvimbe ni siriangoma.


Je, siriangoma ni saratani?

Kwa kawaida, hapana. Siriangoma ni uvimbe usio wa saratani. Haimaanishi kwamba mtu ana saratani ya ngozi na kwa kawaida haihusiani na kuenea kwa seli za saratani kwenye mwili.


Hata hivyo, si kila kijivimbe kinachoonekana karibu na macho ni siriangoma. Kuna magonjwa mengine ya ngozi ambayo yanaweza kufanana nayo. Ndiyo maana uvimbe mpya, unaobadilika au usio na uhakika unapaswa kutathminiwa na mtaalamu.


Siriangoma husababishwa na nini?

Chanzo kamili cha siringoma hakijulikani. Inaaminika kuwa inahusiana na kuongezeka kwa seli kutoka kwenye sehemu za tezi za jasho za eccrine. Hii si sawa na kusema kwamba mtu amekuwa akitokwa na jasho nyingi au kwamba uchafu wa jasho umejikusanya chini ya ngozi.


Mambo ya kijenetiki yanaweza kuwa na mchango katika baadhi ya watu, hasa pale siriangoma inapojitokeza kwa watu kadhaa katika familia.


Siriangoma pia inaweza kuonekana katika mazingira mbalimbali ya kitabibu, lakini uwepo wake pekee hauwezi kutumiwa kusema kwamba mtu ana ugonjwa mwingine fulani.


Je, siriangoma inatokana na uchafu wa ngozi?

Siriangoma si uchafu unaojikusanya kwenye ngozi na haiwezi kuondolewa kwa kuosha uso mara nyingi au kutumia sabuni kali.


Kwa sababu hii, kusugua ngozi kwa nguvu, kutumia kemikali kali au kukamua vijivimbe hakusaidii kuviondoa na kunaweza kusababisha muwasho, majeraha, maambukizi au makovu.


Usafi wa ngozi ni muhimu kwa afya ya ngozi, lakini hauwezi kuzuia au kuondoa siriangoma iliyokwisha kutokea.


Je, siriangoma huambukiza?

Hapana. Sariangoma si maambukizi. Huwezi kupata siriangoma kwa kumgusa mtu mwenye siriangoma, kushirikiana naye taulo au kutumia vifaa sawa vya kawaida.


Kwa hiyo, mtu mwenye siriangoma hahitaji kutengwa na watu wengine na si ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya ngozi kwa ngozi.


Ni watu gani hupata siriangoma?

Siriangoma inaweza kumpata mtu yeyote, lakini huonekana zaidi kwa wanawake kuliko wanaume na mara nyingi huanza kuonekana wakati wa ujana au utu uzima.


Kwa baadhi ya watu, vijivimbe vinaweza kuongezeka polepole kwa miaka mingi. Kuna pia aina ya siriangomainayotokea kwa watu wengi wa familia moja, jambo linaloashiria kwamba sababu za kijenetiki zinaweza kuwa na mchango katika baadhi ya visa.


Je, siriangoma ina uhusiano na kisukari?

Kuna hali inayojulikana kama vipele mlipuko vya siriangoma mchanganyiko, ambayo inaweza kuonekana kwa watu wenye magonjwa fulani au katika mazingira maalumu ya mwili, lakini uwepo wa siriangoma usoni hauwezi kutumiwa peke yake kugundua kisukari.


Kwa hiyo, si sahihi kumwambia mtu mwenye siriangoma kwamba lazima ana kisukari. Ikiwa mtu ana dalili au sababu nyingine za hatari za kisukari, anaweza kufanyiwa vipimo vya sukari kwa sababu hizo, lakini si kwa sababu ya siriangoma pekee.


Siriangoma inaweza kuongezeka?

Ndiyo. Kwa baadhi ya watu, siriangomainaweza kuongezeka taratibu kwa muda. Mtu anaweza kuanza akiwa na vijivimbe vichache, kisha vingine vikaonekana katika eneo hilo hilo.


Hata hivyo, ukuaji wa siriangoma kwa kawaida huwa wa taratibu. Kijivimbe kinachokua kwa kasi, kutokwa damu, kuwa na kidonda, kubadilika rangi sana au kuwa na maumivu kinapaswa kuchunguzwa kwa sababu kinaweza kuwa tatizo jingine la ngozi.


Utambuzi wa siriangoma

Mara nyingi daktari wa ngozi anaweza kushuku siriangoma kwa kuangalia muonekano wa vijivimbe na eneo vilipo.


Dematoskopi

Daktari anaweza kutumia kifaa cha kukuza ngozi kinachoitwa dematoskopu ili kuangalia maumbo na alama za uvimbe kwa undani zaidi.


Biopsi

Ikiwa kuna mashaka kuhusu utambuzi, daktari anaweza kuchukua kipande kidogo cha ngozi (biopsi ya ngozi) na kupeleka maabara kwa uchunguzi wa histopatholojia.


Biopsy inaweza kusaidia kutofautisha siriangoma na uvimbe au magonjwa mengine ya ngozi yanayofanana kwa muonekano.


Magonjwa yanayoweza kufanana na siriangoma

Vijivimbe vidogo usoni vinaweza kusababishwa na hali mbalimbali. Baadhi yake ni:

  • Milia

  • Xanthelasma

  • Haipaplezia ya tezi sebashazi

  • Sunzua tambalale

  • Fibrofolikuloma

  • Trikoepithelioma

  • Vipele vya chunusi

  • Baadhi ya uvimbe wa ngozi

Kwa hiyo, si kila kijivimbe kidogo karibu na macho ni siriangoma.


Je, siriaingoma inahitaji matibabu?

Kwa kawaida, siriangoma haihitaji matibabu kwa sababu za kiafya ikiwa haina dalili na utambuzi umehakikishwa.


Matibabu hufanywa zaidi kwa sababu ya muonekano, hasa ikiwa vijivimbe viko usoni na vinamsumbua mtu.

Ni muhimu kuelewa kwamba matibabu hayalengi "kuponya" ugonjwa hatari, bali kuondoa au kupunguza mwonekano wa vijivimbe.

Matibabu ya siriangoma

Hakuna njia moja inayofaa kila mtu. Uchaguzi hutegemea idadi ya vijivimbe, ukubwa wake, eneo, aina ya ngozi na uwezekano wa kupata kovu au kubadilika kwa rangi ya ngozi.

Matibabu yanayoweza kutumika ni pamoja na:

  • Leza

  • Kukaza kwa kisu cha umeme

  • Kuvikata

  • Kuvikata kwa kugandisha katika baadhi ya mazingira

  • Kuvikata kwa kisu cha upasuaji kwa vijivimbe vilivyochaguliwa

  • Baadhi ya kemikali zinazotumiwa na daktari wa ngozi

  • Mbinu nyingine za matibabu ya ngozi kulingana na hali ya mgonjwa.


Matibabu kwa leza

Laser inaweza kutumika kuharibu au kupunguza vijivimbe vya siriagoma. Aina ya laser huchaguliwa kulingana na ngozi na eneo linalotibiwa. Kwa kuwa siriangoma mara nyingi hutokea karibu na macho, matibabu yanahitaji kufanywa na mtaalamu mwenye uzoefu ili kupunguza hatari ya kuumia ngozi au macho. Kwa baadhi ya watu, matibabu zaidi ya kikao kimoja yanaweza kuhitajika.


Upasuaji wa kisu cha umeme

Katika njia hii, nishati ya umeme hutumika kuharibu tishu ya siriangoma. Inaweza kuwa na ufanisi kwa vijivimbe vidogo, lakini inaweza kusababisha mabadiliko ya rangi ya ngozi au kovu, hasa kwa watu wenye ngozi yenye rangi nyeusi.


Kwa hiyo, daktari anapaswa kuzingatia aina ya ngozi ya mgonjwa kabla ya kuchagua njia hii.


Kuondoa kwa kukuna

Kukuna ni kuondoa tishu ya uvimbe kwa kutumia kifaa maalumu. Inaweza kutumika kwa baadhi ya siriangoma, lakini kwa sababu uvimbe unaweza kuwa na sehemu inayopenya ndani ya ngozi, kuondoa sehemu ya juu pekee kunaweza kuongeza uwezekano wa kurudi tena.


Kungadisha

Kugandisha hutumia baridi kali kuharibu tishu. Inaweza kutumika katika baadhi ya visa, lakini eneo la uso—hasa karibu na macho linahitaji tahadhari kubwa. Kwa watu wenye ngozi yenye rangi nyeusi, mabadiliko ya rangi ya ngozi yanaweza kuwa jambo muhimu la kuzingatia.


Je, siriangoma inaweza kuondolewa kabisa?

Inaweza kuondolewa au kupunguzwa kwa kiwango kikubwa kwa baadhi ya watu, lakini hakuna uhakika kwamba haitarudi au kwamba haitatokea mingine.


Siriangoma nyingi huwa na mizizi au sehemu za tishu ndani ya ngozi, hivyo kuondoa sehemu ya juu pekee kunaweza kusababisha uvimbe kuonekana tena.


Pia, mtu ambaye ana tabia ya kutengeneza siriangoma anaweza kupata vijivimbe vipya hata baada ya vile vya awali kutibiwa.


Je, krimu zinaweza kuondoa siriangoma?

Krimu za kawaida za uso kwa ujumla haziondoi siriangoma. Baadhi ya dawa za kupaka au kemikali zinaweza kutumika na wataalamu katika mazingira maalumu, lakini hazipaswi kutumiwa kiholela, hasa karibu na macho.

Bidhaa zinazodai "kuyeyusha siriangoma" bila usimamizi wa mtaalamu zinaweza kusababisha kuungua kwa ngozi, makovu na kubadilika kwa rangi ya ngozi.


Je, ni salama kukamua siriangoma?

Hapana, haishauriwi. Siriangomasi chunusi iliyojaa usaha ambayo inaweza kukamuliwa. Kukamua au kuchoma kwa sindano kunaweza kuharibu ngozi bila kuondoa tishu zote za uvimbe.


Matokeo yake yanaweza kuwa maambukizi, kutokwa damu, kovu au mabadiliko ya rangi ya ngozi.

Ikiwa mtu anataka kuiondoa kwa sababu ya muonekano, ni salama zaidi kumuona daktari wa ngozi kwa tathmini na kuchagua njia inayofaa.


Siriangoma na ngozi nyeusi

Kwa mtu mwenye ngozi yenye rangi nyeusi, uchaguzi wa matibabu unahitaji uangalifu zaidi kwa sababu baadhi ya matibabu yanaweza kusababisha madoa baada ya michomo kinga, yaani ngozi kuwa nyeusi zaidi baada ya kuumia au kuvimba.


Kwa hiyo, si kila laser au njia ya kuchoma ni sawa kwa kila aina ya ngozi. Daktari wa ngozi anapaswa kutathmini rangi ya ngozi, eneo la siriangoma na uwezekano wa kupata kovu au mabadiliko ya rangi kabla ya kuanza matibabu.


Siriangoma inaweza kuzuilika?

Kwa sasa hakuna njia iliyothibitishwa ya kuzuia siriangoma kwa mtu ambaye ana mwelekeo wa kuipata.

Kwa kuwa chanzo chake hakijulikani kikamilifu na kinaweza kuhusisha mambo ya kijenetiki na maendeleo ya tezi za jasho, kuosha uso mara nyingi au kubadilisha chakula hakuwezi kuzuia kwa uhakika.

Jambo muhimu ni kuepuka kujichoma, kukamua au kutumia kemikali kali kwenye vijivimbe.


Wakati gani kumuona daktari?

Muone daktari wa ngozi ikiwa:

  • Vijivimbe vipya vinaanza kuonekana kwa wingi

  • Huna uhakika kama ni siriangoma

  • Kijivimbe kinakua haraka

  • Kinabadilika rangi au umbo

  • Kinatoa damu

  • Kinauma au kuwasha sana

  • Kinatoa usaha au kuwa kidonda

  • Viko karibu sana na macho na unataka kuviondoa

  • Unataka matibabu kwa sababu ya muonekano

Kijivimbe kinachobadilika haraka au kuwa na dalili zisizo za kawaida hakipaswi kudhaniwa kuwa siriangoma bila uchunguzi.


Hitimisho

Siriangoma ni vijivimbe vidogo visivyo vya saratani vinavyotokana na miundo ya tezi za jasho na mara nyingi huonekana karibu na macho, hasa kwenye kope na chini ya macho. Si ugonjwa wa kuambukiza, si uchafu wa ngozi na kwa kawaida si hatari kwa afya.


Kwa mtu anayesumbuliwa na muonekano wake, matibabu kama laser, ukataji kwa kisu cha umeme au njia nyingine za matibau ya ngozi yanaweza kusaidia, lakini uchaguzi wa matibabu unapaswa kufanywa na daktari wa ngozi kwa kuzingatia aina ya ngozi na hatari ya kovu au kubadilika kwa rangi.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu siriangoma

1. Je, siriangoma inaweza kugeuka kuwa saratani?

Kwa kawaida siriangoma ni uvimbe usio wa saratani na haugeuki kuwa saratani. Hii ni tofauti na baadhi ya uvimbe wa ngozi ambao unaweza kuwa na uwezo wa kuongezeka kwa ukali au kuenea.


Hata hivyo, mtu anaweza kuwa na uvimbe mwingine wa ngozi unaofanana na siriangoma. Kwa hiyo, ikiwa uvimbe unaonekana tofauti na vijivimbe vya kawaida vya siriangoma, ni muhimu kupata uchunguzi.


Kijivimbe kinachokua haraka, kutokwa damu au kuwa kidonda hakipaswi kupuuzwa kwa sababu dalili hizo zinaweza kuonekana katika magonjwa mengine ya ngozi.

2. Je, siriangoma inaweza kuondoka yenyewe?

Kwa kawaida siriangoma hudumu kwa muda mrefu na haiwezi kutegemewa kuondoka yenyewe. Baadhi ya vijivimbe vinaweza kubadilika kwa ukubwa au kuonekana zaidi kadiri muda unavyopita.


Hii ndiyo sababu mtu anaweza kuwa navyo kwa miaka mingi bila kupata tatizo lolote la kiafya.


Ikiwa havimsumbui mtu, mara nyingi hakuna ulazima wa kuviondoa. Matibabu huzingatiwa zaidi pale vinaposababisha usumbufu wa kimuonekano au, mara chache, dalili nyingine.

3. Je, siriangoma inahusiana na homoni?

Siriangoma inaweza kuonekana zaidi wakati wa ujana na imejadiliwa kuwa na uhusiano na mabadiliko ya homoni katika baadhi ya watu, lakini ushahidi hauonyeshi kwamba homoni fulani ndiyo chanzo cha moja kwa moja cha kila siriangoma.


Kwa hiyo, si sahihi kusema kwamba mtu mwenye siriangoma lazima ana tatizo la homoni.


Ikiwa kuna dalili nyingine zinazoashiria tatizo la homoni, daktari anaweza kufanya uchunguzi unaofaa, lakini siriangoma pekee haitoshi kuanzisha utambuzi wa ugonjwa wa homoni.

4. Je, siriangoma inaweza kuondolewa nyumbani?

Haishauriwi kujaribu kuiondoa nyumbani. Siriangoma iko ndani ya ngozi na si kama chunusi ambayo inaweza kutolewa kwa kukamuliwa.


Kuchoma, kukata au kutumia asidi kali kunaweza kuharibu ngozi inayozunguka na kusababisha kovu au mabadiliko ya rangi.


Hii ni muhimu zaidi kwa siriangoma iliyo karibu na macho, ambako majeraha ya kujitibu yanaweza kuwa hatari zaidi.

5. Je, dawa za asili zinaweza kuondoa siriangoma?

Hakuna ushahidi wa kutosha wa kisayansi unaothibitisha kwamba dawa za asili zinazopakwa nyumbani zinaweza kuondoa siriangoma kwa usalama na kwa kudumu.


Baadhi ya vitu kama limau, siki, vitunguu au kemikali nyingine kali vinaweza kuunguza ngozi badala ya kuondoa uvimbe.


Kwa kuwa siriangoma hutokana na tishu zilizo ndani ya ngozi, kutumia kitu kinachochoma juu ya ngozi kunaweza kusababisha madhara bila kuondoa chanzo cha uvimbe.

6. Je, siriangoma inaweza kusababisha upofu ikiwa iko karibu na macho?

Siriangoma yenyewe kwa kawaida haisababishi upofu kwa sababu ni uvimbe wa ngozi. Tatizo kubwa zaidi linaweza kutokea wakati mtu anajaribu kujitibu kwa kemikali, sindano, kuchoma au kukata eneo lililo karibu na jicho.


Matibabu ya siriangoma karibu na macho yanahitaji mtaalamu mwenye uzoefu na ulinzi unaofaa wa macho.


Kwa hiyo, ikiwa vijivimbe viko kwenye kope au karibu sana na jicho, usitumie kemikali au bidhaa za kuondoa uvimbe bila ushauri wa daktari.

7. Je, siriangoma inaweza kusababisha kuwasha?

Siriangoma nyingi hazisababishi dalili yoyote na mara nyingi tatizo kubwa huwa ni muonekano wake.


Hata hivyo, baadhi ya watu wanaweza kupata kuwasha au usumbufu, hasa katika aina fulani za siriangoma au wakati eneo la ngozi linapokuwa limewashwa.


Ikiwa kuwasha ni kikubwa, kuna wekundu, maumivu, usaha au mabadiliko mengine, ni muhimu kuchunguza kama kuna tatizo jingine la ngozi badala ya kudhani kuwa siriangomandiyo sababu.

8. Je, siriangoma inaweza kuenea kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine?

Hapana. Siriangoma si ugonjwa wa kuambukiza. Mtu hawezi kupata siriangoma kwa kumgusa mtu mwenye vijivimbe hivi, kushirikiana naye taulo au kuwa na mawasiliano ya kawaida ya ngozi.


Kwa hiyo, hakuna sababu ya kumtenga mtu mwenye siriangoma au kumzuia kushirikiana na wengine.

9. Je, siriangoma inaweza kurudi baada ya kuondolewa?

Ndiyo, inaweza kurudi katika eneo lililotibiwa au vijivimbe vipya vinaweza kutokea.


Sababu ni kwamba baadhi ya matibabu yanaweza kuondoa sehemu ya uvimbe bila kuondoa kila sehemu ya tishu inayohusika. Pia, mtu mwenye mwelekeo wa kupata siriangoma anaweza kutengeneza vijivimbe vipya baadaye.


Kwa hiyo, daktari anapopendekeza matibabu anapaswa kueleza kwamba lengo ni kupunguza au kuondoa vijivimbe vilivyopo, lakini hakuna uhakika wa kuzuia vijivimbe vipya milele.

10. Ni daktari gani anayepaswa kutibu siriangoma?

Daktari bingwa wa ngozi ndiye anayefaa zaidi kutathmini siriangoma na kuamua kama inahitaji matibabu.


Daktari wa ngozi anaweza kutofautisha siriangoma na magonjwa mengine ya ngozi na, ikiwa kuna mashaka, kufanya au kuagiza bayopsi.


Ikiwa matibabu yanahitajika, daktari wa ngozi anaweza kuchagua njia kama laser,ukataji w akisu cha umem au mbinu nyingine kulingana na eneo, ukubwa wa vijivimbe na aina ya ngozi ya mgonjwa.


Imeandikwa:

2 Septemba 2026, 17:43:53

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Rejea za mada hii:

  1. DermNet NZ. Syringoma [Internet]. Hamilton: DermNet NZ; [cited 2026 Sep 2]. DermNet NZ – Syringoma

  2. Pizzichetta MA, Talamini R, Stanganelli I, Puddu P, Gentile G, Soyer HP. Dermoscopic features of syringoma. Arch Dermatol. 2005;141(8):1033-5. PubMed – Dermoscopic features of syringoma

  3. Elder DE, Massi D, Scolyer RA, Willemze R, editors. WHO classification of skin tumours. 4th ed. Lyon: International Agency for Research on Cancer; 2018. WHO/IARC – WHO Classification of Skin Tumours

  4. Van der Putte SCJ. The embryologic development of the sweat glands and the pathogenesis of syringoma. J Cutan Pathol. 1992;19(3):201-6.

  5. Ghanadan A, Kamyab-Hesari K, Hashemi M, Daneshpazhooh M. Multiple syringomas in a patient with diabetes mellitus. Dermatol Online J. 2011;17(8):7.

  6. Soler-Carrillo J, Estrach T, García M. Eruptive syringoma: 27 cases and review of the literature. Dermatology. 2001;203(1):63-5.

  7. Tay YK, Goh CL. Eruptive syringoma in a patient with Down syndrome. Clin Exp Dermatol. 2001;26(3):282-4.

bottom of page