Mwandishi:
Mhhariri
Dkt. Benjamin L, MD
Dkt. Salome A, MD
Jumamosi, 29 Januari 2022

Ugumba
Ugumba ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa uzazi wa mwanaume na mwanamke, unaelezewa kuwa ni kukosa uwezo wa kutungisha au kushika mimba licha ya kujamiana pasipo kutumia kinga au njia za uzazi wa mpango angalau kwa mwaka mmoja kwa watu walio chini ya miaka 35 na miezi sita kwa walio zaidi ya umri huu. Kwa Afrika, matatizo ya ugumba usio wa kuzaliwa husababishwa sana na magonjwa ya mfumo wa uzazi wa mwanamke kama vile PID, matatizo ya mirija ya uzazi, na utoaji mimba. Sababu kuu za ugumba kwa wanaume ni pamoja na kuzalisha manii kidogo, kutozalisha manii kabisa na ngiri maji, hata hivyo baadhi ya wakati sababu huwa hazifahmiki.
Kuna matibabu aina mbalimbali yaliyo salama na fanisi kwa ajili ya kukabilia na utasa-ugumba. Matibabu hayo kwa kiasi kikubwa huboresha ama kurudisha uwezo wa kupata mimba.
Wapenzi wengi walio wagumba, hupata mimba ndani ya miezi sita ya kwanza baada ya kupata ushauri kutoka kwa daktari. Kwa ujumla, baada ya miezi 12 ya kujamiana mara kwa mara bila kinga, asilimia 90 yawanandoa hupata mimba. Wengi wa wanandoa wenye ugumba huweza kupata mimba bila matibabu yoyote
Ukubwa wa tatizo
Kutopata mimba imekuwa tatizo kubwa linaloathiri mamilioni ya watu duniani walio kwenye umri wa kuzaa. Taarifa za WHO zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 186 wasio kwenye ndoa na milioni 48 walio kwenye ndoa wanaishi na ugumba.
Kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, ukubwa halisi wa tatizo haufahamiki kutokana na kukosekana kwa tafiti za kuaminika.
Dalili za Ugumba
Mara nyingi hakuna dalili za wazi au kuonekana zinazoashiria mtu kuwa ugumba.Ishara kuu ya ugumba ni kukosa uwezo wa kutungusha mimba.
Dalili za uumba kwa wanawake
Baadhi ya dalili za ugumba kwa wanawake ni;
Kuwa na hedhi ya kawaida au kutokwenda hedhi kabisa
Kutokwa na damu kidogo au nyingi kuliko kawaida wakati wa hedhi
Kubadilika kwa mzunguko wa hedhi
Maumivu makali ya hedhi
Mabadiliko ya ngozi kama vile kupata chunusi
Kupungua kwa hamu na hamasa ya kufanya ngono
Kuota ndevu
Kupoteza nywele (upara)
Kuongezeka uzito
Maumivu makali wakati wa kujamiana
Maumivu sugu ya tumbo la chini ya kitovu
Muwasho na kuvimba baada ya kumwagikiwa na manii
Dalili za ugumba kwa wanaume
Baadhi ya dalili za ugumba kwa wanaume ni;
Kupungua hamu ya tendo la ndoa
Matatizo kusimamisha uume na umwagaji wa mbegu
Kuwa na korodani ndogo
Kuwa na uvimbe au maumivu ya korodani
Nini husababisha ugumba
Ili kutungusha mimba, mchakato tata ndani ya mwili unaohusisha utoaji, usafilishaji na uchavushaji wa yai kwa manii hutakiwa kutokea ipasavyo pasipo. Kwa baadhi ya wagumba, matatizo yanayosababisha huweza kuwa ya kuzaliwa nayo, au kupata ukubwani kutokana magonjwa au sababu yoyote inayoharibu utendaji kazi wa mfumo wa uzazi.
Sababu za ugumba huweza kuchangiwa na mwanamke au mwanaume huku kila mmoja akichangia asilimia kadhaa. Tafiti zinaonyesha kwamba, zaidi ya theluthi moja ya sababu za ugumba hutokana na mwanaume na theluthi moja nyingine hutokana na mwanamke na zilizobaki huchangiwa sawa sawa na mwanamke na mwanaume
Sababu zinazosababisha ugumba kwa Mwanaume
Sababu za mwanaume zinachochangia ugumba ni;
Matatizo ya utoaji wa manii
Kushindwa kutoa manii ya kutosha
Kufunga mirija ya uzazi
Kumwaga manii kabla ya wakati
Kumwaga manii ndani ya kibofu
Manii zenye maumbile yasiyo ya kawaida
Manii zizisoweza kujongea vema
Kuziba kwa mirija ya kupitisha manii
Magonjwa ya kuambukizwa ( magonjwa ya zinaa kama vile gono)
Magonjwa ya kuzaliwa
Kufanyika kwa uvimbe maji au kusinyaa kwa mirija ya kupitisha manii
Uharibifu au kuumia kwamirija ya uzazi
Madhaifu ya vichochezi
Mfano wa madhaifu yanayoweza kupelekea uharibifu wa usawa wa homoni ni saratani ya korodani au tezi pituitari
Kushindwa zalisha manii
Inaweza kusababishwa na kuvimba kwa mishipa inayotoa damu kwenye kododani
Matibabu yanayopelekea kupungua kwa uzalishaji wa manii mfano matibabu ya kutumia dawa za saratani na jamii ya steroid ikiwa pamoja na testosterone na matibabu ya kuondoa korodani.
Mtindo wa maisha
Utumiaji wa tumbaku
Matumizi ya kupitiliza ya pombe
Obeziti
Sababu za kimazingira
Huathiri manii hivyo kusababisha kupungua kwa idadi na ubora duni
Mfano
Mionzi
Sumu
Moshi
Joto kali (kwenye maeneo ya korodani
Madhaifu ya kuzaliwa
Kutoshuka kwa korodani kwenye mfuko wa kutunzia korodani
Kasoro za maumbile ya mfumo wa uzazi wa kiume na uume
Matatizo ya utoaji wa manii-shahawa wakati wa kujamiiana
Magonjwa yasiyo ya kuambukizwa
Magonjwa ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kisukari, ngiri maji
Sababu za Ugumba kwa mwanamke
Sababu za ugumba kwa mwanamke ni pamoja na:
Matatizo ya utoaji mayai, yanayozuia mayai kutoka kila mwezi. Mifano matatizo ya homoni yanayoweza kusababishwa na magonjwa kama Polisistiki ovariani sindromu- hupelekea ovari kuzalisha kwa wingi homoni testosterone na prolactine. Sababu nyingine za msingi zinazoweza kusababisha tatizo hili ni pamoja na kufanya mazoezi makali kupita kiasi , matatizo ya kula, jeraha/kuumia au uvimbe ndani ya kizazi.
Matatizo katika mfuko wa uzazi, mirija ya uzazi na mlango wa uzazi, ikiwa pamoja na matatizo ya kutofunguka kwa shingo ya uzazi wakati wa kujamiiana kwa sababu ya ute mzito unaozuia kitu chochote kuingia ndani ya mji wa uzazi ikiwemo manii, matatizo ya umbo au kuta za ndani ya uzazi.
​
Vimbe za fibroid ndani ya mfuko wa uzazi ni vimbe zinazotokea kwa wanawake wengi, mara chache zinaweza kusababisha ugumba endapo zimekuwa na kuziba mirija ya uzazi haswa ile inayopitisha mayai. Mara chache pia, fibroid inaweza kuharibu kuta za uzazi na hivyo kushindwa kujipandikiza kwa kijisu.
Kuziba au kuharibika kwa mirija ya kupitisha mayai, mara nyingi tatizo hili hutokana na makovu katika mirija ya uzazi. Makovu kwenye mirija ya uzazi husababishwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa
​
Kujipandikiza kwa tishu za ndani ya uzazi nje kizazi yaani tatizo la endometriosis, tatizo hili husababisha makovu kwenye mirija ya uzazi na maeneo mengine ambapo tishu hizo zimejipandikiza.
Uzalishaji duni wa homoni zinazotolewa na ovari, tatizo hili hutokea kwa baadhi ya wanawake, uzalishaji wa vichochezi huwa wa kiwango kidogo au kutozalishwa kabisa kabla mwanamke hajafikia umri wa miaka 40.
Makovu kwenye kuta ya mfuko wa uzazi au kushikamana kwa tishu. Makovu yanaweza kutokea baada ya maambukizi kwenye viungo vya uzazi, maambukizi ya kidole tumbo, au kufanyiwa upasuaji unaohusishaa tumbo na viungo vya uzazi. Makovu ndani ya mfumo wa uzazi hutengeneza mazingira yasiyo rafiki kwa yai lililochavushwa kujipandikiza
Sababu zingine
Matatizo ya tezi. Matatizo ya tezi ikiwa pamoja na tezi pituitari na thairoidi. Endapo tezi thairoidi itazalisha homoni kwa kiwango kidogo au kikubwa huweza kuharibu mzunguko wa hedhi au kusababisha ugumba.
Saratani na tiba zake. Baadhi ya saratani hasa saratani za mfumo wa uzazi mara nyingi husababisha matatizo ya uzazi. Dawa za kutibu saratani na mionzi inaweza kuathiri uwezo wa mwanamke wa kubeba ujauzito.
Magonjwa mengine. Magonjwa yanayosababisha kuchelewa kubalehe kama vile ugonjwa wa seliac, kushing, seli mundu, magonjwa ya figo au kisukari, huweza kuathiri uzazi wa mwanamke.
Matatizo ya maumbile yanaweza kusabisha kutungwa au mimba kukua kwa shida.
Baadhi ya dawa. Baadhi ya dawa huweza kusababisha ugumba wa muda, endapo dawa hizo zitaacha kutumiwa, tatizo hili linaweza kuisha baada ya muda. Dawa hizi mfano wake ni dawa za uzazi wa mpango.
Kufunga uzazi. Kufunga uzazi kwa kukata mirija ya uzazi huzuia yai kukutana na manii ili kufanya uchjavushaji
Mazio wa manii. Baadhi ya wanawake huwa na mzio mkali kwenye manii, manii huharibiwa na kinga ya mwili mara zinapoingia kwenye mfumo wa uzazi na hivyo kupelekea kutopata ujauzito.
​
Vihatarishi vya kupata ugumba kwa mwanamke na mwanaume
Vihatarishi vingi vya ugumba kwa mwanamke na mwanaume hufanana.
Vihatarishi hivyo ni pamoja na:
Umri. Uzazi wa mwanamke (uwezo wa kupata mimba) hupungua hatua kwa hatua kulingana na umri unavyoongezeka. Kasi ya kupungua uwezo wa kupata mimba huzidi mwanamke anapofikisha umri wa miaka 30. Ugumba kwa wanawake wenye umri mkubwa huweza kutokana na kupungua kwa ubora au idadi ya mayai yanayozalishwa. Umri mkubwa pia huambatana na matatizo ya afya katika viungo vya uzazi. Wanaume wenye umri chini ya miaka 40 huwa na uwezo wa kutungisha mimba zaidi, na wale wenye zaidi ya umri huu uwezo wao hupungua. Mwanaume anapofikisha umri wa miaka 50 na zaidi kiwango cha homon testoseterone hupungua na hivyo kusua sua kwa uzalishaji wa manii na kushindwa tungisha mimba.
Matumizi ya tumbaku. Nafasi ya wanandoa kupata mimba hupunguzwa kama mpenzi mmojawapo anatumia tumbaku. Kemikali zilizo ndani ya tumbaku pia huingiliana na matibabu ya matatizo ya uzazi kwa wale wanaotafuta kupata mtoto. Madhara yanayosababishwa na tumbaku ni kuharibika kwa uajauzito na uzalishaji mdogo wa manii
Matumizi ya pombe . Kwa wanawake, hakuna kiwango cha salama cha matumizi ya pombe wakati wa kubeba mimba au kulea mimba. Epuka pombe kama unatarajia kupata mimba wiki mbili kabla ya kutafuta ujauzito. Matumizi ya pombe huongeza hatari na kasoro za uzazi na mtoto, na pia inaweza kusababisha ugumu zaidi wa kupata mimba. Matumizi makubwa ya pombe kwa wanaume, hupunguza kiwango na uwezo wa manii kujongea kwa kasi yake asili
Kuwa na uzito mkubwa zaidi (obeziti) Uzito kupita kiasi huongeza hatari ya kupata utasa. Aidha, uzalishaji wa manii hupungua kwa wanaume walio wanene kupita kiasi.
Uzito mdogo kupita kiasi. Wanawake walio katika hatari ya matatizo ya uzazi ni pamoja na wale wenye matatizo ya kula, kama vile anorexia au bulimia, na wanawake ambao wanapata kiwango kidogo cha nishati kutoka kwenye chakula kwa sababu ya kujinyima kula.
Masuala ya mazoezi. Kutofanya mazoezi ya kutosha huchangia ongezeko la uzito na kuweza sababisha tatizo la ugumba. Kwa mara chache sana mazoezi kupita kiasi huchangia kuleta matatizo ya hedhi na ugumba
Vipimo na utambuzi wa tatizo
Vipimo vifuatavyo vinaweza kuagizwa vifanyike ili kuwza tambua tatizo lako
Vipimo kwa wanaume
Kipimo cha manii. Huangalia idadi, ubora na uwezo wa kujongea kwa manii
Ultrosound ya mfumo wa uzazi. Huangalia korodani na mirija ya uzazi ili kugundua kama kuna makovu, uvimbe na ngiri maji.
Kipimo cha biopsi. Nyama kidogo huchukuliwa kwenye korodani kwa ajili ya kipimo hiki
Kiwango cha homoni. Hulenga kugundua matatizo ya vichochezi
Kipimo cha mkojo. Huangalia tatizo la kucheua kwa manii ndani ya kibofu cha mkojo
Vipimo kwa mwanamke
Antibodi dhidi ya manii. Hupima uwepo wa kinga za mwili zinazoshambuliwa manii hivyo usababisha kutungishwa kwa yai
Ultrosound ya mfumo wa uzazi. Huweza kugundua uvimbe na matatizo mbalimbali kwenye mfumo wa uzazi
Uchunguzi wa mirija ya uzazi na kizazi. Hulenga kudungua matatizo ya mirija ya uzaz kama makovu n.k
Kiwango cha homoni. Huangaliwa kiwango cha homoni mbalimbali zinazohusiana na uzazi
Matibabu
Matibabu ya ugumba hutegemea kisababishi, umri wa tatizo la ugumba na umri wa mtu. Sababu hufahamika baada ya kufanyiwa uchunguzi na daktari . Matibabu yanaweza kuhusisha matumizi ya dawa ,upasuaji au vyote kwa pamoja.
Dawa
Baadhi ya dawa zinazotumika kwenye matatizo husika ni
Dawa za kurekebisha vichochezi
Dawa za kuchavusha mayai ( clomofen citrate, gonadotrophin n.k)
Dawa za antibayotiki (Matibabu ya maaambukizi kwenye mfumo wa uzazi kama PID n.k)
Upasuaji
Kuzibua mirija ya uzazi
upasuaji wa kuondoa uvimbe
Kupandikiza yai lililochavushwa nje ya kizazi kwenye uzazi
Matibabu mbadala
Tafiti zinaonyesha baadhi ya dawa asili na viinilishe vimechangia kukabiliana na tatizo la ugumba kwa wanaume na wanawake. Dawa nyingi hufanya kazi ya kuongeza uchavushaji na uzalishaji wa manii na mayai yenye ubora zaidi. Baadhi ya dawa pia hutibu madhaifu ya mfumo wa kinga ya mwili na magonjwa yanayopelekea ugumba.