top of page

Mwandishi:

Mhhariri

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

ULY CLINIC

2 Septemba 2026, 18:10:13

Vipele vya jasho

Vipele vya jasho

Upele wa jasho(vipele vya jasho), unaojulikana kitabibu kama miliaria au vipele vya joto, ni tatizo la ngozi linalotokea pale mirija midogo inayosafirisha jasho inapoziba na jasho kushindwa kufika kwenye uso wa ngozi na kutoka nje vizuri. Hali hii hutokea zaidi wakati wa joto na unyevunyevu, na inaweza kumpata mtu wa umri wowote, ingawa watoto wachanga huathirika zaidi.


Upele wa jasho kwa kawaida si ugonjwa hatari na mara nyingi huisha wenyewe baada ya ngozi kupozwa na sababu zinazochochea jasho nyingi kuondolewa. Hata hivyo, wakati mwingine unaweza kusababisha kuwasha sana, maumivu, vidonda au maambukizi ya ngozi ikiwa ngozi itakwaruzwa sana.


Upele wa jasho ni nini?

Upele wa jasho ni aina ya mwitikio wa ngozi unaotokea kutokana na kuziba kwa mirija ya jasho. Jasho linapozuiwa kutoka vizuri, hujikusanya ndani au karibu na ngozi na kusababisha muwasho, vijipele au vijivimbe vidogo.


Ndiyo maana upele huu huonekana zaidi katika mazingira ambayo mtu anatokwa na jasho nyingi, kama wakati wa hali ya hewa ya joto, kufanya mazoezi, kufanya kazi nzito au kuvaa mavazi mazito yasiyoruhusu hewa kupita.


Upele wa jasho unaweza kutokea mara kwa mara kwa mtu ambaye anaishi au kufanya kazi katika mazingira yenye joto na unyevunyevu.


Upele wa jasho unaonekanaje?

Muonekano wa upele wa jasho hutegemea aina yake na kina ambacho mirija ya jasho imeziba.

Unaweza kuonekana kama:

  • Vijipele vidogo vyekundu.

  • Vijivimbe vidogo vinavyowasha.

  • Malengelenge madogo yaliyojaa maji.

  • Ngozi kuwa nyekundu na yenye muwasho.

  • Hisia ya kuchomachoma au kuungua kwenye ngozi.

  • Maeneo ya ngozi kuwa na vijipele vingi vilivyokusanyika pamoja.

Kwa baadhi ya watu, upele unaweza kuwa na rangi inayotofautiana na ngozi ya kawaida, hasa ikiwa kuna uvimbe au muwasho mkubwa.


Upele wa jasho hutokea sehemu gani za mwili?

Upele wa jasho unaweza kutokea sehemu yoyote inayotoka jasho, lakini huonekana zaidi katika maeneo ambayo:

  • Jasho hukaa kwa muda.

  • Ngozi hukunjamana.

  • Mavazi hubana.

  • Hewa haizunguki vizuri.


Maeneo yanayoweza kuathirika ni pamoja na:

  • Shingo

  • Kifua

  • Mgongo

  • Tumbo

  • Kwapa

  • Kinena

  • Chini ya matiti

  • Sehemu za mikunjo ya ngozi

  • Paji la uso na kichwa, hasa kwa watoto

  • Sehemu nyingine zinazofunikwa na nguo

Kwa watoto wachanga, upele wa jasho unaweza kuonekana shingoni, mgongoni, kifuani au kwenye mikunjo ya ngozi.


Aina za upele wa jasho

Kuna aina mbalimbali za miliaria kulingana na sehemu ya mirija ya jasho inayoziba.


Miliaria kristalina

Hii ndiyo aina ya juu zaidi na kwa kawaida huwa nyepesi.

Huonekana kama malengelenge madogo sana yaliyojaa maji, ambayo yanaweza kupasuka kwa urahisi. Mara nyingi hayawashi sana na yanaweza kuisha haraka baada ya mwili kupozwa.


Miliaria rubra

Hii ndiyo aina inayojulikana zaidi kama vipele vya joto. Uonekana kama vijipele vidogo vyekundu( zambarau kwa watu weusi) vinavyoweza kuwasha au kuchomachoma. Mtu anaweza kuhisi kama sindano ndogo zinachoma ngozi, hasa anapotoka jasho. Aina hii hutokea zaidi katika maeneo yenye joto, unyevunyevu na msuguano.


Miliaria profunda

Hii ni aina isiyotokea mara kwa mara na hutokea ndani zaidi ya ngozi. Inaweza kuonekana kama vijivimbe vidogo vya rangi ya ngozi na inaweza kutokea baada ya mtu kuwa na vipindi vinavyorudiwa vya miliaria rubra.


Katika hali hii, uwezo wa ngozi kutoa jasho unaweza kupungua katika eneo lililoathirika, jambo ambalo linaweza kuongeza hatari ya mwili kushindwa kujipoza vizuri katika mazingira yenye joto kali.


Upele wa jasho unasababishwa na nini?

Sababu kuu ni kuziba kwa mirija ya jasho.

Mambo yanayoweza kuongeza uwezekano wa kuziba kwa mirija hiyo ni pamoja na:

  • Hali ya hewa yenye joto

  • Unyevunyevu mwingi

  • Kutokwa na jasho nyingi

  • Kufanya mazoezi katika mazingira ya joto

  • Kufanya kazi nzito

  • Kuvaa nguo nzito au zinazobana

  • Ngozi kugusana katika maeneo ya mikunjo

  • Kulala katika mazingira yenye joto

  • Homa inayosababisha kutokwa na jasho

  • Kukaa muda mrefu kwenye mazingira yenye joto bila kupozwa


Je, upele wa jasho unasababishwa na uchafu?

Hapana, upele wa jasho hausababishwi moja kwa moja na uchafu wa mwili. Mtu anaweza kupata upele huu hata akiwa anaoga na kutunza usafi wa mwili vizuri.


Tatizo kubwa ni joto, jasho na kuziba kwa mirija ya jasho, pamoja na mazingira yanayofanya ngozi ibaki yenye joto na unyevunyevu.


Hata hivyo, usafi wa kawaida wa ngozi ni muhimu kwa sababu ngozi iliyowashwa na kukwaruzwa inaweza kupata maambukizi.


Je, upele wa jasho unaambukiza?

Upele wa jasho hauambukizwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Mtu mwenye upele huu anaweza kuendelea kuishi na watu wengine bila kuwaweka katika hatari ya kupata upele huo.


Hii ni tofauti na baadhi ya magonjwa ya ngozi yanayosababishwa na bakteria, fangasi au vimelea kama scabies ambayo yanaweza kuambukiza.


Ni nani yuko katika hatari kubwa ya kupata upele wa jasho?

Mtu yeyote anaweza kupata upele wa jasho, lakini baadhi ya watu wana uwezekano mkubwa zaidi.


Watoto wachanga

Watoto wachanga huathirika zaidi kwa sababu tezi zao za jasho na mirija yake bado haijakomaa kikamilifu.

Pia mtoto anaweza kufunikwa kwa nguo nyingi au blanketi, jambo linaloweza kuongeza joto la mwili.


Watu wanaoishi kwenye maeneo yenye joto

Hali ya hewa yenye joto na unyevunyevu huongeza kutokwa na jasho na hivyo kuongeza uwezekano wa miliaria.


Watu wanaofanya kazi au mazoezi kwenye joto

Watu wanaofanya kazi za mikono, kilimo, ujenzi, michezo au shughuli nyingine zinazofanyika katika mazingira yenye joto wanaweza kupata upele wa jasho mara kwa mara.


Watu wenye mikunjo mingi ya ngozi

Mikunjo ya ngozi inaweza kuzuia hewa kupita na kufanya jasho likusanyike.


Je, upele wa jasho unaweza kuwasha?

Ndiyo. Muwasho ni mojawapo ya dalili zinazojulikana zaidi, hasa katika miliaria rubra. Mtu anaweza pia kuhisi kuchomachoma, kuungua au kama kuna sindano ndogo zinazochoma ngozi.


Kukwaruza kunaweza kuharibu ngozi na kuongeza hatari ya kupata maambukizi, hivyo ni vizuri kupunguza joto na jasho badala ya kukuna ngozi mara kwa mara.


Upele wa jasho na chunusi vina tofauti gani?

Upele wa jasho na chunusi vinaweza kufanana kwa baadhi ya watu, lakini si kitu kimoja.


Chunusi huhusishwa zaidi na kuziba kwa vinyweleo na mabadiliko yanayoathiri tezi zinazozalisha mafuta ya ngozi. Upele wa jasho, kwa upande mwingine, huhusishwa na kuziba kwa mirija ya jasho.


Chunusi huonekana zaidi usoni, kifuani na mgongoni, wakati upele wa jasho unaweza kuonekana katika maeneo yoyote yenye joto, jasho na mikunjo.


Upele wa jasho na fangasi vina tofauti gani?

Fangasi wa ngozi na upele wa jasho vinaweza kutokea katika maeneo yenye unyevunyevu, lakini sababu zake ni tofauti.


Maambukizi ya fangasi yanaweza kuleta wekundu, kuwasha, ngozi kuchubuka au upele wenye mipaka inayoweza kuonekana vizuri. Upele wa jasho mara nyingi huonekana kama vijipele vidogo au malengelenge vinavyohusiana na joto na kutokwa jasho.


Kwa kuwa zinaweza kufanana, hasa katika maeneo ya mikunjo, daktari anaweza kuhitajika kufanya uchunguzi ikiwa upele hauponi baada ya kupozwa na kukausha ngozi.


Upele wa jasho na skabizi vina tofauti gani?

Skabizi husababishwa na vimelea vidogo vinavyoingia kwenye ngozi na huambukizwa kwa mawasiliano ya karibu.


Muwasho wa scabies mara nyingi huwa mkali, hasa usiku, na upele unaweza kuonekana kwenye maeneo maalumu kama kati ya vidole, mikono, kiunoni na sehemu nyingine za mwili.


Upele wa jasho hauambukizi na kwa kawaida huongezeka wakati wa joto na kupungua ngozi inapopozwa.


Upele wa jasho unatibiwaje?

Katika hali nyingi, hatua muhimu zaidi ni kupunguza joto na kuzuia kutokwa na jasho kupita kiasi.

Mambo yanayoweza kusaidia ni:

  • Kuhamia sehemu yenye ubaridi

  • Kuoga maji ya kawaida au ya baridi kiasi

  • Kuweka kitambaa chenye ubaridi kwenye eneo lililoathirika

  • Kuvaa nguo nyepesi na zinazopitisha hewa

  • Kuepuka mavazi yanayobana

  • Kuweka ngozi katika hali ya ukavu

  • Kuepuka shughuli zinazoongeza jasho mpaka upele upungue

  • Kuepuka kujikuna


Mara nyingi, upele hupungua baada ya ngozi kupozwa na jasho kupungua.


Je, ni lazima kutumia dawa?

Si kila mtu mwenye upele wa jasho anahitaji dawa. Ikiwa upele ni mdogo, kupunguza joto, kuvaa nguo zinazopitisha hewa na kuweka ngozi katika hali ya baridi na ukavu kunaweza kutosha.


Ikiwa muwasho ni mkubwa, mtaalamu wa afya anaweza kupendekeza matibabu ya kupunguza muwasho kulingana na umri wa mtu, eneo lililoathirika na hali ya ngozi.


Usitumie dawa kali za kupaka, hasa steroid zenye nguvu, bila ushauri wa mtaalamu wa afya.


Je, losheni ya calamine inaweza kusaidia?

Losheni ya calamine inaweza kusaidia kupunguza muwasho kwa baadhi ya watu, lakini si lazima kwa kila mtu.

Ni muhimu kuitumia kwa usahihi na kuepuka bidhaa zinazoweza kuziba zaidi ngozi au kuongeza muwasho.

Kwa watoto wadogo sana au maeneo nyeti, ni vizuri kupata ushauri wa mtaalamu kabla ya kutumia dawa yoyote.


Je, poda inaweza kusaidia upele wa jasho?

Poda si tiba ya lazima kwa upele wa jasho. Baadhi ya poda zinaweza kusaidia kupunguza unyevunyevu wa ngozi, lakini matumizi mengi yanaweza pia kusababisha matatizo mengine, hasa kama poda inatengeneza tabaka linaloziba ngozi.


Kwa watoto wachanga, hasa, haishauriwi kutumia poda ya talc kwa sababu ya hatari za kuvuta chembe zake kupitia hewa.


Je, mafuta ya kupaka yanafaa?

Mafuta mazito na krimu zinazoziba ngozi zinaweza kuongeza tatizo kwa baadhi ya watu kwa sababu zinaweza kuzuia joto na jasho kutoka vizuri.


Ikiwa ngozi ina upele wa jasho, ni bora kuepuka bidhaa nzito sana zinazofanya ngozi ibaki na mafuta na joto.

Ikiwa ngozi imekauka au imekuwa na muwasho mkubwa, daktari au mfamasia anaweza kupendekeza bidhaa inayofaa zaidi.


Upele wa jasho hupona kwa muda gani?

Miliaria nyepesi mara nyingi huanza kupungua baada ya ngozi kupozwa na mazingira yenye joto kuondolewa.

Muda wa kupona hutofautiana kulingana na aina ya upele, kiwango cha kuziba kwa mirija ya jasho na kama mtu anaendelea kukaa katika mazingira ya joto.


Ikiwa upele unaendelea kwa muda mrefu licha ya hatua za kupunguza joto, ni muhimu kuonana na mtaalamu wa afya ili kuhakikisha kwamba si ugonjwa mwingine wa ngozi.


Je, upele wa jasho unaweza kurudi?

Ndiyo. Mtu anaweza kupata upele wa jasho zaidi ya mara moja. Ikiwa mtu anaishi katika mazingira yenye joto na unyevunyevu au anafanya kazi zinazomsababisha kutokwa jasho sana, upele unaweza kurudia.

Kuzuia joto kupita kiasi, kuvaa nguo zinazopitisha hewa na kupunguza jasho ni hatua muhimu za kupunguza uwezekano wa kurudia.


Jinsi ya kuzuia upele wa jasho

Upele wa jasho (miliaria) hutokea zaidi wakati wa joto na unyevunyevu, hasa pale jasho linapozidi na kushindwa kutoka vizuri kupitia mirija ya jasho. Kwa hiyo, njia kuu ya kuuzuia ni kupunguza joto la mwili, kupunguza unyevunyevu kwenye ngozi na kuruhusu ngozi kupata hewa ya kutosha.

1. Epuka joto kupita kiasi

Kaa sehemu yenye hewa ya kutosha na yenye ubaridi inapowezekana. Epuka kukaa muda mrefu kwenye jua kali au kufanya shughuli nzito wakati wa joto kali.

2. Vaa nguo nyepesi

Chagua nguo zilizolegea na zinazopitisha hewa, kama za pamba. Epuka nguo nzito zinazoweza kuongeza joto na unyevunyevu kwenye ngozi.


3. Oga baada ya kutokwa jasho nyingi

Kuoga husaidia kuondoa jasho kwenye ngozi na kuifanya ipoe. Tumia maji ya kawaida au ya uvuguvugu kuelekea baridi na kausha ngozi taratibu.


4. Badilisha nguo zenye jasho

Badilisha nguo zilizolowa jasho baada ya kufanya mazoezi au kazi nzito. Kuvaa nguo kavu husaidia kupunguza unyevunyevu unaoweza kuchangia upele.


5. Epuka mavazi yanayobana

Mavazi yanayobana huongeza joto, msuguano na unyevunyevu kwenye ngozi. Vaa nguo zinazokaa kwa uhuru, hasa katika maeneo yenye mikunjo ya ngozi.


6. Usimfunike mtoto kupita kiasi

Mvalishe mtoto kulingana na hali ya hewa na epuka kumfunika kwa tabaka nyingi za nguo au blanketi wakati wa joto. Hakikisha pia analala katika sehemu yenye hewa ya kutosha.


Je, upele wa jasho ni hatari?

Mara nyingi si hatari. Tatizo kubwa zaidi linaweza kutokea ikiwa mtu anakaa katika mazingira ya joto sana na mwili unashindwa kujipoza. Hali hii inaweza kuhusishwa na magonjwa yanayotokana na joto, kama mchosho wa jasho na katika hali kali mshituko wa joto.


Dalili kama kuchanganyikiwa, kupoteza fahamu, mwili kuwa na joto kali sana, udhaifu mkubwa au degedege katika mazingira ya joto ni ishara za dharura na zinahitaji huduma ya haraka.


Je, upele wa jasho unaweza kuambatana na maambukizi?

Ndiyo, ingawa si jambo la kawaida kwa upele wa jasho usiochanganyika na majeraha.

Kukwaruza sana kunaweza kuvunja ngozi na kuruhusu bakteria kuingia. Hii inaweza kusababisha maambukizi ya ngozi.


Dalili zinazoweza kuashiria maambukizi ni pamoja na:

  • Usaha

  • Maumivu yanayoongezeka

  • Uvimbe mkubwa

  • Wekundu unaoenea

  • Ngozi kuwa yenye joto sana katika eneo hilo

  • Homa

Mtu mwenye dalili hizi anapaswa kuchunguzwa na mtaalamu wa afya.


Wakati gani kumuona daktari?

Muone daktari ikiwa:

  • Upele haupungui baada ya kupunguza joto na jasho

  • Upele unaendelea kuongezeka

  • Kuna usaha au maambukizi

  • Kuna maumivu makali

  • Kuna homa

  • Ngozi inakuwa na vidonda

  • Upele unarudia mara kwa mara bila sababu inayoeleweka

  • Huna uhakika kama ni upele wa jasho

  • Mtoto mchanga ana upele mwingi unaoambatana na hali isiyo ya kawaida


Ikiwa mtu aliyekuwa kwenye joto kali ana kuchanganyikiwa, kupoteza fahamu, degedege au joto la mwili kuwa juu sana, hiyo si hali ya kusubiri nyumbani; anahitaji huduma ya dharura.


Hitimisho

Upele wa jasho ni tatizo la ngozi linalotokana hasa na kuziba kwa mirija ya jasho, na hutokea zaidi wakati wa joto, unyevunyevu na kutokwa jasho nyingi. Kwa kawaida si hatari na hupungua baada ya ngozi kupozwa, kukaa katika mazingira yenye hewa na kuvaa mavazi mepesi.


Ikiwa upele unaendelea, unaambatana na usaha, maumivu, homa au dalili zisizo za kawaida, ni muhimu kumuona mtaalamu wa afya kwa sababu unaweza kuwa ugonjwa mwingine wa ngozi au maambukizi.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu upele wa jasho

1. Je, upele wa jasho unaweza kuenea mwili mzima?

Ndiyo, hasa ikiwa mtu yuko katika mazingira yenye joto sana na anatokwa na jasho katika sehemu nyingi za mwili. Upele unaweza kuonekana kwenye shingo, kifua, mgongo, tumbo na maeneo ya mikunjo kwa wakati mmoja.


Hata hivyo, upele unaoonekana karibu kila sehemu ya mwili haupaswi kudhaniwa moja kwa moja kuwa ni upele wa jasho. Magonjwa kama mzio, maambukizi ya virusi, dawa fulani na magonjwa mengine ya ngozi yanaweza pia kusababisha upele mpana.


Ikiwa upele umeenea haraka, unaambatana na homa, kuvimba uso, shida ya kupumua au hali ya mgonjwa kubadilika, anapaswa kutafuta huduma ya kitabibu haraka.

2. Je, mtoto anaweza kupata upele wa jasho usoni?

Ndiyo. Watoto wachanga wanaweza kupata miliaria kwenye uso, kichwa, shingo na maeneo mengine kwa sababu mfumo wao wa kudhibiti joto bado unaendelea kukomaa.


Kumfunika mtoto kwa nguo nyingi au kumweka katika chumba chenye joto kunaweza kuongeza hatari ya kutokwa jasho na kupata upele.


Njia muhimu ni kumweka katika mazingira yenye joto linalofaa, kumvalisha nguo nyepesi na kuepuka kumfunika kupita kiasi. Ikiwa mtoto ana homa, hana nguvu, anakataa kunyonya au anaonekana mgonjwa, usidhanie kuwa ni upele wa jasho pekee.

3. Je, kuoga maji baridi kunaondoa upele wa jasho?

Kupooza ngozi kunaweza kusaidia kupunguza joto, muwasho na kuchomachoma vinavyotokana na upele wa jasho.


Hata hivyo, si lazima kutumia maji ya barafu. Maji ya kawaida au yenye ubaridi wa wastani yanaweza kutosha na yanaweza kuwa na usumbufu mdogo kwa mtu mwenye ngozi iliyowashwa.


Baada ya kuoga, ngozi inaweza kukaushwa kwa kupapasa taratibu badala ya kusugua. Muhimu zaidi ni kuendelea kuzuia mazingira yanayosababisha jasho nyingi.

4. Je, upele wa jasho unaweza kusababisha makovu?

Upele wa jasho usio na matatizo kwa kawaida hauachi makovu ya kudumu.


Hatari ya ngozi kuharibika huongezeka ikiwa mtu anakwaruza sana, anachoma vijipele, anavipasua au anatumia kemikali kali kwenye ngozi.


Kwa watu wenye ngozi yenye rangi nyeusi, kuvimba au kuumia kwa ngozi kunaweza kuacha eneo likiwa na rangi nyeusi zaidi kwa muda. Hivyo, kuepuka kujikuna na kutumia matibabu yasiyofaa ni muhimu.

5. Je, mtu anaweza kupata upele wa jasho hata kama hajafanya mazoezi?

Ndiyo. Mazoezi ni moja tu ya sababu zinazoweza kuongeza jasho.


Mtu anaweza kupata upele akiwa amelala katika chumba chenye joto, amevaa nguo nzito, ana homa au anaishi katika mazingira yenye joto na unyevunyevu.


Kwa hiyo, kutopafanya mazoezi hakumaanishi kwamba mtu hawezi kupata miliaria. Jambo muhimu ni kiasi cha joto na jasho pamoja na jinsi ngozi inavyoweza kutoa jasho.

6. Je, upele wa jasho unaweza kutokea wakati wa homa?

Ndiyo. Homa inaweza kuongeza joto la mwili na kusababisha kutokwa jasho, hali inayoweza kuchochea miliaria.


Hata hivyo, upele unaotokea pamoja na homa haupaswi kuitwa moja kwa moja upele wa jasho. Homa na upele vinaweza pia kutokea katika maambukizi mbalimbali.


Ikiwa mtu ana homa pamoja na upele mpana, maumivu makali, hali ya kuchanganyikiwa, shingo kukakamaa au hali nyingine mbaya, anahitaji uchunguzi wa kitabibu.

7. Je, upele wa jasho unaweza kusababisha mtu kutotokwa jasho?

Katika aina ya kina zaidi ya miliaria, mirija mingi ya jasho inaweza kuziba kiasi cha kupunguza uwezo wa eneo lililoathirika kutoa jasho.


Hali hii inaweza kuwa muhimu zaidi ikiwa mtu anaendelea kuwa katika mazingira yenye joto, kwa sababu jasho ni mojawapo ya njia muhimu za mwili kujipoza.


Mtu anayeshindwa kutokwa jasho katika mazingira ya joto na kuanza kupata udhaifu, kizunguzungu, kuchanganyikiwa au joto kali la mwili anapaswa kuondoka kwenye mazingira ya joto na kutafuta huduma ya haraka.

8. Je, dawa za steroid zinaweza kutibu upele wa jasho?

Steroidi za kupaka si tiba ya msingi ya upele wa jasho. Katika baadhi ya mazingira, mtaalamu wa afya anaweza kutumia dawa maalumu kwa muda mfupi kupunguza uvimbe au muwasho, lakini matumizi yake yanapaswa kuzingatia eneo na umri wa mgonjwa.


Kutumia steroidi kali usoni au kwenye maeneo nyeti bila ushauri wa daktari kunaweza kusababisha madhara kama ngozi kuwa nyembamba, kubadilika rangi, chunusi za steroidi na matatizo mengine.


Kwa hiyo, usitumie krimu yenye steroid kwa sababu tu umeona inaondoa muwasho. Ni muhimu kwanza kujua aina ya upele.

9. Je, upele wa jasho unaweza kufanana na mzio?

Ndiyo. Hii ni moja ya sababu zinazofanya wakati mwingine iwe vigumu kujitambua mwenyewe.


Mzio unaweza kusababisha vipele vinavyowasha, wekundu au uvimbe, wakati miliaria mara nyingi huhusishwa na joto na kuziba kwa mirija ya jasho.


Ikiwa upele hutokea baada ya kutumia dawa, chakula, sabuni, vipodozi au kitu fulani na unaambatana na kuvimba midomo/uso au shida ya kupumua, hiyo inaweza kuwa allergic reaction na inahitaji huduma ya haraka.

10. Je, ni lazima kwenda hospitali kila ninapopata upele wa jasho?

Hapana. Upele mdogo unaoonekana wazi wakati wa joto na unaopungua baada ya kupooza ngozi mara nyingi unaweza kudhibitiwa nyumbani.


Hata hivyo, ni muhimu kwenda kwa mtaalamu wa afya ikiwa upele unaendelea, unarudia mara kwa mara, unauma sana, una usaha, unaambatana na homa au kuna mashaka kwamba huenda si upele wa jasho.


Lengo la uchunguzi si tu kutibu upele, bali pia kuhakikisha kwamba hali nyingine kama fangasi, skabizi, mzio, maambukizi ya bakteria au magonjwa mengine ya ngozi hazijafichika nyuma ya upele unaodhaniwa kuwa wa jasho.


Imeandikwa:

2 Septemba 2026, 17:44:55

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Rejea za mada hii:

  1. Guerra KC, Toncar A, Krishnamurthy K. Miliaria [Internet]. Treasure Island (FL): StatPearls Publishing; 2026 Jan- [updated 2024 Sep 1; cited 2026 Sep 2].
    https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK537176/

  2. Wenzel FG, Horn TD. Nonneoplastic disorders of the eccrine glands. J Am Acad Dermatol. 1998;38(1):1-17. doi:10.1016/S0190-9622(98)70532-8.
    https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/9448199/

  3. Palaniappan V, Sadhasivamohan A, Sankarapandian J, Karthikeyan K. Miliaria crystallina. Clin Exp Dermatol. 2023;48(5):462-467. doi:10.1093/ced/llad032.
    https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/36692206/

  4. Carter R, Garcia AM, Souhan BE. Patients presenting with miliaria while wearing flame resistant clothing in high ambient temperatures: a case series. J Med Case Rep. 2011;5:474. doi:10.1186/1752-1947-5-474.
    https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/21939537/

  5. El Anzi O, Hassam B. Widespread miliaria crystallina: about a case. Pan Afr Med J. 2018;30:69. doi:10.11604/pamj.2018.30.69.15572.
    https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/30344853/

  6. Kirk JF, Wilson BB, Chun W, Cooper PH. Miliaria profunda. J Am Acad Dermatol. 1996;35(5 Pt 2):854-856.
    https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/8912605/

bottom of page